Brian Chira: Mazishi ya nyota wa TikTok yawaacha Wakenya na mshangao

.

Chanzo cha picha, Coutesy

Maelezo ya picha, Pich ya Brian Chira katika mazishi yake
Iliyochapishwa

Mazishi yanaweza kuwa wakati wa kutafakari kwa kina kwa familia na marafiki lakini katika enzi hii ya mitandao ya kijamii, ambapo marehemu anaweza kuwa alishiriki habari za ndani kuhusu maisha yake kwa wafuasi wengi, mashabiki ambao wanahisi kuwa wanawajua wanaweza kuwa na mawazo tofauti.

Nchini Kenya, mazishi ya kawaida ya mwanamume yatima mwenye umri wa miaka 23 huenda yangehudhuriwa na wale waliokuwa karibu naye.

Lakini haikuwa hivyo kwa TikToker Brian Chira aliyefariki wiki mbili zilizopita katika ajali ya barabarani, karibu na mji mkuu, Nairobi.

Alikuwa amekusanya ufuasi wa zaidi ya 400,000 katika muda mfupi wa mwaka mmoja. Video zake za uwazi, za ustadi, zinazoshughulikia maswala ya kijamii na uhusiano, ziliwasilishwa moja kwa moja kwa kamera, zikiwafurahisha, na wakati mwingine ziliwashtua, watu wengi.

Mashabiki wake - wanaojulikana kama "Chira Clan" - pia walitaka kuomboleza baada ya maisha yake kukatizwa ghafla. Walisaidia kuchangia hazina ya mazishi, ambayo ilichangisha zaidi ya $60,000 (£48,000) kwa ajili ya mazishi hayo, na kuwaacha waandalizi wakishangaa.

Lakini familia ya Chira na majirani bado wanataabika baada ya maelfu kuhudhuria mazishi katika kijiji cha Gitei, katikati mwa Kenya.

Hafla ya Jumanne ilipangiwa kuhudhuriwa na watu 500 lakini idadi ya waliohudhuria iliongezeka hadi zaidi ya 5,000.

Wengi na Wakorofi

.

Chanzo cha picha, Courtesy

Maelezo ya picha, Vijana wengi wakiwemo 'TikTokers' walihudhuria mazishi yake

"Hawa walikuwa watumiaji wa TikTok, hauna aliyewaleta. Kwa hakika tulidhani walikuwa wakihudhuria maziko mengine katika kwa jirani," mmoja wa waandalizi wa hafla hiyo, rafiki wa Chira, Faustine Lukale aliambia BBC. Lukale pia anajulikana kama Baba Talisha kwenye mitandao ya kijamii, ambapo yeye mwenyewe ana wafuasi wengi katka mtandao wake wa TikTok.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Anasema walilazimika kuongeza kwa haraka mahema na viti zaidi kwa ajili ya umati wa waombolezaji waliokuwa wakiongezeka.

Ingawa vijana walikuwa wamesifiwa kwa kufanikisha mazishi hayo, baadhi yao walionekana kukosa nidhamu.

Wanakijiji walisema hawajawahi kuona umati mkubwa wa vijana na wakaidi namna hii, ambao baadhi yao walikuwa wamelewa.

Viongozi wa kidini hawakuweza hata kupata fursa ya kuongoza ibada ya mazishi kwani wengine walionekana kuwasukuma waombolezaji, au kurekodi video na kupiga picha za selfie karibu na kaburi la Chira, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.

Video na picha za mazishi zilijaa mitandao ya kijamii.

Chira bado alikuwa mada inayovuma nchini Kenya ikiwa na machapisho zaidi ya 7,000 kwenye X, siku chache baada ya kuzikwa.

TikToker huyo alijipatia umaarufu mnamo Desemba 2022 alipohojiwa na kituo kimoja cha runinga kama shahidi wa ajali ya barabarani. Katika mahojiano yaliyoenea, ufasaha wa Chira katika Kiingereza na haiba yake ya kuvutia ilivutia watazamaji.

Alitumia umaarufu huo wa ghafla ili kujenga uwepo wake mkubwa mtandaoni.

Akiwa yatima utotoni, Chira alilazimika kuacha chuo kikuu kwa sababu ya ukosefu wa karo. Bibi yake Esther Njeri alisema kuwa Chira aliachwa chini ya uangalizi wake akiwa na umri wa miaka minane baada ya kifo cha mamake.

Kukamatwa na kushtakiwa

Chira baadaye alifichua katika mahojiano ya redio kwamba alikuwa na VVU, jambo ambalo lilimfanya anywe pombe kupita kiasi na kumfanya aanguke kwenye msongo wa mawazo.

Matatizo yake ya maisha kwa kiasi fulani yalimfanya kustawi kama mtayarishaji wa maudhui huku akitumia jukwaa lake kushiriki uzoefu wake wa kibinafsi kwa uaminifu wa kuvutia.

Lakini kama TikToker mwenye shauku, Chira hakuwa mgeni kwenye mabishano na milipuko yake ya mtandaoni mara nyingi ilimtia matatani. Mnamo Agosti mwaka jana, alikamatwa na kushtakiwa kwa unyanyasaji wa mtandao dhidi ya TikToker mwenzake.

Pia alivaa nguo za kike katika baadhi ya video, jambo ambalo liliwakasirisha baadhi ya watu.

Usiku wa Machi 16, mwili wake ulipatikana barabarani baada ya kugongwa na lori ambalo lilitoroka kwa kasi katika kaunti ya Kiambu - takriban kilomita 16 (maili 10) kutoka Nairobi.

Polisi walisema bado wanamtafuta dereva.

Kufuatia kifo chake, jamii yake ya TikTok ilikusanyika pamoja na siku ya mazishi waliwasli kwa mabasi ya kukodishwa, wengine wakiwa na fulana za ukumbusho na kofia.

.

Chanzo cha picha, Courtesy

Maelezo ya picha, Zaidi ya watumiaji mitandao ya TikTok 5000 walihudhuria mazishi yake

Lakini umati uliinyima familia na wanakijiji fursa ya kumzika Chira kwa heshima, kulingana na waandalizi.

"Hatukupenda jinsi walivyovalia, kuvuta sigara na kunywa pombe mbele yetu. Hata hawakuwaheshimu makasisi," mwanakijiji mmoja aliambia tovuti ya habari ya Nation.

Mwanakijiji mwingine alisema alisikitishwa na matumizi ya maneno ya kuudhi wakati wa maziko.

Chira alizikwa karibu na babu yake, na wanakijiji walitazama jinsi waundaji wa maudhui wakikanyaga makaburi, kinyume na mila za jamii ya Wakikuyu.

Maafisa wachache wa polisi waliotumwa kudhibiti umati wa watu walionekana kuzidiwa na kutazama kwa mbali huku baadhi yao wakihangaika kupiga picha za selfie kwenye kaburi hilo.

"Ilinibidi nimuondoe bibi ya Chira hata kabla ya mazishi kuisha," Lukale alisema.

"Hata baada ya mazishi hakuna TikToker aliyekuja kwa familia kuomba pole kwa msiba huo, nyanyake Chira alikatishwa tamaa sana," aliongeza.

Baada ya mazishi hayo, baadhi walionekana wakimwagilia maua yaliyowekwa kwenye kaburi la Chira kwa pombe kali, hali iliyowashangaza zaidi viongozi wa dini na wanakijiji.

Takriban $6,000 zilitumika kwa gharama za mazishi na kiasi kingine ambacho hakijabainishwa kilienda kulipia uharibifu uliosababishwa na TikTokers wakati wa hafla hiyo.

Pesa zilizosalia zilipaswa kukabidhiwa kwa familia - baadhi yake ili kujenga au kununua nyumba kwa ajili ya nyanya yake Chira.

Lakini wakosoaji wanasema TikTokers walimwacha Chira wakati akipambana na shida zake za maisha lakini wakakongamana kusherehekea kifo chake.