Ndani ya gereza maarufu la Atlanta ambalo Trump atazuiliwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika siku zijazo, Donald Trump atajisalimisha kwa polisi huko Georgia. Majadiliano yake ya awali na mfumo wa haki ya jinai ya eneo hilo yanatarajiwa kudumu kwa saa chache, Hatahivyo washtakiwa wengine wengi wamekuwa hawana bahati.
Mamlaka ilitangaza Jumatano kwamba Bw Trump na washtakiwa wenzake 18 "wanatarajiwa" kuzuiliwa katika jela ya Fulton County huko Atlanta kabla ya kufikishwa katika mahakama hiyo, ingawa walionya "hali huenda zikabadilika".
Ni lazima afike tarehe 25 Agosti kujibu mashtaka ya kujaribu kutengua matokeo ya uchaguzi wa 2020 katika jimbo hilo.
Kiongozi wa eneo hilo, Pat Labat, amesema maafisa watafuata "muongozo wa kawaida" wakati wa kumshughulikia Bw Trump.
Lakini wataalam walisema pengine atakuwa na mazoea tofauti sana na wale wanaohudumu katika jela ya kaunti hiyo inayojulikana kuwa si salama kwa wiki, miezi au hata miaka wakisubiri kesi zao.
Nchini Marekani, washtakiwa wa uhalifu husubiri jela iwapo wamekamaatwa , wanasubiri kusikilizwa kwa kesi bila dhamana, au wanatumikia kifungo kifupi gerezani. Magereza ni mahali ambapo wahalifu hutumikia vifungo virefu zaidi baada ya kupatikana na hatia.
Mamia ya watu walizuiliwa katika Jela ya Kaunti ya Fulton kwa zaidi ya siku 90 kwa sababu walikuwa bado hawajafunguliwa mashtaka rasmi au hawakuwa na uwezo wa kulipa dhamana inayohitajika ili kuachiliwa kwao, kulingana na ripoti ya Septemba 2022 kutoka Muungano wa Uhuru wa Kiraia wa Marekani (ACLU). )
Ripoti hiyo pia iligundua watu 117 walikuwa wamekaa jela kwa zaidi ya mwaka mmoja kwa sababu hawakufunguliwa mashtaka; 12 walikuwa wameshikiliwa kwa miaka miwili kwa sababu hiyo hiyo.
"Kimsingi imejaa watu wengi tangu ilipojengwa," Fallon McClure wa ACLU ya Georgia alisema. "Hili limekuwa jambo la kawaida mara kwa mara kwa miaka."
Mazingira yanayoendelea ‘kuzorota kwa kasi’
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ilijengwa mnamo 1985 kuwahifadhi wafungwa 1,300, Jela ya Kaunti ya Fulton inawazuilia zaidi ya watu 3,000 katika miaka ya hivi karibuni.
Jela hiyo inatoa "Mazingira machafu" ambayo yamesababisha milipuko wa Covid-19, chawa na upele, ripoti ya Kituo cha Kusini cha Haki za Kibinadamu ilisema. Iligundua wafungwa "walikuwa na utapiamlo" na kushughulika na hali inayoitwa cachexia, pia inajulikana kama hali ya kupotea.
Kusubiri katika mazingira haya duni kumethibitika kuwa hatari kwa wengine.
Wiki iliyopita, mwanamume mwenye umri wa miaka 34 alipatikana akiwa amepoteza fahamu katika seli ya kitengo cha matibabu katika jela hiyo, ambapo alikuwa amefungwa tangu 2019.
Alifufuliwa, lakini kisha akafa hospitalini, kulingana na ofisi ya Sheriff wa Kaunti ya Fulton.
Alikuwa mtu wa sita mwaka huu kufariki katika jela hiyo mwaka wa 2023.
Noni Battiste-Kosoko alikuwa na umri wa miaka 19 pekee alipofariki akiwa kizuizini katika Jela ya Kaunti ya Fulton mnamo Julai baada ya kukamatwa kwa shtaka la makosa madogo.
Manaibu walimpata hana fahamu katika seli yake katika Kituo cha Kizuizi cha Jiji la Atlanta, nafasi ya ziada ambayo kaunti inakodisha ili kupunguza msongamano katika jela kuu.
Familia ya Battiste-Kosoko bado haijapewa sababu za kifo chake au kupata matokeo ya uchunguzi wa maiti yake, wakili wa familia yake aliambia BBC.
"Kumekuwa na mtindo thabiti na usio na utulivu wa huduma duni za afya na wafungwa kufia jela katika mazingira ya kutatanisha," alisema Roderick Edmond.
Ofisi ya Sheriff ya Kaunti ya Fulton iliambia BBC kuwa bado inasubiri ripoti ya mwisho kutoka kwa uchunguzi wa maiti, na kwamba inachunguza tukio hilo.
Kifo cha Battiste-Kosoko kilijiri muda mfupi kabla ya Kaunti ya Fulton mwezi huu kukubali kulipa $4m (£3.1m) kwa familia ya mwanamume aliyefariki katika jela hiyo huku mwili wake ukiwa umeumwa na kunguni .
Uchunguzi wa kujitegemea wa maiti ulipata Lashawn Thompson mwenye umri wa miaka 35 alikufa katika kitengo cha magonjwa ya akili cha jela Septemba iliyopita kwa sababu ya "kutelekezwa sana" na wafanyikazi wa jela.
Kifo chake kilisababisha uchunguzi kutoka kwa Idara ya Haki ya Marekani kuhusu hali ya jela, upatikanaji wa matibabu na matumizi ya nguvu kupita kiasi miongoni mwa maafisa.
Tatizo linaloongezeka
Ilipojengwa katika miaka ya 1980, jela hiyo ilikuwa "ya hali ya juu", alisema Dkt. Edmond, wakili. "Lakini sivyo tena. Jela hiyo inahitaji kubomolewa na wananchi wa Kaunti ya Fulton wanahitaji kutoa fedha zaidi za ushuru ili ‘’.
Ofisi ya Sherifu wa Kaunti ya Fulton yenyewe imekiri kuwa hali katika jengo hilo "ni chakavu na mazingira yanazidi kuzorota kwa kasi". Pia imetoa wito wa kujengwa kwa jela mpya itakayogharimu dola $1.7bn.
"Kumekuwa na mazungumzo mengi juu ya kuisafisha," alisema Bi McClure wa ACLU. "Hatujaona au kusikia chochote muhimu sana. Inaonekana kama maneno mengi tu"
Bi McClure alisema sababu kadhaa zimesababisha msongamano katika mfumo wa Jela la Kaunti ya Fulton. Kwanza, watu wanaoshtakiwa kwa makosa katika kaunti wanakamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi, tofauti na maeneo mengine ya Georgia, ambapo washtakiwa kwa ujumla huachiliwa na kupewa tarehe ya baadaye ya mahakama kwa makosa madogo, alisema.
Kaunti hiyo pia imekabiliwa na mrundikano wa kesi kwa sababu ya janga la Covid-19, na hivi majuzi, idadi kubwa ya mashtaka chini ya Sheria ya Mashirika Yanayoathiriwa na Ufisadi (Rico) ambayo hayahusiani na kesi ya Trump, alisema.
Bw Trump na washtakiwa wenzake walishtakiwa kwa kukiuka sheria hiyo wiki hii. Lakini mashitaka chini ya sheria, yaliyopitishwa katika miaka ya 1970 kusaidia kukabili makundi ya uhalifu uliopangwa kama vile mafia, ni magumu na yanahitaji rasilimali nyingi, wanasema wataalam.
"Kuna dhana kwamba kesi zingine hazijafunguliwa mashtaka kwa sababu hii inachukua muda mwingi," Bi McClure alisema.
'Jinsi Trump atakavyochukuliwa'

Chanzo cha picha, Getty images
Bw Trump huenda akaepuka matatizo haya yote atakaposhughulikiwa katika Kaunti ya Fulton, wataalam walisema.
Ingawa waendesha mashtaka hawajatoa maelezo kuhusu jinsi Bw Trump atakavyofungiwa wakati huu, kuna vidokezo kutokana na mchakato huo ulioharakishwa katika kesi zake tatu za awali huko New York, Florida na Washington DC, ambapo amekana mashtaka yote.
Alipofika katika mahakama hizi, Bw Trump alichukuliwa maelezo yake ya msingi na alama za vidole kama mshtakiwa yeyote.
Lakini alitengwa na washtakiwa wengine wa uhalifu na haraka akapelekwa hadi kwenye chumba cha mahakama, akiwa amezungukwa na Maafisa wa kikosi cha Secret Service na Marshals wa Marekani. Mamlaka imetaja wasiwasi mkubwa wa usalama katika kupanga mpango huo.












