Je, unataka kumiliki bunduki nchini Kenya? fuata masharti haya

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Asha Juma
- Nafasi, BBC, Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Nchini Kenya katika siku za hivi majuzi kumezuka mijadala mitandaoni kuhusu watu kumiliki silaha hasa baada ya kutokea mara kadhaa matukio ya watu mashuhuri kutakikana kurejesha silaha kwa sababu ya kuzitumia vibaya.
Lakini ni mchakato gani unaofuatwa hadi mtu anaruhusiwa kumiliki bunduki?.
Mtu anaweza kuhitaji kumiliki silaha kwa sababu ya usalama wake, michezo kama vile uwindaji ama ulengaji shabaha.
Sio kwamba kuna idadi ya bunduki ambayo mtu anaweza kumiliki kulingana na uwezo wake, la hasha, ukweli ni kwamba hakuna mtu anaruhusiwa kumiliki silaha zaidi ya moja.
Lakini pia ni muhimu kujua kwamba maafisa wa usalama nchini wapo kwa ajili ya usalama wa kila mmoja wetu.
Mahitaji ya kuweza kuomba umiliki wa silaha
- Lazima uwe na miaka 21 na zaidi
- Lazima awe amepata mafunzo ya kutumia silaha
- Usiwe na rekodi ya kufanya uhalifu
- Na mwenye akili timamu
Hata hivyo, kulingana na sheria, raia haruhusiwi kumiliki silaha inayotumiwa na maafisa wa usalama kwa mfano, AK47 au G3.
BBC Swahili imezungumza na mchambuzi wa masuala ya usalama kutoka nchini Kenya, George Musamali kutaka kujua zaidi kuhusu suala hili ambaye ameanza kwa kufafanua kuwa kipengele cha katiba cha 114 kinaangazia ni mwongozo gani unahitajika kufuatwa ili mwananchi wa kawaida aweze kumiliki silaha.
Mchakato ni upi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Lazima wewe kama mwananchi uonyeshe nia ya kutaka kumiliki silaha kwa kutuma maombi binafsi.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Maombi yako yatapelekwa hadi kitengo cha ofisi ya maafisa wanaosimamia utoaji wa leseni ya umiliki wa bunduki, mjini Nairobi.
Lazima upate kibali cha maadili mema yaani good conduct kutoka afisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), ukiwasilishe pamoja na maombi yako na kima fulani cha malipo.
‘’Lazima utoe sababu inayokufanya uhitaji kumiliki silaha, na mara nyingi, huwa ni ikiwa unaona maisha yako, yako hatarini na unahitaji ile silaha kuhakikisha usalama wako,’’ George Musamali alisema.
Kisha utachunguzwa na kuhojiwa na Huduma ya Taifa ya Ujasusi. Kama haitoshi, bado utahojiwa tena na Bodi ya utoaji Leseni ya Kumiliki silaha hiyo. Bodi hiyo inaweza kukubali au kutupilia mbali ombo lako.
Ikiwa bodi itaidhinisha ombi hilo, jina lako litatumwa kwa Inspekta Jenerali wa Polisi, ambaye pia naye, anaweza kuidhinisha au kukataa ombi hilo.
Ikiwa Inspekta Jenerali ataidhinisha ombi lako, Bodi ya Utoaji Leseni ya Umiliki wa Silaha itatoa leseni kwa aliyetuma maombi kwa kipindi cha mwaka mmoja na mmiliki atalazimika kuwasilisha maombi mengine kila baada ya mwaka mmoja.
Kufikia hapo, inamaanisha kuwa aliyetuma maombi ameonyesha sababu za kuridhisha kwamba kuna umuhimu wa yeye kupewa kibali cha kumiliki bunduki hiyo.
Ufuatiliaji wa silaha
Usichokifahamu ni kwamba unapokabidhiwa silaha sio mwisho wako wa kuwa na mawasiliano na serikali. Kuna utaratibu wa kufuatilia silaha hiyo.
‘’Ni lazima uwe unapeleka ile silaha katika kituo kilicho karibu na wewe mara moja kila mwezi,’’ George Musamali anaelezea.
Madhumuni ya kufanya hivyo, ni kuhakikisha kuwa kamanda wa kituo cha polisi, anathibitisha kuwa ile silaha uliopewa iko salama na kwamba risasi bado hazijatumika.
‘’Ikiwa utatumia risasi kwa sababu yoyote, ni lazima uripoti kwa kituo cha polisi kilicho karibu na wewe na uelezee ulitumia risasi hiyo kivipi, na pia kuhakikisha kuwa uliitumia kwa mujibu wa sheria,’’ Musamali anasema.
Kwanini ombi hilo linaweza kukataliwa
Sababu nyingi zinaweza kuchangia ombi la kutaka kumiliki silaha kutupiliwa mbali. Kwa mfano:
- Ikiwa itathibitishwa kuwa aliyeomba hana akili timamu.
- Pengine ni mtu mwenye hasira
- Hawezi kuweka salama au kuitunza kwa uangalifu mkubwa.
Kupokonywa silaha unayomiliki
Pia, kulingana na mchambuzi wa masuala ya kisiasa George Musamali, unaweza kupokonywa silaha ikiwa itathibitishwa kwamba ulitumia silaha vibaya, kwa mfano, ‘’kuzusha vurugu kwenye maeneo ya umma,’’au ikiwa unatumia silaha kumjeruhi mwingine ambaye kisheria hukustahili kuitumia.’’
Aidha, ikiwa utaiweka vibaya kiasi cha kuhatarisha maisha ya wengine, kuondoa nambari ya usajili ya silaha hiyo, kushindwa kukidhi tena vigezo vya kukata leseni mpya kila mwaka kama inavyohitajika, ikiwa aliyemiliki silaha amethibitishwa kuwa tishio kwa umma ama amani.
Ikifikia kiwango hicho, mtu hupokonywa silaha hiyo kwa kukosa kutimiza na kushindwa kufuata kanuni zilizowekwa.
Lakini pia ikafikia kiwango unapokonywa silaha, bado utakuwa na fursa ya kutuma maombi kwa Inspekta Jenerali ili kesi yako iliyosababisha hatua hiyo iweze kupitiwa tena.
Hata hivyo, kulingana na Musamali, changamoto kubwa inayokumba suala hili kwa hivi sasa ni kuingia kwa ufisadi na siasa kwenye mchakato na suala zima la utoaji na umiliki wa silaha.















