WARIDI WA BBC: Safari ya Judy akitafuta mafanikio Marekani

Chanzo cha picha, Judy Maina
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Kwa baadhi ya watu kutoka bara Afrika , wana maoni kuwa mojawapo ya njia rahisi ya kufanikiwa maishani ni kuishi nchi za Ulaya pia Marekani.
Bilashaka kwenye vyombo vya habari na kwenye mitandao kuna simulizi kuhusu jinsi watu walivyohatarisha maisha yao, wengine hawakunusurika wakivuka bahari mediterrania au bahari nyingine kuingia nchi za Ulaya.
Je ni kipi husukuma watu kuwaza hivyo?
Na kwa hiyo simulizi yake Judy Maina ambaye ni mkazi wa Seattle nchini Marekani japo haijazingirwa na hali ya kuhatarisha maisha yake ili aishi Marekani yeye anakiri kuwa hapo awali alikuwa na ndoto na maono kuwa ili afanikiwe na aiishi maisha ya juu mno ni lazima angeishi na kufanya kazi Marekani .
Aidha anasema kuwa alidhani kuwa wakati angefika marekani hivi pesa na mali vingemmiminikia kama mvua bila kujua kuwa barabara ya kufanikiwa ilijaa panda-shuka .
Mojawapo ya azma zake kuu ilikuwa jinsi angesafiri nchi ambayo wengi wanaifahamu kama ya ‘asali na maziwa’.
”Nilipowasili Marekani baada ya kupata mwaliko , akilini mwangu nilikuwa nafikiria kuwa , itakuwa rahisi kufikia makuu, nisijue kuwa ingekuwa safari ya kunipa mafunzo tele ya maisha katika nchi ya kigeni ” anakumbuka Judy.
Ndoto ya kuishi na kufanya kazi Marekani , mwanadada huyu anasema ilianza zamani akiwa msichana mdogo , anasema kuwa anakumbuka akimueleza mama yake kuwa siku mmoja angeishi na kufanya kazi huko.
Mwanadada huyu anasema kuwa kwa wengi ambao walikuwa wandani wake akiwa binti waliwaona watu wa rangi nyeusi waliokuwa Marekani kama waliofanikiwa .
Mwanamke huyu anaongeza kuwa mawazo yake yalitokana na kwamba alikuwa anawaona hasa Wakenya ambao alikuwa anawafahamu, waliokuwa wanaishi na kufanya kazi Marekani au nchi za Ulaya walionekana kuwa na maisha ya juu, na maisha ya kufanikiwa.
Nyuma ya pazia hilo hakujua kuwa kufikia hadhi ya kuishi kwa mfano Marekani ni mahAngaiko makubwa weka kando kupata ajira.
Changamoto za kuishi Marekani
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwaka jana Judy aliwasili Marekani hakufahamu kuwa ingebidi aishi katika makazi ya watu wengine , hii ni kutokana na sheria za nchi hiyo zinazotaka mtu kwanza ajiandikishe na kupata nambari spesheli ambayo inamsaidia kupata ajira , kusajiliwa kwenye laini ya simu , kupata huduma kwenye benki ,na hata kukodi au kununua nyumba kumaanisha kila kitu ambacho mtu anatamani kufanya kilikuwa kinategemea iwapo unanambari hio maalumu, akiitaja kama SSN.
Kwa miezi sita kabla ya kupata nambari ya usajili ilibidi aishi kwa rafiki mmoja ambaye anasema kuwa baada ya muda alijikuta ametupwa nje asijue wa kumgeukia , kipindi hicho Judy anasema kuwa aliyemsitiri ni shangazi wake ambaye alimkodisha chumba kidogo ndani ya nyumba yake kabla hajapata uhuru wa kufanya kazi na kuishi peke yake .
Mwanamke huyu alikuwa amesomea uuguzi akiwa nchini Kenya na pia alikuwa ameajiriwa kwenye hospitali mmoja kuu ya kimatifa nchini Kenya , japo anasema alipata mshahara wa wastani katika uchunguzi wake aligundua kuwa wauguzi kutoka nchi za Marekani na Ulaya walikuwa wanapata mishahara mikubwa zaidi .

Chanzo cha picha, Judy Maina

Chanzo cha picha, Judy Maina
Kabla hajasajiliwa rasmi na kupata kibali cha kufanya kazi Judy alikuwa anawahudumia wagonjwa ambao wanaishi na magonjwa ya muda mrefu , au wagonjwa ambao hawana nguvu ya kujihudumia .
''Ajira ya kwanza ambayo nilifanikiwa kupata , ilikuwa ni kuwahudumia wagonjwa katika nyumba za wazee na hata kwenye makao ya watu , hawa ni watu ambao hawana uwezo wakujifanyia chochote kutokana na makali ya magonjwa ”anasema Judy.
Anasema kuwa kazi hii ilimuwezesha kumudu maisha .
Judy Maina alipokuwa anaamua kusafiri kuelekea Marekani alikuwa ameacha mume na watoto wake wawili , kulingana naye walikuwa na maelewano kuwa kama jamii watatafuta njia ya kuishi kama jamii Marekani.
Judy ametangulia japo anasema kuwa changamoto ya hapo awali kabla hajapata nyaraka rasmi vya kumruhusu aondoke nchi ya Marekani na kurudi alikaa kwa muda mrefu bila kuwaona watoto wake na mume wake ,Hivi majuzi mwanadada huyu alitembelea jamii yake ambayo kwa sasa wanaishi nchini Tanzania ambako mume wake anahudumu kikazi
”Ndoto yangu ni kuwa mwishoni mwa mwaka huu familia yangu yote itaungana nami huku ninajizajititi na kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha kuwa jamii yangu itafurahia maisha ya Marekani ”anasema Judy.
Kwa sasa Judy anafanya kazi ya uuguzi katika baadhi ya hospitali zilizopo jimbo la Washington Marekani. Hatimaye anasema kuwa ndoto yake imeanza kuchukua sura aliyokuwa anaitazamia maisha ambayo hana mahangaiko.
Ila anatoa nasaha hasa kwa vijana kutokimbilia kuishi maisha ya Ulaya au Marekani kwani kwa sasa teknolojia imetoa utandawazi mkubwa ambao umefanya dunia iwe kijiji na kwa hiyo nafasi za ajira na kujiari zinapatikana angalau kwa wepesi hasa kwa wale wanakuwa na shauku ya teknolojia.












