WARIDI WA BBC:'Wasanii wa sasa wanaweza kupata funzo kutokana na maamuzi niliyofanya'-Marya
Na Ann Ngugi
BBC Swahili,Nairobi

Chanzo cha picha, Marya
Marya Maina Wanjiru kwa jina la usanii akijulikana kama Marya kutoka Kenya, ni mwanamke wa miaka 31 ambaye ameyaona mengi tangu alipoamua kujitosa katika ulimwengu wa sanaa akiwa na miaka 22.
Ni mwanadada ambaye aliingia kwa kishindo kwenye sanaa na kushabikiwa sana hasa kutokana na mtindo wake wa muziki kama binti ambaye alisifiwa sana na kuenziwa kama mlimbwende.
Wakati alipoingia kwenye ulingo wa muziki kwa mtindo wa ‘genge tone’ ambao ulikuwa ni maarufu miongoni mwa vijana kwa wakati huo nchini Kenya anasema kwamba alipata umaarufu wa haraka sana ambao hakuwa tayari kisaikolojia kuupokea.
“Kwa kweli mara tu nilipojitosa kwenye muziki sikutarajia kishindo cha ufuasi niliyoupata ghafla , nilijikuta nimeingiwa na kiburi cha umaarufu. Nilijihisi shujaa sana na ilikuwa vigumu kunishauri”anasema Marya.
Msanii huyu anasema kwamba alipoanza usanii wake hakupata mshauri na wachache ambao walithubutu kumpa muongozo wa jinsi ya kujisimamia kama msanii mchanga japo mwenye umaarufu aluupuza. Anakiri kwamba hali hii ilipelekea maisha yake kubadilika na kuwa ya anasa na raha za kila siku.
Marya anafahamika sana kwa kibao ‘chokoza’ na ‘get baby’ wakati wimbo huo unavuma anasema kwamba alikuwa anapokea nafasi za kutumbuiza watu katika sehemu mbalimbali za burudani.
“Kwa kweli nilikuwa situmii pesa vizuri nilikuwa ninalipwa kiasi kikubwa cha pesa lakini sikuwa na maarifa ya kutumia , nilikuwa bado nina umri mdogo na nilikosa hekima ya kuweka akiba kwa siku za usoni, ni ajabu pia sikununu shamba au hata kujenga, ninajutia sana”, Marya alikiri.
Maisha ya msanii huyu akiwa na umri kati ya 22-25 anasema kwamba yalikuwa na baraka nyingi sana kifedha na umaarufu na iwapo angechukua fursa hiyo kujijenga wakati huo basi hii leo angekuwa ni mwanamke mwenye mali yake.

Chanzo cha picha, Marya
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ila sasa inasalia kuwa somo na funzo kwake. Alitupa mfano wa wakati mmoja ambao hatawahi kusahau alipojikuta amekula raha kupitiliza alipotoka kwenye kazi moja ya kutumbuiza na akalipwa kiasi kikubwa cha pesa taslimu kilichofuata anasema hatosahau.
“Nililipwa pesa taslimu dola elfu mbili , amini usiamini kiasi hiki cha pesa nilitumia kwa siku mbili .Nilikuwa kama nimepagawa kwa anasa mbalimbali za maisha. Kwa mfano unywaji wa pombe kupitiliza na safari ambazo zilikuwa hazina maana yeyote,”anakumbuka Marya.
Mambo yalianza kugeuka, mifuko yake ilianza kukauka na akajikutan katika wakati mgumu. Ni hali iliyompelekea kuwa na madeni mengi mnoo kutoka kwa marafiki na wandani wake wa karibu. Mwisho wa anasa ulikuwa ni majuto makubwa kwake asijue la kufanya.
Kipindi hicho hicho Marya anasema kwamba aliamua kusafiri hadi Dubai baada ya kukutana na mwanamume waliofanya urafiki naye, ni mahusiano yalioishia wao kujaliwa mtoto wa kiume. Msanii huyu alikuwa ameacha sanaa na kujishughulisha na kazi zingine. Mahusiano yake baadae yalivunjika na kurejea Kenya yeye na mwanae wa kiume.
Tangu aliporejea nchini Kenya alianza kuyatathmini maisha yake upya , na kukubali mianya mingi ya fursa za maisha kuporomoka na kusababisha kufilisika kwake kama msanii maarufu Kenya.
Marya anasema kwamba majuto ni mjukuu na yeye amejutia hali ya ukosefu wa maadili hasa kuhusiana na matumizi ya fedha na maisha ya hali ya juu aliyoyaishi kama msanii.
Anakiri kwamba wasanii wengi huishi maisha ambayo kihalisia sio maisha yao, ila wanaiga maisha ya hali ya juu ilhali fedha na kiwango cha maisha yao hakiwaruhusu kuwa hapo.
Kwa hiyo baadhi ya wasanii wanajikuta wakiwa katika njia panda kimaisha wakati wanakosa maisha ya kugharamikia maisha hayo ya juu .

Chanzo cha picha, Marya
Kwake yeye ameamua kwamba maisha yake ya karibia miaka kumi iliyopita ni somo kwake na pia anatumia fursa hiyo kuzungumza na wasanii hasa wanawake wanaochipuka katika ulingo huo kuishi maisha wakifahamu kwamba kesho ipo na ni muhimu kuwekeza na kuokoa kiasi fulani cha fedha kwa siku ambazo mvua inanyesha ghafla .
“japo uhusiano wangu na jamii yangu ya karibu imeimarika hapo awali wakati nilikuwa msanii tajika nilikuwa nimewasahau kabisa, nilikuwa na fedha nyingi ndio lakini sikuwa na wakati nao, nilijipata nikiwa katika makundi ya marafiki ambao hawakuwa wananipa ushauri wa kujihusisha na watu wa jamii yangu najutia lakini pia nimetumia matukio hayo kama somo kuu kwangu ”anasema Marya.
Kwa hivi sasa Marya anapambana sana kama msanii kurejea katika nafasi aliyokuwa nayo hapo awali hivi maajuzi alitoa kibao kwa jina ‘bumshakala’ anasema kwamba anahisi amepewa nafasi ya pili kama msanii wa kike kufuata kipaji chake. Marya anasema kwamba yeye amepitishwa kwenye shule ngumu ya kufilisika na kuhangaika baada ya kutumia fedha vibaya lakini sasa anajutia.















