Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mgonjwa wa saratani Uganda: Jinsi kitanda kilivyookoa maisha yangu
- Author, By Anne Okumu
- Nafasi, BBC
- Iliyochapishwa
Wakati familia ya Dorcas Cherop mwenye umri wa miaka 14 ilipoambiwa anahitaji kufanyiwa matibabu ya mwaka mzima ya saratani ya kibofu cha mkojo nchini Uganda, mustakabali wake ulionekana kuwa mbaya.
Changamoto haikuwa kupata huduma ya matibabu, ambayo ni kama bure katika Taasisi ya Saratani ya Uganda (UCI), lakini ni zile gharama za safari kwenda na kurudi Kampala na kutafuta makazi atakapokuwa anakwenda mara kwa mara hospitalini.
"Mama na baba yangu ni wakulima kwa hivyo hawakuwa na pesa za kutosha kunisafirisha kutoka Kapchorwa mashariki mwa Uganda hadi Kampala," kijana huyo aliambia BBC.
Aligunduliwa na saratani akiwa na umri wa miaka 11, 2020 alipokuwa akifanyiwa vipimo. Kabla ya matibabu kuanza, shangazi yake Stella Chepchirir anasema walilazimika kufanya safari kuwaona madaktari kila baada ya wiki mbili.
"Hali ilikuwa mbaya. Wakati fulani, familia ilifikiria kukata tamaa na kurejea nyumbani," Bi Chepchirir anaeleza.
"Tulikuwa tumeishiwa pesa. Lakini cha kusikitisha zaidi ni kumuona akiwa na maumivu wakati tuliposafiri saa saba kwenda Kampala na kurudi."
Katika taifa hilo la Afrika Mashariki, hadi 2021 inakadiriwa kuwa mtoto mmoja kati ya watatu waliokuwa na saratani hutelekeza matibabu kwa sababu ya gharama za aina hiyo.
Dk Joyce Balagadde-Kambugu, mkuu wa kitendo cha saratani ya watoto UCI, anasema, sawa na Dorcas, watoto wengi wenye saratani wanaishi vijijini.
"Asilimia 80 hadi 85% ya idadi ya watoto walio na saratani hapa katika taasisi hiyo ni wakulima ambao wanaishi chini ya dola ya kimarekani 3 kwa mwezi."
"Hali inasikitisha kwani zaidi ya 50% huachana na matibabu kwa sababu ya umasikini," anasema.
Idadi ya walioacha matibabu inatofautiana mwaka hadi mwaka, lakini ilikuwa karibu 30% mwaka 2021 - ikimaanisha takribani wagonjwa 1,000 wa saratani wanaolazwa UCI kila mwaka, ni 300 pekee wanaomaliza matibabu yao.
Dkt. Balagadde-Kambugu anasema wagonjwa wengi wanaotoka sehemu mbalimbali za nchi wanahitaji kukaa Kampala kwa miezi sita hadi saba, na wakati mwingine miaka.
Matibabu mengi ya saratani huhusisha dawa za kula mara kwa mara - ni matibabu yanayohusisha madawa ambayo huharibu seli za saratani zinazokua kwa kasi katika mwili.
Baadhi ya familia huja na suluhisho la muda la hupiga kambi katika korido za hospitali, kulala kwenye sakafu baridi na blanketi za ngozi.
Hii pia ina madhara makubwa kwa afya ya watoto, huku wengine wakiishia kuambukizwa magonjwa kama vile malaria na kuhara, anasema Dk Balagadde-Kambugu.
Kitengo cha saratani ya watoto sasa kimeungana na shirika la hisani ambalo limetokeza kutoa msaada.
Familia ya Dorcas huko Kapchorwa, ambaye miaka mitatu iliyopita alikuwa amekata tamaa ya kuendelea na matibabu yake, alipokea simu asiyoitarajia kutoka UCI.
Waliunganishwa na Taasisi ya Bless a Child Foundation (BCF), inayotoa hifadhi ya bure kwa watoto wenye saratani wanapopatiwa matibabu.
BCF ilifungua milango yake mwaka 2010, awali ikitoa malazi kwa hadi watoto 10 wenye saratani katika nyumba moja mjini Kampala.
Tangu wakati huo imepanuka na kufikia nyumba nne, mbili Kampala, moja katika mji wa magharibi wa Mbarara na nyingine Gulu kaskazini mwa nchi.
Kila nyumba inaweza kuchukua watoto wapatao 100 na mlezi mmoja na sasa inatoa chakula, mwalimu wa nyumbani, msaada wa kisaikolojia na kijamii na usafiri wa kwenda na kurudi hospitalini kwa siku za matibabu.
"Tunapata kila kitu, kuanzia malazi, chakula hata nguo," Dorcas aliambia BBC alipokuwa ameketi kwenye bembea katika bustani ya BCF mjini Kampala.
Baadhi ya watoto waliokuwa karibu walionekana wakicheza mchezo wa kuteleza, wengine wakicheza drafti na kikundi kingine kikicheza muziki.
Kicheko cha furaha
Katika kipindi cha miaka 13 iliyopita, nyumba za BCF zimehudumia zaidi ya watoto 6,000, anasema mwanzilishi mwenza Peter Genza.
"Nyumba hizo hutoa malazi, msaada wa kisaikolojia, msaada wa kufiwa, matibabu kwa michezo, elimu, kurekebisha tabia na chochote wanachohitaji ili wapate huduma," aliambia BBC.
Kulingana na Dk Balagadde-Kambugu, mpango huo unaonekana kuwa na matokeo chanya - huku kiwango cha walioacha shule kikishuka katika mwaka uliopita hadi 9%.
Kwa Dorcas, ambaye amedhamiria kuushinda ugonjwa huo, hakika makaazi hayo yamemletea mabadiliko makubwa.
"Nina furaha sana na sina tena maumivu kama zamani," anasema. "Ninashukuru kwa kunipa maisha mapya."
Kijana huyo sasa amerejea nyumbani na atarejea Kampala mwezi wa Disemba kuona hali yake inaendeleaje.