Kwanini 'Mr Flag Man' wa Nigeria amesubiri mwaka mzima kuzikwa?

Chanzo cha picha, Akinwumi Akinkunmi
Familia ya mwanamume aliyebuni bendera ya taifa la Nigeria imeambia BBC kuwa wamekata tamaa kusubiri mazishi ya serikali iliyoahidiwa, mwaka mmoja baada ya kifo chake.
Badala yake Taiwo Michael Akinkunmi, aliyefariki mwaka mmoja uliopita akiwa na umri wa miaka 87, atazikwa wiki hii katika jimbo la Oyo, alikokuwa akiishi.
Akinkunmi, anayejulikana na wengi kama "Mr Bendera Man" na ambaye nyumba yake ilipakwa rangi ya kijani kibichi na nyeupe ya bendera ya taifa, alikuwa mtu mnyenyekevu.
Lakini mwanae anatumai kuwa wakati wa mazishi yake , ambayo jimbo la Oyo limekubali kufadhili, atakumbukwa kwa ubunifu wake ambao ulikuja kuwa ishara ya umoja wa Nigeria.
"Tunapaswa kumpa mazishi yanayostahili," mwanaye Akinwumi Akinkunmi alikiambia kipindi cha podcast cha BBC Focus on Africa.
Taiwo Akinkunmi alisema kila mara alikuwa mbunifu wa bendera asiyetarajiwa. Aliingia katika shindano la kubuni bendera mpya kabla ya Nigeria kupata uhuru wake kutoka kwa Uingereza mnamo Oktoba 1960.
Wakati huo alikuwa akisomea uhandisi wa umeme jijini London na alikuwa ameona tangazo la gazeti kuhusu shindano hilo.
Kulingana na mtaalam wa bendera Whitney Smith, mapendekezo ya mitindo 3,000 ya bendera yaliwasilishwa liwasilishwa - "mingi ikiwa ni yenye utata mkubwa".
Lakini ubunifu wa Akinkunmi ulikuwa ni rahisi, alipendekeza bendera yenye milia ya wima yenye rangi za kijani-nyeupe-kijani – na ubundifu wake ulifanikiwa kuchukua nafasi ya bendera ya kikoloni iliyokuwa na alama ya jeki ya muungano wa Uingereza na nyota ya kijani yenye ncha sita chini ya duara jekundu.

Chanzo cha picha, AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ubunifu wa muundo wa asili wa Akinkunmi ulijumuisha jua jekundu lililozungukwa na miale katikati ya pendera. Hii ilikusudiwa kama "ishara ya ulinzi na mwongozo wa Mungu", Bw Smith aliandika katika Encyclopaedia Britannica .
Hata hivyo jua liliondolewa na kamati hiyo, ambayo ilimzawadia kijana Akinkunmi aliyekuwa na umri wa miaka 23 wakati huo £100 (wakati huoi kiwa na thamani ya $280) kwa ushindi wa ubunifu wake wa bendera ya taifa.
Akinkunmi kila mara alisema msukumo wake ulitoka utotoni mwake alipokuwa amesafiri na kuishi sehemu mbalimbali za Nigeria.
Akiwa mzaliwa wa Ibadan kusini-magharibi, ambao sasa mji mkuu wa jimbo la Oyo, aliishi miaka miaka yake ya kwanza kaskazini mwa nchi kwa sababu ya kazi ya wazazi wake. Alikulia katika kile alichosema ni familia yenye furaha ya wake wengi na alikuwa mmoja wa watoto 10 wa baba yake.
Alirudi Ibadan kumalizia elimu yake. Aliwahi kumwambia mwandishi wa habari wa ThisDay Funke Olade kwamba shule yake ya sekondari ilikuwa kama "Nigeria-ndogo" kwani ilikuwa na wanafunzi kutoka kote nchini.
Nigeria ina makabila zaidi ya 300 na wakati nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika haina dini rasmi, taifa hilo limegawanyika takribani kati ya eneo la kaskazini lenye Waislamu wengi na Kusini lenye Wakristo wengi, ingawa jamii nyingi zimechanganyika.
Kwa Akinkunmi rangi ya kijani kwenye bendera yake iliashiria urithi wa kilimo wa taifa, huku nyeupe ikiwakilisha amani na umoja.
"Ni kawaida kwa Nigeria, kama nchi nyingine zenye tamaduni nyingi kuchagua muundo rahisi wa bendera.
Muundo tata zaidi unaweza kuwa uliheshimu waziwazi baadhi ya makabila na makabila fulani na kuyatenga mengine,” Bw Smith aliandika.
Akinkunmi alipenda sana kilimo na alifurahi kurudi Nigeria baada ya uhuru kufanya kazi katika Wizara ya Kilimo, ambapo alifanya kazi kama mfanyakazi wa serikali hadi alipostaafu mnamo 1994.
Lakini kwa muda mrefu wa maisha yake watu wachache sana walijua kuhusu mchango wake katika nchi, ingawa popote alipokuwa akiishi inasemekana alikuwa akipaka nyumba nye ya nyumba yake rangi za kijani na nyeupe.
Hakuwahi kutambulika hadi Nigeria iliposherehekea mwaka wake wa 50 wa uhuru ndipo alipotambuliwa kama mmoja wa Wanigeria 50 mashuhuri.

Chanzo cha picha, Akinwumi Akinkunmi
Mwanaye anasema mwanasiasa wa jimbo la Oyo baadaye alishawishi apewe heshima ya kitaifa na pensheni - na mwaka wa 2014 alipewa tuzo ya Afisa wa Mamlaka ya Shirikisho la Jamuhuri (OFR), mojawapo ya tuzo za juu zaidi za Nigeria.
Baada ya kifo cha Akinkunmi mwaka jana, seneta mmoja alifadhili hoja iliyofaulu kwamba afanyiwe mazishi ya kitaifa.
Hata hivyo, hakuna mipango iliyowahi kufanywa na walipokuwa wakingoja, familia ya Akinkunmi imekuwa ikilipa naira 2,000 ($1.30; £1.00) kwa siku kuweka mwili kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.
Mtoto wa mbunifu huyo wa bendera alisema kuwa mnamo mwezi Juni waligundua kuwa Taasisi ya Kitaifa ya masuala ya Kitamaduni ya wizara ya sanaa (Nico) iliagizwa kutatua suala la mazishi ya kitaifa ya baba yake. Lakini mbali na kupigiwa simu mara moja, alisema taasisi hiyo imeshindwa kuwasiliana zaidi na familia.
Anahisi kuchelewesha tena mazishi kungechafua jina la baba yake.
Hapo ndipo serikali ya jimbo la Oyo ilipoamua kuingilia kati kufadhili ibada ya mazishi ya mbunifu huyo wa bendera.
"Marehemu baba yangu alikuwa mtu mpole ambaye hakutaka chochote kumharibia sifa," mwanaye aliambia BBC.
"Alilelewa vizuri, alikuwa mtu mwenye akili sana, na mtu mzuri ambaye kila mtu alitaka kuwa na urafiki naye," aliongeza.














