Waziri wa Madagascar aogelea saa 12 kujiokoa baada ya ajali ya helikopta baharini

Iliyochapishwa

Waziri mmoja wa serikali nchini Madagascar amesema aliogelea kwa saa 12 kujiokoa baada ya helikopta aliyoipanda kuanguka baharini wakati wakifanya shughuli ya uokoaji.

"Sio wakati wangu wa kufa," waziri huyo wa polisi aliyekuwa amechoka Serge Gelle, alisema alipokuwa akipata nafuu kwenye machela.

Maafisa wengine wawili wa usalama waliokuwa wakisafiri naye kwenye ndege hiyo pia nao waliponea ajali hiyo.

Walikuwa wakikagua eneo moja lililo kaskazini mashariki mwa nchi ambapo mashua ya abiria ilizama.

Takriban watu 39 walifariki kwenye ajali hiyo kwa mujibu wa maafisa.

Kupitia mtandao wa Twitter Rais Andry Rajoelina aliwaomboleza waliofariki na kuwapongeza Bw Gelle na maafisa wengine wawili waliowasili kwenye mji ulio kando mwa bahari wa Mahambo.

Haijulikani sababu ya kutokea ajali hiyo ya siku ya Jumatatu lakini Bw Gelle, mwenye umri wa miaka 57 alisema kuwa baada ya ndege kuanguka aliogelea kuanzia saa 1:30 usiku hadi 1:30 asubuhi hadi Mahambo.

Alisema hakuwa na majeraha lakini akaongeza kuwa alikuwa akihisi baridi.

"Ningependa mpeperushe video hii kwa familia yangu waione, wafanyakazi wenzangu waione, serikali iione, niko hai na salama," Bw Gelle aliwaambia wanakijiji huko Mahambo.

Mkuu wa polisi Zafisambatra Ravoavy aliliambia shirika la habari la AFP kuwa Bw Gelle alitumia moja ya viti vya helikopta hiyo kama kifaa cha kuelea.

"Daima amekuwa na stamina kubwa katika michezo na amedumisha mdundo huu kama waziri, kama mtu wa miaka 30…ana mishipa ya chuma," Bw Ravoavy alisema.

Bw Gelle amehudumu kama polisi kwa miongo mitatu kabla ya kuteuliwa kuwa waziri mwezi Agosti.