Silaha au kujiondoa kwanza, ni uamuzi upi umesalia kwa Hezbollah?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 8

Hezbollah inakabiliwa na mtihani mgumu zaidi wa kisiasa na kijeshi katika kipindi cha miaka mingi.

Kufuatia hasara iliyopata katika uongozi na mfumo wake wa kijeshi, swali si tena jinsi ya kuijibu Israel pekee, bali pia ni nani atakayefanya mazungumzo kwa niaba ya Lebanon, na iwapo chama hicho kinaweza kuhifadhi silaha na nafasi yake ya kijeshi katika mazingira ya mchakato wa amani unaoongozwa na serikali ya Lebanon na kufadhiliwa na Marekani,mchakato ambao chama hicho kinaupinga.

Uamuzi uliopo kwa Hezbolla ni tatu kuu:

kusubiri makubaliano kati ya Iran na Marekani yatakayojumuisha Lebanon, kukubaliana na mpango unaofadhiliwa na Washington kati ya Lebanon na Israel ambao ungesababisha kupelekwa kwa jeshi la Lebanon na kutolewa silaha, au kurejea kwenye mzozo wa kijeshi wenye hatari zote zinazoambatana na hatua hiyo kwa maeneo ya Kusini, Beirut, vitongoji vya kusini, na wafuasi wake.

Hakuna uamuzi unaoonekana kutokuwa na gharama au madhara makubwa.

Chama hiki kimefika vipi hapa?

Mnamo Machi 2, Hezbollah ilitangaza kuingia katika makabiliano ya kikanda kufuatia shambulio la Marekani na Israeli dhidi ya Iran, ikisema kuwa mashambulio yake yalitokana na mauaji ya Kiongozi Mkuu wa Irani Ali Khamenei na ukiukaji wa Israeli wa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyokamilika Novemba 2014.

Lakini hesabu za chama hazikuwa za kijeshi tu. Ripoti zilionyesha kuwa pia ilibahatisha kuhusu kuhusika kwake katika makabiliano hayo kungesababisha Lebanon kujumuishwa katika suluhu lolote kati ya Iran na Marekani, na hivyo kutoa hakikisho la kusitishwa kwa mashambulizi, mauaji na ubomoaji wa nyumba, na kuondolewa kwa majeshi ya Israel kutoka kusini mwa Lebanon.

Tangu wakati huo, zaidi ya makubaliano ya kusitisha mapigano yametangazwa, lakini hakuna hata mmoja kati yao ambaye amemaliza operesheni za Israel upande wa kusini au kuweza kujiondoa kabisa.

Hili ndilo tatizo la msingi: Iran inataka kuihusisha Lebanon katika mazungumzo yake na Washington, huku serikali ya Lebanon ikisisitiza kuwa ni serikali yake pekee inayoweza kujadiliana kuhusu eneo lake, silaha na mipaka yake.

Njia ya mazungumzo na Iran

Msimamo wa Hezbollah wa kuwa na matumaini katika mfumo wa Iran uliimarika baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran kuanza kutekelezwa tarehe 8 Aprili, na pande hizo mbili kukubaliana kufanya mazungumzo mjini Islamabad.

lakini kutokubaliana kuliibuka tangu mwanzo kuhusu Lebanon. Iran ilisema kusitisha mapigano kunapaswa kujumuisha pande zote, ikiwa ni pamoja na upande wa Lebanon, huku Marekani na Israeli zikiichukulia Lebanon kuwa si sehemu ya makubaliano.

Saa chache baada ya kusitisha mapigano kuanza, jeshi la Israeli lilizindua mashambulizi zaidi ya 100 ya anga katika muda wa takriban dakika kumi huko Beirut, vitongoji vyake vya kusini, Bonde la Bekaa, na maeneo kusini mwa Lebanon. Kulingana na mamlaka ya Lebanon, mashambulizi hayo yaliwaua mamia na kuwajeruhi zaidi ya watu 1,000.

Jeshi la Israeli lilisema kwamba lililenga vituo vya Hezbollah, makazi, na makamanda.

Kisha Tehran ilihusisha ushiriki wake katika mazungumzo hayo na kusimamishwa kwa shughuli za Israeli nchini Lebanon, na dhamana ya kusitisha mapigano ya kudumu kama sharti la kufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz. Mashambulizi ya anga huko Beirut na vitongoji vyake yalikoma kwa muda kufuatia kuingilia kati kwa Rais wa Marekani Donald Trump, lakini yaliendelea kusini.

Hezbollah ilianza tena mashambulizi yake, ikisema yalikuwa ni kujibu ukiukwaji wa Israel. Hata hivyo, ilibaki imejitolea kwa suluhu ya kikanda, ikisema imepokea uhakikisho kwamba makubaliano yoyote kati ya Tehran na Washington yangejumuisha kukomesha uhasama nchini Lebanon.

Lakini hatua hii ya kubahatisha bado haijaishinikizaa Israeli kujiondoa au kusitisha kwa ubomoaji na mashambulizi ya mabomu. Kadri mazungumzo yanavyoendelea, kusubiri kumekuwa ghali: uharibifu zaidi, kurudi kwa wakazi kumesitishwa, na shinikizo linaloongezeka kwa chama ndani ya kambi yake maarufu.

Uwezo wa kuzuia mashambulizi unapungua

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Hezbollah, Hassan Nasrallah, alizungumzia mara kwa mara uwezo uliotegemea kukabiliana na mashambulizi ya mabomu katika vitongoji vya kusini mwa Beirut kwa kulenga Tel Aviv. Hata hivyo, uwezo wa chama hicho kutekeleza kukabiliana huko kulipungua baada ya vita vya mwaka 2014.

Chama hicho kilipoteza idadi kubwa ya viongozi wake wa kijeshi, akiwemo Nasrallah na Hashem Safieddine, ambaye alichaguliwa kumrithi lakini akauawa kabla ya kuapishwa rasmi. Miundombinu yake ya kijeshi pia iliharibiwa vibaya, ikiwemo maeneo ya kurushia makombora na ghala za silaha, kulingana na taarifa kutoka kwa maafisa wa chama hicho.

Katika awamu ya hivi karibuni, uwezo mpya wa kijeshi ulijitokeza,mashambulizi ya mabomu dhidi ya Beirut na vitongoji vyake yalisitishwa kwa sharti la Hezbollah kutorusha makombora na ndege zisizo na rubani kuvuka mpaka, huku ikiendeleza operesheni zake dhidi ya vikosi vya Israel ndani ya kusini mwa Lebanon.

Kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano ya mwezi Aprili, operesheni nyingi za Hezbollah zililenga vikosi vya Israel ndani ya kusini mwa Lebanon,hasa kwa kutumia ndege zisizo na rubani zenye masafa mafupi kulenga askari, magari, na ngome za kijeshi, pamoja na roketi na mizinga,huku mashambulizi yake ya kuvuka mpaka kuelekea kaskazini mwa Israel yakipungua.

Hali hii iliendelea hadi makubaliano ya kusitisha mapigano ya mwezi Juni, ambayo yalifuatiwa na kupungua kwa kasi kwa operesheni hizo.

Uwezo huo wa kuzuia ulivipa vitongoji vya kusini kipindi cha utulivu, lakini ulipunguza wigo wa Hezbollah kuchukua hatua za kijeshi. Ingawa iliweza kuendelea kuweka shinikizo kwa vikosi vya Israel kusini, ilikabiliwa na hatari ya mashambulizi mapya ya anga dhidi ya Beirut, vitongoji vya kusini, na pengine maeneo mengine, iwapo ingepanua operesheni zake hadi ndani ya Israel.

Aidha, kuendesha mapambano ya muda mrefu kama yale yaliyotangulia kuondoka kwa majeshi ya Israel mwaka 2000 inaonekana kuwa vigumu zaidi leo. Jiografia ya eneo la kusini imebadilika kutokana na uharibifu na kuhama kwa watu, wigo wa udhibiti wa Israel umepanuka, na uwezo wake wa ufuatiliaji wa anga na wa kielektroniki pamoja na kupenya katika mifumo ya usalama umeimarika zaidi.

Mazungumzo ya Washington

Wakati wakiendelea kuangazia ukakamavu wa Iran, serikali ya Lebanon ilifungua mfumo tofauti uliofadhiliwa na Marekani na Israel. Ilishikilia kuwa ni jimbo pekee lililoidhinishwa kufanya mazungumzo kwa niaba ya Lebanon, na kukataa kuhusisha hatima ya nchi hiyo na mazungumzo kati ya Tehran na Washington.

Njia hii ilipelekea kufikiwa kwa mfumo ulioweka masharti ya kuondoka taratibu kwa Israel kutoka maeneo ya kusini, kupelekwa kwa jeshi la Lebanon katika maeneo hayo, na kupokonywa silaha kwa Hezbollah katika maeneo ya majaribio kabla ya kupanua operesheni.

Hezbollah inakataa makubaliano hayo, ikisema kwamba inaweka silaha zake mezani kwa ajili ya majadiliano kabla ya Israel kujiondoa kabisa. Hata hivyo, serikali imeanza kutekeleza hilo, na jeshi la Lebanon liliingia katika mji wa Zawtar al-Gharbiya baada ya majeshi ya Israel kuondoka, ikiwa ni mtihani wa kwanza wa kivitendo wa makubaliano hayo.

Mamlaka ya Lebanon iliwasilisha hatua hii kama dhibitisho kwamba mazungumzo kwa niaba ya serikali yanaweza kufikia uondoaji wa taratibu na kurudi. Hata hivyo, makubaliano hayo hayakusababisha kusitishwa kabisa kwa operesheni za Israel, na Israel inaendelea kuhusisha kukamilika kwa uondoaji wake na kupokonywa silaha kwa Hezbollah.

Hapa ndipo penye mtanziko mkubwa wa chama: kukataa makubaliano hayo kunahifadhi msimamo wake kuhusu silaha, lakini kunaweza kuuweka kinyume na mbinu inayofadhiliwa na serikali ambayo inaruhusu baadhi ya wakazi kurejea makwao. Kuikubali, kwa upande mwingine, kunaweza kufungua njia ya kujiondoa na kujenga upya taratibu, lakini kunatishia jukumu la kijeshi ambalo chama kimedumisha kwa miongo kadhaa.

Lipi la kwanza,Silaha kujiondoa?

Israel inasema haitajiondoa kikamilifu kabla ya Hezbollah kutolewa silaha, jeshi la Lebanon kupelekwa eneo hilo, na kuondolewa kwa kile inachokiona kuwa tishio kwa mpaka wake wa kaskazini.

Kwa upande mwingine, Hezbollah inakataa kujadili hatima ya silaha zake kabla ya mashambulizi ya Israel kusitishwa, Israel kujiondoa kikamilifu, na watu waliokimbia makazi yao kurejea. Katibu Mkuu wake, Naim Qassem, anasisitiza kuendeleza operesheni za kijeshi hadi pale kujiondoa huko kutakapofanyika.

Hata hivyo, mzozo huu hauko tena kati ya chama hicho na Israel pekee. Serikali ya Lebanon imepitisha sera ya kudhibiti silaha ili ziwe mikononi mwa serikali pekee, na imepiga marufuku shughuli za kijeshi na kiusalama za Hezbollah, bila kupiga marufuku chama hicho chenyewe kama shirika la kisiasa.

Hii ina maana kwamba suala la silaha limebadilika kutoka kuwa dai lililotolewa na wapinzani wa chama hicho na kuwa sera rasmi iliyopitishwa na serikali.

Je, ni uamuzi upi halisi uliopo?

Uamuzi wa kwanza ni kuendelea kusubiri makubaliano kati ya Iran na Marekani. Hili linaweza kuipa Hezbollah fursa ya kufanikisha uondoaji wa majeshi ya Israel bila kutoa masharti au makubaliano ya moja kwa moja kuhusu silaha zake, lakini muda na matokeo ya makubaliano kama hayo bado hayajulikani wazi.

Chaguo la pili ni kufuata mkakati unaoongozwa na serikali. Hili linaweza kuruhusu uondoaji wa taratibu wa majeshi ya Israel, kupelekwa kwa jeshi la taifa, na kuanza kwa ujenzi mpya, lakini lingeweka mustakabali wa silaha za Hezbollah na mrengo wake wa kijeshi katika kiini cha mazungumzo hayo.

Chaguo la tatu bado lipo: kurejea katika hali ya kuongezeka kwa uhasama. Hili linaweza kukipa chama hicho nguvu ya ziada dhidi ya Israel, lakini linahatarisha kutanuka tena kwa vita na kurejesha mashambulizi ya mabomu dhidi ya Beirut na vitongoji vyake vya kusini. Pia linakiweka chama hicho katika hatari ya kukabiliwa na shutuma kutoka kwa wapinzani wake kwamba kinaendesha vita vinavyoendana na vipaumbele vya Iran.

Hezbollah inasisitiza kuwa ushirikiano wake na Iran haimaanishi kuwa Tehran ndiyo huamua maamuzi yake, na kwamba hatua zake zinatokana na nia ya kuilinda Lebanon. Hata hivyo, kuendelea kuhusishwa kwa uwanja wa mapigano wa Lebanon na mazungumzo kati ya Iran na Marekani kunafanya shutuma hiyo iendelee kuwepo katika mijadala ya ndani.

Maamuzi haya hayawezi kutenganishwa na hali halisi ya mambo uwanjani. Uwezo wa jeshi la Israel wa kufuatilia na kuchunguza mambo umeimarika,kuanzia matumizi ya ndege zisizo na rubani, hadi udukuzi wa kielektroniki, na jiografia ya eneo la kusini imebadilika kutokana na vita, jambo ambalo linaweza kuilazimu Hezbollah kubadili mbinu zake iwapo itaamua kuendeleza mapambano ya kijeshi.

Mahesabu ya chama hicho hayazuiliwi tu na uwezo wake wa kijeshi. Pia kinakabiliwa na changamoto ya kudumisha uungwaji mkono kutoka kwa wafuasi wake, ikizingatiwa kuendelea kwa hali ya wakazi wengi kuhama makazi yao kutoka kusini na vitongoji vya kusini, pamoja na kutokuwepo kwa ratiba wazi ya kurejea, ujenzi mpya, na malipo ya fidia.

Changamoto hizi zitaendelea kuwepo hata kama Iran na Hezbollah zitafanikiwa kufanikisha usitishaji wa mapigano wa kina na uondoaji kamili wa majeshi ya Israel kutoka kusini mwa Lebanon.

Hezbollah bado itakabiliwa na migawanyiko ya ndani kuhusu hatima ya silaha zake na nafasi yake ya kijeshi, kufuatia maamuzi ya serikali ya kudhibiti umiliki wa silaha mikononi mwa dola pekee na kupiga marufuku shughuli zake za kijeshi na kiusalama. Hali hii inajitokeza huku kukiwa na kutokubaliana kuhusu nani anayewajibika kwa kuzuka kwa vita na jinsi ya kushughulikia suala la silaha bila kusababisha mzozo wa ndani.