'Kamera yako ni silaha': Wanawake wa Iraq wapinga vitisho vya kuuawa katika mapambano dhidi ya ukatili wa kingono

.
Maelezo ya picha, "Kamera yako ni silaha yako," anasema Sarah Jassim, akieleza kuwa video anazochapisha husaidia kuweka kumbukumbu za ushahidi wa unyanyasaji.
    • Author, Sally Nabil
    • Nafasi, BBC News Arabic
    • Akiripoti kutoka, Baghdad
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Tahadhari: Habari hii inaelezea matukio ya ukatili wa kingono.

"Shuka kwenye gari!" anapiga kelele mwanamke mmoja, akimtuhumu dereva kwa kujianika na kutoa matamshi machafu alipokuwa akipita karibu naye. Mwanamke huyo anarekodi tukio hilo kwa simu yake katika barabara yenye shughuli nyingi mjini Baghdad, huku kamera ikimnasa dereva huyo akipinga juhudi zake za kufungua mlango wa gari anapomkabili.

Video hiyo, pamoja na nyingine zinazofanana nayo, inaweza kuonekana kwenye ukurasa wa Instagram wa Sarah Jassim, mwanaharakati wa haki za wanawake nchini Iraq. Anazichapisha kwa niaba ya wanawake wanaolalamikia unyanyasaji na udhalilishaji wa kingono unaofanywa na wanaume na wavulana nchini humo.

"Kamera yako ni silaha yako," anaiambia BBC. "Ni njia ya kurekodi ushahidi iwapo mwanamke ataamua kumfungulia mashtaka mtu aliyemnyanyasa, au angalau njia ya kumwaibisha."

Anasema moja ya video alizochapisha ilisababisha kukamatwa kwa mtuhumiwa, ambaye ni polisi anayetuhumiwa kuwanyanyasa wasichana wa shule.

.
Maelezo ya picha, Video iliyochapishwa na Jassim inamuonesha mwanamke akimfokea mwanaume anayemtuhumu kujianika, kisha akijaribu kufungua mlango wa gari lake.

Jassim anasema kuchapisha video hizo ni jambo hatari kwake na kwa wanawake wanaohusika. Tumezungumza na wahanga wengi wa unyanyasaji wa kingono nchini Iraq ambao wanasema kuwa jamii mara nyingi humlaumu mhanga badala ya mtenda kosa.

"Nimepokea vitisho vya kuuawa, na pia nimetishiwa kushambuliwa kwa tindikali," anasema Jassim. "Nimetuhumiwa kuchochea vitendo vya utovu wa maadili kwa sababu ninawahimiza wanawake kuzungumza katika jamii inayotarajia tukae kimya."

Sasa anatoka nyumbani mara chache sana kwa ajili ya usalama wake, na badala yake hutumia saa nyingi kucheza na mbwa wake.

Anasisitiza kuwa kuna haja ya kuwa na sheria kali zaidi, zikiwemo sheria zinazotaja wazi kuwa unyanyasaji na ukatili wa kijinsia ni makosa ya jinai. Kwa sasa, maneno hayo hayapo katika sheria ya adhabu nchini Iraq.

"Kutambua tatizo ndiyo njia bora ya kulikabili," anasema. "Tunahitaji ulinzi, na wanaowanyanyasa wengine lazima waogope kufanya hivyo."

'Hakuna atakayesikia nikikuua'

Wanawake wengi nchini Iraq wameiambia BBC kuwa wanahisi mifumo ya haki na polisi imewaangusha. Kwa mujibu wa wanaharakati na mawakili kadhaa tuliozungumza nao, kufungua mashtaka dhidi ya mtu anayekunyanyasa au mbakaji ni mchakato mrefu nchini Iraq, wenye taratibu ngumu na matokeo yasiyo na uhakika.

Ukatili dhidi ya wanawake na wasichana nchini Iraq ni "ulioenea sana na hauripotiwi vya kutosha", kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa mwezi Mei na kamati ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia ubaguzi dhidi ya wanawake, ambayo ilitaka sheria kuimarishwa.

Miongoni mwa mapendekezo kadhaa, kamati hiyo ilizitaka mamlaka kufuta sheria zinazobagua wanawake na zinazowasamehe wabakaji iwapo watawaoa wahanga wao. Pia ilitaka kufutwa kwa sheria zinazoruhusu kupunguziwa adhabu watu wanaoua kwa kile kinachoitwa "mauaji ya heshima".

Amal - si jina lake halisi - amekuwa akipambana mahakamani kwa takribani miaka mitano. Anamtuhumu aliyekuwa mume wake kumbaka mara kwa mara binti yao, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa chini ya miaka 18, huku akimtishia kwa bunduki.

Anakumbuka maelezo ya kutisha ya binti yake kuhusu tukio hilo. Anasema baba yake aliingia chumbani kwa msichana huyo na kuweka silaha yake juu ya kitanda.

Anasema alimwambia: "Hakuna atakayesikia ukipiga kelele nikikuua."

.
Maelezo ya picha, Amal anamtuhumu aliyekuwa mume wake kumbaka binti yao mara kwa mara, wakati binti huyo akiwa na umri wa chini ya miaka 18.

Unyanyasaji wa kingono umekuwa suala linalochukuliwa kuwa mwiko nchini Iraq kwa muda mrefu. Nimewasiliana na manusura wengi ambao wanasema wanapendelea kuficha yaliyowapata kwa hofu ya kukumbana na chuki au hatua kali kutoka kwa familia zao.

Wengine wametuambia kuwa wanaogopa kwenda polisi kwa sababu ya unyanyapaa wa kijamii na uwezekano wa kunyanyaswa zaidi.

Lakini Amal alikuwa amedhamiria kutafuta haki, hivyo alikimbilia polisi kuripoti tukio hilo.

"Alikuwa na michubuko mingi kuzunguka vifundo vya mikono yake kwa sababu alikuwa akimshikilia kwa nguvu. Kila alipojaribu kupiga kelele, alikuwa akimziba mdomo kwa mikono yake," anasema Amal.

Amal alinionyesha nyaraka za kitabibu, zikiwemo ushahidi wa vinasaba (DNA), zinazounga mkono maelezo yake.

Amal anasema ukatili wa aliyekuwa mume wake ulidhihirika zaidi aliposikia akimwambia mwanafamilia mmoja kwamba, iwapo angekamatwa, "aoshe aibu yetu".

Kauli hiyo hutumiwa nchini Iraq kurejelea kile kinachoitwa mauaji ya heshima, yanayofanywa kwa imani kwamba mwanamke amechafua sifa ya familia yake.

Amal anasema anaamini baba huyo alitishia kumuua binti yake "ili ripoti ya kitabibu isitolewe na unyanyasaji huo usithibitishwe".

Anasema aliyekuwa mume wake amekimbia na kesi hiyo bado inaendelea mahakamani.

"Nilipambana peke yangu," anasema Amal huku akitokwa na machozi. Anasema aliyekuwa mume wake aliajiri mawakili kadhaa, lakini yeye hakuwa na uwezo wa kumudu gharama za uwakilishi wa kisheria, huku familia yake ikifumbia macho yaliyokuwa yakitokea.

Sasa hana tena imani kwamba mahakama itatoa uamuzi kwa niaba yake.

"Ninachotaka tu ni yeye akae mbali nami milele," anasema huku akivuta pumzi kwa kukata tamaa.

Mwanaharakati auawa

Binti wa Amal ana bahati zaidi kuliko baadhi ya wanawake waliopitia unyanyasaji wa kingono ndani ya familia nchini Iraq, kwa sababu ana mahali salama pa kuishi.

Manusura wengi hawana kipato chao binafsi wala mahali pa kwenda. Iraq ina makazi machache sana ya kuwahifadhi wanawake wanaofanyiwa ukatili.

Makazi tunayoyafahamu yalianzishwa na shirika lililoshirikishwa kuanzishwa na Yanar Mohammed, mtetezi wa haki za wanawake anayetambulika kimataifa. Mwezi Machi mwaka huu, aliuawa nje ya nyumba yake mjini Baghdad na watu wenye silaha. Waliotekeleza mauaji hayo bado hawajulikani.

Wataalamu wanaofanya kazi kwa niaba ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa waliandika mwezi Aprili kwamba Mohammed alikuwa akipokea vitisho vya kuuawa na kufanyiwa unyanyasaji mtandaoni kwa miaka kadhaa. Vitisho hivyo vinaaminika kutoka kwa wanamgambo wenye misimamo mikali ya kidini.

.
Maelezo ya picha, Picha ya Hanaa Edwar (kushoto) aliyoipiga akiwa na Yanar Mohammed na kwa mujibu wa kumbukumbu zake, ilikiuwa siku mbili tu kabla ya mwanaharakati huyo kuuawa.

Wanaharakati wametuambia mara kadhaa kuwa mashambulizi yanayolenga wenzao yameongezeka katika miaka ya hivi karibuni.

Hanaa Edwar, mwanaharakati mwingine mashuhuri wa haki za wanawake, anasema alimwona Mohammed siku mbili tu kabla ya kuuawa kwake. Anasema yeye pia ametishiwa.

"Hakuna sheria, hakuna ulinzi, na hakuna haki kwa wanawake nchini Iraq," anaiambia BBC.

"Tatizo nchini Iraq si kwamba wanawake wanakaa kimya. Tatizo ni kwamba wanapozungumza, mifumo iliyopo haijaandaliwa vya kutosha kuwasikiliza," anasema Mustafa Saadoon, mkuu wa Kituo cha Uangalizi wa Haki za Binadamu nchini Iraq, akizungumza na BBC.

"Mwanamke anayeripoti ukatili wa kingono lazima kwanza apambane na familia yake, kisha kituo cha polisi, halafu mahakama. Na katika kila hatua hizo, kuna uwezekano wa mtu kumwambia atatue suala hilo kimya kimya."

'Alinifuata kwa gari'

Miongoni mwa wanawake wa Iraq wanaosema kuwa wameangushwa na mfumo huo ni Samira — si jina lake halisi.

Anaiambia BBC kuwa kutembea barabarani kunamfanya ajisikie hofu na kutokuwa salama kutokana na matukio ya mara kwa mara ya unyanyasaji aliyopitia.

Katika tukio moja, anasema mwanamume fulani alikuwa akitazama filamu ya ponografia kwenye simu yake katika usafiri wa umma, kisha akamsogezea simu hiyo usoni mwake.

.
Maelezo ya picha, Samira anasema amekuwa akinyanyaswa katika usafiri wa umma na kufuatwa na mwanaume kwa gari alipokuwa akielekea kazini.

Katika tukio jingine mjini Baghdad, anasema mwanaume mmoja alimfuata kwa gari lake kwa zaidi ya dakika 10.

"Ilikuwa hali ya kusikitisha sana... Niliona gari la polisi. Nilikwenda kuwaeleza kilichotokea. Waliniambia hawakuwa na mamlaka ya kuchukua hatua yoyote."

Ingawa mama yake ni mwenye upendo na humuunga mkono, Samira hamwelezi matukio ya unyanyasaji wa kingono anayokumbana nayo.

"Nikiieleza familia yangu, mara moja wataniambia nisiwe natoka nyumbani ili niwe salama," anasema.

Amepoteza imani na taasisi za serikali.

"Wanaume wengi, wakiwemo maafisa wa polisi, hawaoni tatizo lolote katika unyanyasaji wa kingono. Kwa mtazamo wao, kama humnyanyasi mtu, basi wewe si mwanaume. Hivi ndivyo wanavyoona," anaongeza.

Wanawake wengi niliozungumza nao nchini Iraq hata waliwatuhumu polisi kwa kuwanyanyasa kingono. Nilimweleza tuhuma hizo Muqdad Miri, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq.

"Kesi za unyanyasaji zinazohusisha maafisa wa polisi hutokea, lakini ni chache sana. Wanaohusika hupewa adhabu kali sana, ikiwemo kifungo cha hadi miaka 10 jela, na hufukuzwa kazi," anasema Miri.

.
Maelezo ya picha, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Muqdad Miri, anasema baadhi ya matukio ya ukatili wa kingono hayaripotiwi kutokana na "jamii, mila na desturi."

Nilimweleza kuwa baadhi ya wanawake sasa wanarekodi na kuchapisha matukio ya unyanyasaji kwenye mitandao ya kijamii kwa sababu wanaogopa kuripoti polisi.

Alisema wanachapisha kwenye mitandao ya kijamii kwa sababu ni rahisi zaidi kuliko kuwasilisha malalamiko rasmi, na kwa sababu njia hiyo imekuwa maarufu katika kuvutia umakini wa watu kuhusu masuala mbalimbali.

Pia nilimweleza kuhusu tukio la Samira, ambaye anasema afisa mmoja wa polisi alimwambia kuwa hakuwa na mamlaka ya kumzuia mtu aliyekuwa akimnyanyasa.

Miri alisema Samira angeweza kuwasilisha malalamiko dhidi ya afisa huyo.

Hakuna takwimu za kuaminika kuhusu ukatili wa kingono au unyanyasaji wa kingono nchini Iraq.

Miri aliniambia kuwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu, polisi wamepokea takribani ripoti 300 za ukatili wa kingono. Hata hivyo, anakubali kuwa idadi halisi ya matukio ni kubwa zaidi.

"Kesi nyingi hazifiki kwa polisi kutokana na jamii, mila na desturi," anasema.

Simulizi za wanawake waliozungumza na BBC zinaonesha mapambano yao dhidi ya ukatili wa kingono wenyewe, lakini pia dhidi ya mitazamo na imani za kijamii zilizokita mizizi ambazo huruhusu ukatili huo kuendelea.

Edwar amekuwa akitetea haki za wanawake kwa zaidi ya miaka 50, lakini tathmini yake ni ya kukatisha tamaa.

"Miaka 23 baada ya utawala wa Saddam Hussein kuondolewa madarakani, inaonekana tunarudi nyuma katika suala la haki za wanawake," anasema.

Hata hivyo, yeye na Jassim wanasema hawatakata tamaa.

"Ikiwa sote tutaogopa, hakuna kitakachobadilika," anasema Sarah.

Habari hii imeandaliwa kwa msaada wa ziada wa taarifa kutoka kwa Salma Khattab.

Iwapo umeathiriwa na masuala yanayohusiana na unyanyasaji au ukatili wa kingono, unaweza kuzungumza na mtaalamu wa afya au shirika linalotoa msaada kwa wahanga.