Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi na wakati wa kuona Mwezi mkubwa na unaong’aa zaidi wa 2022 wiki hii
Utakuwa Mwezi mkubwa na unaong’aa zaidi wa 2022. Jumatano hii, satelaiti ya asili ya Dunia itaonekana katika uzuri wake wa ajabu.
Mwezi mkuu hutokea wakati awamu ya mwezi mzima inapatana na mwezi ukiwa karibu na sayari yetu.
Tukio hili litatokea saa 09:00 GMT siku ya Jumatano, wakati Mwezi utakuwa katika umbali wa kilomita 357,264 kutoka sayari yetu, kulingana na data ya NASA.
Zaidi ya saa tisa baadaye, awamu ya mwezi ukiwa kamili pia itatokea.
Na ingawa kwa nadharia matukio yote mawili hudumu kwa muda mfupi tu, wanaastronomia wanasema kwamba mwezi uliong’aa sana unaweza kuonekana kuliko kawaida kwa wiki nzima.
Mwezi kamili wa Julai pia utakuwa wa kwanza wa msimu na unaitwa na wenyeji huko Amerika Kaskazini Mwezi wa kulungu, yaani ‘Moon of the deer’, kwa sababu, kama wanavyoelezea katika Jarida la Amerika la ‘The Old Farmers Almanac, ni wakati wa mwaka ambao wanyama hao wa kiume kulungu wanamea pembe zao.
Jinsi ya kuuona mwezi huu vizuri
Wanaastronomia wanaeleza kuwa hakuna ‘’wakati mzuri’’ wa kuona mwezi mkuu, ingawa wanaonyesha kuwa kati ya Jumanne hii na, zaidi ya yote, Jumatano, zitakuwa nyakati ambazo mwezi utakuwa kamili zaidi.
Kwa uchunguzi bora zaidi, wanaastronomia wanapendekeza kutafuta maeneo yenye majengo au miti machache na kutotazama taa au vifaa vya kielektroniki (kama vile simu yako ya mkononi) kwa dakika 20 hadi 30 kabla ya kuutazama.
Na ikiwa unapenda upigaji picha wa usiku, wanapendekeza kujaribu kupiga Mwezi wakati unachomoza au unatua, wakati unaonekana kuwa mkubwa zaidi.
Athari halisi
Ingawa jambo hili la wanaastronomia huvuta hisia za mamilioni ya watu ulimwenguni kote, ufafanuzi wake ni wa hivi karibuni na unategemea unajimu.
Kwa hakika alikuwa mnajimu Richard Nolle aliyebuni neno hili mwaka wa 1979 kufafanua ‘’mwezi mzima unaotokea mwezi ukiwa karibu (ndani ya 90% ya) mkaribiano wake wa karibu zaidi na Dunia katika obiti.
Na ingawa kwa waumini wa mambo mengi ya nyota za kwenye anga yanaweza kutokea katika mpangilio huu wa wazi kati ya Jua, Mwezi na Dunia, ukweli ni kwamba sayansi haijapata msingi wowote wa imani hii.
Hata hivyo, NASA inaonya kuwa mawimbi ya juu wakati wa mwezi ukiwa mzima yanaweza kusababisha mafuriko kwenye baadhi ya ufuo.
‘’Mawimbi ya juu na ya chini yatakuwa makali zaidi kukiwa na mwezi mpevu,’’ linasema shirika hilo a Marekani.
Hii ni kutokana na tofauti ya mvuto wa Mwezi katika kipenyo cha Dunia.
Wakati Mwezi uko karibu zaidi, kipenyo cha Dunia ni sehemu kubwa kidogo ya mgawanyiko wa Dunia na Mwezi.
Hii ina maana kwamba mvuto wa Mwezi juu ya bahari (na tabaka la juu la Dunia) ni mkubwa zaidi katika hatua ya Dunia iliyo karibu na katikati ya Mwezi kuliko katika hatua ya Dunia ikiwa kinyume chake.