Tatizo la kisiasa linalomzunguka Uhuru Kenyatta na umuhimu wake kudhibiti chama cha Jubilee

Iliyochapishwa

Na David Burare

Mchambuzi wa kisiasa Kenya

.

Chanzo cha picha, JUbilee Party

Maelezo ya picha, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta

Chama tawala cha zamani cha Jubilee nchini Kenya kimekumbwa na matatizo ya uongozi, huku mirengo miwili ikipigania kudhibiti chama kilichokuwa na nguvu na ambacho kilitawala nchi hiyo kwa muongo mmoja, kati ya 2013 na 2022.

Mnamo tarehe 26 Aprili, kundi moja lenye uhusiano na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta (kwa sasa ni kiongozi wa Jubilee) na lingine linalomuunga mkono Rais William Ruto, lilivamia makao makuu ya chama hicho jijini Nairobi, huku kila mmoja akidai kuwa na mamlaka.

Huku malumbano hayo yakiendelea, Wakenya wengi wanashangaa ni kwa nini rais huyo wa zamani ana nia ya kukiongoza chama cha Jubilee licha ya sheria kwamba lazima aondoke baada ya miezi sita ili afurahie marupurupu yake ya kustaafu.

Sababu ya Uhuru kusalia katika siasa

Akiwahutubia wajumbe wa chama hicho hivi karibuni, alisema kuwa awali alipanga kuachana na siasa na kushughulikia masuala mengine yanayomsumbua lakini alilazimika kusalia kutokana na shinikizo kutoka nje.

Ikiwa hii ni sababu kuu ya mtu yeyote kuamini ni swali ambalo Wakenya wengi sasa wanakabiliana nalo.

Wengi wanaamini kuwa hatua hii ya hivi punde zaidi ya rais huyo wa zamani ni mkakati wa kujikinga na mashambulizi ya utawala wa Ruto kwa sababu ya makosa ya kisiasa na kiuchumi ambayo huenda aliyafanya.

Hivi majuzi alizungumzia unyanyasaji na vitisho visivyokoma ikiwa ni pamoja na shambulio kwenye shamba la familia ambapo mali wakiwemo kondoo waliibiwa.

Rais huyo wa zamani alionekana kutojiamini na anaamini njia pekee ya kujilinda ni kusalia kisiasa katika usukani wa uongozi wa chama chake cha Jubilee.

.

Chanzo cha picha, Sabina Chege

Maelezo ya picha, Sabina Chege ni mwanasiasa kutoka Mlima Kenya

Uongozi katika mkoa wa kati

Uhuru Kenyatta anafahamu kikamilifu mabadiliko ya uongozi wa eneo la Mlima Kenya.

Kufikia uchaguzi uliopita, hakuweza kuwashawishi watu wake kumpigia kura mgombea wake wa urais Raila Odinga.

Rais huyo wa zamani anaelewa hali ya kisiasa ya eneo la kati vizuri kabisa na anadhani uongozi wa eneo hilo unaweza kuangukia kwenye mikono 'mibaya' kwa urahisi.

Ni kwa sababu hiyo anaona ni busara kubaki kwa muda na kukuza uongozi mpya anaoweza kuuamini na unaoweza kujali maslahi yake na ya familia yake.

Kulingana naye, si salama kuweka uongozi huo mikononi mwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ambaye anadhani ana kisasi kupindukia.

Uchungu wa uchaguzi uliopita wa Urais

.

Chanzo cha picha, Jubilee Party

Maelezo ya picha, Viongozi wa Muungano wa Azimio ambao Jubilee ni chama tanzu ndani ya muungano huo
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika uchaguzi uliopita wa rais, rais huyo wa zamani alikuwa katikati ya urithi wake. Alimchagua Raila kuwa mgombeaji wake na akaendelea kuwahamasisha wahusika wakuu wa kisiasa kufanya kampeni na kuwasilisha mradi wa Raila hadi ikulu.

Ukweli ni kwamba kila kitu kiliporomoka na William Ruto alishinda hali ambayo hakuipendelea kwa kuzingatia mazingira yaliyosababisha tofauti yao.

Kwamba rais aliyeketi alimpigia kampeni sana mgombea wake na akashindwa ni jambo lisilopendeza kwake. Ndio maana rais huyo wa zamani anahisi kuwa ana shughuli ambayo haijakamilika ya kukabiliana na rais Ruto na kumwondoa mamlakani 2027.

Hilo ni jambo analojua linaweza kutokea iwapo tu yuko kwenye siasa hai hivyo kuamua kung'ang'ania uongozi wa chama chake.

Hii pia inaeleza ni kwa nini viongozi wa Azimio wakiongozwa na Raila Odinga wanamlinda sana Uhuru Kenyatta kwa sababu wanajua kukaa kwake kwenye usukani wa chama cha Jubilee kutawafaidi kisiasa.

Ndiyo maana hata walihudhuria Kongamano la Wajumbe wa Kitaifa wa Jubilee na kutoa kauli nzito za kumuunga mkono Uhuru Kenyatta na chama chake.

Pia wametishia kujiondoa katika mazungumzo ya pande mbili isipokuwa utawala wa Ruto ukiacha chama cha Jubilee pekee.

Mipango ya mazungumzo ya kisiasa ya 2027

.

Chanzo cha picha, JUbilee Party

Maelezo ya picha, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta katika mkutano wa Chama cha Jubilee uliofanyika hivi karibuni

Rais huyo wa zamani pia anafahamu kikamilifu chama kikuu pekee cha watu wa kati mwa Kenya ni chama cha Jubilee.

Ni chama pekee ambacho wanaweza kukitumia kufanya mazungumzo kupata mgao wa keki ya kitaifa.

Ingawa watu wa Mlima Kenya walipigia kura kwa wingi chama tawala cha UDA, Uhuru na wenzake wanaamini kuwa hicho si chama chao na hiyo ndiyo sababu serikali ya wakati huo inataka kukiteka pengine kwa maandalizi ya mipango ya kisiasa ya 2027.

Mrengo wa Sabina Chege na Kanini Kega wa Jubilee tayari umetangaza kumuunga mkono rais Ruto, sasa na katika uchaguzi ujao wa urais.

Huenda Rais Ruto vilevile akakiwezesha Jubilee na kuiimarisha katika eneo hili kwa azma yake ya kuchaguliwa tena. Hili ni jambo ambalo Uhuru Kenyatta ana wasiwasi nalo na yuko tayari kupigana vikali kwa ajili ya udhibiti wa chama hicho.

Ikiwa atapoteza chama, mipango yake yote ya kisiasa pia itapotea na hatakuwa na njia nyingine zaidi ya kujisalimisha kwa vijana wake wa kisiasa kama Sabina Chege.

Katika siku zijazo, mengi yatatokea na tutajua ni nani atakuwa na kicheko cha mwisho kuhusiana na udhibiti wa chama cha Jubilee.

Ni hali ya kufa na kupona kwa rais huyo wa zamani kwa sababu chochote kitakachotokea kitaunda mwelekeo ujao wa kisiasa. Uhuru Kenyatta anasimama katikati ya wakati huu muhimu.