'Nilifikiri mwanangu alikuwa mazoezini kumbe alikuwa amekufa'

Februari 20, Valya alipokea simu kutoka kwa mtoto wake aliyekuwa katika jeshi la Urusi. Kitengo chake kilikuwa "kwenye mazoezi" karibu na mpaka wa Ukraine.
"Alisema walikuwa wakifanya mazoezi ya kurusha risasi na kuishi kwenye mahema," Valya alisema. "Hiyo ilikuwa mara yangu ya mwisho kuzungumza naye."
Siku nne baadaye, wanajeshi wa Urusi walivamia Ukraine.
Mashambulizi ya Urusi yameleta mateso mengi kwa nchi hiyo ya jirani. Tangu Rais Vladimir Putin kuamuru uvamizi huo, maelfu ya raia wameuawa nchini Ukraine.
Lakini nyumbani, kuna madhara pia, kwa familia za wanajeshi wa Urusi ambao wametumwa vitani.
Valya sio jina lake halisi. Kwa kuhofia madhara kutoka kwa mamlaka kwa kuzungumza, mama huyo ametutaka kuficha utambulisho wake.
Lakini ana hamu ya kuitoa hadithi yake. Anataka kuzungumza nasi kuhusu mwanae na anachofikiria kuhusu "operesheni maalum ya kijeshi" ya Kremlin.

"Mwanzoni mwa Machi, sajenti alinipigia simu kutoka kituo cha mwanangu. Pengine aliwapigia simu wazazi wote," anasema.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Aliniambia vijana hapo sawa, wanawasiliana nao kila siku. Tuliendelea kuwasiliana mwezi mzima wa Machi na aliendelea kusema kwamba walikuwa sawa.
“Ndipo mtu mmoja anayedai kuwa ni rafiki wa mwanangu alinitumia meseji, sikumfahamu, alinikuta kwenye mitandao ya kijamii, akaniambia mguu wa mwanangu umelipuliwa na amefariki, nilipiga simu nyingi na kujaribu kukutana na maafisa, lakini hakuna mtu aliyeweza kuniambia chochote.
"Mwishowe sajenti niliyekuwa nikizungumza naye aliniambia: 'Mtoto wako niliwasiliana naye mara ya mwisho tarehe 23 Februari.'
"'Kwa hiyo kwa nini umekuwa ukipiga simu [kusema kila kitu kiko sawa]? Ili tu kututuliza?'
"'Samahani, mimi ni sajenti tu,' alisema."
Valya alijaribu kujua zaidi. "Niliandikia kitengo cha mwanangu," anakumbuka.
"Niliandikia ofisi ya wilaya ya kijeshi. Niliandikia Wizara ya Ulinzi. Na kisha nikawaandikia wote tena.
"Hakuna mtu aliyenipa taarifa za msingi wapi, lini na jinsi gani mwanangu alifariki. Nilichoambiwa ni kwamba alikuwa akishiriki 'operesheni maalum ya kijeshi' na kwamba hayupo."
Ni wanajeshi wangapi wa Urusi wameuawa nchini Ukraine? Ni kosa la jinai nchini Urusi kuripoti chochote isipokuwa takwimu rasmi.

Chanzo cha picha, Reuters
Lakini takwimu rasmi ni ngumu kupata. Wizara ya ulinzi ya Urusi haijatoa idadi rasmi mpya ya vifo vya wanajeshi tangu tarehe 25 Machi.
Wakati huo, ilisema askari 1,351 wa Urusi ndio waliouawa. Mwezi uliofuata, Kremlin ilikubali kupoteza askari nchini Ukraine.
Katika jitihada za kuhalalisha uvamizi huo, mamlaka ya Urusi na vyombo vya habari vya serikali vinajaribu kuwadhalilisha Waukraine mbele ya Urusi.
Wanashutumu askari na maafisa wa Ukraine kama "wazalendo wa hali ya juu" na "Wanazi". Wanadai kwamba Ukraine ni mchokozi na Urusi mkombozi.
Lakini Valya haoni Ukraine kama adui.
"Kama nchi yetu ingeshambuliwa hivi, tungekuwa tunajilinda, kama wao. Tungejilinda na tungekuwa na hasira pia," anasema.
Warusi wengi wanaamini serikali wanaunga mkono "operesheni maalum ya kijeshi", kama inavyowasilishwa kwao kwenye runinga ya serikali. Katika Urusi Kremlin inadhibiti TV.
Lakini si kabisa. Valya anawasiliana na mama wa askari wa Urusi. Anadai kuwa miongoni mwa akina mama kunaongezeka chuki dhidi ya mamlaka kuhusu nani anatumwa kupigana nchini Ukraine.
"Wanachukia serikali. Wanamchukia Putin," Valya ananiambia. "Wote wanataka vita hivi viishe. Kina mama wote wataka hivyo.

"Sisi ni tabaka la chini kabisa. Sisi ni watu wa kawaida katika nchi. Vijana wote wanaopigana wanatoka mikoa ya mbali ya Urusi. Sio Muscovites. Hakuna watoto wa maafisa wa serikali huko.
"Ikiwa wakina mama wa askari wote waliopo huko sasa na akina mama ambao wamepoteza watoto watasimama pamoja, ungeweza kuona jinsi jeshi hilo lilivyo kubwa? Na watafanya hivyo.
"Acha haya yote, acha tuwalinde watoto wetu."
Tangu alipozungumza na sisi, Valya amepokea taarifa rasmi kwamba mtoto wake aliuawa nchini Ukraine. Ni mmoja wa askari wa Urusi ambaye hatarudi nyumbani.
















