Pele: Gwiji wa Brazil asema yuko 'imara na mwenye matumaini mengi'

Iliyochapishwa

 

Gwiji wa Brazil Pele anasema "yuko imara na mwenye matumaini makubwa" alipokuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya Sao Paulo.

Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi alisema jumbe za kumuunga mkono pamoja na kutazama Brazil kwenye Kombe la Dunia zimempa "nguvu".

Hapo awali hospitali hiyo ilisema "bado anaendelea na matibabu na yuko sawa".

Inafuatia ripoti nchini Brazil kwamba alikuwa anaanza huduma ya mwisho wa maisha baada ya tiba ya kemikali ya chemotherapy kushindwa kufanya kazi.

"Rafiki zangu, ninataka kila mtu kuwa mtulivu na chanya," alisema katika taarifa kwenye Instagram.

"Niko imara, nina matumaini makubwa na ninafuatilia matibabu yangu kama kawaida. Napenda kuwashukuru timu nzima ya madaktari na wauguzi kwa huduma zote nilizopata.

"Nina imani kubwa kwa Mungu na kila ujumbe wa upendo ninaopokea kutoka kwako duniani kote hunifanya niwe na nguvu nyingi.

Pia mimi natazama Brazil inapocheza kwenye Kombe la Dunia!

"Asante sana kwa kila kitu."

 Mshindi huyo wa Kombe la Dunia mara tatu, 82 amekuwa hospitalini tangu Jumanne, na Alhamisi usiku alisema ilikuwa ni "ziara ya kawaida ya kila mwezi".

Aliondolewa uvimbe kwenye utumbo wake mnamo Septemba 2021.  

Taarifa kutoka Hospitali ya Israelta Albert Einstein siku ya Jumamosi ilisema Pele "alikuwa na mwitikio mzuri wa matibabu ya maambukizo ya kupumua".

Iliongeza kuwa alikuwa akipitia "utathmini upya wa matibabu ya chemotherapy".

Mshambuliaji huyo mashuhuri aligundulika kuwa na maambukizo ya kupumua na mnamo Ijumaa hospitali ilikuwa imesema alikuwa katika hali nzuri.

Siku ya Jumamosi, taarifa hiyo mpya ilisema hali yake haijazidi kuwa mbaya katika saa 24 zilizopita.

Wakati huo huo, ujumbe wa kumpa moyo umetumwa kutoka kote ulimwenguni.

'Ametoa hamasa kwa wengi'

Akizungumza Jumamosi, nahodha wa Uingereza Harry Kane alisema: "Tunasikitika sana kusikia habari za yeye kuwa mgonjwa lakini tunamtakia heri, si mimi tu bali timu yote ya  maandalizi ya Uingereza. Yeye ametoa hamasa, ni mtu wa kipekee sana."

Mshambulizi wa zamani wa Ujerumani aliyeshinda Kom be la Dunia, Jurgen Klinsmann, akizungumza kwenye matangazo ya Kombe la Dunia la BBC One Jumamosi, alisema: "Pele ni mtu mzuri sana. Mtu bora wa kandanda duniani. Tunaweza tu kuomba na kutumaini mema."

Beki wa zamani wa Argentina Pablo Zabaleta aliongeza kwenye BBC One: "Ni habari za kusikitisha sana kusikia kuhusu Pele. Amekuwa msukumo wa kweli kwetu sote, ndani na nje ya uwanja. Daima amekuwa mtu mashuhuri."

"Tunamuombea Mfalme," mshambuliaji wa Ufaransa Kylian Mbappe aliweka ujumbe kwenye mtandao wa Twitter."

Taifa mwenyeji wa Kombe la Dunia Qatar lilionyesha kumuunga mkono Pele siku ya Jumamosi, na kuwasha majengo kwa ujumbe wa "Pona haraka Pele".

Uwanja wa Lusail mjini Doha, ambao utakuwa mwenyeji wa fainali ya Kombe la Dunia tarehe 18 Desemba, na Aspire Tower karibu na Uwanja wa Khalifa, ulipambwa kwa picha za Pele katika shati lake maarufu namba 10.

Wasiwasi ulizuka hapo awali Jumatano wakati ESPN Brasil iliporipoti Pele alikuwa amelazwa, huku binti yake Kely Nascimento akisema "hakuna dharura" iliyohusika, yaani alikuwa akipata matibabu ya kawaida.

Pele aliwashukuru watu waliomtakia heri siku ya Ijumaa kwa kutuma "ujumbe wa matumaini" na kusema kukaa kwake hospitalini ni katika "ziara ya kawaida".

Mshambuliaji huyo wa zamani ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Brazil akiwa na mabao 77 katika michezo 92 na alifunga katika michuano minne ya Kombe la Dunia.

Santos, klabu yake pekee ya Brazil, iliweka ujumbe kwenye mtandao wa Twitter: "Dunia nzima inakutakia mema, Mfalme Pele".