Sudan: Raia hawajasalimika wakati mapigano ya Khartoum yakikumba makazi

Chanzo cha picha, REUTERS/ABDULLAH ABDEL MONEIM
Wakazi katika mji mkuu wa Sudan Khartoum wako kwenye dhoruba kali huku mapigano ya bunduki na milipuko ya mabomu yakitikisa mitaa ya mji huo.
Ndege za kivita na helikopta za mashambulizi zinapaa angani.
Wamenaswa katika vita. "Ilisikika kama mvua ya radi," alisema mwanamke mmoja alipokuwa akiweka video kutoka kwenye roshani yake karibu na uwanja wa ndege wa Khartoum wikendi.
Kelele hizo zilitoka kwenye helikopta za kijeshi zilizokuwa zikipaa chini chini juu ya vitalu vya minara ya makazi.
"Tuliamka na kwenda nje - kulikuwa na ndege za kivita. Ilisikika tu kama milio ya risasi. Kuna fujo nyingi tu zinazoendelea. Kulikuwa na moshi kila mahali."
Tumepitia picha kadhaa na vipande vya video kutoka mji mkuu ili kupata hisia ya jinsi hii inavyoathiri maeneo ya makazi ya jiji.
Jeshi la Sudan, na kundi la wanamgambo la Rapid Support Forces (RSF), wanapigania madaraka huku nchi hiyo ikielekea kwenye utawala wa kiraia.
Tishio kwa wakazi linakuzwa na jiografia fulani ya Khartoum - maeneo yake muhimu ya kimkakati, ambayo inalengwa na maeneo ya makazi.
Kitongoji kimoja ambacho kimekabiliwa na moto mkubwa ni Kafouri, si mbali na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum.

Baadhi ya wakazi tajiri zaidi wa Khartoum wanaishi huko, ikiwa ni pamoja na familia ya rais wa zamani wa Sudan Omar al-Bashir. Pia ni eneo lenye vikosi kadhaa vya usalama.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Uwanja wa ndege wa Khartoum pia upo kati ya maeneo yenye makazi mengi.
"Ninaweza kuona kutoka kwa makazi yangu moshi ukitoka kwenye majengo fulani," mwanaume mmoja anayeishi karibu alituambia.
"Naweza kusikia milipuko, mabomu, naweza kuona ndege za kijeshi."
Alisema nyumba iliyo karibu na anakoishi ilishambuliwa Jumatatu asubuhi.
"Sasa ni kifusi tu."
Takribani raia 100 wamefariki dunia wakati wa duru hii ya ghasia, unasema muungano wa madaktari katika nchi hiyo kubwa ya kaskazini-mashariki mwa Afrika.
Zaidi ya raia 1,000 wanaaminika kujeruhiwa.
Idadi ya vifo vya wanajeshi inadhaniwa kuwa kubwa zaidi.
Picha za satelaiti za tarehe 16 Aprili huko Khartoum zinaonesha ukubwa wa ghasia hizo - huku moshi ukipanda kutoka uwanja wa ndege.
Picha hizo zinaonesha moshi ukifuka kutoka kwa ndege zinazowaka moto kwenye barabara ya uwanja wa ndege.
Picha nyingine ya satelaiti iliyopigwa kwenye uwanja wa ndege tarehe 17 Aprili inaonesha ndege zaidi zilizoharibiwa.

Miundombinu muhimu imeathiriwa, ikiwa ni pamoja na Daraja la Kobar, ambalo liko karibu na uwanja wa ndege na linaunganisha kusini na kaskazini mwa Khartoum.
Shahidi mmoja alituambia kuwa hii imezuia ufikiaji wa Hospitali ya Universal Sudan upande wa kaskazini wa daraja.

Mwanaume huyo aliyetembelea Hospitali ya Universal mwishoni mwa wiki, alituambia: "Waliwataka wagonjwa na majeruhi kuondoka hospitalini saa 10 jioni Jumapili, na hali ilikuwa ngumu nje.
"Walijaribu sana kuleta madaktari wengine kutoka hospitali nyingine lakini hakuna mtu anayeweza kufika Hospitali ya Universal.
Magari ya wagonjwa yanakataa kusafirisha majeruhi na maiti."
Kumekuwa na ripoti kwamba hospitali nyingine kadhaa katika mji mkuu aidha zimeharibiwa au kuhamishwa.
Ripoti ya Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan ilisema Hospitali ya Chuo Kikuu cha Bashayer, kusini mwa Khartoum imeshambuliwa.
Kituo cha reli kusini mwa jiji pia kinaonekana kulengwa, na picha za satelaiti kutoka 16 Aprili zikionyesha moshi mwingi kuzunguka eneo.

Ripoti ya ziada ya Daniele Palumbo, Joshua Cheetham, Tom Edgington, Richard Irvine-Brown na Mohanad Hashim
Michoro na Erwan Rivault na Kate Gaynor
Tunaendelea kuchunguza video nje ya Khartoum.

















