Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi wa Tanzania 2020: CCM yazindua rasmi kampeni Tanzania
- Author, Aboubakar Famau
- Nafasi, BBC Africa, Tanzania
- Iliyochapishwa
Chama tawala nchini Tanzania CCM, hii leo kinazindua rasmi kampeni yake huko jijini Dodoma, katikati mwa Tanzania.
Taswira ya jiji hii leo imebadilika huku kijani ikitawala kila pembe ya mji.
Bendera za chama zinaonekana kuning'izwa na kupepea kila sehemu huku picha za Rais John Magufuli ambae ndie anaepeperusha bendera ya chama na mgombea mwenza wake Bi Samia Suluhu Hassan ambae ndie makamu wa rais zimezagaa kila pembe.
Shughuli yote inafanyika katika uwanja wa Jamuhuri uliopo katikati mwa mji.
Viongozi mbalimbali wa serikali na Chama Tawala wakiwemo marais wastaafu ni miongoni mwa waliofurika katika uzinduzi huo.
Wananchi kutoka pande mbalimbali za nchi wanafuatia shughuli hiyo inayorushwa moja kwa moja katika vyombo vya habari.
Shauku iliyopo miongoni mwa wananchi ni kutaka kusikia jinsi vyama vya kisiasa vitakavyonadi sera.
Rais Magufuli ambae anaomba ridhaa ya kuongoza muhula wa pili, miongoni mwa mafanikio atakayojinasibisha nao atakapokuwa katika majukwaa ya kisiasa ni pamoja na kupambana na rushwa na kuleta nidhamu serikalini.
Huku wapinzani wake wakicheza na kete ya kubinywa kwa uhuru wa kujieleza, na haki nyingine za msingi za kiraia.
Kati ya vyama 15 ambavyo vimesimamisha wagombea urais, CCM inakuwa ya pili kuzindua kampeni baada ya chama kikuu cha upinzani Chadema kufanya uzinduzi wake jana jijini Dar es Salaam.