Alexander Geniez ashinda mzunguko wa kwanza wa Tour du Rwanda’

Iliyochapishwa

Mwendesha baiskeli Mfaransa, Alexandre Geniez wa timu ya TotalEnergies, ameshinda mkondo wa kwanza wa mashindano ya kimataifa ya mbio za baiskeli maarufu Tour du Rwanda kutumia dakika 4 na sekunde 41-raundi iliyokuwa ya umbali wa kilomita 4.

Katika mbio za baiskeli raundi hiyo inafahamika kama 'Prologue' ambapo kila mchezaji hucheza peke yake na huzingatia mtu ambaye ametumia wakati mzuri zaidi.

Mashindano ya mwaka huu yameanza kutimua vumbi jumapili hii ambapo washindani 89 kutoka timu 19 za nchi mbali mbali duniani wameshiriki raundi ya kwanza wakikabiliana na mvua kubwa iliyonyesha mjini Kigali.

Alexandre Geniez, 33, alimpita Restrepo Johnathan wa Drone Hopper-Androni ya Italia ambaye aliibuka wa pili kwa muda wa dakika 4 na sekunde 47.

Miongoni mwa waendesha baiskeli kutoka Rwanda Uhiriwe Byiza Renus ndiye aliyekuwa karibu zaidi, akimaliza katika nafasi ya 25 kwa kutumia muda wa dakika 5 na sekunde 1 huku mshindi wa kwanza akimzidi kwa sekunde 20.

Mbio za mkondo wa pili zitachezwa kesho kati ya mji wa Kigali na mjini wa Rwamagana upande wa mashariki mwa Rwanda - umbali wa kilomita 148.

Kwa ujumla mbio za baiskeli za Tour du Rwanda zitakuwa na raundi 8 za kilomita 937washindani wakizunguka katika maeneo tofauti ya mikoa ya Rwanda.

Ni shindano linalojumuisha baadhi ya timu zinazotambulika zaidi katika mashindano maarufu duniani ya Tour de France, Giro Italia na Tour d 'Spain timu kama Israel-Premier Tech, TotalEnergies, B&B Hotels-KTM, Drone Hopper-Androni na Burgos-BH ya Uhispania.

Pia wanashiriki mashindano hayo wachezaji ambao wameshinda Tour du Rwanda, Samuel Mugisha ambaye alitwaa (2018) Natnael Tesfazion wa Eritrea (2020) ambaye sasa anachezea timu ya Italia Drone Hopper-Androni.

Timu bora zaidi barani Afrika-timu ya Erytrea haikushiriki mashindano ya mwaka huu kwa kutotimiza masharti ya kuwa na chanjo kamili ya Covid-19.