Jinsi kukoroma kunaweza kuathiri uhusiano

Chanzo cha picha, Getty Images
"Nilikuwa na wasiwasi kwamba ikiwa ningezungumza na mume wangu kuhusu hili, angeudhika."
Alifikiri kukoroma ni sehemu ya kifurushi kinachokuja na ndoa. Lakini ilikuwa ikimuumiza mumewe, na uhusiano wao.
"Alianza kuamka sana wakati wa usiku na akawa na huzuni asubuhi," aliambia BBC.
Kukoroma kwa mume wake pia kulimzuia kupata raha ya usiku, na utendaji wake kazini ukadorora kutokana na kukosa usingizi.
Ni jambo la kawaida sana kupuuza mwenza anayekoroma anapolala, lakini wataalam wa afya na uhusiano wanaonya kuwa inaweza kuwa na athari kubwa kwa afya ya wenzi wao na uhusiano wao.
Apnoea ya kulala ni nini?
Kukoroma kwa sauti kubwa mara nyingi huhusishwa na ugonjwa wa kulala unaojulikana kama apnea ya kuzuia usingizi (OSA), hali ambayo kupumua hukoma na kuanza kurudia wakati wa kulala, wataalam wanasema.
Ugonjwa huo husababisha kuta za koo kupumzika na nyembamba, kukatiza kupumua kwa kawaida na kusababisha upungufu wa oksijeni.

Kulingana na Dk Ramamurthy Sathyamurthy, daktari mshauri wa kupumua katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha James Cook cha Uingereza, dalili za apnea zinaweza kutofautiana, kuanzia upole hadi wastani au kali, lakini kwa kawaida huwa mbaya zaidi.
Alionya kuwa hali hiyo isiyotibiwa inaweza kuathiri mambo mengi ya mkoromaji na afya ya kimwili na kiakili ya wenzi wao, ikiwa ni pamoja na hamu yao ya tendo.
Je, dalili za apnoea ya kulala ni zipi?
Dalili hutokea hasa unapolala, na ni pamoja na:
- Kukoroma kwa sauti
- Kupumua kuacha na kuanza
- Kufanya miguno, kukoroma, au kelele za kukaba
- Kuamka mara kwa mara
Wakati wa mchana, wagonjwa wanaweza pia:
- Kuumwa na kichwa wanapoamka
- Kujisikia uchovu sana
- Kupata ni vigumu kuzingatia
- Kuwa na kumbukumbu mbaya
- Kuhisi huzuni, kukasirika au kupata mabadiliko mengine ya hisia
- Uzoefu wa uratibu duni
- Kupoteza hamu ya tendo
Maswala mengine ya kiafya
Zaidi ya hayo, apnoea ya kuzuia usingizi inaweza kusababisha masuala mengine ya afya pia.
Kushuka ghafla kwa viwango vya oksijeni ya damu ambayo hutokea wakati wa apnea inaweza kuongeza shinikizo la damu, wataalam wanaonya, na hii inaweza kuongeza hatari ya masuala kadhaa ya matibabu yanayohusiana.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ingawa baadhi ya wanandoa wanaweza kuona kukoroma kwa wapenzi wao ni jambo la kuchekesha, linaweza kuwa jambo zito kwa uhusiano wao, Dk Sathyamurthy alisisitiza.
"Kwa kawaida, aslimia 90 ya wagonjwa ninaowaona, rufaa imeanzishwa kwa sababu mshirika ameathirika pakubwa," aliambia BBC.
Inaweza kusababisha wenzi kuanza kulala katika vyumba tofauti, dhana inayojulikana kama 'talaka ya kulala'.
Hili si lazima liwe jambo baya - mtaalamu wa masuala ya uhusiano wa Marekani Sara Nasserzadeh mara nyingi anapendekeza wapenzi walale peke yao, kwa kukoroma au bila kukoroma. Kuanzia siku kwa kulala vizuri kunaweza kukuza uhusiano mzuri kwa wenzi wote wawili, aliiambia BBC, ingawa bila shaka hii inawezekana tu ikiwa chumba cha kulala cha ziada kinapatikana.
Lakini kwa wanandoa wengine, 'talaka ya usingizi' inaweza kuwa hatua ya kwanza kwenye njia ya kutengana kwa kudumu zaidi.
Kuzungumzia mada
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hata ingawa Arunika Selvam anaishi Singapore - nchi iliyostawi sana na mojawapo ya Pato la Taifa la juu zaidi kwa kila mtu duniani - kupata kitanda mahali pengine ndani ya nyumba si jambo linalowezekana kwake.
"Ilitubidi kukodisha chumba chetu cha wageni ili kupata mapato ya ziada kutokana na gharama kubwa ya maisha hapa Singapore," mama wa mtoto mmoja, ambaye ameolewa kwa miaka 15, alieleza.
Hata hivyo, baada ya kukosa usingizi usiku mwingi, Selvam alizungumza na mume wake kuhusu tatizo lake la kukoroma.
Hakutaka kushauriana na daktari kwani baba yake na babu yake walikoroma na aliamini ni jambo la kawaida kabisa.
Kukoroma kwa sauti kubwa kwa wanaume mara nyingi huchukuliwa kuwa sehemu ya uanaume, hasa katika tamaduni fulani za Asia, Selvam aliongeza.
Sara Nasserzadeh alisema katika hali kama hizi, ni muhimu kupata wakati mwafaka wa kuzungumzia suala hili na mshirika wako kwa "njia ya hila na maridadi".
"Labda, baada ya kufanya ngono, labda baada ya kuwa katika hali nzuri na kushikamana," Nasserzadeh, mwandishi wa Love by Design - 6 Ingredients to Build a Lifetime of Love, aliongeza.
Mtaalamu huyo wa saikolojia ya kijamii alisema ni muhimu pia kukumbuka kuwa mtu anayekoroma mara nyingi huona aibu kuhusu hali hiyo.
Madhara makubwa
Kulingana na Jumuiya ya Uingereza ya Kukoroma na Kupumua Usingizi, kuna takriban watu milioni 15 wanaokoroma nchini Uingereza, na huathiri watu milioni 30 nchini humo - karibu nusu ya watu wote.
Takwimu kutoka kwa uchunguzi wa hivi majuzi zinaonyesha kuwa idadi ya wanaume wanaokoroma ni kubwa zaidi kuliko wanawake, chama hicho kilisema.
Lakini bila kujali ni nani anakoroma, zoea hilo linaweza kuwa na matokeo makubwa.
Baadhi ya ripoti zinaonyesha kukoroma kuwa miongoni mwa sababu za kawaida za talaka nchini Marekani na Uingereza, ingawa ni vigumu kupata data halisi ya kuunga mkono dai hilo.
Unaweza kufanya nini kuhusu kukoroma au kukosa usingizi?
Matibabu ya apnoea ya usingizi inaweza kuhusisha kupitisha mabadiliko ya mtindo wa maisha kama vile:
- Kupungua uzito
- Kuacha kuvuta sigara
- Kupunguza unywaji wa pombe

Chanzo cha picha, Getty Images
Hata hivyo, kwa watu wengi, matumizi ya kifaa kinachojulikana kama CPAP (Shinikizo linaloendelea la njia ya hewa) ni muhimu.
Hutoa hewa kwa upole kwenye barakoa unayovaa mdomoni au puani unapolala.
Dk Ramamurthy Sathyamurthy alisema ni muhimu kuweka kipaumbele kwa afya ya mwenzi na mkoromaji, na kuwahimiza kutafuta ushauri wa matibabu.
"Itakuwa na manufaa sio tu kwa uhusiano bali pia kiuchumi, kwani watu watatumia pesa kidogo kununua dawa kwa maswala mengine ya kiafya yanayosababishwa na hali hiyo. Kwa hivyo, ni faida ya jumla kwa familia nzima," aliongeza.
Vikwazo vya kiuchumi, kijamii na kitamaduni
Mitazamo kuhusu kukoroma inaweza kutofautiana kimataifa na kibinafsi, ikiathiriwa na mambo ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni, na hata jinsia na ujinsia.
Saman (si jina lake halisi), shoga mwenye umri wa miaka 40 ambaye anafanya kazi kama mpokeaji wageni wa hoteli huko Colombo, Sri Lanka, huweka ngono yake kuwa siri kutoka kwa familia yake. Wanaamini kuwa mpenzi wake ni rafiki tu anayekodisha chumba cha ziada katika nyumba yake.
"Mpenzi wangu anakoroma kwa sauti ya juu, na siwezi kulala kwa sababu ya kukoroma kwake. Mimi hupata usingizi mzuri tu mama yangu anaponitembelea," Saman aliambia BBC.
"Kwa siku hizo, mwenzangu kwa hiari yake anampa mama yangu chumba cha ziada, na kumfanya aamini kuwa ni chumba chake, wakati yeye analala kwenye sofa," alisema.
"Huo ndio wakati pekee ambao ninaweza kupata usingizi mzuri."
"Mpenzi wangu anajiona ni shoga mwenye sifa za kike, lakini kukoroma kunachukuliwa kuwa ni kitu cha kiume katika tamaduni zetu. Ninahofia kuwa kujadili suala hili kunaweza kumuumiza na kupelekea kuniacha," aliongeza.
Imetafsiriwa na Jason Nyakundi












