Mzozo DRC: Ituri na Kivu Kaskazini zakabidhiwa kwa jeshi rasmi

Rais wa DRC Felix Tshisekedi amesema ni wakati sasa kwa raia wa nchi hiyo kutoa ushirikiano kwa jeshi na serikali ili kumaliza tatizo la usalama Mashariki mwa nchi hiyo.
Akizungumza katika hotuba kwa njia ya televisheni, Rais Tshisekedi amesema hatua ya baadhi ya maeneo ya Mashariki mwa nchi hiyo kuwa chini ya jeshi ni muhimu ili kuleta hali ya amani.
Tangu kuingia kwake madarakani mnamo mwaka 2019, Rais huyo amekua akisisitiza kuwa moja ya azma yake kuu ni kuleta utulivu katika maeneo hayo.
Rais ametoa tarehe rasmi ambayo wanajeshi wanapaswa kupewa uongozi wa majimbo mawili yenye ukosefu wa usalama.
Jimbo la Ituri limekuwa na vita vya kikabila na jimbo la Kivu Kaskazini ambapo wapiganaji wa kundi la ADF wamekuwa wanawashambulia raia.

Hatua hii ikiwa ina maanisha kuwa wanasiasa inabidi wasijihusishe na wanajeshi maana wanajeshi walikuwa wanalalamika kuwa hawana vifaa tofauti na vile ambavyo wanavipata Umoja wa mataifa na kwa upande wa raia wanapaswa kutoa ushirikiano kuonesha maadui.
Aidha mashirika ya kiraia yamekuwa yakilalamika kuhusu uhusiano wa wanajeshi wa ngazi za juu kutojali uimarishwaji wa usalama kwa raia na kuwa ni hatua ni nzuri ila ni vyema wabadilishe viongozi wa juu wa maeneo hayo.

Jumatatu, iliripotiwa kuwa wapiginaji wenye silaha wamewaua takriban watu 19 wakiwemo wanajeshi kumi baada ya kushambulia vijiji viwili mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo siku ya Jumamosi muda muda mfupi baada ya Rais Felix Tshisekedi kutangaza kwamba mikoa miwili mashariki mwa nchi hiyo Ituri na Kivu Kaskazini ,imezingirwa .
Ongezeko la mashambulizi ya makundi yaliyojihami na machafuko ya kikabila yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 300 tangu mwanzoni mwa mwaka huu huku wanajeshi wa serikali na walinda amani wa umoja wa mataifa wakijaribu kuleta utulivu mashariki mwa nchi hiyo .
Shambulio la hivi punde limefanyika siku ya Jumamosi wakati wapiganaji wenye silaha waliposhambulia vijiji viwili katika mji wa Kivu kaskazini wa Beni, mamlaka za jimbo hilo zimesema.
Baadaye siku hiyo imam mwenye ushawishi mkubwa aliuawa kwa kupigwa risasi msikitini mjini Beni alipokuwa akiwaswalisha watu wakati wa jioni . Alitambulika kwa kupinga itikadi kali za kidini kupitia kituo kimoja cha redio katika jimbo hilo.
Siku ya Ijumaa Polisi katika mji wa Beni waliwatawanya wanafunzi waliokuwa wakifanya maandamano ya kuketi katika ukumbi mmoja wa mji huo kulalamikia ongezeko la hali ya ukosefu wa usalama.
Watu kadhaa walijeruhiwa na wengine kukamatwa kulingana na shahidi mmoja aliyezungumza na shirika la habari la Reuters.
Ni makundi yapi yanayotekeleza mauaji?
Kundi moja la waasi kutoka Uganda kwa jina Allied Democratic Forces (ADF) limekuwa mashariki mwa DRC tangu miaka ya 1990 na linaaminika kuhusika na visa vingi vya mashambulizi katika eneo hilo .
Kundi hilo limefanya msururu wa mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya raia tangu jeshi lilipoanza oparesheni ya kuliangamiza mwaka wa 2019 na liliwaua watu 850 mwaka jana kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa .
Ghasia hizo zimesababisha mgogoro wa kibinadamu mashariki mwa DRC ambapo Zaidi ya watu milioni 1.6 wameachwa bila makazi huko Ituri ,mkoa wenye jumla ya watu milioni 5.7 shirika la UNICEF lilisema mwezi Aprili . Watu wengine miloni 2.8 wanahitaji usaidizi wa dharura ,shirika hilo lilisema .














