Baa za maziwa zinavyoshamiri duniani

Milk

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Yusuph Mazimu
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Dar es salaam
  • Iliyochapishwa

 Faida za maziwa hasa ya ng’ombe yanayopatikana katika maeneo mengi duniani ni kubwa. Ni chanzo cha Protini, Vitamin D, Vitamin A, kalshiam ambazo ni muhimu kwenye kuboresha afya yako, kuimarisha mifupa, meno, misuli na mengine.

Watafiti wanataja maziwa kusaidia sana kwenye kukabiliana na baadhi ya magonjwa ikiwemo kisukari aina ya pili, na shinikizo la damu la juu.

Haishangazi kuona uzalishaji wa maziwa duniani ukipanda kutoka tani 497milioni mwaka 2015 mpaka kufikia 544milioni kwa mwaka 2021. Na hilo linasukuma sasa mataifa na wafanyabiashara kuanza kufikiria na kuwekeza kwenye mazao ya maziwa kwa kuanzisha mabaa katika maeneo mbalimbali.

Asili ya baa za maziwa         

Milk

Chanzo cha picha, Getty Images

Biashara ya kwanza ya baa ya maziwa ilianzishwa na Muingereza huko India mwaka 1930, James Meadow Charles alipofungua baa yake huko Bangalore iliyoitwa Lake View Bar. Wazo hilo likaanza kusambaa kwa kasi katika maeneo mbalimbali duniani, ikiwemo Uingereza. Katika muda mfupi tu  zaidi ya baa 1000 zilifunguliwa mpaka kufikia mwaka 1936. Nchini Marekani baa hizo zilianza kushika kasi mwishoni mwa mwaka 1940

Awali baa za maziwa zilikuwa maalumu kwa ajili ya kuuuzia magazeti na vyakula vya  harakaharaka  kama chipsi, samaki, vitafunwa. Lakini uwepo wa maziwa mengi na mahitaji makubwa ya maziwa,  mabaa mengi ya maziwa yakatumika sawia na lengo lake la kuuza kwa wingi maziwa.              

Nchi zenye baa nyingi za maziwa duniani  

Milk

Ikiwa 70% ya wanyarwanda wanajishughulisha na kilimo, kuwa na ng’ombe Rwanda ni ishara au alama ya mtu anyejiweza na mwenye hadhi hasa katika maeneo ya vijijini. Baadhi ya baa za maziwa Rwanda zinauzwa pia na vitafunwa ama chakula cha kuvutia kikienda na maziwa.

Warwanda walianza kuuza maziwa mwanzoni mwa miaka 1990 wakati huo ikitawaliwa na wajerumani. Wakati huo walikuwa wakisafiri umbali mrefu kwenda kujenga barabara, shule na makanisa kama sehemu ya German East Africa. Walishuhudia wenzao wa Sudan, Uganda, na Tanzania waliokuwa wanasafiri na wajerumani wakiuza maziwa waliyoyanunua kwa wenyeji na kuwauzia wafanyakazi.

Hapo ndipo walipoanza kuuziana wao kwa wao, na biashara ikaanza kukua kwa kazi  na sasa maziwa ni moja ya vinjwaji pendwa Rwanda na vyenye heshima. Katika maeneo mengi kumefunguliwa baa za maziwa, zinazouza maziwa ya kawaida, yanayouzwa ya moto ama ya baridi, chai ya maziwa, mtindi, siagi na bidhaa zingine za maziwa.

Nchi zingine ambazo baa za maziwa zimeanza kushamiri ni pamoja na New Zealand wanaotumia jina ‘dairy shop’, Poland wao baa zao za maziwa wanaziita ‘bar mleczny’ ambazo awali zilitumika sana kuuza bidhaa zilizopewa ruzuku na serikali ambapo mwaka 2011, serikali ilianza mpango wa kuacha kutoa ruzuku, hatua iliyozodolewa na wengi wakisema, ni kuua baa za maziwa.

Mataifa kama Marekani, Australia na Afrika Kusini kumekuwa na baa za nyingi za maziwa.

Baa za maziwa na baa za pombe  

Milk

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kuna baadhi ya mataifa wanajaribu kuchanganya bidhaa. Wanauza maziwa na wanauza pombe, ili mtu anayekunywa pombe akiambatana na mtu asiyekunywa waweze kujumuika pamoja bila tashwishwi ya vinywaji.

Ingawa baa nyingi duniani haziweki maziwa kama sehemu yao ya vinywaji baridi, baa za maziwa hasa katika nchi za Ulaya zinaweka aina fulani ya vileo, ili kuongeza wigo wa wateja wake na kuvutia aina mbalimbali za wateja.

Utofauti wa baa za pombe na baa za maziwa unajionyesha kwa bidhaa zinazouzwa na namna zinavyouzwa. Kwenye baa nyingi za pombe utakuta bia, vinjwaji vikali, mvinyo na baadhi ya vinywaji baridi kama soda na maji.

Lakini mazingira ya baa za pombe yanaendana yanajengwa na matamanio ya mnywaji mwenyewe na huambatana na vitu vingi kama uuzaji wa sigara, shisha na mara nyingi baa za pombe hujaza wateja wakat iwa usiku ikiwa na wahudumu kadhaa wanaovalia mavazi maluumu kuhudumia wateja.

Baa za maziwa zenyewe zinakuwa na harakati nyingi kuanzia asubuhi na kupungua shughuli jioni inapozidi kufika. Mara nyingi huuza maziwa yenyewe yakiwa ya moto, ya baridi, maziwa ya pakti, maziwa ya boksi, mtindi, biskuti na chokoleti za maziwa na na bidhaa zingine zinazotengenezwa na maziwa.

Baa ya maziwa ni heshima

Milk

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa Rwanda baa za Maziwa ni heshima kubwa na ni mahala panapotajwa kama sehemu muhimu ya kuimarisha mahusiano. Hivyo hivyo kwa mataifa hasa ya kiislam yanayoanza kutumiwa baa kuuza maziwa badala ya pombe.

Ukiwa na mazungumzo ama vikwao nchini Rwanda katika baadhi ya maeneo, baa hizi zinatumika sana hasa katika maeneo ya nje ya mji. Mazungumzo yanayokwenda na ikivuguto (maziwa yaliyochachuliwa) ya baridi yanayowekwa asali ama sukari.

Unapotaka pia kumtakia mtu mema nchini Rwanda unasema ‘gira inka’ kwa maana isiyo rasmi ‘uwe na ng’ombe’ ama ukimwambiwa ‘amashayo’ kwa tafsiri isiyo rasmi ni sawa na kutakiwa heri ya kuwa na maelfu ya ng’ombe’.

Unapotaka kutoa shukrani unasema  ‘nguhaye inka’ kwa maana ya ‘nakupa ng’ombe’.