Tetesi za Soka Ulaya Jumatano 14.02.2024

Conor Gallagher

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa

Tottenham watamnunua Conor Gallagher wa Chelsea msimu huu wa joto ikiwa kiungo huyo wa Uingereza mwenye umri wa miaka 24 hataafikiana na The Blues kuhusu kuongeza mkataba wake wa sasa, ambao unamalizika mwishoni mwa msimu ujao. (Telegraph - usajili unahitajika)

Newcastle na Arsenal wako macho baada ya mazungumzo ya kandarasi kati ya Brentford na mshambuliaji wao wa Uingereza Ivan Toney, 27, kukwama. (TeamTalk)

Brentford imemtambua mshambuliaji wa Lille wa Canada Jonathan David, 24, kama mbadala wake iwapo Toney ataondoka katika klabu hiyo msimu huu wa joto. (Football Transfers)

Ivan Toney

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mshambuliaji wa Brentford Ivan Toney

Manchester United na Tottenham wanafanya bidii zaidi kumsajili Jarrad Branthwaite wa Everton, huku klabu za Chelsea, Arsenal na Real Madrid zikimuulizia beki huyo wa Uingereza wa chini ya umri wa miaka 21, 21. (Mail)

Manchester City wamekubali mkataba wa kumnunua winga wa Brazil Savio, 19, ambaye kwa sasa yuko kwa mkopo katika klabu ya Girona ya Uhispania kutoka Troyes ya Ufaransa. (Fabrizio Romano)

Newcastle wameungana na West Ham katika kinyang'anyiro cha kumsajili mshambuliaji wa Genoa wa Iceland Albert Gudmundsson, 26. (Gazzetta dello Sport - kwa Kiitaliano)

Arsenal wanafikiria kumuuza kiungo wa kati wa Ujerumani Kai Havertz mwenye umri wa miaka 24 msimu huu wa joto. (Fichajes - kwa Kihispania)

''

Bayern Munich walitaka kumsajili Mykhailo Mudryk kwa mkopo mwezi Januari lakini Chelsea hawakuwa na nia ya kumruhusu winga huyo wa Ukraine mwenye umri wa miaka 23 kuondoka. (Fabrizio Romano)

Mkurugenzi wa michezo wa Newcastle Dan Ashworth analengwa na Manchester United kuchukua nafasi ya John Murtough, ambaye anatarajiwa kuacha nafasi yake kama mkurugenzi wa soka mara tu dili la Sir Jim Ratcliffe la kununua asilimia 25 ya hisa za Red Devils kukamilika. (I)

The Magpies wana wasiwasi kwamba Ashworth hajatulia na wanataka hakikisho kwamba atajitolea kwa muda mrefu katika klabu hiyo. (Telegraph - usajili unahitajika)

Kocha wa Bayern Munich Thomas Tuchel yuko kwenye orodha ya Barcelona ya mameneja wanaopigiwa upatu kurithi mikoba ya Xavi wakati kiungo huyo wa zamani wa Uhispania atajiuzulu mwishoni mwa msimu huu. (Sport - kwa Kihispania)

''

Chanzo cha picha, Getty Images

Wawakilishi wa Kylian Mbappe waliwasiliana na Liverpool kuhusu uhamisho mwaka jana, lakini klabu hiyo haikutaka kuvuruga mkakati wao mzima wa kifedha ili kumsajili nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 wa Paris St-Germain na Ufaransa. (Independent)

Barcelona hawana uwezo wa kumteua Roberto de Zerbi kama kocha wao mpya kwa sababu ya kitita kinacohitajika ili kumpata kocha wa Brighton. (Matteo Moretto)

Crystal Palace wamechanganyikiwa katika jitihada zao za kumshawishi Kieran McKenna kuondoka Ipswich na kuchukua nafasi ya Roy Hodgson kama kocha lakini wanatumai raia huyo wa Ireland Kaskazini anaweza kuchukua mikoba mwishoni mwa msimu huu. (Guardian)

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi