Virusi vya corona: Marufuku ya mirungi yawaacha matatani watafunaji Somalia

Chanzo cha picha, Getty Images
Ndege zinazobeba kichocheo cha mirungi au miraa zimezuiwa kuingia nchini Somalia, na kuwaacha watafunaji wa majani hayo katika kitoweo, wanaeleza waandishi wa BBC Mary Harper na Bella Hassan.
Kwa kawaida, mida ya saa sita, wakati mizigo ya matawi ya miraa yanapoawasili katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu kwa ndege ya Kenya, wanaume hutoweka na kukongamana katika maduka madogo ya miraa au kutafuna majumbani mwao.
Matawi hayo ambayo yanatambulika zaidi kama miraa nchini Somalia , hutumika kama kichocheo , na kuwafanya watumiaji kuchangamka. Mipango ya biashara hufanywa na kuvunjwa, na kuwafanya wanaohangaika kwa uchovu na usingizi kuwa macho.
Mwezi Machi, serikali ya Somalia ilipiga marufuku safari za ndege za kimataifa, zikiwemo ndege za miraa, kama sehemu ya juhudi za kudhibiti virusi vya corona.
Yalipoweka masharti ya kukaa nyumbani, watu walizuiwa kukusanyika kutafuna majani hayo wanayoyapenda kwa sababu kufanya hivyo kungekiuka sheria za kutokaribiana.
Maafisa walionya kwamba kwa sababu ya mikono yao hutumiwa katika kuvuna, kuuza na kutafuna miraa inaweza kusaidia kusambaza Covid-19.

Chanzo cha picha, AFP
Lakini kichocheo hiki bado kinapenya na kuingia ndani ya Somalia.
Baadhi yake huingia kwa njia ya barabara kutoka Ethiopia huku baadhi husafirishwa kwa boti kutoka Kenya, mbako wakulima wengi na wafanyabiashara wanasema wamepoteza maisha yao.
Hali inakuwa mbaya zaidi hususan katika kaunti ya kati mwa Kenya ya Meru kitovu cha ukulima wa miraa nchini Kenya.
Wafanyabiashara
Mwenyekiti wa Nyambene Miraa Traders' Association, Kimathi Munjuri, anasema kuwa wajumbe wa shirika lake waliuza nje mirungi yenye thamaini ya $250,000 (£200,000) kwa siku katika mji mkuu wa Somalia , Mogadishu.
Karibu wakulima nusu milioni wanaolima kichocheo hicho katika upembe wa Afrika, ,wengi wao wataathiriwa na marufuku.
Ingawa wengi wa wauzaiji wa miraa nchini Somalia hawana cha kuuza, wachache wamepata faida kubwa.
"Kabla ya Covid-19, tulipata majani mabichi kutoka Kenya," anasema mwanamke anayeuza miraa mjini Mogadishu. "Kwa sasa tunaipata kinyume cha sheria kutoka katika mji wa mwambao wa Kismayo, na kwasababu haipatikani kwa urahisi tunaweza kupandisha juubei yake. Nilikua ninauza kilo moja ya majani ya miraa kwa karibu $20 hadi $25. Sasa ninauza kwa $120. Marufuku hii imekua nzuri sana kwetu ."


"Mwanaume bila miraa ni kama samaki nje ya maji ," anasema Mohamed Abdi mtafunaji maarufu mjini Mogadishu. "Nanapenda sana . Lakini siwezi kuhimili kupanda kwa bei yake, kwa hiyo ninakuwa kama nimechanganyikiwa."
"Nimeacha kutafuna mirungi kwa sababu ya bei yake kubwa," anasema mtafunaji mwingine, Hassan Abdiwali. "Baadhi ya marafiki zangu wameanza kutumia vitu vingine kama dawa haramu au pombe zinazotekenezwa nyumbani . Wengine wameanza wizi ili waweze kununua miraa. Kwetu sisi wapenzi wa miraa, hali hii ni mbaya sana kuwahi kushuhudiwa ."
Miraa inayokamatwa inachomwa
Jani la milungi ni maarufu sana miongoni mwa maafisa wa usalama, ambao malipo yao ni ya chini sana kwao kuweza kununua kwa bei ya sasa .
Kumekua na ripoti kwamba polisi na wanajeshi wanaiba simu na pesa kulipia miraa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kichocheo cha miraa ni maarufu sana hususan katika jimbo lililojitangazia uhuru wake la Somaliland, ambako pia kimepigwa marufuku kwa muda kwasababu ya virusi vya corona.
Maafisa wanasema kinafanya hatua za kutokaribiana kwa watu zisitekelezwe na kwamba watathmini upya hali baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Miraa nyingi zinazoingia nchini humo husafirishwa kwa barabara kutoka Ethiopia.
Malori yaliyosheheni magunia ya miraa huingia kwa honi na kasi, kuhakikisha yanafikisha majani mabichi kabla hayajakauka . Magari yanayokamatwa wakati huu wa marufuku hukamatwa na miraa yoyote inayopatikana huchomwa.
Wasambazaji wakuu wa Somaliland wamekubaliana kupiga marufuku, wakisema afya ndio muhimu zaidi. Lakini baadhi hupenya na kuingia katika eneo hilo, pia kutafuta mauzo ya bei ya juu.
"Nilitarajia baadhi ya watu watajaribu kuuza kimagendo miraa ndani ya eneo hili wakati wa marufuku ," alisema mkazi wa Somaliland, Muse Bihi. "Lakini sikutarajia zaidi ya 30% ya watu wana uraibu kwa miraa kwamba watafanya kila kitu kuifikia ."
Baadhi ya watu wanafurahia marufuku, hususan wanaharakati wanaokampeni dhidi ya mmea huo kama Abukar Awale.
"Marufuku ni baraka kutoka angani.Unayanyasaji umepungua majumbani , talaka chache, wanawake wanafuraha kwa sababu waume zao wanatoa pesa za matumizi ya familia zao, na sio kwa dawa ya kulevya," anasema.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Uzalishaji umeongezeka kwa sababu wanaume sasa hawawezi kutumia saa sita kwa siku za kutafuna miraa.Kama Somalia inataka kustawi tena, inapaswa kutumia mamilioni ya dola zinazotumiwa katika miraa kwa ajili ya maendeleo ya nchi ,"anasema.
Bwana Awale anasema kuwa mirungi pia huharibu afya ya watu. Inaweza kuharibu meno na kuna hofu kuwa huenda miraa inasababisha saratani ya mdomo.
Baadhi ya madaktari wanasema utafunaji wa mara kwa mara wa miraa unaweza kusababisha uhaibu wake na matatizo ya kisaikolojia, ingawa Tume ya wizara ya mashauri ya kigeni ya Uingereza ambako majani hayo yalipigwa marufuku mwaka 2014 inasema hakuna ushahidi wa uhusiano wa miraa na uraibu wala matatizo ya kisaikolojia
Bwana Awale anatumai marufuku itadumu daima. Lakini huenda hilo lisiwezekane kwa sababu marufuku za awali za ndege za miraa kutoka Kenya hazijadumu.
Kuna uungaji mkono mkubwa wa biashara ya miraa nchini Somalia. Huenda wanasiasa wasipinge dawa hiyo kwani ni moja wapo ya bidha zinazochangia kwa kiwango kikubwa pato la kiuchumi na maisha ya watu kwa ujumla.
Zaidi ya hayo wengi miongoni mwa wale wanaoshikilia nyadhifa zenye mamlaka makubwa binafsi hujumuika katika utafunaji wa miraa.













