Je, ubunifu ni silaha mpya ya Tanzania katika nishati safi ya kupikia Afrika?

Jiko

Chanzo cha picha, Hannyg

Maelezo ya picha, Ubunifu wa majiko banifu unaibuka kama moja ya suluhisho zinazoiwezesha Tanzania kusukuma ajenda ya nishati safi ya kupikia huku ukifungua fursa mpya za ajira kwa vijana.
    • Author, Yusuph Mazimu
    • Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Kiwandani ni taka. Shambani ni mabaki ya mazao. Lakini kwa kundi linalokua la wabunifu wa Tanzania, vifuu vya nazi, mabaki ya miwa, masuke ya mpunga na taka nyingine za kilimo vinaanza kuonekana kama sehemu ya suluhisho la changamoto kubwa ya nishati ya kupikia inayolikabili bara la Afrika.

Kutoka karakana ndogo za ubunifu hadi viwanda vinavyochipuka, mawazo yanayobadilisha taka kuwa nishati yanaanza kupata nafasi katika safari ya Tanzania ya kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.

Mabadiliko hayo yanakuja wakati Tanzania ikitekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia 2024–2034 uliozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, huku nchi ikiendelea kujijengea nafasi katika mjadala wa Afrika kuhusu mustakabali wa nishati safi ya kupikia.

Mkakati huo uliozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2024 unalenga kufikia angalau asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Kwa mujibu wa wataalamu wa maendeleo, mapinduzi ya nishati safi hayawezi kuletwa na sera pekee wala uwekezaji pekee. Yanahitaji pia ubunifu unaozalisha suluhisho zinazolingana na mazingira halisi ya wananchi.

Lakini je, ubunifu wa Watanzania unaweza kuwa silaha mpya inayoiwezesha nchi hiyo kujenga nafasi yake katika mapinduzi ya nishati safi ya kupikia Afrika?

Janga la nishati ya kupikia

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kwa mujibu wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024–2034, takribani watu 33,000 hufariki kila mwaka nchini Tanzania kutokana na uchafuzi wa hewa ya ndani unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa.

Kwa Haji Kunte, mkazi wa Dar es Salaam, kupika kwa kutumia mkaa ilikuwa sehemu ya maisha ya kawaida kwa miaka mingi. Kama ilivyo kwa maelfu ya kaya nyingine, moshi wa jikoni ulionekana kuwa jambo la kawaida lisiloepukika.

Leo, baada ya kuhamia matumizi ya nishati safi ya kupikia, anasema tofauti imeonekana si tu kwenye matumizi ya fedha bali pia kwenye mazingira ya nyumbani.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Zamani tuliona moshi ni sehemu ya maisha. Lakini sasa unaona tofauti kwenye usafi wa nyumba, afya na hata muda unaookolewa," anasema.

Anachokisema Haji ni sehemu ya changamoto kubwa inayolikabili bara la Afrika, ikiwemo Tanzania.

Kwa mujibu wa Shirika la Nishati Duniani (IEA) pamoja na Benki ya Dunia, zaidi ya watu bilioni 2.1 duniani bado wanategemea nishati zisizo safi za kupikia, wengi wao wakiwa katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa hali hiyo ni janga la kimya kimya linaloendelea kuathiri maisha ya mamilioni ya watu kila siku. Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa zaidi ya watu 800,000 barani Afrika hufariki kila mwaka kutokana na uchafuzi wa hewa ya ndani unaosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa.

Kwa upande wa Tanzania, Kwa mujibu wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024–2034, takribani watu 33,000 hufariki kila mwaka.

Kwa sasa nchini humo takribani asilimia 28.6 ya wananchi sasa wanatumia nishati safi ya kupikia, hatua inayodhihirisha maendeleo ikilinganishwa na miaka michache iliyopita.

Athari za matumizi ya kuni na mkaa zinaonekana pia kwenye mazingira. Kwa mujibu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), takribani hekta 46,606 za misitu huharibiwa kila mwaka kutokana na mnyororo wa uzalishaji wa mkaa na matumizi ya kuni.

Mhadhiri na mtaalamu wa nishati safi, Gerutu Bosinge, anasema utafiti unaonyesha tofauti kubwa kati ya kuni, mkaa na gesi.

"Kwenye kuni, familia ya watu watano hutumia takribani tani 2.3 kwa mwaka. Kwa mkaa, matumizi hayo huzalisha hewa chafu nyingi zaidi. Lakini kwa gesi, athari za kiafya na kimazingira hupungua kwa kiwango kikubwa," anasema.

Kwa lugha nyepesi, Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay, anaitafsiri nishati safi ya kupikia kama uwezo wa kupika bila kutumia kuni wala mkaa.

Katika mazingira hayo, hitaji la suluhisho mbadala linaendelea kuwa kubwa kila mwaka.

Suluhisho nyingi, lengo moja

a

Chanzo cha picha, Hannyg

Maelezo ya picha, Kuni poa, moja ya ubunifu wa kuni zisizotoa moshi na zisizoathiri mazingira

Suluhisho la Tanzania halionekani kuja kwa teknolojia moja. Linaonekana kujengwa na mkusanyiko wa bunifu ndogo ndogo zinazojaribu kutatua tatizo moja kwa njia tofauti ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa huku zikizalisha ajira na fursa za kiuchumi.

Katika baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam, Morogoro, Pwani, Arusha, Mwanza na Dodoma, mabaki ya mazao ambayo zamani yalionekana kuwa taka sasa yanageuzwa kuwa nishati ya kupikia.

Vifuu vya nazi, mabaki ya miwa, masuke ya mpunga, mimea mikavu na hata unga wa muhogo vinatumika kutengeneza mkaa mbadala unaojulikana kama briquettes.

George Lawrence Swai, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa kampuni ya Hanny G Investment, anasema wengi hawakuamini wazo lake la kutengeneza teknolojia ya kuni poa hapo mwanzoni.

"Kuna waliodhani nimerukwa na akili baada ya kuwapa wazo hilo miaka ile, kwani msisitizo ulikuwa kwenye matumizi ya majiko ya gesi na majiko ya umeme," ananukuliwa na TRT.

Leo anaamini mkaa mbadala unaweza kusaidia mazingira huku ukipunguza gharama kwa watumiaji. "Hata ukijaribu kuilinganisha na kuni za misituni, bidhaa hii ina uwezo wa kupunguza gharama kwa asilimia 20."

Kwa Rachel Kimiti, ambaye ni mtumiaji wa mkaa mbadala na majiko banifu, mabadiliko hayo yameonekana moja kwa moja nyumbani kwake. "Mimi ni mtumiaji mzuri wa mkaa mbadala na majiko banifu. Sijutii kuhamia huku. Muda, gharama na afya yangu najiona salama."

a

Chanzo cha picha, Mwananchi/Johnson James

Maelezo ya picha, Baadhi ya mashine za kutengeneza mkaa mbadala, majiko bunifu zilizobuniwa na Leonald Kushoka wa Tabora.

Mbali na mabaki ya mazao, baadhi ya wabunifu wameanza kutumia taka za viwandani kutengeneza nishati safi. Helena Pius ni miongoni mwa wanaewake wanaobuni mkaa mbadala kutoka mabaki ya ngozi yanayotoka viwandani, taka ambazo zamani zilionekana kutokuwa na thamani yoyote.

Kwa Helena, changamoto kubwa si ukosefu wa mawazo bali namna vijana wanavyochukulia ubunifu. "Vijana wengi wana changamoto ya ubunifu. Wanasubiri kitu kiwe mezani ndiyo waanze kuchakarika."

Mwenyekiti wa Wazalishaji na Wasambazaji wa Nishati Safi Tanzania, Phinias Magesa, anaamini wabunifu wa teknolojia za nishati mbadala bado hawajatambuliwa vya kutosha licha ya mchango wao katika kupunguza ukataji miti.

"Watu wanaozalisha teknolojia kama hizi wanaonekana hawana chochote lakini wana mchango mkubwa sana. Tukijikita katika mkaa mbadala tutapunguza ukataji miti."

Kauli hii inaungwa mkono na Leonald Kushoka wa Tabora, mmoja wa wabunifu wa muda mrefu wa mashine za kutengeneza mkaa mbadala, majiko bunifu kutoka Tabora.

Taaasisi za utafiti za Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) na aasisi ya Utafiti wa masuala ya Kiuchumi na Umaskini (REPOA) wamekuwa wakiwajengea uwezo wazalishaji wa mkaa mbadala baada ya tafiti kubaini changamoto za viwango na ubora wa baadhi ya bidhaa sokoni.

Mashirika hayo pia yamefanikiwa kubuni mashine inayopunguza matumizi ya nishati ya kuchomea kwa karibu asilimia 50, hatua inayolenga kuongeza tija na ushindani wa teknolojia hizo.

Ubunifu pekee unatosha?

s

Chanzo cha picha, Hannyg

Pamoja na kuongezeka kwa bunifu mbalimbali, je, ubunifu pekee unatosha kubadili mfumo wa nishati ya kupikia nchini?

Anthony Raphael, mtaalamu wa biashara na maendeleo, anaamini ubunifu ni hatua muhimu lakini si mwisho wa safari. "Ubunifu ni muhimu, lakini bila mtaji, viwango na soko unaweza kubaki maabara," anasema.

Kwa mtazamo wake, changamoto kubwa kwa wabunifu wengi si kutengeneza bidhaa, bali kuifikisha kwa mamilioni ya wananchi wanaohitaji suluhisho hizo.

Imanuel Muro, Meneja wa Mradi wa Nishati Safi ya Kupikia anasema, mradi huo chini ya Wizara ya Nishati, unafanya mambo makubwa matatu kutatua changamoto zinazoelezwa na wengi akiwemo Raphael.

Anasema mradi huo wenye mabilioni ya fedha uko pale kuwasaidia wabunifu na wafanyabiashara katika ameneo matatu; "Moja kuwasaidia kupata mitaji, kuhakikisha wanakuwa na nguvu ya kuwafikia wananchi wengi zaidi, na kutumia ruzuku kupunguza makali ya bei kwa mtumiaji wa mwisho," anasema.

Hata hivyo, kadiri bunifu zinavyozidi kuingia sokoni, suala la ubora na usalama wa bidhaa hizo linaendelea kuwa muhimu.

Afisa Viwango wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mhandisi Spiradson Kagaba, anasema taasisi hiyo imeandaa viwango vya chini vya ufanisi wa nishati vinavyotumika kudhibiti ubora wa vifaa vinavyotumia nishati nchini.

Viwango hivyo vinahusisha bidhaa mbalimbali zinazotumika majumbani, ikiwemo majiko banifu, majiko ya umeme, majokofu, viyoyozi, mota za umeme, taa, runinga na feni.

"Lengo la viwango hivi ni kuhakikisha vifaa vinavyotumika na wananchi vinatumia nishati kwa ufanisi mkubwa, hivyo kupunguza matumizi ya umeme na gharama kwa mtumiaji," ameeleza.

Kwa wataalamu wa sekta hiyo, hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha kuwa ukuaji wa ubunifu unaenda sambamba na ubora wa bidhaa zinazowafikia wananchi, huku ukijenga imani ya watumiaji katika teknolojia mpya za nishati safi ya kupikia.

Pamoja na kusifu jitihada za tasisi za Serikali kwenye mbio za nishati safi, Raphael, anasema, nguvu ya Tanzania inaweza kuwa katika uwezo wa wabunifu wake kutengeneza suluhisho zinazolingana na mazingira ya ndani kuliko kutegemea teknolojia zinazoagizwa kutoka nje.

Tanzania na safari ya kujenga mfumo wa nishati safi Afrika

s

Chanzo cha picha, AfDB

Maelezo ya picha, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa pamoja na viongozi wa Afrika na washirika wa kimataifa katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kwenye ajenda ya nishati safi ya kupikia barani Afrika.

Tanzania si nchi pekee inayotafuta suluhisho la nishati safi ya kupikia. Kenya imewekeza katika LPG na biogas, Rwanda imeendelea kusukuma matumizi ya majiko safi, huku Ghana ikihamasisha matumizi ya gesi ya kupikia kama sehemu ya mkakati wake wa nishati safi.

Lakini kinachoanza kuitofautisha Tanzania ni mchanganyiko wa sera za kitaifa, ushiriki wa sekta binafsi na ubunifu unaozalishwa ndani ya nchi.

Baada ya mwaka 2024, Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia, msingi wa kuratibu sera, mifumo ya kifedha na uwekezaji katika sekta hiyo ukaanza, sasa upatikanaji wa nishati safi umeongezeka.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nishati, Dkt. Deogratius Ndejembi, upatikanaji wa nishati safi ya kupikia Tanzania umeongezeka mara tatu ndani ya miaka minne iliyopita, akitaja juhusu za kisektra lakini pia hamasa ahadi ya dola bilioni 2.2 za Marekani kwa ajili ya kuendeleza sekta hiyo barani Afrika.

Mbali na afya na mazingira, serikali sasa inaiona nishati safi ya kupikia kama sekta inayoweza kuzalisha ajira na fursa mpya za kiuchumi. "Nishati safi ya kupikia inapaswa kuangaliwa pia kama sekta ya kiuchumi inayoweza kuzalisha ajira katika uzalishaji, usambazaji na matengenezo ya vifaa," anasema Ndejembi.

Katika juhudi za kuharakisha mabadiliko hayo, serikali imepiga marufuku matumizi ya kuni na mkaa katika taasisi zinazohudumia zaidi ya watu 100, zikiwemo shule na vituo vya afya.

Sasa wakati Afrika ikitafuta njia za kuwawezesha mamilioni ya watu kuachana na kuni na mkaa, baadhi ya majibu yanaonekana kuanzia katika karakana ndogo, mitaani, viwanda vidogo, nyumbani na mawazo ya wabunifu wa Tanzania.

Ikiwa ubunifu mbalimbali kwenye sekta ya nishati unaweza kufikia mamilioni ya wananchi wanaoupika kila siku, huenda ukawa silaha mpya ya Tanzania katika safari ya nishati safi ya kupikia Afrika.