Majengo ya Kariakoo: Serikali ya Tanzania yatakiwa kuchukua hatua kali kuepusha majanga

    • Author, Alfred Lasteck
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Tanzania
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6
sdzx
Maelezo ya picha, Takribani watu 20 wamefariki hadi sasa kwa mujibu wa serikali ya Tanzania

Wataalamu wa ujenzi nchini Tanzania wamezitaka mamlaka nchini humo kuzingatia na kutekeleza yale yanayoshauriwa na tume zinazoundwa kuchunguza hali ya majengo yaliyopo Kariakoo na katikati ya jiji la Dar Es salaam ili kuwa na suluhu ya kudumu na kuepusha ya madhara yanayoweza kuletwa na majengo yaliyo chini ya kiwango.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, ubora hafifu na mabadiliko ya matumizi ya majengo huenda yakasababisha majengo mengi kuanguka katika eneo hilo.

Jumamosi ya Novemba 16 jengo la ghorofa nne lilianguka Kariakoo na kusababisha vifo vya watu takribani 20. Mamlaka za Tanzania sasa zinaendelea na shughuli za kusafisha eneo hilo na kuendelea kutafuta miili iliyonasa kwenye vifusi ili isitiriwe kwa heshima.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassana mabaye amezuru eneo la tukio jana Jumatano naye amepaza sauti yake juu ya hali ya majengo ya Kariakoo. Rais Samia ameeleza kuwa ni wazi kuwa jengo lililoporomoka halikujengwa kwa viwango stahiki na ameahidi kuwa uchunguzi utaangazi ubora wa majengo yote ya Kariakoo.

“…Tukio hili ukiangalia kwa macho tu, hata kama si mtaalamu linaashiria kuwepo kwa mapungufu ya kiutendanji na uwajibikaji…ukiangalia hili jengo lilivyojengwa, bila shaka lilipata vibali kutoka ofisi husika za serikali…lakini kibali ni jambo moja na ujenzi ni jambo lengine. Jengo lile halikutazamwa ubora wake wakati wa ujenzi,” amesema rais Samia.

“Kwa hivyo niwaombe watu wote wanaohusika kwenye mambo haya, tuseme kwa pamoja kuwa matukio ya namna hii yasijirudie tena,” amesisitiza rais Samia.

Mhandisi majengo Innocent Ben anasema, “wakati mwingine ni hatari sana, maendeleo yanaenda kwa kasi sana lakini baadhi ya maeneo yaliyojengwa kwa ajili ya makazi yamebadilishiwa matumizi na kufanywa ya kibiashara na zaidi kuhifadhi mizigo.”

Innocent anasema, ni vyema majengo yaliyojengwa yaendelee kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa kwa kuwa mabadiliko yanaweza kusababisha madhara makubwa. “Uchunguzi utupe matokeo na ushauri uzingatiwe kwasababu wananchi wengi waliopo ndani ya majengo hayo hawafahamu kuhusu ubora hivyo hawawezi kuchukua tahadhari stahiki.”

Sakata la sasa linachunguzwa na akina nani?

SD
Maelezo ya picha, Juhudi za uokoaji zikiendelea katika jengo lililoporomoka Kariakoo
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuelekeza majengo yote Kariakoo kufanyiwa ukaguzi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema tayari tume ya watu 19 imeundwa ili kujua ubora wa majengo pamoja na shughuli zinazoendelea katika eneo hilo.

Akizungumza wakati wa kuaga miili ya watu waliofariki baada ya jengo kuporomoko eneo la Kariakoo Novemba 16, 2024, amesema tume hiyo itakayoongozwa na Bregedia Jenerali Hosea Ndagala ambaye ni Mkuu wa Idara ya Menejimenti ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, itaisadia kuishauri Serikali kujua ni hatua gani ifanye baada ya uchunguzi huo.

“Mahitaji ya Soko la Kariakoo bado yako palepale. Soko la Kariakoo ni soko la kimataifa kwa sasa linalotegemewa na nchi zote zinazotuzunguka hapa jirani, kwahiyo tunayo sababu ya kuimarisha lakini pia kutambua ubora wa majengo tuliyonayo,” alisema Majaliwa.

Rais Samia jana ameeleza kuwa endapo tume hiyo itashauri majengo yaliyojengwa chini ya kiwango yavunjwe, serikali yake haitasita kufanya hivyo.

Wengine wapanga kukimbia eneo hilo

“Familia yangu haitafanya kazi tena Kariakoo. Mimi, mke wangu na watoto wangu wawili tumekuwa tukifanyabiashara Kariakoo kwa miaka minne sasa. Sidhani kama tutaendelea kuwa katika sehemu tunayofanyia biashara, kama yalivyo maeneo mengi mengin” Mfanyabiashara Obadia Munuo ameiileza BBC.

Kwa upande wake mbunifu majengo, Joseph Magida anasema,"Tunatumai mapendekezo ya timu inayochunguza yatatekelezwa. Kariakoo inahitaji suluhisho la kudumu. Mwaka 2006 jengo la kibiashara liliporomoka kilomita chache kutoka eneo la Kariakoo. Na licha ya pendekezo la timu kuhusu hali ya majengo ya biashara jijini, hakuna hatua iliyochukuliwa…

“…Serikali inapaswa kutambuana kutekeleza mapendekezo kama ilivyopendekezwa na timu ya uchunguzi ikiwemo kuwawajibisha watu wote ambao hawafuati taratibu,” alisema.

Je hatua huchukuliwa?

wsd
Maelezo ya picha, Maafisa wa Jeshi la Tanzania, wakibeba miili ya waliofariki katika jengo hilo

Hili si tukio la kwanza la jengo kuporomoka katika jiji la Dar es salaam katika miaka ya hivi karibuni. Mwaka 2006, jengo liliporomoka eneo la Changombe jijini Dar es Salaam na kuua watu wanne

Juni 2008, ghorofa lililokuwa likijengwa jijini Dar es Salaam liliangukia jengo jengine dogo ambapo walikuwa wakiishi watu.

Machi 2013, jengo la ghorofa 16 katika eneo jiji hilo, lilianguka na kuua watu 36

Kamati iliyoteuliwa mwaka 2006 na Waziri Mkuu wa wakati huo Edward Lowassa, ilibaini kuwa majengo 147 kati ya 505 yaliyokaguliwa jijinu hayakuwa nyaraka na vibali sahihi vya ujenzi.

Kwa mujibu wa gazeti moja la nchini humo, ‘The Citizen’ aliyempokea kijiti Lowassa katika nafasi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliliambia Bunge mwaka 2008 kuwa kamati hiyo pia iligundua kuwa kanuni zilikiukwa kwenye ujenzi wa nyumba 81 huku wamiliki wa majengo 22 hawakufahamika.

Msanifu Magida anadai kuwa changamoto haswa iliyopo Kariakoo, kuna miradi mingi imesajiliwa kihalali lakini ujenzi unafanywa na madalali na wahandisi wasiokuwa na sifa.

"Baada ya matatizo haya kutokea ni wazi hatuhitaji watu kuadhibiwa tu bali tunahitaji suluhu za kudumu hata kama ikiwalazimu kubomoa majengo mengi kuliko wananchi kupata matatizo kila mwaka yanayotokana na ubora wa majengo.

Mtaalamu huyo anaeleza kuwa leo hii jengo moja Karikakoo limetengana lingine kwa mita moja au mbili, suala ambalo anasema ni hatari.

Tafiti Kariakoo ziko vipi?

fc
Maelezo ya picha, Waombolezaji katika viwanja vya Mnazimmoja, jijini Dar es Salaam

Magida ambaye anadai kufanya tafiti kwa miaka miwili katika eneo hilo anasema, “ usanifu wa eneo la kariakoo ulianza enzi zile za mkoloni Mjerumani, uboreshaji ukafanywa na Uingereza na haswa eneo lililngwa kuwa la makazi na hivyo maeneo mengi yalikuwa madogo.

Anasema, kuna mambo makuu matatu Kariakoo kwa tafiti na kulijua eneo hilo, kwanza majengo mengi hayana ubora, pia wanaofanya ujenzi hawana utaalamu, mikataba ya uendeshaji majengo unachangia kuwepo kwa majengo yasiyokuwa bora.

Mhandisi Innocent anasema, ukoaji wa haraka kwenye lile jengo na mengineyo ni mgumu kwasababu majengo huwa yamesongamana sambamba na kuwa na mizigo mingi.

Kwa upande wake, Mhandisi Magida anasema, “ Kwa mtaalamu yoyote anavyoona jinsi lile jengo lilivyoboka, kwa kujikusanya kwa kifusi ni wazi kuwa jengo halikuwa na ubora unaostaili kwani jengo lililokwenye ubora linapokubwa na hitilafu hubomoka kwa vipande, na pengine sehemu nyingine hubaki haijabomoka.”

Sakata hilo pia limemuibua Waziri wa zamani wa ardhi nchini Tanzania Profesa Anna Tibaijuka ambaye amesema kuwa sheria ya mipango miji inakiukwa katika ujenzi wa maghorofa ya Kariakoo.

Kwa mujibu wa Prof Tibaijuka, sheria za mipango miji zinataka viwanja vinne vya ‘high density’ (makaazi yenye msongamano) viunganishwe mbele na nyuma kipatikane kiwanja kimoja kikubwa cha kujenga ghorofa moja imara.

Anadai kuwa ushauri uliotolewa wakati wa Serikali awamu ya tatu na watalaamu wa mipango miji ulipuuzwa na viongozi kwa presha ya wawekezaji kwa hiyo maghorofa Kariakoo na kwingineko yanajengwa kiholela kwenye viwanja visivyokidhi vigezo.

“Naendelea kuhimiza kurekebisha kosa hilo. Sasa tunavuna hasara kubwa ya upotevu wa mali na maisha ya watu, fursa za ajira na aibu ya kushindwa kusimamia viwango vya ujenzi Miaka 63 baada ya uhuru,”alieleza Tibaijuka kwenye taarifa yake mtandaoni.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

Mwisho wa X ujumbe

Bodi ya Usajili wa Wahaandisi (ERB) imeahidi kuchunguza chanzo cha ajali hiyo na kusema kuwa kuna kasoro huenda zimejitokeza na kwamba maswala kadhaa huwa yanapaswa kutimizwa ili kuwa na jengo imara.

“Jengo linapaswa kuhimili mazingira ya asili ikiwemo upepo, tetemeko la ardhi na majanga mengine. Kwa hili jengo hata sisi tutachunguza kubaini nini kilisababisha kubomoka.” Meeleza msajili wa ERB Bernard Kavishe.

Kariakoo ni soko la aina gani ?

ERDF
Maelezo ya picha, Soko la Kariakoo wakati wa mgomo wa wafanyabiashara

Soko la Kariakoo linatajwa kuwa soko kubwa zaidi kati ukanda wa Afrika Mashariki. Mwaka 2016, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) lilifanya eneo hilo mkoa maalumu wa kodi kutokana na kuwa ni sehemu inayoongoza kwa kuchangia kwa ukubwa Kodi ya Ongezeko la thamani (VAT).

Katika takwimu za kila mwaka, eneo hilo huonekana kukusanya zaidi pato hilo la Serikali kutokana na bidhaa zinazouzwa kwa watumiaji na wafanyabiashara mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Sehemu hiyo ni maarufu kwa kuuza mavazi, vifaa mbalimbali vya magari, vifaa vya ujenzi, dawa za pembejeo na bidhaa zingine nyingi.

Pia Kariakoo ndipo ilipo maskani ya klabu kongwe nchini Tanzania ambazo ni Simba na Yanga.