Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini mzozo wa mafuta kati ya Kenya na Uganda unasababisha wasiwasi katika kanda hii
Na Basilioh Rukanga
BBC News, Nairobi
Mzozo mkali kuhusu usambazaji wa mafuta umezuka kati ya Kenya na jirani yake Uganda isiyo na bandari, huku kiongozi wa Uganda Yoweri Museveni akisema nchi yake "inadanganywa" na "vimelea" na wafanyabiashara wanaohudumu kama 'mawakala'.
Kwa miongo kadhaa, Kenya imekuwa ikiagiza mafuta kutoka nje na kuyauza kwa majirani zake wa Afrika Mashariki - lakini jukumu lake kama lango kuu la kusambaza mafuta katika eneo hilo sasa liko hatarini.
Yote yalitimia mapema mwezi huu wakati Rais wa Uganda Yoweri Museveni aliposhutumu wafanyabiashara wa kati wa Kenya kwa kupandisha bei ya mafuta kwa hadi asilimia 58, na kusababisha "hasara kubwa" kwa nchi yake.
Pia alikashifu "vimelea vya ndani" kwa "kulaghai" Uganda kwa kushindwa kuingilia kati tangu bei ilipoanza kupanda mapema mwaka jana.
Uganda kwa miaka mingi imeagiza 90% ya mafuta yake kutoka kwa makampuni ya uuzaji wa mafuta ya Kenya, ambayo huuza kwa kampuni zao tanzu za Uganda - yanayosalia hununuliwa kupitia Tanzania.
Shambulio la Bw Museveni lilikuja huku bunge la Uganda likiidhinisha uamuzi wa kusitisha hili.
Serikali yake imeweka wazi kuwa inataka uhuru zaidi juu ya mikataba ya baadaye ya mafuta.
"Kenya kwa miongo kadhaa imeamua ni bidhaa gani za petroli Uganda itanunua, lini, wapi, kiasi gani, nani ananunua na kwa bei gani," alielezea Waziri wa Nishati wa Uganda Ruth Nankabirwa.
Lakini kampuni za uuzaji wa mafuta nchini Kenya zimenyooshea kidole cha lawama kwa bei ya juu ya hivi majuzi kwa serikali ya Kenya.
Hapo awali, mchakato wa kutoa zabuni na makampuni mbalimbali ya Kenya ulifanyika. Kampuni iliyoshinda zabuni ingeagiza mafuta kwa niaba ya wengine. Ilikuwa ni shughuli ya kulipa kadri uwezavyo kwenda iliyotekelezwa kwa dola za Marekani.
Lakini mwezi Machi, serikali ya Kenya iliingilia kati kwa sababu ya uhaba wa dola za Marekani nchini humo, jambo ambalo lilisababisha matatizo kwa wafanyabiashara wote wanaoagiza bidhaa kutoka nje kwa vile benki zilikuwa zikitoa mgao wa dola.
Serikali ilijadiliana kwa upande mmoja kuhusu bei na makampuni ya kimataifa ya mafuta ili kusambaza mafuta kwa mkopo kwa soko la ndani na nje ya nchi.
Mpangilio huu unamaanisha malipo kwa wasambazaji wa kimataifa yanacheleweshwa kwa miezi sita.
Chini ya mpango huo, wateja wa ndani wa makampuni ya uuzaji wa mafuta ya Kenya hulipa bidhaa zao kwa shilingi za Kenya, lakini wale wa nchi jirani hulipa kwa dola.
Pesa zote huwekwa kwenye akaunti ya kupata riba kubwa kwa muda wa miezi sita kabla ya malipo kufanywa - na hivyo kupunguza mzigo wa uhaba wa dola.
John Njogu, Afisa mkuu Mtendaji wa Chama cha Wauzaji wa Mafuta nchini Kenya, anaelezea hii kama "laini ya mkopo" na anasema mpangilio kama huo unafanya mafuta kuwa ghali zaidi kwa wanunuzi.
Aliambia BBC kwamba Uganda ilikuwa na haki ya kuikataa kwani haikuwa na tatizo la uhaba wa dola na haipaswi kutarajiwa kulipa zaidi.
Huku Uganda sasa ikijiondoa, Kenya sasa itapata tatizo lake la uhaba wa dola kukithiri zaidi - kwani Bw Njogu anasema Uganda inalipa $180m (£143m) kwa mwezi kwa makampuni ya Kenya kwa ajili ya mafuta.
Mkataba huo pia umekosolewa na kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga, ambaye aliutaja kama "ulaghai kubwa" - akipendekeza Wakenya wanalazimishwa kulipa bei ya juu huku wengine, zikiwemo baadhi ya makampuni ya uuzaji wa mafuta, wakipata faida.
Anataka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi nchini Kenya (EACC) kuchunguza masharti ya mpango huo, ambayo alisema yanafaa kuwekwa hadharani.
"Watu wa kati anaowazungumzia Rais Museveni ni maafisa wa serikali ya Kenya," alisema.
Lakini Waziri wa Nishati wa Kenya Davis Chirchir ametetea mpango huo wa mkopo, akiwaambia wabunge kwamba umesaidia kuwaepusha Wakenya kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta na mishtuko kutoka nje.
Bila hivyo bei inaweza kuwa kubwa zaidi, hasa kutokana na kushuka kwa thamani ya sarafu dhidi ya dola, alisema.
Vita hivi vya maneno vimeambatana na kashfa ya kutatanisha nchini Kenya kuhusu uagizaji wa tani 100,000 za mafuta yenye thamani ya $110m - ambayo umiliki wake umebishaniwa na kesi iko mahakamani.
Wakili wa mfanyabiashara huyo Mkenya anayehusika na madai kuwa alitekwa nyara kwa siku kadhaa na wale waliokuwa wakitaka "kuiba" shehena hiyo.
Serikali ya Kenya inakanusha kuhusika na imesema kampuni yake haina leseni.
Sio tu watumiaji wa Kenya na rais wa Uganda ambao hawana furaha. Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda na Sudan Kusini pia hupata kiasi kikubwa cha bidhaa zao za petroli kupitia Kenya.
"Kanda inanung'unika," Dzombo Mbaru, Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya mafuta ya Kenya ya Mardin Energy, aliambia BBC.
Anasema sio mpango mpya pekee ambao una makosa, akipendekeza ushuru wa Kenya unaotozwa kwa bidhaa zote za petroli unaweza kuwa sababu na unahitaji "mapitio muhimu".
"Eneo hili halijalala na limeunganisha miradi ya miundombinu ili kudhibiti udhibiti wetu. Lina chaguzi na baada ya muda Kenya itapoteza mengi," Bw Mbaru anaonya.
Tayari Uganda imesema imeafikia makubaliano na kampuni ya Vitol Bahrain kufadhili hatua ya Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda kutafuta na kusambaza mafuta. Pia imetangaza kuwa itaweka akiba yake ya mafuta nchini Tanzania.
Miundombinu nchini Tanzania haijaendelezwa kama ilivyo nchini Kenya, lakini kwa ushirikiano mpya hili inaweza kubadilika, Bw Mbaru anasema.
Kwa kuwa Uganda hivi karibuni itaanza kuzalisha mafuta yake yenyewe na kupanga kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta itaweza kutoa "bidhaa za petroli zenye ushindani, bila [gharama] zinazosababishwa na wafanyabiashara wa kati" ndani ya miaka michache kwa Afrika Mashariki, anaongeza.
Kwa Bw Njogu, hatua ya Uganda ni mwamko unaohitajika kwa tasnia ya uagizaji mafuta nchini Kenya: "Tunahitaji kuwa mpango bora zaidi katika kuwa washindani na kuwa na weledi katika kupata biashara."
Lakini ni somo chungu ambalo litaathiri pakubwa uchumi wa Kenya kwa siku zijazo , anasema.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah