Shigella: Ni ugonjwa gani huu wa tumbo na kwa nini unawaambukiza wanajeshi wa Israel?

Chanzo cha picha, Getty Images
Madaktari nchini Israel wanasema baadhi ya wanajeshi wa nchi hiyo wanaoshiriki katika mashambulizi ya ardhini huko Gaza wanaugua ugonjwa mbaya wa tumbo uitwao "shigella".
Unafikiriwa kuenea kwa sababu ya hali duni ya usafi na chakula kisicho salama katika eneo la vita.
Shigella ni nini, na dalili zake ni zipi?
Shigella ni aina ya bakteria. Inapoingia ndani ya mwili, husababisha aina ya ugonjwa wa kuhara unaoitwa "shigellosis".
Dalili zake ni:
• homa
• kuhara damu au kwa muda mrefu
• tumbo kuuma sana
• upungufu wa maji mwilini
Watu ambao wana afya mbaya, au ambao kinga yao imedhoofika kutokana na magonjwa kama vile VVU, wanaweza kuteseka na dalili hizi kwa muda mrefu.
Ikiwa haitatibiwa, shigella inaweza kusababisha ugonjwa mbaya, au hata kifo.
Hatari ya kifo ni kubwa sana mara tu bakteria inapoingia kwenye damu. Watoto, walio na VVU, kisukari, saratani, au walio na utapiamlo wako hatarini sana.
Shigella inaeneaje?
Kulingana na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC), shigella huenea "kwa urahisi" kwa kugusa moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kinyesi cha mtu aliyeambukizwa.
Hii inaweza kutokea kama :
kula chakula kilichoandaliwa na mtu mwenye shigella
maji ya kunywa yaliyochafuliwa na maji taka
kugusa sehemu za choo au vitu vingine vilivyochafuliwa na shigela na mtu aliyeambukizwa
kubadilisha nepi za mtoto mwenye shigella
kugusa kinyesi wakati wa kujamiiana na mtu aliyeambukizwa
Shigella mara nyingi hupatikana miongoni mwa watu wasio na makazi, wasafiri wa kimataifa, wanaume wanaofanya ngono na wanaume, na wale ambao miili yao ina viwango vya chini vya kinga.
Je, shigella ipo wapi zaidi duniani ?
CDC inakadiria kuwa kuna kesi kati ya milioni 80 na 165 za shigella kila mwaka kote ulimwenguni, na kusababisha vifo 600,000.
Mnamo 2022, WHO ilisema kuwa 99% ya maambukizo ya shigella yalipatikana katika nchi zenye kipato cha chini au cha kati.
Vifo vingi vinavyotokana na shigella hutokea katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na Asia Kusini, na takriban 60% ni miongoni mwa watoto wa chini ya miaka mitano.
Utafiti mmoja wa wanasayansi katika Taasisi ya Kimataifa ya Chanjo nchini Korea Kusini unaonyesha kwamba ugonjwa wa shigellosis unatokea mara mia zaidi katika nchi za Asia kama vile Bangladesh, Uchina, Pakistani, Indonesia, Vietnam, na Thailand kuliko katika nchi zilizoendelea kiviwanda.
Je, shigella inawezaje kutibiwa au kuzuiwa?
CDC inasema kwamba shigella inaweza kuzuiwa kwa kunawa mikono mara kwa mara, kwa mfano:
• kabla ya kupika au kula
• baada ya kutoka chooni au kubadilisha nepi
• kabla ya shughuli za ngono
Kesi nyingi zinaweza kutibiwa kwa kunywa maji mengi na kupumzika.
Aina tano za antibiotiki zinafaa dhidi ya ugonjwa huo.
Hata hivyo, maafisa wa afya wa Marekani wamegundua aina ya bakteria ya shigella ambayo ni sugu kwa antibiotiki, iitwayo Shigella XDR au Shigella sonnei.
CDC inasema kuwa mnamo 2022, asilimia tano ya visa vya shigella nchini Marekani vilihusishwa na daalili za kuwa sugu dhidi ya dawa. Imeita hii "tishio kubwa la afya ya umma".
WHO pia imegundua kuongezeka kwa idadi ya kesi zinazohusishwa na aina ya XDR nchini Uingereza na kote Ulaya tangu 2020.
Shigella imeenea vipi miongoni mwa wanajeshi wa Israel?
Madaktari kadhaa katika Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) wameripoti ugonjwa mbaya wa matumbo kati ya wanajeshi wanaohudumu huko Gaza, kulingana na Dk Tal Brosh, mkurugenzi wa Kitengo cha Magonjwa ya Kuambukiza katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Assuta Ashdod.
Anasema aliutaja ugonjwa huo kuwa ni shigella.

Chanzo cha picha, Getty Images
Askari walioambukizwa hutengwa na kurudishwa kwa matibabu.
Dk Broch anasema "sababu moja wazi" ya mlipuko huo ni chakula kilichopikwa na raia wa Israeli ambacho kimetumwa kwa wanajeshi huko Gaza.
Anasema chakula hicho kinaweza kuwa kimechafuliwa na shigella, na bakteria nyingine hatari, kutokana na kutokupoa wakati wa kusafirishwa, au kutopashwa kikamilifu kabla ya kuliwa.
"Mara baada ya askari kupata ugonjwa wa kuhara, [hali] duni ya usafi ambayo ni ya kawaida katika uwanja wa vita husababisha maambukizi ya mtu hadi mwingine," anasema.
Dk Broch anasema wanajeshi wanapaswa kupelekewa vyakula vikavu pekee kama vile vyakula vya makopo, protini na karanga.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












