Waridi wa BBC: Kutoka ukahaba wa kuibia wateja, kifungo, majuto, hadi uandishi wa kitabu

Iliyochapishwa

Na Anne Ngugi

BBC Swahili

Shee Gathumbi

Chanzo cha picha, Shee Gathumbi

Japo Shee Gathumbi alibadilika kutoka ukahaba, ambao pia amekiri alikuwa anawaekea wateja wake kidonge cha dawa inayosababisha mtu kuchanganyikiwa, na baadaye kuwapora wakiwa hoi, anajutia tabia hiyo mno licha ya kuwa kwa baadhi ya makosa hayo alitumikia vifungo gerezani.

“Ninajihisi kana kwamba nilikubali ulimwengu unifisadi, wakati mwingine najihisi mzee ambaye hawezi pendwa kutokana na tabia zangu za hapo awali”anasema.

Mwanadada huyu alianza ukahaba akiwa bado mwanafunzi wa shule ya sekondari, anasema kuwa hali hii ilichangiwa na maisha duni na ya ufukara ambayo jamii yao waliishi.

Alichagua kuwafuata wanaume wenye umri mkubwa kuliko umri wake kuhusika nao kingono ili apate fedha za kusukuma maisha.

Mwanamke Huyu alikuwa amepata mimba ya utotoni na ilibidi aache mwanae mikononi mwa mama mzazi ili aendelee na masomo yake .

Changamoto ilikuwa mawazo yake hayakutulia darasani, alijikuta akiwaza shida na mahangaiko ya nyumbani kwao , kiasi cha kuingia kwenye ukahaba.

Aliingia vipi kwenye ukahaba?

Shee Gathumbi

Chanzo cha picha, Shee Gathumbi

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwaka wa 2005 alifukuzwa shuleni, kutokana na karo ya shule , badala ya kurudi nyumbani mwanadada huyu alielekea kwenye vilabu kuungana na wanawake wengine na kuanza kuona jinsi shughuli ya kujiuza kimwili hufanyika . Ila baada ya wiki mmoja alirudi nyumbani.

“Mama yangu alikuwa ananitafuta, shuleni pia walikuwa wananitafuta, Mama alinipeleka shuleni na kuwaeleza kuwa nilikuwa sipatikani.Nilifukuzwa shuleni na ilipelekea mimi kufanya mtihani Mkuu wa kuhitimisha shule ya sekondari nikiwa nyumbani.”

Baada ya kukamilisha shule ya Sekondari, moja kwa moja alijiunga na wasichana wa usiku, katika Kaunti ya Nyeri nchini Kenya, baada ya muda yeye na swahiba wake walihamisha shughuli zao hadi Kaunti ya Nakuru , Japo Shee anakiri kwamba hakupendelea mno mazingira ya kazi hiyo , wakati mwingi alikuwa na tabia ya kukaa ndani pekee yake kwa kuogopa watu .

Kipindi kilichofuata mwanadada huyu anasema kwamba alifundishwa kile anachokitaja njia rahisi ya kupata fedha.

Kama kahaba wakati alipata mteja wakaingia chumbani na vileo alikuwa anarusha tembe kwa haraka ndani ya kinywaji cha mteja na baada ya muda mteja anazimia, kuanzia hapo alikuwa anapora kila kitu cha mteja wake.

Shee anakiri kuiba maelfu ya madola kwa mfano anasema

“ Kuna nyakati niliiba fedha nyingi kama dola alfu mbili , Dola Mia saba , dola alfu moja na kadhalika, ila hizo pesa zilikuwa na nuksi , hazikunisaidia kwa njia yeyote isipokuwa kuishi siku baada ya nyingine , najuta mno” anasema Shee

Mwanamke Huyu anasema maisha yake yalijaa sarakasi kwani alinunua bidhaa za nyumbani za hela nyingi , na anasa za kila aina na baadaye kuziuza kwa bei ya kutupa katika misimu ambayo hakupata wateja na alikuwa amefilisika .

Kisa kimoja ambacho hajakisahau kwani kilimsukuma jela , usiku moja aliingia kwenye kilabu na kupata mteja, baada ya kuburudika waliamua kubeba vileo vingine hadi chumbani, sheila alikuwa tayari na dawa ,anakiri kutumbukiza ile dawa ndani ya kinywaji na mteja alilala ghafla! Mwanamke huyu alianza msako na kupata dola alfu 2 ndani ya mfuko wa suruali ya mteja.

“ Nilifahamu ningekuwa na changamoto ya kutoroka , nilipokutana na mlinzi nilimpa pesa ya kinywaji na kutoroka eneo hilo . “ anakumbuka.

Kutumikia kifungo

Shee Gathumbi

Chanzo cha picha, Shee Gathumbi

Kwa miaka 10 Shee alitumika kama kahaba, wakati mmoja alirudi nyumbani baada ya mama kumsihi aache ile kazi hio , alikubali na kuingia taasisi mmoja kwa lengo la kupata masomo maalumu ili kujitafutia ajira . ila anasema ukahaba ulikuwa umemuingia na aliuona kama barabara rahisi ya kupata hela , upande mwengine alijihisi ni mchafu na kujiona kama mwanamke aliyezeeka Kwani wateja walikuwa wameanza kumfahamu na kumtambulisha na tabia zake . Alihama kutoka Kaunti ya Nakuru na kuanza ukahaba mji Mkuu Nairobi.

“Japo nilikuwa kwenye uhusano wa kimapenzi na mwanaume mmoja , tayari hata yeye alikuwa amefungwa jela , na kwa hiyo sikuona ni kwanini niendelee kuishi sehemu ambayo watu wengi walikuwa wamenitambua kwa mienendo yangu hasa kwenye vilabu”anasema Shee.

Alipowasili Nairobi hakukaa muda mwingi na Usiku mmoja aliamua kuingia kwenye kilabu kama ada kusaka wateja , kwa saa nyingi alitumia vileo huku akidodosa macho kuwinda mteja, wakati wa saa za asubuhi bwana mmoja alianza kumchokoza na wakawa wanaburudika pamoja , mwanadada huyu anakiri kuwa alikuwa mlevi chakari , juu ya meza mlikuwa na vileo vyao , ghafla alirusha tembe ndani ya kinywaji cha yule mtu waliyekuwa naye huku watu wengi wakishuhudia kitendo hicho.

Watu walimkamata na kumpeleka katika kituo cha polisi, alikuwa mlevi na hakuwa anajielewa, kwa hiyo alipowekwa mahabusu alilala usingizi hadi masaa ya jioni, alipopata fahamu aliwapigia simu jamaa wake.

Jamaa zake walifika kwenye kituo cha polisi wakiwa na fedha za kumlipia faini atoke, ila Mkuu wa kituo hicho alisisitiza kuwa Shee afikishwe kortini ili ashike adabu ya kutowaekea watu dawa ndani ya pombe zao , na pia iwe funzo kwa wengine.

Kortini alishindwa kugharamia rufaa ya dola alfu mbili na aliwekwa rumande kwa miezi saba.

Maisha ya gerezani

Shee Gathumbi

Chanzo cha picha, Shee Gathumbi

Gerezani alianza kumrejea Mungu, na akaanza kuwa na saa nyingi za kutubu pia alipata muda wa kujitathmini kimaisha. Akiwa jela alifahamu kuwa hakuna uhuru.

Jamii yake ilipambana sana atoke jela . Shee kupitia dada yake walimsaka mlalamishi wa kesi hiyo alifika kortini na kumsamehe, hapo ndipo aliachiliwa kutoka gerezani.

Alipofika nyumbani juma moja halikupita na akakamatwa kwa mara nyingine , mteja wa zamani alikuwa amemuibia alimfumania akiwa kwenye kilabu, alirejeshwa jela na akakaa kwa miezi miwili. Shee hakuwa na uwezo wa kulipia rufaa tena , alimsaka mlalamishi hadi akaomba msamaha aliachiliwa kwa mara nyingine.

Baada ya hapo Shee alisafiri hadi nchi ya Misri kusaka kazi za nyumbani, akiwa huko alipata msongo wa mawazo akifikiria mengi aliyoyafanya, na huko alianza kuandika kitabu kuhusu maisha yake , kitabu kwa jina ‘the secret is out’ ikimaanisha siri imetoka , kwa miaka mitatu aliishi Misri alitumia muda mwingi kuponyesha majeraha ya moyo na mafikra kuhusu mengi aliyoyafanya akiwa Kahaba.

Shee anasema alipo sasa amejisamehe na kwa baadhi ya wanaume aliowadhuru na dawa ya usingizi aliwaomba msamaha hasa waliompeleka mahakamani.

Shee anakiri kuwa maisha yake ya hapo awali yalikosa msingi wa nidhamu na pia alikosa upendo na mawaidha ya kumwelekeza pazuri, anajutia mengi ila anatumai kuwa kitabu chake kitasaidia jamii kubadilika hasa kwa wanawake vijana ambao wanaweza kuwa na mawazo ya kutafuta pesa za haraka na kuhatarisha maisha yao na watu ya wengine.

Shee Gathumbi

Chanzo cha picha, Shee Gathumbi

Kwa mujibu wa Daktari Garvin Orangi ambaye ni Mwanafamasia kutoka Kenya, tembe au ‘mchele’ ambao unatumiwa na baadhi ya makahaba kwenye vilabu na maeneo ya starehe vinaweza kuwa na madhara sio haba kwa mtu kwa mfano, mtu huenda akachanganyikiwa kwa kiasi cha kuwa na shida ya kukumbuka alipo na alikuwa na akina nani , pia anasema kwamba anaweza kusahau alikuwa wapi na alifika eneo hilo kivipi pamoja na kuwasahau watu ambao anawafahamu vizuri , pia anaweza athirika na shida ya kupumua , na huenda akatumia nguvu nyingi kupumua , aidha anakuwa na upungufu wa sukari mwilini ,na kumpelekea kuwa na udhaifu mwilini .

Daktari Garvin anaonya kuwa kwa ishara hizo ni rahisi kumtambua mtu ambaye hajatumia pombe nyingi lakini akawa na mienendo ya mtu ambaye hajielewi , anaongeza kuwa cha haraka ni mtu kupelekwa hospitalini ili hali hiyo itathiminiwe na wataalamu