Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Maadui wa Samia na kihunzi alichokwepa kuelekea 2025
Na Ezekiel Kamwaga
Mchambuzi wa Masuala ya kisiasa Tanzania
MMOJA wa waliokuwa wasaidizi wa Rais Donald Trump kwenye masuala ya habari, Anthony Scaramucci, ameeleza kwa kifupi sana kuhusu nini tatizo la Rais wa sasa wa Marekani, Joe Biden, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Marekani mwaka Novemba mwaka huu. Kwa maelezo, ni kuwa Biden hajafanya kazi nzuri kueleza mafanikio aliyopata kama ambavyo Trump anaeleza mapungufu ya utawala wake.
Maelezo haya ya Scaramucci ambaye sasa anamuunga mkono Biden ingawa alikuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu ya Trump – kwa chini ya wiki mbili, yanasadifu kinachoendelea Tanzania hivi sasa kwenye kuangalia miaka mitatu ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa takribani vigezo vyote vinavyotumika kupima viongozi, Rais Samia amepiga hatua kubwa kuliko wengi walivyotarajia. Chukulia mfano wa eneo muhimu zaidi katika uongozi wa uchumi. Ingawa ameingia madarakani wakati taifa likitoka katika tatizo la ugonjwa wa Covid 19, Pato la Taifa la Tanzania (GDP) limeongezeka kutoka dola bilioni 69 hadi dola bilioni 85 kwenye miaka yake mitatu ya uongozi.
Sekta ya utalii ambayo ilikuwa katika hali mbaya kutokana na Covid 19, sasa imeweka rekodi ya kuingiza zaidi ya dola bilioni tatu – kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa na Tanzania katika historia yake. Mradi mkubwa wa Bwawa la Umeme la Nyerere ambao yeye alikuta ukiwa umefikia takribani theluthi moja tu, sasa umeanza kuzalisha umeme.
Kwenye eneo la Maridhiano ya Kisiasa ambalo ni miongoni mwa ngome za kile anachokiita R nne za utawala wake, mambo yamebadilika kwa kiasi kikubwa kwenye utawala wake. Mikutano ya hadhara ya kisiasa imeruhusiwa na vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa kabla yake, vimefunguliwa. Kuna uhuru zaidi wa kutoa maoni sasa kuliko wakati anaingia madarakani miaka mitatu iliyopita.
Kwa kiongozi mwingine yeyote, vigezo vilivyotajwa hapo juu pekee, vingeweza kutosha kusema amekuwa na miaka mitatu yenye mafanikio. Lakini, kwa sababu tofauti, ikiwemo ya kwanza kwamba bado mafanikio yake hayajapata fursa ya kuelezwa na kueleweka vizuri kama ilivyo kwa Biden wa Marekani, kuna vitu vingine vinavyochochoea hali hii.
‘Maadui’ wa Rais Samia
Rais Samia ana changamoto kadhaa kwenye utawala wake. Changamoto ya kwanza na kubwa zaidi inayomkabili inahusu mazingira yaliyomwingiza madarakani. Kwa sababu ndiye Rais pekee aliyeingia madarakani nchini Tanzania bila kupigiwa kura, imemlazimu kucheza kete zake za kisiasa tofauti na marais waliomtangulia.
Jambo hili limemfanya ahakikishe anaatumia makundi yote makubwa ya kisiasa yaliyo ndani ya chama hicho. Mpaka sasa, hakuna kundi ndani ya chama hicho linaloweza kujidai kwamba limebebwa au kupendelewa kuliko mengine. Hii ni mbinu itakayofanya iwe rahisi kwake kuungwa mkono na makundi yote kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Tabia hii ya kutumia makundi yote, imempa Rais Samia shida kubwa moja – kwamba wale wasio nyuma ya miongoni mwa makundi hayo au waliokuwa wahanga wa utawala uliomtangulia, wanashindwa kuelewa baadhi ya uteuzi au tabia za utawala wake.
Hakuna mfano mzuri wa hili kuliko hatua yake ya kumteua Paul Makonda kuwa Katibu Mwenezi wa CCM. Mwanasiasa huyo ni mmoja wa wale wanaohusishwa kwa karibu na utawala wa Rais John Magufuli ambaye hakuamini katika demokrasia wala utawala bora. Na kwa sababu ya tabia ya Makonda ya kuingia mzimamzima katika majukumu anayopewa, wale wasiompenda yeye na watu wa aina yake, wameshindwa pia kumuelewa Rais.
Lakini katikati ya uteuzi huu wa Makonda, kuna picha nyingine kubwa ambayo wakosoaji wa Rais Samia wanashindwa kuiona. Nafasi ya Katibu Mwenezi wa CCM si nafasi ya maamuzi au yenye mamlaka makubwa ndani ya chama. Kuondoa Mwenyekiti, nafasi kubwa zinazofuata ndani ya CCM ni ile ya Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu wa CCM ambazo kwa sasa zinashikwa na watu wasio na uhusiano wowote na kundi la kisiasa analowakilisha Makonda.
Uteuzi wa Makonda unamsaidia zaidi Samia kujenga ngome nyingine ndani ya CCM kuelekea uchaguzi wa 2025 pasipo kulipa kundi nguvu kubwa ya kimaamuzi kama ambayo – kwa mfano, Balozi Emmanuel Nchimbi amepewa kwa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho kikongwe zaidi nchini.
Adui mwingine wa Rais Samia ni suala la mfumuko wa bei uliosababisha kuongezeka kwa gharama ya maisha. Mfumuko huo ulikuja kuendana na mgawo wa umeme uliosababisha biashara nyingi – zikiwemo za watu wa hali ya chini kuathirika. Hali ingekuwa mbaya zaidi kama serikali isingeamua kufanya jitihada ya kuweka ruzuku kwenye bei ya mafuta iliyosababisha walau bei ya mafuta isiwe kubwa zaidi.
Suala hili la kupanda kwa gharama ya maisha ndilo jambo linalosumbua serikali nyingi kwa sasa duniani, kuanzia kwa William Ruto wa Kenya hadi Rishi Sunak wa Uingereza. Ni suala ambalo ndilo msingi wa kukua na kuongezeka kwa ushawishi wa wanasiasa na siasa za kihafidhina duniani.
Na hili ndilo linalomleta adui wa tatu wa Rais Samia. Adui huyu si mwingine bali ni ukweli kwamba aliingia madarakani kuchukua nafasi ya mwanasiasa aliyeamini katika udikteta na mwenye kuhakikisha hakuna uhuru wa mawazo mbadala kuondoa yak wake. Kwa sababu Rais Samia ameachia uhuru kidogo, kasoro na mapungufu ya serikali yake yanawekwa hadharani na kujadiliwa zaidi kuliko ilivyokuwa kwa mtangulizi wake.
Kama ripoti ya CAG imezungumzia ufisadi ndani ya serikali yake, Bunge na vyombo vya habari vinajadili kwa kina zaidi kuliko ilivyokuwa kwa mtangulizi wake. Pia wale waliozibwa midomo kwa takribani miaka sita, sasa wamepata uhuru na jukwa la kupumulia.
Kuelekea 2025
Ni wazi kwamba mkakati wa Rais Samia kuelekea 2025 ni kuhakikisha kuwa na CCM iliyoungana na isiyo na makundi. Kwa namna siasa za Tanzania zilivyo, hakuna uwezekano wa CCM iliyoungana kushindwa kwenye uchaguzi.
Kitu ambacho amefanikiwa hadi sasa ni kuwa hakuna mwanachama wa CCM anayeamini kuwa Urais na Uenyekiti wa CCM wa Samia umemnyima fursa ya namna yoyote. Kimsingi, hata wale wana CCM ambao kwa sasa wako benchi, ni kama wanapiga jaramba wakiamini wakati wowote wanaweza kuitwa kwenye timu na kurejea kwenye majukumu.
Ninaamini pia kwamba Rais Samia ameamua kwamba urais wake utafanya mambo mawili; kuendeleza kilichoachwa na mtangulizi wake na pia kufanya mabadiliko pale anapoweza. Kama mradi wa Bwawa la Nyerere utakamilika kwa walau asilimia 100 huku mradi mwingine wa kimkakati wa SGR ukiwa unafanya kazi kufikia 2025, atakuwa amefanya la kwanza kwa uhakika.
Ni baada ya uchaguzi wa mwaka 2025, wakati atakapokuwa na urais alioupata kwa kupigiwa kura na wananchi na kuwa na turufu ya kuamua, ndipo ninapoamini Samia atafanya mabadiliko makubwa zaidi na kuonyesha rangi yake halisi. Katika miaka yake hii ya kwanza, hatari kubwa zaidi ilikuwa ni kukigawa au kukipasua chama kwa kufanya kwa ghafla na kwa nguvu mabadiliko makubwa ambayo wahafidhina ndani ya chama wangemkatalia.
Inaonekana kirunzi hicho amekiruka. Maoni yangu ni kuwa Samia wa mabadiliko makubwa ataonekana baada ya uchaguzi wa mwaka 2025. Kwa sasa, la muhimu kwake kuliko yote ni kukiweka chama pamoja na kushinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.