Ngozi Okonjo-Iweala kuweka historia ya mwanamke na mwafrika wa kwanza kuongoza WTO

Chanzo cha picha, Reuters
Baada ya kunusurika kuchafuliwa katika siasa za Nigeria, ambako mama yake mzazi alitekwa nyara na kupanda ngazi hadi kuwa katika wadhifa wa pili katika Benki ya Dunia, Ngozi Okonjo-Iweala hatarajiwi kupata changamoto katika kuendesha majadiliano ya kibiashara kimataifa katika wadhifa wake mpya kwenye Shirika la Biashara Duniani (WTO).
Bi. Ngozi Okonjo-Iweala, 66, atakuwa mwanamke wa kwanza na mwafrika wa kwanza vilevile kushika wadhifa huo.
Licha ya kwamba hivi karibuni alipata uraia wa Marekani, alisema kwamba yeye ni raia wa Nigeria na kujivunia kuwa mzalendo - mwafrika aliyekuwa amevaa nguo yenye utambulisho wa Afrika maarufu kama kitenge.
Akizungumza na BBC mwaka 2012, alisema kwamba yeye kama mama anayefanyakazi mwenye watoto wanne, anapenda sana nguo za aina hiyo, ni nzuri na pia gharama yake ni ya chini.
Akiwa amehitimu katika chuo kikuu cha Havard, mwanamke huyo mwanauchumi anaonekana kuwa mnyenyekevu na mchapa kazi, akizungumza na kipindi cha HardTalk cha BBC mnamo mwezi Julai, alielezea kuwa kile kinachohitajika katika Shirika la Biashara Duniani ni mabadiliko.
"Wanahitaji kitu tofauti, haiwezekani mambo yakawa yanachukuliwa kama kawaida tu kwa WTO - [wanahitaji] mtu ambaye yuko tayari kufanya mabadiliko na kuongoza."
Mabadiliko aliyofanya nchini Nigeria
Katika kipindi cha miaka 25 alipokuwa akifanyakazi katika Benki ya Dunia, anatambulika kwa kuongoza miradi kadhaa kusaidia nchi zenye kipato cha chini, hasa kwa kukusanya karibu dola bilioni 50 mwaka 2010 kuotka kwa wafadhili wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kimataifa (IDA), mfuko wa Benki ya Dunia kwa ajili ya nchi maskini.
Lakini katika mabadiliko aliyoleta nchini Nigeria anayojivunia hasa -ni kuhudumu kama waziri wa fedha mara mbili chini ya rais Olusegun Obasanjo na Goodluck Jonathan.

Chanzo cha picha, Getty Images
Moja ya mafanikio yake makubwa ilikuwa ni kuongoza timu ambayo matokeo yake, nchi ya Nigeria ilifutiwa deni la dola bilioni 18.
Deni hilo lilikuwa ni la tangu miaka ya 1980 na lilikuwa limeongezeka hadi zaidi ya dola bilioni 35 kwasababu ya makosa ya kuchelewa kulilipa miaka ya 1990.
Mabadiliko yake ya kiuchumi yalikuwa na athari kubwa na kuinusuru Nigeria ilipokuwa katika kipindi kigumu, kulingana na mwanaumi mkongwe wa Nigeria, Bismarck Rewane.
Hiyo ilikuwa ni pamoja na kutenganisha bajeti yao na bei ya mafuta, na kuiruhusu nchi hiyo kuweka akiba katika akaunti maalum wakati ambapo bei ya mafuta ilikuwa juu.
"Njia hii ndio iliyonusuru uchumi wa Nigeria kutoporomaka kati ya mwaka 2008 na 2009," Bwana Rewane amezungumza na BBC.
Bi. Okonjo-Iweala aliacha kazi yake aliyokuwa analipwa mshahara mzuri na kuacha familia yake mjini Washington, ambako mume wake anafanyakazi kama bingwa wa upasuaji mfumo wa neva, ili kwenda kufanyakazi nchini Nigeria ambako tofauti na mawaziri wengine, hakuwa na bidhaa za kifahari za nyumbani au magari ya kifahari.
Yaani, alipenda sana kujipikia mwenyewe alipokuwa na wakati huku chakula maalum nchini Nigeria kikiwa ndicho anachokipenda kulingana na mahojiano aliyofanya na gazeti la Financial Times mwaka 2015.
Mbinu ya kutotaka upuuzi
Lakini mabadiliko yake hasa jinsi alivyokabiliana na ufisadi katika sekta ya mafuta ambako baadhi ya wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi walikuwa na nguvu - walidai kiasi kikubwa cha pesa kama ruzuku kutoka serikali kwa ajili ya mafuta ambayo hawakuwa wameyauza kilipatikana kwa gharama ya mtu binafasi.
Mama yake, Kamene Okonjo - daktari na profesa wa sosholojia - alitekwa nyara kutoka nyumbani kwake kusini mwa Nigeria mwaka 2012, akiwa na umri wa miaka 82.
Kutekwa nyara nchini Nigeria ni jambo la kawaida ambako biashara hiyo inasemekana kuwa na faida kubwa kwa wahalifu, na familia mara nyingi hulazimika kulipa fidia kwasababu maafisa wa kiusalama mara nyingi huwa hawafanikiwa kunasa wahalifu waliotekeleza utekaji nyara.
Mwanamke huyo aliyekuwa waziri wa fedha alisema waliomteka nyara mama yake kwanza walitaka ajiuzulu kisha wapewe fidia.
Lakini alisema alikataa kufanya yote hayo.
"Nilijua kwamba wengi wangetetea maslahi yao kwa namna yoyote ile kwasababu walikasirishwa na hatua yangu ya kupiga vita ufisadi, baadhi yao ni wahalifu waliokuwa wauzaji wa mafuta nchini," alisema alipozungumzia tukio hilo.
Bi. Okonjo aliachiwa huru ndani ya siku tano katika hali ambayo haikueleweka lakini huenda tabia ya binti yake ya kutotaka upuuzi ilihusika katika hili.
Mmoja wa vijana wake - Uzodinma Iweala, mwandishi wa riwaya ya 'Beast of No Nation' ya mwaka 2005 - amezungumzia jinsi mama yake asivyotaka upuuzi: "Mama yangu ni mwanamke mwenye nguvu. Anajua vile anavyotaka mambo kufanywa na ikiwa hutafanya anavyotaka yeye, utakuwa matatani."

Wasifu wake
- Alizaliwa mwaka 1954 nchini Nigeria
- Alisomea Harvard 1973-76 na kupata PhD yake katika Chuo cha Teknolojia cha Massachusetts (MIT) mwaka 1981
- Alifanyakazi katika Benki ya Dunia kwa miaka 25 na kupanda ngazi hadi wadhifa ambao ni wa pili kiuongozi kama mkurugenzi (2007-11)
- Alikuwa waziri wa fedha nchini Nigeria mara mbili - 2003-2006 na 2011-2015 - na mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa huo
- Alikuwa waziri wa mambo ya nje kwa kipindi kifupi mwaka 2006 na pia mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo
- Pia ni mwanachama wa bodi za Twitter, Benki ya Standard Chartered na Shirika la Kimataifa la ushirikiano wa Chanjo Duniani (GAVI)
- Aliteuliwa na rais Mohammadu Buhari kama mgombea wa wadhifa wa WTO Juni 2020

'Ninaweza kuvumilia shida'
Huenda hamasa yake ya kusonga mbele inachochewa na historia yake ya kutoka familia ya kimaskini. Aliishi na bibi yake hadi akiwa na umri wa miaka 9 kwasababu wazazi wake walikuwa nje ya nchi kusoma.
"Waliokuwa huko kwa karibu miaka kumi kabla ya mimi kuwaona na kuanza kuwatambua.
Nilifanya kila kitu ambacho msichana aliyekuwa kijijini alikifanya, kuchota maji, kwenda shambani na bibi yangu na kufanya kazi zingine zote za nyumbani, niliona na ninajua umaskini ni nini," alielezea BBC mwaka 2012.
Alichopitia akiwa kijana wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Biafra 1967-1970 kulimfanya kuwa mkakamavu zaidi.
Wazazi wake walipoteza akiba yao yote wakati wa mapigano hayo kwasababu baba yake, aliyekuwa Profesa maarufu, alikuwa Brigedia Jenerali katika vikosi vya Biafra.
"Naweza kuvumilia shida. Naweza kulala nje kwenye sakafu iliyobaridi muda wowote ule," alisema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Lakini pia ni rahisi sana kwake kucheka akiwa kwenye mahojiano, aliongeza: "Pia naweza kulala kwenye kitanda kilichotengenezwa kwa manyoya.
Lakini kujiamini kwake na kujitegemea kumemsaidia kuleta mbadiliko nchini Nigeria - kama uamuzi wake wa kuweka wazi pesa zilizotengwa kwa mwezi kwa ajili ya mamlaka za eneo katika masuala kama vile ujenzi wa barabara, uendeshaji wa shule na kliniki.
Mwanauchimi Pat Utomi anasema raia wa Nigeria hawakuwahi kujua utawala wa eneo ulikuwa unapoka kiasi gani cha pesa.
"Lakini alikuja na wazo la kuchapishwa kwa pesa hizo na kwa kifupi ikawa ni kuaibisha watu wengi," Profesa Utomi alisema.
Pia alianzisha mfumo uliosaidia kuondoa maelfu ya wafanyakazi bandia na malipo ya uzeeni kwa watu wasiokuwepo katika orodha ya wanaolipwa mshahara na serikali.
Lakini serikali ilipoamua kuondoa ruzuku ya mafuta mwaka 2012, mambo hayakwenda vizuri.
Bi. Okonjo-Iweala anasema ruzuku hiyo haikustahili kwasababu ilikuwa inagharimu serikali dola bilioni 8 kwa mwaka na kuhamasisha ufisadi.
Hata hivyo, serikali ililazimika kulegeza msimamo wake kwasababu ya maandamano yaliofanyika kote nchini humo - ingawa ruzuku hiyo imeondolewa mapema mwaka huu huku serikali ikiahidi kuweka ukomo wa kiwango cha bei inayojulikana.
Hata hivyo, wengine wanaamini kuwa ingawa mabadiliko yake yalikuwa mazuri nchini humo hayakuwa na muda mrefu."












