Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Israel Gaza: Umoja wa Mataifa waonya shambulio dhidi ya Rafah linaweza kusababisha 'mauaji'
Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa shambulio la Israel dhidi ya Rafah, mji wa kusini kabisa wa Gaza, huenda likasababisha "mauaji".
Moja kwa moja
Dinah Gahamanyi and Yusuf Jumah
Urusi yakanusha kwamba ilitaka kusitisha vita vya Ukraine
Kremlin inakanusha kuwa Putin alipendekeza kuwa Marekani izuie mzozo nchini Ukraine
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliita "sio kweli" ripoti ya Reuters kwamba Vladimir Putin, kupitia waamuzi, aliitaka Marekani kusitisha vita nchini Ukraine, na kwamba mazungumzo hayakufua dafu.
Kulingana na Reuters, ikinukuu vyanzo vyake, mnamo 2023, Putin hadharani na kwa faragha kupitia waamuzi, pamoja na washirika wa Waarabu wa Moscow katika Mashariki ya Kati, aliweka wazi kwa Washington kwamba yuko tayari kuzingatia uwezekano wa kusitisha mapigano nchini Ukraine.
Wakati huo huo, rais wa Urusi anadaiwa alipendekeza kusimamisha mzozo Ukrainee lakini hakutaka kuachilia eneo lolote la Ukraine ambalo Urusi ilikalia.
"Mawasiliano na Waamerika hayakuongoza popote," afisa mkuu wa Urusi anayefahamu majadiliano mwishoni mwa 2023 na mapema 2024 aliiambia Reuters kwa sharti la kutokujulikana. Wakati huo huo, chanzo cha Marekani kilikanusha habari juu ya mawasiliano yoyote yasiyo rasmi na kusema kuwa Washington haitajadili bila ushiriki wa Kyiv.
Wiki iliyopita, wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari wa Marekani Tucker Carlson, Putin kwa hakika alihutubia Wamarekani kuhusu faida za mazungumzo kwa Marekani: "Je, Marekani inahitaji mzozo huu? Kwa ajili ya nini? Hii ni maelfu ya maili kutoka eneo lako la kitaifa.
Habari za hivi punde, Bei ya mafuta Kenya yashuka kwa shilingi moja
Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli (EPRA) imetangaza kupunguza bei ya mafuta.
Bei ya mafuta yote ,ikiwemo dizeli, mafuta ya taa na petroli sasa imeshuka kwa shilingi moja kila moja.
Kwa hivyo, lita moja ya petroli itauzwa kwa Ksh206.36 huku dizeli ikiuzwa kwa Ksh195.47 Nairobi. Mafuta ya taa, kwa upande mwingine, yatauzwa kwa Ksh 93.23 kuanzia hapo kesho.
EPRA ilibaini kuwa bei hizo mpya ni pamoja na asilimia 16 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kama ilivyoainishwa na Sheria ya Fedha ya 2023, Sheria ya Kodi (Marekebisho) ya Sheria ya 2020.
Hapo awali, Super Petrol iliuzwa kwa Ksh207.36, Dizeli kwa Ksh196.47, na Mafuta ya Taa kwa Ksh194.23.
Haya yanajiri huku shilingi ikiendelea kuimarika dhidi ya dola baada ya kudorora kwa zaidi ya mwaka mmoja .
Kulingana na Benki Kuu ya Kenya, kiwango cha ubadilishaji cha Dola ya Marekani dhidi ya Shilingi ya Kenya ni Ksh158.66.
Kwa zaidi ya wiki moja mfululizo, Benki kuu ya Kenya CBK ilifichua kuwa shilingi imeendelea kuimarika, ikihusisha faida hiyo kutokana na fedha za kigeni na sekta ya Utalii inayostawi.
Habari za hivi punde, Israel yatekeleza mashambulizi makubwa dhidi ya Lebanon
Israel imeanzisha "wimbi kubwa la mashambulizi" nchini Lebanon baada ya mwanamke mmoja kuuawa na wengine kujeruhiwa katika shambulio la roketi kaskazini mwa Israel.
Vyombo vya habari vya Lebanon viliripoti kwamba vijiji vimeshambuliwa na majengo yameteketea.
Hezbollah, ambayo inadhaniwa kufanya mashambulizi dhidi ya Israel, haijadai kuhusika.
Pande hizo mbili zimekuwa zikichokozana mara kwa mara katika mpaka wa kaskazini wa Israel tangu mashambulizi ya Oktoba 7 yaliyofanywa na Hamas.
"Ndege za kivita zilianza wimbi kubwa la mashambulizi katika eneo la Lebanon," msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF), Daniel Hagari, aliandika kwenye X (zamani Twitter) siku ya Jumatano.
Bw Hagari alisema IDF itatoa maelezo zaidi kuhusu mashambulizi yake ya hivi punde katika saa zijazo.
Mashambulizi kutoka Lebanon kaskazini mwa Israeli yalipiga eneo la Safed, na yalilenga katika kituo cha amri cha kaskazini cha jeshi la Israeli, IDF ilisema.
Video inaonyesha roketi moja ikitua karibu na lango la hospitali.
Hezbollah - shirika la Waislamu wa Shia - ni mojawapo ya vikosi vya kijeshi vilivyo na silaha nyingi, zisizo za serikali duniani.
Ilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1980 na mamlaka kuu ya Shia katika eneo hilo, Iran, ili kuipinga Israel.
Video: Tazama meli ya Urusi ikishambuliwa na Ukraine na kuzamishwa baharini
Ukraine yadai kuishambulia na kuizamisha meli ya Urusi Ceasar Kunikov huko Crimea
Meli kubwa ya kivita ya Urusi, Caesar Kunikov, imezama kwenye pwani ya Crimea inayokaliwa na Urusi kulingana na vikosi vya jeshi vya Ukraine.
Milipuko mikali ilisikika mapema Jumatano asubuhi, kulingana na mtandao wa kijamii wa eneo hilo, ambao ulisema meli hiyo iliyokuwa ikiwasili ilishambuliwa karibu na kusini mwa mji wa Yalta.
Ukraine imeshambulia mara kwa mara meli za Bahari Nyeusi za Urusi katika eneo linalokaliwa la Crimea.
Picha za satelaiti mwaka jana zilionyesha sehemu kubwa ya meli zilikuwa zimeondoka kwenye rasi hiyo.
Kurugenzi Kuu ya Ujasusi wa Ukraine ulichapisha video ya kile ilichosema ni ndege zisizo na rubani za Magura V5 zikiishambulia meli hiyo iliyowasili.
Vita kamili vya Urusi nchini Ukraine vinatarajiwa kuingia mwaka wake wa tatu wiki ijayo na mkuu wa majeshi ya Ukraine amekiri kuwa hali ni "tata mno".
Kanali Jenerali Oleksandr Syrskyi, ambaye aliteuliwa kuwa kamanda mkuu wiki iliyopita, alitembelea mstari wa mbele siku ya Jumatano saa chache baada ya shambulio la kombora la Urusi kuwaua watu watatu katika mji wa mashariki wa Selydove.
Hakukuwa na uthibitisho kutoka kwa jeshi la wanamaji la Urusi kwamba meli ya Kaisari Kunikov ilizamishwa katika Bahari Nyeusi, isipokuwa tu kwamba ndege sita zisizo na rubani za Ukraine ziliharibiwa. Video inayoonekana kuonyesha matokeo ya shambulizi la Ukraine ilipakiwa hivi majuzi tu, BBC Verify ilithibitisha.
"Caesar Kunikov ilipata mashimo makubwa katika upande wa bandari yake na kuanza kuzama," idara ya ujasusi ya Ukraine ilisema kwenye tovuti ya ujumbe wa Telegram, na kuongeza kuwa ilikuwa imeharibiwa katika eneo la maji la Ukraine na kitengo kinachoitwa Kundi la 13.
Meli za amphibious hutumiwa kuhamisha askari wa mashambulizi ili kuwasili haraka, hasa katika eneo la adui. Urusi pia imetumia meli za kutua katika miaka ya hivi karibuni kusafirisha vifaa vya kijeshi hadi Syria, ili kuunga mkono serikali ya Bashar al-Assad.
Wanablogu wa kijeshi wa Urusi hawakukanusha kuwa Caesar Kunikov ilishambuliwa , wakisema tu kwamba wafanyakazi walikuwa wamenusurika. Jeshi la Urusi mara chache huripoti hasara kubwa na Warusi hutegemea wanablogu wachache maarufu kwa habari.
Kaisari Kunikov ilianzia mwisho wa enzi ya Soviet. Ikiwa kuzama kwake kutathibitishwa, litakuwa shambulio la pili lenye mafanikio katika Bahari Nyeusi mwezi huu.
Meli ndogo ya kivita, Ivanovets, ilipigwa na ndege zisizo na rubani katika operesheni maalum karibu wiki mbili zilizopita.
Meli nyingine ya Urusi iliyowasili, Novocherkassk, ilishambuliwa ikiwa bandarini Feodosiya mwezi Desemba.
Racheal Kundananji: Safari ya mshambuliaji wa Zambia kuvunja rekodi ya uhamisho wa wanawake
Racheal Kundananji alikuwa akicheza kwenye viwanja vichache vya Jimbo la Copperbelt nchini Zambia miaka sita iliyopita - lakini sasa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 ndiye mwanasoka mwenye gharama ghali zaidi wa kike duniani katika historia.
Imekuwa hatua ya kushangaza kwa fowadi huyo, mwenye talanta kali ambaye alishawishi Bay FC ya Ligi ya Soka ya Kitaifa ya Wanawake ya Marekani (NWSL) kutoa $860,000 (£685,000) ili kuondokaMadrid CFF.
Ada hiyo inazidi kiwango kilichowekwa na Keira Walsh cha uhamisho wa£400,000 kutoka Manchester City kwenda Barcelona mnamo 2022.
Cha muhimu ni kwamba Kundananji ndiye mchezaji wa kwanza wa Kiafrika, mwanamume au mwanamke, kuvunja rekodi ya uhamisho ya dunia.
Anahamia Marekani baada ya muda mwingi wa miezi 18 huko Madrid ambapo alifunga mabao 33 ya Liga F katika michezo 43.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Zambia bado anakubaliana na ukubwa wa ada yake ya uhamisho lakini anajua mahali pa kwanza anapoweza kupata usaidizi ni kutoka nchi yake.
"Watu nchini Zambia watashangaa lakini watafurahi sana," Kundananji aliambia BBC Sports Africa
“Watu wengi wamenitia moyo kufanya kazi kwa bidii na wengine hata wakasema ‘labda siku moja utavunja rekodi’.
"Nataka kuwapa mashabiki wa [Bay FC] kile wanachotaka - kufurahia michezo, kufurahia kuniona nikicheza na kufunga."
Mayai ya uzazi yaliyogandishwa yahofiwa kupata hitilafu katika kliniki London
Zaidi ya wanawake 100 waliokuwa na mayai na viinitete vilivyogandishwa katika kliniki maarufu wameambiwa kuwa huenda vimeharibiwa kutokana na hitilafu katika mchakato wa kugandisha.
Kliniki hiyo, iliyopo katika Hospitali ya Guy's mjini London Uingereza, imesema huenda ilitumia bila kukusudia baadhi ya chupa zenye hitilafu za kugandisha mayai hayo na viini tete mnamo Septemba na Oktoba 2022.
Lakini ilisema haikujua iwapo kimiminika hicho cha kugandisha mayai kilikuwa na kasoro wakati huo.
Mamlaka ya udhibiti wa viwango vya Urutubishaji wa Binadamu na Kiinitete (HFEA), inachunguza tukio hilo.
Inaaminika kuwa wagonjwa wengi kati ya 136 walioathiriwa wamepata matibabu ya saratani tangu mayai au viini vyao vigandishwe, jambo ambalo linaweza kuwafanya wagumba. Hii inamaanisha kuwa sasa huenda wasiweze kupata mimba kwa mayai yao wenyewe.
Wagonjwa wameambiwa hivi majuzi tu kwamba mayai yao na viinitete huenda visiweze kustahimili mchakato wa kuyeyushwa iwapo vingegandishwa kwa kutumia myeyusho usiofaa.
Afrika Kusini yawasilisha ombi la dharura kwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki kusitisha shambulio la Israel dhidi ya Rafah
Afrika Kusini imewasilisha ombi la dharura kwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuzingatia kuwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Rafah yanaweza kusababisha ukiukwaji zaidi wa haki za Wapalestina, Gaza.
Serikali ya Afrika Kusini inasema "ina wasiwasi" kuhusu uwezekano wa mauaji makubwa zaidi.
Mwezi uliopita, Mahakama ya Kimataifa ya Haki iliiamuru Israel kuchukua hatua zote zinazowezekana kuzuia vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina.
Afrika Kusini ilisisitiza kwamba kuanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Rafah "itakuwa ni ukiukaji wa Mkataba wa Mauaji ya Kimbari.’’
Unaweza pia kusoma:
- Kivuko cha Rafah ni nini na kwa nini ndicho kivuko pekee 'kinachoipa uhai' Gaza?
- Israel Gaza: Biden aitaka Israel kuwalinda raia wa Rafah
Mshukiwa wa mauaji wa Marekani aliyetoroka kutoka kituo cha polisi cha Kenya akamatwa
Kevin Kinyanjui Kangethe mkimbizi wa Marekani ambaye alitoroka kutoka kituo cha polisi kwa siri amekamatwa kwa mujibu wa polisi wa Kenya.
Ncha kutoka kwa wananchi iliwafanya polisi mafichoni kwake katika mji wa Ngong kilomita 23 nje kidogo ya jiji la Nairobi
Wiki iliyopita, polisi walizindua msako baada ya Kevin kuteleza mikononi mwa maafisa.
Mtu mmoja aliyejitambulisha kama wakili wake aliwaomba polisi wazungumze naye kabla ya kukatiza usafiri wa umma.
Mkuu wa polisi wa Nairobi alisema kuwa kutoroka kwa mshukiwa huyo mikononi mwa maafisa wa usalama ni aibu. Maafisa wanne wa polisi waliokuwa kazini wakati wa kutoroka kwake- pamoja na wakili huyo walikamatwa.
Siku ya Jumanne, watu wengine wawili akiwemo kaka yake Kevin pia walikamatwa.
Maafisa nchini Marekani wanasema kuwa Kevin alimuua mpenzi wake Margaret Mbitu mwezi Oktoba mwaka jana, na kuutelekeza mwili wake katika gari katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Boston Logan.
Kisha akapanda ndege kwenda Kenya, nchi yake ya nyumbani.
Polisi wa Kenya walimkamata miezi kadhaa baadaye wakati alipokuwa nje usiku mjini Nairobi.
Mahakama ilitarajiwa kutoa uamuzi siku ya Ijumaa iwapo Kevin ashtakiwe nchini Kenya au apelekwe mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji ya kiwango cha kwanza nchini Marekani, baada ya kudai kuwa aliachana na uraia wake wa Marekani mwaka jana.
Mawakili wake walimtaka mwendesha mashtaka kuonyesha ushahidi kwamba alitoroka akisema kuwa maisha yake yalikuwa hatarini.
Kevin kwa sasa yuko rumande akisubiri mashtaka zaidi kufuatia kutoroka kwake.
Mwanzilishi wa Amazon Jeff Bezos auza hisa zenye thamani ya zaidi ya $4bn
Bilionea Jeff Bezos ameuza zaidi hisa zake za Amazon, na kufikisha jumla ya thamani ya mauzo ya hadi zaidi ya $4bn (£3.2bn) katika siku za hivi karibuni.
Kampuni hiyo kubwa ya teknolojia, ambayo aliianzisha mwaka wa 1994, ilisema Bw Bezos ameuza hisa milioni 24 za Amazon mwezi huu.
Bw Bezos, ambaye ndiye mwenyekiti mkuu wa kampuni hiyo, mara ya mwisho aliuza hisa za Amazon mnamo 2021.
Mapema mwezi huu, kampuni hiyo ilisema inapanga kuuza hisa milioni 50 katika mwaka ujao, ambazo zina thamani ya karibu $ 8.4bn kwa bei ya sasa.
Uuzaji wa kwanza wa hisa milioni 12 ulitangazwa katika jarida la taarifa za kibiashara mnamo siku ya Ijumaa, ukifuatiwa na tangazo la uuzaji wa pili wa hisa nyingine milioni 12 siku ya Jumanne.
Bw Bezos ataokoa karibu dola $280 kwenye hisa zenye thamani ya $4bn ambazo ameuza alipokuwa akihamia Miami-Florida kutoka Seattle Washington mwaka jana.
Faida ya zaidi ya $250,000 kutokana na mauzo ya hisa au uwekezaji mwingine wa muda mrefu, hutozwa ushuru wa 7% katika jimbo la Washington. Florida haina ushuru wa serikali juu ya mapato au faida ya mtaji.
Lakini bado atawajibika kutoa ushuru wa shirikisho kwa kuuza hisa zake.
Bw Bezos alipotangaza kuhamia Florida ulizuka uvumi kuhusu iwapo ni kwa sababu ya bili ya kodi ambayo angekabiliana nayo Washington baada ya serikali kuidhinisha ushuru mpya kwa mauzo makubwa ya hisa.
Mnamo mwezi Novemba Bw Bezos alisema kwamba wazazi wake walirudi Miami hivi karibuni ambako aliishi katika maisha yake ya utotoni na kwamba alitaka kuwa karibu nao na mradi wake wa anga za juu wa Blue Origin, ambao "ulikuwa ukihamia Cape Canaveral".
“Lauren and I love Miami,” aliandika kwenye Instagram, akimzungumzia mchumba wake Lauren Sánchez.
"Kwa hayo yote, ninapanga kurudi Miami, nikiondoka Kaskazini Magharibi mwa Pasifiki," aliongeza.
Bw Bezos anasalia kuwa mbia mkubwa wa Amazon na ni mmoja wa watu tajiri zaidi duniani, akiwa na utajiri unaokadiriwa kuwa zaidi ya $190bn.
Unaweza pia kusoma:
- Jeff Bezos: Mtindo wa uhisani wa Marekani unafanana na ule wa Uingereza?
- Jeff Bezos: Fahamu safari ya dakika 11 kwenda angani iliofanywa na bilionea
- Jeff Bezos: Ijue siri ya mafanikio ya mtu tajiri zaidi duniani
Rwanda yasitisha kwa muda mkataba wa mchezaji wa DRC baada ya kuonyesha ishara ya kisiasa uwanjani
Chama cha Soka cha Rwanda kimemsimamisha kwa muda kucheza soka nchini humo mchezaji wa kimataifa wa Congo Héritier Luvumbu kwa kuonyesha ishara ya kisiasa wakati wa mashindano .
Mchezaji huyo raia wa Congo anayechezea klabu ya Rayon Sport ya Rwanda anadaiwa kuonyesha ishara hiyo wakati timu yake ilipokuwa ikicheza dhidi ya timu ya polisi ya Rwanda- Polisi Football Club, Jumapili iliyopita wakati wa Ligi Kuu ya Rwanda.
Inasemekana Héritier Luvumbualionekana akifunga mdomo wake kwa mkono wake wa kushoto, huku akielekeza vidole vyake viwili kichwani, baada ya kufunga bao moja kwa bila.
Ishara hiyo hiyo inalenga kukemea ukimya wa Jamii ya Kimataifa kuhusu mauaji ambayo yamekuwa yakifanyika nchini mwake, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Serikali ya DRC inailaumu Rwanda kama nchi inayotoa msaada kwa moja ya makundi makuu ya waasi yaliyoteka maeneo ya mashariki mwa DRC, M23
Tuhuma kama hizo pia zimeungwa mkono na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini Rwanda inakanusha kuhusika na mzozo huo.
Ishara hiyo pia kilionyeshwa na Timu ya Taifa ya DRC katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, wakati ikicheza dhidi ya wenyeji, Ivory Coast wakati wa nusu fainali, tarehe 7 Februari 2024.
Héritier Luvumbu anadai kuwa ishara hiyo imemfanya akemewe mtandaoni, na sasa ana wasiwasi kuhusu usalama wake nchini Rwanda.
Kabla ya kuondoka DRC, mshambuliaji huyo alikuwa akiichezea AS Vita Club, iliyoanzishwa mwaka 1935 na klabu moja kongwe ya soka katika mji mkuu Kinshasa.
Taarifa za hivi punde zinasema kuwa Rayon Sports inasema imeachana na kiungo wa zamani wa Congo, Nzinga Luvumbu.
Rayon Sports inasema kuwa uamuzi huo ulifanywa "kwa makubaliano ya pande zote mbili", lakini ulitokea baada ya shirikisho la soka nchini Rwanda, FERWAFA, kumuadhibu Luvumbu kwa kusimamishwa kwa miezi sita kwa 'ishara za kisiasa' uwanjani.
Biden autaja ukosoaji wa Trump dhidi ya Nato kama "aibu"
Rais Joe Biden ameutaja ukosoaji wa NATO na mpinzani wake wa uchaguzi wa 2024, Donald Trump, kama usio na maana wa "aibu" na "kinyume na usio wa Kimarekani’’.
Bw Biden alimkemea Bw Trump kwa kusema "ataihimiza" Urusi kumshambulia mwanachama yeyote wa Nato ambaye hafikii kiwango chake cha matumizi ya ulinzi.
Rais huyo wa Marekani alisema matamshi hayo yanasisitiza udharura wa kupitisha kiwango cha msaada wa kigeni cha $95bn (£75bn) kwa washirika wa Marekani.
Mswada huo ndio umepitishwa na Seneti, lakini unakabiliwa na upinzani wa kisiasa katika Bunge hilo.
Katika Ikulu ya Marekani Jumanne, Bw Biden alisema kushindwa kupitishwa kwa kiasi hicho cha pesa - ambacho kinajumuisha $60bn kwa Ukraine - "kutakuwa ni sawa na kuchezea mikononi mwa Putin".
Alisema hatari hiyo imeongezeka kwa sababu ya matamshi "hatari" ya Bw Trump mwishoni mwa juma.
"Hakuna rais mwingine katika historia ambaye amewahi kumsujudia dikteta wa Urusi," Bw Biden alisema.
"Hebu niseme hili kwa uwazi niwezavyo. Siwezi kamwe. Kwa ajili ya Mungu. Ni aibu. Ni hatari. Sio umarekani."
Katika mkutano wa Jumamosi huko South Carolina, Bw Trump, ambaye ni mwanachama wa Republican, alikosoa alichokiita malipo ya "ukaidi" ya wanachama wa Nato.
Trump alielezea kuhusu mazungumzo ya siku za nyuma ambayo alisema alikuwa nayo na mkuu wa "nchi kubwa" kuhusu mashambulizi yanayoweza kufanywa na Urusi.
Bw Trump alisema afisa huyo aliuliza ikiwa Marekani ingemtetea mwanachama wa Nato ambaye hajatimiza wajibu wake wa kifedha.
"Nilisema: 'Hukulipa? Wewe ni mhalifu?'" Bw Trump aliuambia umati. "'Hapana nisingekulinda, kwa kweli ningewahimiza kufanya chochote wanachotaka. Lazima ulipe."
Bw Biden alisema mtangulizi wake alikuwa akiuchukulia muungano wa kijeshi kama njama ya ulinzi.
Israel Gaza: Umoja wa Mataifa waonya shambulio dhidi ya Rafah linaweza kusababisha 'mauaji'
Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ameonya shambulio la Israel dhidi ya Rafah, mji wa kusini kabisa wa Gaza, huenda likasababisha "mauaji".
Mkuu wa masuala ya kibinadamu Martin Griffiths amesema Wapalestina mjini Gaza tayari wanateseka kutokana na "mashambulizi makubwa yasiyo na mfano, na ukatili mkubwa".
Matokeo ya uvamizi wa Rafah yatakuwa "janga", alisema.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kuwashinda wapiganaji wa Hamas anaosema wamejificha katika mji huo.
Katika taarifa yake yenye maneno makali , Bw Griffiths alisema zaidi ya watu milioni moja "wamejazana mjini Rafah, wakitazama kifo usoni". Alisema raia katika jiji hilo wana chakula kidogo na upatikanaji wa dawa ni wa kiwango cha chini na "hakuna mahali salama pa kwenda".
Aliongeza kuwa uvamizi wa Israeli katika mji huo, "utaacha operesheni dhaifu ya kibinadamu kwenye mlango wa kifo".
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alikiambia kipindi cha BBC cha Newshour kuwa Umoja wa Mataifa ghautapokea mpango wowote wa kuwahamisha wa Rafah kutoka kwa Israel na hautashiriki katika uhamishaji wowote wa lazima.
Stephane Dujarric alisema: "Umoja wa Mataifa hautakuwa sehemu ya kuwalazimisha watu kuhama."
Unaweza pia kusoma:
- Kivuko cha Rafah ni nini na kwa nini ndicho kivuko pekee 'kinachoipa uhai' Gaza?
- Israel Gaza: Biden aitaka Israel kuwalinda raia wa Rafah
Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja, leo ikiwa ni tarehe 14.02.2024