Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Eudy Simelane: Jinsi mauaji ya mchezaji maarufu yanavyobali fikra kuhusu wapenzi wa jinsia moja
Mchezaji mpira wa kimataifa, kocha na mtu aliyekuwa na mipango ya kuwa mwamuzi, Eudy Simelane aliwekeza Maisha yake yote katika mchezo wa kandanda.
Alikuwa ni mmoja wa wanawake wa kwanza kuishi wazi kama mpenzi wa jinsia moja na mwanaharakati katika eneo la Kwa-Thema nchini Afrika Kusini.
Lakini kutokana na maisha yake ya kimapenzi, Simelane alibakwa kisha kuuawa kikatitili mwaka 2008, akiwa na umri wa miaka 31 tu.
Hii ni hadithi ya maisha yake na namna gani mpaka sasa kifo chake bado kinaiathiri jamii ya Afrika Kusini.
'Alikuwa ni almasi'
Simelane alizaliwa Machi 11, 1977, mji wa Kwa-Thema, uliopo katika jimbo la Gauteng, kusini mashariki mwa jiji la Johannesburg.
Kupendelea kwake mpira kulianza akiwa na umri wa miaka minne, akimlazimisha kaka yake Bafana kwenda naye mazoezini licha ya kuwa bado halikuwa jambo la kawaida kusakata kabumbu katika miaka hiyo.
Punde si punde, mapenzi yake katika mpira yakadhihiri huku akinoa kipaji chake kila siku.
"Alikuwa mazoezini saa 11 alfajiri - mpira ndio ulikuwa kitu akipendacho na kipaumbele chake," marehemu mama yake alieleza wakati wa mhadhara wa kumbukizi yake mwaka 2016.
Alibatizwa jina la uwanjani la 'Styles' kutokana na kuwa kiungo aliyetumia mguu wa kushoto.
Simelane alijiunga na timu yake ya nyumbani, Kwa-Thema Ladies, ambayo sasa inafahamika kama 'Springs Home Sweepers'.
Akizungumza na BBC mwaka 2018 kuhusu umaarufu wa Simelane uwanjani, baba yake, mzee Khotso alisema: "Kila mtu alikuja uwanjani alipokuwa akicheza, kiungo nambari 6."
Klabu ya Springs Home Sweepers imezalisha nyota wengi Pamoja na Janine van Wyk nahodha wa timu ya wanawake ya Afrika Kusini, na mchezaji aliyeichezea mechi nyingi timu hiyo maarufu kama 'Banyana Banyana', ikimaanisha 'wasichana.'
Simelane pia amecheza timu ya taifa, akafundisha timu nne za vijana na alitaka kufuzu kuwa mwamuzi wa kwanza wa kike nchini mwake.
Alikuwa pia ni moja ya wanawake wa mwanzo kujitokeza hadharani kama mshiriki wa mapenzi ya jinsi moja nchini Afrika Kusini na alikuwa pia mwanaharakati aliyepigania usawa na haki za wapenzi wa jinsia moja nchini humo.
Katika Mhadhara wa Kumbukizi ya Eudy Similane 2020, kaka yake, Bafana alisema:
"Katika mpira alikuwa ni almasi, akifunga magoli mazuri kabisa. Aliwa mtu mzuri sana, mwenye akili na kila kitu. Alikuwa ni mtu aliyekamilika. Kila kitu ungekipata kwa Eudy. Alikuwa akicheza na kuwafurahisha wenzie kwa matani. Hicho ndicho kikubwa ninachokikosa kutoka kwake."
Aprili 27, 2008 mwili wa Simelane ulikutwa kwenye mto mdogo ulio umbali mdogo kutoka nyumbani kwao mjini Kwa-Thema.
Ripoti zilidai kuwa alifuatwa akitoka kilabuni, akabakwa na kisha kuchomwa visu mara kadhaa.
Licha ya kifo chake kuwashitua wengi, wanaharakati wanaeleza kuwa wapenzi wengi wa jinsi moja nchini Afrika Kusini hulengwa kwa 'mashambulizi ya kubwakwa ya kurekebishwa' ambapo wahalifu hulenga 'kumponya' mhanga wao ili kumrejesha katika mahusiano ya kimapenzi ya kawaida.
Thatho Mphuthi alikiri mahakamani Februari 2009 kumbaka na kumuua Simelane in February 2009 na akahukumiwa kifungo cha miaka 32 jela. Mwezi Septemba mwaka huohuo Themba Mvubu pia alikutwa na hatia ya makosa hayo na kuhukumiwa kifungo cha maisha gerezani. Alipoulizwa na waandishi wa Habari mahakamani kuhusu tukio hilo, alijibu: "Sijutii."
'Ilifungua macho ya wengi'
Maisha ya kimapenzi ya Simelane yalimfanya awe katika hatari, kitu ambacho mama yake alikigundua, akiiambia BBC, "nchi yote ya Afrika Kusini ilijua kuwa Eudy alikuwa mpenzi ya jinsia."
Kitu cha kusikitisha ni kuwa - hadithi ya Simelane si ngeni katika jamii - yeye ni miongoni mwa waathirika wengi mashambulizi mabaya nchini Afrika Kusini.
Mwaka mmoja kabla ya kifo chake, Sizakele Sigasa, mwanaharakati wa haki za wanawake na wapenzi wa jinsia moja pamoja na rafiki yake Salone Massooa, walishambuliwa nje ya baa moja. Walibakwa na genge la wanaume, wakateswa na kisha kuuawa kwa kupigwa risasi.
Miaka michache baada ya kuuawa kwa Simelane, Noxolo Nogwaza, mpenzi wa jinsia moja wa kike aliyekuwa na miaka 24 alikutwa amefariki baada ya kushambuliwa kwa mawe katika eneo ambalo pia Simelane aliishi.
Licha ya matukio hayo, Afrika Kusini kama nchi ipo katika mstari wa mbele katika haki za wapenzi wa jinsia moja na ilikuwa nchi ya kwanza kuruhusu mahusiano ya jinsia moja mwaka 1998.
Nchi hiyo pia ilihalalisha ndoa za wapenzi wa jinsia moja mwaka 2006, miaka saba kabla kabla ya sheria hiyo kupitishwa Uingereza na miaka miwili kabla ya kuuawa kikatili kwa Simelane.
Hata hivyo, Afrika Kusini ndiyo nchi yenye kurekodi matukio mengi zaidi ya ubakaji kulingana na idadi ya watu duniani. Katika janga hilo, wasichana weusi na wapenzi wa jinsia moja ndio wanaoathirika zaidi wa 'mashambulizi ya kubwakwa ya kurekebishwa'.
Kwamujibu wa takwimu zilizotolewa mwaka 2017, asilimia 49 ya wapenzi wa jinsi moja wa kike nchini humo wana uwezekano mkubwa wa kumfahamu mtu ambaye ameuawa kwa kuwa tu ni mpenzi wa jinsia moja, ikilinganishwa na asilimia 26 ya wapenzi wa jinsia moja wa Kizungu.
Mara nyingi zaidi, wanaotekeleza mashambulizi hayo ya kinyama hawachukuliwi hatua za kisheria kwa matendo yao maovu.
Mauaji ya Similane hata hiyo yamekuwa na utafauti kidogo. Jina lake ma hadithi yake inaffahamika kote nchini Afrika kusini na imefanya mjadala juu ya 'mashambulizi ya kubwakwa ya kurekebishwa' kutiliwa maanani.
Baada ya kifo chake, mama yake, Mally alikuwa mstari wa mbele katika harakati za za kubadili fikra za jamii yake juu ya mapenzi ya jinsia moja kwa kutumia jukwaa la kanisa. Aliungana na mchungaji wake Smadz Matsepe katika mapambano hayo. Mali alijitoa kwa hali na mali katika harakati hizo mpaka alipofikwa na umauti mwaka 2019.
"Ilifungua macho ya wengi na ikatupa sote changamoto ya namna ya kushughulikia masuala ya wapenzi wa jinsia moja," mchungaji Matsepe ameiambia BBC.
Daraja limejengwa katika mto ambao mwili wa Simelane ulitupwa katika eneo la Kwa-Thema. Sura yake imechorwa katika daraja hilo kama kumbukumbu ya uhuru, utu na usawa kwa wote kwa mujibu wa maradi wa kutetea usawa wa wapenzi wa jinsia moja nchini humo.
Kitu kingine kinachofanyika ili kubadili fikra za watu ni kuandaliwa kwa Mhadhara wa Kumbukizi ya Eudy Similane kila mwaka. Mhadhara huo unaandaliwa na familia yake pamoja na taasisi nyengine nne ikiwemo Baraza la Wakristo la KwaZulu-Natal.
Taasisi hizo zinatambua kuwa ili kuwe na mabadiliko tarajiwa katika jamii lazima taasisi za kidini na wafuasi wake wawe na mtazamo tofauti na uliopo sasa juu ya wapenzi wa jinsia moja ili wanaotekeleza mashambulizi dhidi yao wasitumie tena vigezo vya kididni katika ukatili wanaoufanya dhidi ya wapenzi hao.
Profesa Charlene van der Walt kutoka Taasisi ya Ujamaa ya Chuo Kikuu cha KwaZulu-Natal ambayo ni moja ya taasisi zinazoandaa mhadhara wa kumbukizi ameiambia BBC kuwa:
"Hadithi ya Eudy inaakisi kinachoendelea katika familia nyingi na jamii nyingi zenye Imani za kidini, japo masuala ya wapenzi wa jinsia moja bado yanapingwa ama kufumbiwa macho katika imani."
Mhadhara huo pia hutumika kama fursa ya kuchochea mazungumzo kuhusu wapenzi wa jinsia moja.
Profesa Van der Walt ameeleza kuwa katika kipindi hiki cha janga la Covid-19 wapenzi wengi wa jinsia moja wamekuwa katika kipindi kigumu kwa kuwa wamelazimika kuwa karibu na mazingira ya kifamilia ambayo hayakubali uhalisia wao.
"Tumepiga hatua kubwa katika kuelekea njia sahihi," ameeleza.
Katika mhadhara wa mwaka 2020, kaka wa Simelane Bafana, alisema: "Historia hujirudia, hivyo kwa sasa, mhadhara huu ni sehemu ya kuizindua jamii yetu kuwa wasimchuklie mtu kuwa kama laana kisa ni mpenzi wa jinsia moja."
Licha ya kifo cha kikatili cha Simelane, tukio hilo limetuma ujumbe muhimu kote Afrika Kusini na imekuwa ni chachu ya miradi na mazungumzo ya kuwalinda wapenzi wa jinsia moja kufanyika.