Jinsi watoto wawili walivyompata mama yao, miaka 13 baada ya kupotea

Chanzo cha picha, NARESH PARAS
Siku moja wakati wa majira ya joto mnamo Juni 2010, watoto wawili wa Kihindi waliondoka nyumbani kwao, wakiwa na hasira kwa wazazi wao kwa kuwapiga.
Ndugu Rakhi, 11, na Bablu, 7, walikuwa wamepanga kwenda kwa bau wao, ambao waliishi kilomita moja tu kutoka hapo. Lakini baada ya makosa kidogo njiani, walipotea.
Iliwachukua zaidi ya miaka kumi na mitatu kumpata mama yao Neetu Kumari kwa msaada wa mwanaharakati wa haki za watoto.
“Nilimkumbuka mama yangu kila siku,” Bablu, ambaye alilelewa katika vituo vya watoto yatima, alisema. "Nimefurahi sana kupata familia yangu."
Video ya kuungana kwao mwishoni mwa Disemba inamuonyesha Neetu akilia huku akimkaribisha Bablu, huku akimkumbatia kwa nguvu na kumshukuru Mungu kwa "kumpa furaha ya kumshika mwanawe tena."
Kisha Bablu anamkumbatia Rakhi, ambaye alikuwa amerejea siku mbili zilizopita. Ingawa ndugu hao wawili walikuwa wamewasiliana kwa miaka kadhaa, walikutana tena baada ya zaidi ya miaka kumi.
Kutenganishwa
Bablu na Rakhi waliishi katika jiji la kaskazini la Agra na wazazi wao Neetu Kumari na Santosh, ambao walifanya kazi kama vibarua wa kila siku.
Mnamo Juni 16, 2010, Neetu, ambaye hakuweza kupata kazi siku hiyo, alitoa hasira yake kwa Rakhi na kumpiga na koleo za chuma alizokuwa akitumia kupika.
Rakhi na Bablu waliondoka nyumbani baada ya mama kwenda nje kwa shughuli fulani.
"Baba yangu pia alikuwa akinipiga wakati mwingine, kama sikusoma vizuri, hivyo Rakhi alipokuja na kusema 'twende kuishi na Dadi', nilikubali," anasema Bablu.
Baada ya kupotea, dereva wa teksi wa baiskeli aliwapeleka kituoni.

Chanzo cha picha, NARESH PARAS
Huko, watoto walipanda treni ambapo waligunduliwa na mwanamke anayefanya kazi katika shirika la watoto.
Treni ilipofika Meerut, mji ulio karibu kilomita 250 kutoka nyumbani kwao, aliwakabidhi kwa polisi, ambao waliwapeleka kwenye kituo cha watoto yatima cha serikali.
“Tuliwaambia tunataka kurudi nyumbani, tulijaribu kuzungumza nao kuhusu wazazi wetu, lakini polisi au maofisa wa kituo cha watoto yatima hawakujaribu kuitafuta familia yetu,” anasema Bablu.
Mwaka mmoja baadaye, ndugu pia walitenganishwa: Rakhi alihamishwa hadi kituo cha wasichana kinachosimamiwa na shirika lisilo la serikali karibu na mji mkuu wa India, Delhi.
Miaka michache baadaye, Bablu alihamishiwa katika kituo kingine cha watoto yatima cha serikali huko Lucknow, mji mkuu wa jimbo la Uttar Pradesh.
Ndugu wanakutana tena
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kila mara maafisa muhimu, wafanyakazi wa misaada au waandishi wa habari walipotembelea kituo cha watoto yatima, Bablu alikuwa akiwaeleza kuhusu Rakhi kwa matumaini ya kukutana naye.
Lakini haikuwa hadi 2017 ndipo ilifanyika. Mmoja wa walezi katika makao hayo mapya aliamua kumsaidia alipomwambia kwamba dada yake alikuwa amepelekwa kwenye kituo cha watoto yatima cha wasichana mahali fulani karibu na Delhi.
"Aliita vituo vyote vya watoto yatima huko Noida na Greater Noida (vitongoji vya Delhi), akawauliza ikiwa walikuwa na mtu anayeitwa Rakhi na baada ya juhudi nyingi, akampata," anasema Bablu.
"Nataka niiambie serikali kuwa ni ukatili kweli kuwatenganisha kaka na dada, kaka na dada wapangiwe vituo vya pamoja, sio sawa kuwatenganisha," anaongeza.
Wawili hao walipokutana, mara nyingi walizungumza kwenye simu. Lakini mazungumzo yalipogeuka kuwa kutafuta familia yake, Rakhi alisisitizaa.
"Miaka kumi na tatu sio kitu bure na nilikuwa na matumaini kidogo ya kumpata mama yangu," aliniambia.
Bablu hakuwa na shaka kama hiyo. "Nilifurahi sana kumpata Rakhi na nilikuwa na uhakika kwamba ningeweza pia kumpata mama yetu," alisema.
Bablu anasema katika moja ya sehemu alizokaa, mara nyingi alikuwa akipigwa na walezi wake na watoto wakubwa. Alisema alijaribu kukimbia mara mbili, lakini aliogopa na kurudi.
Rakhi, kwa upande wake, anabainisha kuwa shirika lisilo la kiserikali alikokulia lilimtunza vizuri sana. Ninamuuliza ikiwa anafikiria maisha yake yangekuwa tofauti ikiwa angebaki nyumbani.
"Nadhani chochote kinachotokea huwa ni bora kila wakati na labda nilikuwa na maisha bora zaidi mbali na nyumbani," anasema.
"Sikuwa wa kwao, lakini walinitunza vizuri sana, hakuna mtu aliyewahi kunipiga na nilitendewa vizuri. Nilisoma shule nzuri, nilipata huduma nzuri za afya na huduma zingine zote ambazo kupata karibu na jiji kubwa,” anaongeza.
Mwanaharakati aliyeileta familia pamoja
Mnamo Desemba 20, Naresh Paras, mwanaharakati wa haki za watoto wa Agra, alipokea simu kutoka kwa Bablu, ambaye sasa anaishi na kufanya kazi huko Bengaluru.
"Umeunganisha familia nyingi, unaweza kunisaidia kupata yangu?" Bablu alimuuliza.
Paras, ambaye amefanya kazi na watoto tangu 2007, anasema hii haikuwa kesi rahisi.
Ndugu hao hawakuweza kukumbuka jina la baba yao na kadi zao za Aadhaar, zilizotolewa na serikali, zilikuwa na majina tofauti.
Hawakujua walitoka jimbo gani au wilaya gani na usajili wao katika kituo cha watoto yatima ulionyesha kwamba walikuwa wanatoka Bilaspur, mji ulio katikati mwa jimbo la Chhattisgarh.
Simu za Paras kwa vituo vya watoto yatima na polisi wa Bilaspur hazikuzaa matunda.

Chanzo cha picha, NARESH PARAS
Kisha kitu kiliibuka pale Bablu alipokumbuka kuona treni feki nje ya kituo walichokuwa wamepanda treni.
"Nilijua lazima kiwe kituo cha Agra Cantonment," anasema Paras.
Akikagua rekodi za polisi wa jiji, alifika kwenye kituo cha polisi cha Jagdishpura, ambapo baba ya ndugu hao alikuwa amewasilisha malalamiko mnamo Juni 2010.
Lakini alipoenda kuitafuta familia hiyo, aligundua walikuwa wanakodisha na walikuwa wamehama.
Baadaye, Rakhi alimwambia kuwa anakumbuka jina la mama yake ni Neetu na alikuwa na kovu lililosababishwa na kuungua shingoni.
Paras alikwenda kwenye kitovu cha wafanyikazi, mahali pa Agra ambapo vibarua wa kila siku hukusanyika kila asubuhi kwa matumaini ya kupata kazi.
Hakumpata Neetu, lakini baadhi ya wafanyakazi walimwambia wanamfahamu na wangepitisha ujumbe huo.
Mara tu Neetu Kumari alipojua kwamba watoto wake wamepatikana, alienda kwa polisi, ambao waliwasiliana na Paras.
Kuunganishwa tena baada ya miaka kumi na tatu
Paras alipomtembelea Neetu, alimuonyesha picha za watoto hao na nakala ya ripoti ya polisi. Alipomuunganisha kupitia simu ya video na Bablu na Rakhi, wote walitambuana.
Neetu Kumari aliiambia Paras kwamba "alijuta kumpiga Rakhi" na akazungumza kuhusu juhudi alizofanya kuungana na watoto wake.

Chanzo cha picha, NARESH PARAS
“Nilikopa pesa na kwenda Patna (mji mkuu wa jimbo la Bihar) baada ya kujua kwamba watoto wangu walionekana wakiomba katika mitaa ya jiji. Nilitembelea mahekalu, misikiti na makanisa kuwaombea warejee salama,” alisema.
Alisema muungano huo na watoto wake ulimpa maisha mapya.
Rakhi alisema alihisi kama yuko kwenye sinema kwani hakutarajia kumuona mama yake tena. "Nilijisikia furaha sana," aliongeza.
Bablu, wakati huo huo, alielezea hisia zake kama "mchanganyiko".
"Inashangaza kwamba ilichukua wiki moja tu kwa Paras kupata familia yangu. Nilikuwa na hasira kwa polisi na wafanyakazi wa NGO ambao hawakuwa wamenisaidia licha ya maombi yangu ya mara kwa mara, lakini "nilifurahi sana kuzungumza na mama yangu. Alikuwa akilia na kuniuliza kwa nini ameniacha. Nilimwambia kwamba sijawahi kumuacha na kwamba nilikuwa nimepotea."
Imetafsiriwa na Jason Nyakundi












