Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi mabadiliko ya tabianchi yanavyobadilisha ladha ya bia
Ikiwa na harufu nzuri, bia baridi ni kinywaji kinachogusa hisia zetu zote. Lakini jinsi hali ya hewa inavyobadilika, ndivyo pia ladha ya mojawapo ya vinywaji maarufu zaidi duniani inavyopungua.
Kwa ladha yake ya kuridhisha na ya kuvutia, vinywaji vichache huibua hisia kama bia baridi iliyomiminwa kwenye glasi. "Sio chungu tu, sio tamu tu, inakuvutia upige tama, na huo ni ubora ambao ni vigumu sana kuelezea," anasema Mirek Trnka, mtafiti katika Chuo cha Sayansi cha Taasisi ya Global Change ya Jamhuri ya Czech.
Ladha ya bia hutokana na kemikali kutoka kwa viungo vitatu; hops, amira na shayiri iliyoyeyuka. Lakini sasa mabadiliko ya tabia nchi yanatishia mazao ya shayiri na hops. Trnka na wenzake wanasema kwamba mazao ya kitamaduni ambayo watengenezaji wa bia wanategemea kutengeneza kinywaji hicho – kwa jina noble hops - itakuwa "ngumu zaidi kuzalisha".
Utafiti wa Trnka unaonyesha kuwa uzalishaji wa hops bora umepungua kwa 20% tangu miaka ya 1970 katika baadhi ya maeneo makubwa zaidi ya Ulaya yanayokuza zao hilo. Asidi za alfa ni kiwanja muhimu katika uzalishaji wa hops bora ambazo huipa bia ladha yake chungu tofauti na utafiti wa Trnka unaohitimisha kuwa viwango vya asidi ya alpha vitapungua kwa 31% ifikapo mwaka wa 2050. Je, bia inakabiliwa na changamoto? Je, lolote linaweza kufanywa ili kupata ladha yake halisi katika siku zijazo?
Bia, mojawapo ya vinywaji vinavyopendwa zaidi ulimwenguni, na kinywaji maarufu zaidi cha kileo kwa kiasi kikubwa, imekuwa sehemu ya jamii tangu wanadamu wagundue kilimo.
Ushahidi wa vinywaji vya kileo vilivyochachushwa na nafaka umepatikana katika maeneo mbali mbali kama Jiahu, tovuti ya Neolithic nchini Uchina iliyoanzia angalau kabla ujio wa Yesu Kristo yapata miaka 5700 BC. Kwa kweli, kuna ushahidi wa bia kutengenezwa katika kila bara katika ulimwengu wa kale.
Iwe ni mahindi, mchele au nafaka, wakulima wa zamani walijifunza kwamba kuchachusha nafaka kunaweza kutoa kinywaji chenye kulewesha. Kilikuwa kilainishi cha kijamii kwa watu katika ulimwengu wa zamani kama ilivyo kwenye baa kote duniani.
Hapo awali, hops zilitumiwa kama kihifadhi, sio ladha. "Iligunduliwa wakati wa enzi za kati kwamba hops iliongeza faida ya antimicrobial kwa bia, kuzuia bia kuharibika kwa njia ambayo inaweza kuifanya iwe chungu - kwa hivyo iliongeza maisha utumizi wake," anasema Thomas Shellhammer, profesa wa sayansi ya uchachishaji katika chuo kikuu cha Jimbo la Oregon.
Bia inatengenezwaje?
Bia tangu jadi imekuwa ikitengenezwa kutoka kwa viungo vinne: maji, shayiri iliyoyeyuka, amira na hops.
Kokwa za shayiri hulowekwa ndani ya maji ili kulainisha ganda na kuanza mchakato wa kuota. Kisha hutolewa maji na kukaushwa kwenye tanuru ili kusitisha kuota. Zinapoanza kuchipua, kimeng'enya cha amylase hugeuza wanga iliyohifadhiwa kwenye kokwa kuwa sukari. Hizi ni muhimu kwa ladha ya bia, na kama chanzo cha chakula cha chachu, ambayo baadaye itachachusha bia kutengeneza pombe.
Baada ya kukaushwa, huchomwa kwenye tanuru. Kadiri choma kinavyokuwa kirefu na cha moto, ndivyo rangi ya mwisho inavyozidi kuwa nyeusi na ladha ya mwisho inavyozidi kuwa tajiri na zaidi.
Kisha, shayiri iliyoyeyuka husagwa na kwa maji ya moto ili kutoa sukari. Mchanganyiko huo huchemshwa kwa hops zilizokaushwa, na kupozwa hadi karibu 20C (68F) .
Mara baada ya baridi, chachu huongezwa. Hatua ya kuchacha kwa kawaida huchukua wiki kadhaa, kabla ya bia kuchujwa na kuwekwa kwenye chupa.
Bia hizi za zamani zingekuwa dhaifu na ladha tofauti sana. Katika utengenezaji wa bia za jadi, "ulimwengu wa mimea na viungo" isipokuwa hops ungetumiwa kama vionjo na vihifadhi mbadala, ikiwa ni pamoja na maua ya heather, viungo vya spruce, sage, rosemary na juniper.
"Wakati wa hatua ya kuchemka, asidi ya alpha unazifanya kuwa chungu zaidi," anasema Shellhammer. Bia chungu sana, kama vile Indian pale ales (IPAs) zimetengenezwa kwa humle zenye maudhui ya juu ya alfa-asidi ili kusisitiza ladha hizo chungu.
Umaarufu wa hops ulianza baada ya Mabadiliko ya Viwandani, asema Trnka, kwa sababu ya ladha katika katika bia nyepesi. Uthabiti ambao watengenezaji pombe wangeweza kutengeneza bia kwa kutumia hops ulilifanya zao hili kuwa muhimu mbele ya vionjo vingine vilivyokuwa maarufu.
Hakuna mahali popote ambapo bia nyepesi zilitoka zaidi katika Ulaya ya Kati - hasa katika mikoa ambayo sasa iko katika Cheki, Slovakia na Ujerumani - ambako bia ilivumbuliwa. Hops zinazokuzwa hapa, kwa jina noble hops, zimeheshimiwa sana kwa kuzipatia bia ladha yao ya kipekee. "Hii ni tasnia ya kiasili," anasema Trnka. "Unapata faida ikiwa utakuza hops hizi nzuri, aina hizi za zamani, haswa katika Czechia ambapo ni sehemu ya utamaduni wa miaka 100."
PICHA......
Utafiti wa mabadiliko ya tabia nchi wa Trnka na wenzake ulilenga aina bora za hop. Kuongezeka kwa hali ya joto kulikosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa kumesababisha kuanza mapema kwa msimu wa kilimo cha hop nchini Ujerumani na Czechia kwa siku 13 kati ya 1970 na 2018, huku pia uvunaji ukiwa umesogea siku 20 mapema.
Makadirio ya Trnka yanadokeza kuwa kufikia mwaka wa 2050 mavuno mazuri ya hop yatapungua kati ya 4.1 na 18.4% ikilinganishwa na 1989-2018, pamoja na kushuka kwa viwango vya asidi ya alpha, kutokana na kuongezeka kwa joto na ukame wa mara kwa mara.
Ingawa baadhi ya athari za joto la juu na ukame zinaweza kushindwa kupitia unyunyizaji, anasema Shellhammer, kwenye joto la juu sana la karibu 46C (116F) mimea huacha kukua, na baadhi ya magonjwa hustawi katika joto kali zaidi.
"Lakini, ikiwa unataka kukuza hops zilezile zilizokuzwa na babu zetu kutoka Karne ya 19 au , hops hizi nzuri ambazo zinathaminiwa sana kwa lager nyepesi ambazo ni maarufu huko Czechia, kuna njia za kuzikuza," anasema Trnka. .
Wakulima wa Hop wana chaguo chache: kuhamisha zao hilo kwenye maeneo yenye maji ya kiwango cha juu, kwa mfano katika mabonde au vijito, ambapo maji hufyonzwa kwa urahisi na mizizi ya mimea, kuongeza unyunyizaji wa maji au kubadili aina nyingi zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi. Haya yote yamethibitisha mikakati ya mafanikio katika utengenezaji wa mvinyo, ambapo kilimo cha mitishamba pia kinatishiwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Kwa njia fulani, asema Shellhammer, watengenezaji bia wana bahati zaidi kuliko watengenezaji wa mvinyo, ambao wanategemea kiungo kimoja tu - zabibu - kurekebisha chachu, ili kuboresha ladha.
Lakini sio rahisi kutekeleza suluhu hizi zote, anaonya Chuck Skypeck, mkurugenzi wa miradi ya utayarishaji pombe wa kiufundi katika Chama cha Watengenezaji Bia nchini Marekani.
Unyunyizaji ni jambo la kawaida katika Amerika ya Kaskazini kuliko ilivyo katika Ulaya, na ni gharama kubwa kuanzisha, anasema Skypeck.
Kubadilisha aina ya hops pia ni rahisi kusema kuliko kufanya. Hops ni mazao ya kudumu, ambayo inamaanisha kuwa mmea hubaki kwenye udongo kila mwaka. Kama mazao mengine ya kudumu, kama vile chai, kahawa au zabibu, kubadilisha aina ya mimea itahitaji kuchimba mmea mzima, anasema. Kubadilisha aina za nafaka ni rahisi zaidi kwani kila mwaka mazao mapya hupandwa kutoka kwa mbegu.
Lakini Shellhammer anafikiri kuwa kubadili aina za hop kunaweza tu kusababisha miaka michache ya mavuno yaliopungua. "Katika eneo la Kaskazini-Magharibi mwa Marekani, nimezungumza na wakulima ambao wanasema wanaweza kubadilisha mazao na kupata karibu 75% ya mavuno katika mwaka wa kwanza," anasema. "Ukiwa na zabibu za divai, unangojea mzabibu mzima kukua na kuzaa - kwa hivyo ni juhudi za miaka mingi."
Skypeck anaongeza kuwa programu za ufugaji zilizopo Amerika Kaskazini na maeneo yote makuu ya kilimo cha hop zinalenga aina mpya za kubadilisha ladha na harufu, na kutafuta aina ambazo zinaweza kubadilishwa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Marekebisho hayo yanajumuisha miundo ya mizizi yenye kina zaidi, mimea minene ambayo inastahimili ukame. Aina hizi mpya zinaonekana kupendwa na watengenezaji bia na watengenezaji wa bia chungu na mivinyo.
Aina mpya za hop zinakuzwa ili kustahimili mabadiliko ya tabianchi, anasema Skypeck, lakini kutengeneza aina mpya ya hop kutoka mwanzo hadi uzalishaji kamili kunaweza kuchukua hadi miaka 10.
Kwa mfano, aina mpya ya hop inapojaribiwa inaweza kuonyesha upinzani zaidi wa joto lakini bado inaweza kuhitaji kiwango sawa cha maji, anasema.
"Watengenezaji bia huchukua mbinu tofauti pia. Watengenezaji bia wa Marekani mara chache hutumia aina moja tu ya hop katika bia zao, badala yake huweka ladha na manukato tofauti ili kuunda vinywaji tofauti unavyovipata katika bia nyingi.
Kwa upande mwingine, watengenezaji pombe wa jadi wa Ujerumani walio wahafidhina wanaweza kusita kupokea aina mpya kwa sababu hawataki kubadilisha ladha ya bia zao ambayo imekuwa thabiti kwa miaka."
Christian Ettinger, mwanzilishi wa Kiwanda cha Bia cha Hopworks Urban huko Portland, Marekani, anasema kwamba moja ya bia zao za kawaida zinaweza kuwa na kati ya aina mbili na tano tofauti za hop, jambo ambalo huwapa watengenezaji bia wigo wa kurekebisha kichocheo kulingana na mabadiliko ya mavuno. "Kuchagua hop na utabiri ni ngumu, na inakuhitaji upitie mipango yako moja ya hadi mwengine ili kurekebisha mapishi yako," anasema.
Uhaba wa maji ni mchangiaji mkuu wa mavuno machache nchini Marekani, ambayo huchangia gharama ya juu, anasema Ettinger. "Bia imekuwa kinywaji maarufu zaidi cha pombe kwa miaka 9,000, na sehemu yake ni kuifikia na uwezo wa kuimudu. Ni wajibu wetu kama wakulima kuhakikisha kuwa bado inapatikana."
Imetafsiriwa na Seif Abdalla