Mwanamke aliyesafiri kwa saa saba kwa ngamia ili kujifungua

Iliyochapishwa

Wakati Mona alipopata uchungu, ngamia alikuwa tegemeo lake.

Mona, 19, alitarajia safari ya kilomita 40 (maili 25) hadi hospitali ingechukua saa nne kutoka nyumbani kwake juu ya milima ya mawe. Lakini bila barabara - kuteseka kwa uchungu wa uzazi na katika hali mbaya ya hewa - ilichukua saa saba badala yake.

"Kwa kila hatua ambayo ngamia alipiga mbele, nilipatwa maumivu makali," alisema.

Ngamia aliposhindwa kwenda mbali zaidi, Mona alishuka na kusogea sehemu ya mwisho ya safari yake kwa miguu na mumewe.

Kaskazini-magharibi mwa mkoa wa Mahweet nchini Yemen, hospitali ya Bani Saad ndiyo kituo pekee cha afya kilichosalia kwa maelfu ya wanawake. Kutoka kwenye nyumba ya Mona, katika kijiji cha Al-Maaqara, kituo kinaweza kufikiwa tu kupitia milima kwa kutumia ngamia au kwa miguu.

Akiwa anang'ang'ania safari yake, Mona alihofia usalama wake na wa mtoto wake ambaye hajazaliwa.

"Barabara ilikuwa ya mawe," alisema, akikumbuka "safari ya kuchosha kimwili na kiakili".

"Kuna wakati niliomba Mungu anichukue na amlinde mtoto wangu ili niepuke maumivu."

Mona hana kumbukumbu ya kufika hospitali lakini anakumbuka kujawa na matumaini baada ya kusikia kilio cha mtoto wake mikononi mwa wakunga na wapasuaji.

Yeye, pamoja na mume wake, walimpa mtoto mvulana huyo jina la Jarrah kwa jina la daktari mpasuaji aliyewaokoa.

Barabara za kwenda hospitali kutoka vijiji vya karibu ni nyembamba. Baadhi yao wamesambaratika au kuzuiwa kutokana na vita vya miaka minane kati ya vikosi vinavyounga mkono serikali vinavyoungwa mkono na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia na waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran.

Wanawake, wanafamilia, au wenzi mara nyingi huwasaidia wanawake wajawazito kwa saa nyingi kupitia milima hadi hospitalini.

Salma Abdu, 33, ambaye alikuwa ameambatana na mama mjamzito, alisema kuwa nusu ya safari yake alimuona mama mjamzito ambaye alifariki usiku akiwa njiani.

Salma anawataka watu kuwahurumia wanawake na watoto.

"Tunahitaji barabara, hospitali, maduka ya dawa, tumekwama kwenye bonde hili, waliobahatika kujifungua salama, wengine wanakufa, pia wamevumilia masaibu ya safari," alisema.

Baadhi ya familia zinaweza kulipia hospitali lakini hazina fedha za kufika huko.

Mwanamke hufariki kila baada ya saa mbili wakati wa kujifungua kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika nchini Yemen, kwamujibu wa Hicham Nahro wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) nchini Yemen.

Bw. Nahro alisema mara nyingi ilikuwa kisa kwamba wanawake katika maeneo ya mbali ya Yemen hawakufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara au kutafuta usaidizi isipokuwa wanapoanza kuvuja damu au kuwa na maumivu makali.

Chini ya nusu ya watoto wanaozaliwa wanasaidiwa na daktari mwenye ujuzi na ni theluthi moja tu ya watoto wanaojifungua katika kituo cha afya, kulingana na UNFPA. Theluthi mbili ya wakazi wa Yemen wanaishi umbali unaofanya watumie zaidi ya saa moja kufika kwenye hospitali ya umma iliyo karibu inayofanya kazi kikamilifu.

Mfumo wa afya wa Yemen ulikuwa ukijitahidi hata kabla ya vita. Mzozo huo, hata hivyo, umesababisha uharibifu mkubwa kwa hospitali na barabara za Yemen, na kufanya familia kusafiri kwa taabu.

Hospitali hazina wafanyakazi wenye sifa, vifaa na madawa, uwekezaji wa barabara na miundombinu umekwama.

Ni moja tu kati ya vituo vitano vinavyofanya kazi vinaweza kutoa huduma za uhakika za afya ya uzazi na mtoto, kwa mujibu wa UNFPA.

'Nilidhani ndio mwisho'

Hadithi ya Mona ni mojawapo tu ya visa vingi vya ugumu wa maisha vinavyowakabili akina mama wajawazito nchini Yemen. Umiliki wa magari haufikiwi na watu wengi wa kawaida nchini Yemen, ambapo 80% ya watu wanategemea misaada.

Mume wa Hailah alitumia pesa kidogo alizohifadhi alipokuwa akifanya kazi Saudi Arabia ili kuhakikisha mke wake anaweza kusafiri hadi hospitali kwa pikipiki ya kuazima.

Maji yalipokatika, shemeji yake alimfunga kwenye baiskeli na kuanza safari, lakini njiani alianguka.

Walipofika katika kituo cha afya cha Hadaka huko Dhamar, Hailah alihamishwa haraka hadi kwenye wadi ya upasuaji.

"Nilidhani ulikuwa mwisho," alisema kijana huyo wa miaka 30. "Hakukuwa na njia kwa ajili yangu na mtoto wangu ambaye hajazaliwa kuishi."

Alionywa katika hatua za mwanzo za ujauzito kwamba kujifungulia nyumbani hakukuwa chaguo kutokana na hatari ya kutokwa na damu nyingi na matatizo mengine ya ujauzito.

Daktari katika kituo cha afya alisema Hailah na mtoto waliokolewa saa 11.

Alimwita mtoto wake wa kike Amal, linalomaanisha "tumaini" kwa Kiarabu.

"Nilikaribia kupoteza mtoto na maisha yakapoteza maana kutokana na vita vya laana, lakini mtoto huyu alinipa matumaini," alisema.

Huku ufadhili wa kimataifa ukipungua, vituo kama hospitali ya Bani Saad vinabanwa zaidi kifedha. Wafanyakazi katika kituo hicho wanahofia mustakabali wa akina mama na watoto wachanga huku wakilazimika kutanguliza wale wanaoweza kuokoa.