Je, Marekani itabadili msimamo na 'kupinga' uhuru wa Taiwan?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Rais wa Marekani Donald Trump na mwezake wa China Xi Jinping walikutana tena baada ya mwaka mmoja.

Tofauti na ilivyokuwa wakati huo, pande zote mbili ziliweka bayana kuanzia mwanzo kwamba "suala la Taiwan" litakuwa mada ya msingi katika majadiliano yao.

Wakati Marekani na China zikiwa makini kulinda maslahi yao, wasiwasi mkubwa wa Taiwan ni kuwekwa kwenye "menyu" ya mikataba mikubwa ya mataifa hayo mawili makubwa.

Je, Marekani itabadilisha msimamo wake?

Wakati wa mazungumzo ya simu kati ya Marekani na China mwishoni mwa mwezi wa Aprili, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa China Wang Yi, alisema kuwa Taiwan ni miongoni mwa maslahi ya China na uhusiano kati ya Marekani na Taiwan ni "hatari"

Dunia imekuwa ikifuatilia kwa makini jinsi matamshi ya Trump kuhusu suala la Taiwan yanavyoweza kuathiri usalama na uthabiti wa eneo hilo.

Patricia Kim, mshirika mkuu wa sera za mambo ya nje katika Taasisi ya Brookings, aliandika kwamba mabadiliko katika maneno ya Marekani ya kutaka suluhu ya kumaliza tofauti iliopo au kutounga Taiwan mkono bado ni jambo kubwa.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na gazeti la Nikkei, Zack Cooper, mfanyakazi mwandamizi katika Taasisi ya Biashara ya Marekani, alitabiri kwamba Trump anaweza kurekebisha maneno yake kuhusu suala la Taiwan, na kuyabadilisha kutoka "Marekani haiungi mkono uhuru wa Taiwan" hadi "inapinga uhuru wa Taiwan."

Aliongezea kuwa mabadiliko haya ya maneno yanaonekana kama Marekani inajaribu "kujitenga" na Taiwan.

Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton alisema mjini Shanghai mwaka wa 1998 kwamba "haungi mkono uhuru wa Taiwan," huku Rais George W. Bush akisema mwaka wa 2003 kwamba "anapinga mabadiliko yoyote ya upande mmoja ya hali ilivyo kwa China au Taiwan."

Hadi kufikia sasa, hakuna rais wa Marekani ambaye ametamka hadharani kwamba "anapinga uhuru wa Taiwan."

Weng Li-chung, profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Sam Houston huko Texas, aliiambia BBC China kwamba kuikana Taiwan sio maslahi ya kisiasa ya Trump, lakini anaweza kurekebisha maneno yake kuhusu utambulishaji wa kisiwa hicho.

Ila iwapo Trump atabadilisha maneno kuhusu uhusiano wao na Taiwan, huenda yatasababisha kuporomoka kabisa kwa uhusiano wa Taiwan na Marekani, na pia inaweza kudhoofisha imani ya watu wa Taiwan kwa Marekani.

"Watu wa Taiwan wako tayari kuwekeza kiasi kikubwa katika bajeti za ulinzi kwa sababu wanaamini kwamba Marekani itatoa msaada katika nyakati ngumu."

Taiwan ina ''wasiwasi''

Sekta mbalimbali nchini Taiwan zinahofia matokeo ya mazungumzo kati ya Marekani na China, huku baadhi ya vyombo vya habari vya Taiwan vikielezea hali ya sasa kama "wasiwasi"

Katika mahojiano na shirika la habari la Bloomberg mnamo Aprili 24, Naibu Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Taiwan Wu Chih-chung alikiri kwamba alikuwa na wasiwasi Taiwan itawekwa kwenye "meza ya mazungumzo" wakati wa mkutano wa Trump na Xi, na kwamba Marekani inaweza kufanya makubaliano juu ya suala la Taiwan, na kusisitiza kuwa Taiwan inajitahidi kuepusha hali hii.

Wakati Marekani na China zilipokutana Korea Kusini mwaka jana, Trump na Xi Jinping hawakugusia hata kidogo suala la Taiwan.

Weng Lizhong aliongeza kuwa mkutano wa mwaka huu ni tofauti na wa mwaka jana kwa sababu Marekani imebanwa na mkwamo wa vita vya Marekani na Iran, na utawala wa Trump kupata "mafanikio" kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula.

Katika mkutano huo Marekani imeweza kutumia mpango wa "3Bs" kama chambo cha mazungumzo katika mkutano huu, ikijumuisha ununuzi wa ndege za Boeing, nyama ya ng'ombe na soya.

Beijing imekuwa ikishinikiza Marekani kutoa "tamko la nne" ambao litaijumuisha Taiwan kama sehemu ya China.

Marekani na China zimetia saini matamko matatu: Tamko la Shanghai, Taarifa ya Pamoja ya Kuanzisha Mahusiano ya Kidiplomasia, na Tamko la Agosti 17. Hizi zinazingatiwa kuwa mfumo wa uhusiano wa Marekani na China.

Marekani "inatambua" msimamo wa China kwamba "Taiwan ni sehemu ya China," lakini haijakiri waziwazi, na kupitisha sera "utata wa kimkakati" ili kudumisha uhusiano mkubwa na Taiwan.

Bajeti ya ulinzi ilipitishwa usiku wa kuamkia mkutano wa Trump na Xi

Wiki moja tu kabla ya mkutano wa Trump na Xi, Wabunge wa Taiwan walipitisha bajeti ya kijeshi ya takribani dola bilioni 25 za Kimarkani kununua makombora na silaha zingine kutoka Marekani.

Mwishoni mwa mwaka jana, utawala wa Lai Ching-te ulipendekeza bajeti maalum ya ulinzi ya jumla ya dola za Marekani bilioni 40 kwa ununuzi wa silaha kutoka Marekani na kuendeleza sekta yake ya ulinzi wa ndani.

Pendekezo hilo lilizuiwa na upinzani bungeni, na kusababisha mkwamo kwa miezi kadhaa. Hatimaye bajeti ya awali ilipunguzwa kwa karibu 40%. Baadhi ya matumizi, yakiwemo yale ya ndege zisizo na rubani zinazozalishwa nchini humo, yalipunguzwa.

Bajeti ya ulinzi ya mamilioni ya fedha iliyopitishwa na Bunge laTaiwan inajumuisha silaha za Marekani zilizoidhinishwa na Washington mwishoni mwa mwaka jana, lakini ununuzi wa silaha zilizopendekezwa bado unasubiri idhini kutoka kwa utawala wa Trump.

Kwa mujibu wa ripoti, serikali ya Marekani imesitisha kwa muda idhini ya mpango wa hivi punde wa mauzo ya silaha kwa Taiwan.