Watu watano waliokuwa wenye ndege ya walinzi wa pwani ya Japan wafariki

Watu watano waliokuwa kwenye ndege ya walinzi wa pwani wamefariki, shirika la habari la AFP limemnukuu waziri wa uchukuzi wa Japan akisema.

Moja kwa moja

Rashid Abdallah and Esther Namuhisa

  1. Habari za hivi punde, Afisa mkuu wa Hamas auawa katika mlipuko wa Beirut

    xx

    Chanzo cha picha, Reuters

    Afisa wa ngazi ya juu wa Hamas aliuawa katika mlipuko huo kwenye vitongoji vya kusini mwa Beirut vya Dahiyeh, ripoti za AFP na Reuters, zikinukuu vyanzo vya usalama.

    Kundi la Hama limethibitisha kifo cha naibu mkuu wake, Saleh al-Arouri katika mlipuko uliotokea kusini mwa Beirut.

    Al-Arouri alikuwa naibu mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, ambaye alijulikana kuhusika sana katika masuala yake ya kijeshi.

  2. Picha za kwanza kutoka Beirut

    Picha za kwanza za mlipuko katika mji mkuu wa Lebanon Beirut sasa zimeanza kutufikia.

    Vyombo vya habari vya serikali ya Lebanon vinaripoti kwamba ofisi ya Hamas huko Dahiyeh, moja ya vitongoji vya kusini mwa mji huo, imeshambuliwa..

    Vyombo vya habari vya nchi hiyo pia vinasema watu wanne wameuawa katika mlipuko huo.

    Kundi kubwa linakusanyika nje ya jengo lililoharibiwa huko Dahiyeh

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Watu wamekusanyika nje ya jengo lililoharibiwa huko Dahiyeh
    xx

    Chanzo cha picha, Reuters

    xx

    Chanzo cha picha, Getty Images

  3. Habari za hivi punde, Watu wanne waliuawa katika mlipuko wa Beirut- Vyombo vya habari vya Lebanon

    Watu wanne wameuawa katika mlipuko huo uliolenga ofisi ya Hamas katika kitongoji kimoja kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.

    BBC bado haijaweza kuthibitisha ripoti hizo, lakini tunajitahidi kukuletea maelezo kadri tutakavyozipokea.

  4. Habari za hivi punde, Mlipuko mkubwa waripotiwa Beirut

    Mlipuko mkubwa umeripotiwa huko Beirut muda wa nusu saa iliyopita.

    Mlipuko huo uliripotiwa Dahieh, kitongoji chenye uhusiano mkubwa na kundi la Hezbollah, mshirika wa Hamas.

  5. Wakenya wahimizwa kutumia barabara mbadala baada ya kupanda kwa ushuru

    Shirika la Barabara na Madaraja la China (CRBC) linaendesha barabara kuu chini ya ubia kati ya sekta ya umma na ya binafsi na hutoza ada za ushuru ili kurejesha gharama za ujenzi

    Chanzo cha picha, AFP

    Mamlaka nchini Kenya imewashauri madereva kutumia barabara mbadala kufuatia malalamishi kuhusu ongezeko la tozo katika barabara kuu katika mji mkuu.

    Serikali imeongeza ada katika Barabara ya mwendo kasi (Nairobi Expressway) barabara kuu ya kilomita 27 (maili 17), kwa hadi 39%. Kwa njia ya gharama kubwa zaidi, ada zimepanda kutoka $2.29 (£1.80) hadi $3.18.

    Hatua hiyo imezua hasira nchini humo. Baadhi ya Wakenya wametaja upandaji huo kuwa kupita kiasi na kusema bei hizo mpya zimewekwa bila idhini ya umma au bunge.

    Ongezeko hilo linakuja huku kukiwa na ongezeko la gharama ya maisha nchini Kenya.

    Serikali pia iliongeza idadi ya kodi na tozo mwaka jana, kama vile gharama ya kupata hati kama vile pasipoti na vyeti vya ndoa.

    Akitetea ongezeko la ushuru, Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen alisema Jumatatu. "Marekebisho hayo yalifanywa kulingana na makubaliano ya mradi kwa kuzingatia kushuka kwa thamani ya shilingi ya Kenya hadi dola ya Marekani tangu wakati wa kutangazwa kwa viwango vya ushuru mnamo Aprili 2022 katika gazeti la serikali.

    ”Barabara ya Nairobi Expressway yenye thamani ya $550m (£410m) ilijengwa ili kupunguza msongamano wa magari huku kukiwa na msongamano ambao umezidi kuwa mbaya katika miaka ya hivi karibuni. Shirika la Barabara na Madaraja la China (CRBC) linaendesha barabara kuu chini ya ubia kati ya sekta ya umma na ya binafsi na hutoza ada za ushuru ili kurejesha gharama za ujenzi.

  6. Watu wawili wafikishwa mahakamani Kenya kwa tuhuma za kumuua mwanariadha wa Uganda

      • Author, Kelvin Kimathi
      • Nafasi, BBC Nairobi
    Benjamin Kiplagat alipatikana amefariki ndani ya gari lake siku ya Jumapili karibu na mji wa Eldoret nchini Kenya

    Chanzo cha picha, AFP

    Washukiwa wawili wamefikishwa mbele ya mahakama mjini Eldoret kuhusu mauaji ya mwanariadha Edward Kiplangat almaarufu Benjamin.

    Washukiwa hao wawili ni pamoja na David Ekhai Lokere almaarufu Timo mwenye umri wa miaka 25 na Peter Ushuru Khalumi mwenye umri wa miaka 30.

    Walifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Kesse Cherono ambaye aliwaruhusu polisi kuwazuia washukiwa hao kwa siku 21 ili kuwezesha upelelezi kukamilika.

    Cherono alisema alikuwa amezingatia ukweli kwamba amani ya umma ilivurugwa kufuatia tukio hilo. Afisa Mkurugenzi wa mashtaka Inyasio Mwaniki anayeishi katika kaunti ndogo ya Moiben huko Uasin Gishu alikuwa ameiambia mahakama kuwa bado wanachunguza kisa hicho.

    Alisema mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa kwenye dimbwi la damu ukiwa na majeraha ya mapanga. Alisema wawili hao walikamatwa mnamo Januari 1, 2024, Eldoret na Kitale na wanashukiwa kumuua mwanariadha huyo.

    "Bado hatujafanya uchunguzi wa marehemu na vielelezo muhimu vilivyokusanywa kutoka kwa washukiwa bado havijachukuliwa ili kuchunguzwa na wakemia wa serikali," afisa huyo wa DCI alisema.

    Alisema picha za CCTV kutoka eneo la uhalifu pia bado hazijachambuliwa na kitengo cha uhalifu wa mtandao.

    Afisa huyo wa DCI pia alibaini kuwa rekodi za simu za mkononi pia hazijachukuliwa pamoja na nambari za usajili za gari na pikipiki iliyopatikana katika eneo la tukio.

    Mwaniki alisema pia bado hawajaandika taarifa kutoka kwa mashahidi katika eneo la tukio. Aliongeza kuwa taarifa muhimu kutoka kwa ubalozi wa Uganda kuhusu hali ya marehemu kabla ya kifo chake bado hazijafahamika. “Ni kwa ajili ya haki walalamikiwa kuzuiliwa kwa siku 21 ili kuwezesha upelelezi kukamilika,” alisema ofisa huyo.

    Wakili George Sonkule wa mshtakiwa alinukuu Muswada wa Haki katika Katiba akisema kuwa washukiwa wana haki ya uhuru.

    Matokeo ya Wavuti yaliyo na Viungo vya Tovuti

  7. Israel kupinga tuhuma za Afrika Kusini The Hague kuhusu 'mauaji ya halaiki' huko Gaza

    Mama na mwana

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Israel itafikishwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kupinga shtaka la Afrika Kusini la "vitendo vya mauaji ya halaiki" huko Gaza, msemaji wa serikali ya Israel amesema.

    Siku ya Ijumaa, Afrika Kusini iliwasilisha kesi katika ICJ, chombo kikuu cha mahakama cha Umoja wa Mataifa.

    Kufuatia maombi yake kwa ICJ, rais wa Afrika Kusini alisema kuwa nchi hiyo inalazimika "kuzuia mauaji ya halaiki kutokea".

    Katika kujibu, msemaji Eylon Levy alisema katika kikao fupi siku ya Jumanne: "Nchi ya Israel itafikishwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki huko The Hague ili kuondoa kashfa ya kipuuzi ya umwagaji damu ya Afrika Kusini.

    "Tunawahakikishia viongozi wa Afrika Kusini, historia itawahukumu, na itawahukumu bila huruma."

    Afrika Kusini imekuwa ikiikosoa sana Israel katika operesheni yake ya kijeshi huko Gaza. Vita vya sasa kati ya Israel na Hamas vilichochewa na shambulio la Oktoba 7 lililofanywa na Hamas kusini mwa Israel.

    Hamas iliua takribani watu 1,200, wengi wao wakiwa raia. Pia walichukua mateka wengine wapatao 240.

    Zaidi ya watu 22,000, wengi wao wakiwa watoto na wanawake, wameuawa huko Gaza wakati wa mashambulizi ya Israel, kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas.

    ICJ iko mjini The Hague, Uholanzi. Inasuluhisha mizozo kati ya nchi na inatoa ushauri kuhusu masuala ya kisheria ya kimataifa.

  8. Hakuna mtu mwenye akili timamu anayekubaliana na matokeo ya uchaguzi DRC, asema Fayulu

    Wito wa Martin Fayulu wa uchaguzi mpya umekataliwa na serikali

    Chanzo cha picha, AFP

    "Hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kukubaliana" kwamba Rais aliye madarakani Félix Tshisekedi alishinda kihalali muhula wa pili katika uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, mgombea wa upinzani amesema.

    Katika mahojiano na kipindi cha Newsday cha BBC mnamo Jumanne, Martin Fayulu alitoa maoni mapya ya kufutwa kwa matokeo ya Jumapili.

    Maafisa walisema Bw Tshisekedi alishinda karibu 73% ya kura.

    Uchaguzi huo, ambao ulifanyika tarehe 20 Desemba, ulikumbwa na matatizo mengi ya vifaa na kiufundi.

    Kufuatia kutangazwa kwa matokeo hayo, Bw Fayulu na wagombea wengine kadhaa wa upinzani walidai kuwa kulikuwa na udanganyifu katika uchaguzi na kukithiri kwa dosari.

    Ujumbe wa uchunguzi unaoendeshwa na Kanisa Katoliki na makanisa ya Kiprotestanti pia ulibainisha "matukio mengi ya ukiukaji".

    Akizungumza na BBC, Bw Fayulu alisema kuwa kutokana na umati wa watu waliokusanyika kwenye mikutano yake ya kampeni, wazo la kwamba alipata asilimia 5 pekee ya kura ni la kushangaza.

    Aliongeza: "Tshisekedi hawezi kunishinda hata hivyo, hawezi kunishinda! "Watu wa Congo wako pamoja nami. Hakuna atakayemfuata Tshisekedi.

    Anaweza kwenda kwa nguvu, lakini hakuna atakayemfuata." Bw Fayulu alitoa wito wa kufanyika uchaguzi mpya, matakwa ambayo yamekataliwa na msemaji wa serikali ya DR Congo na Waziri wa Habari Patrick Muyaya.

    "Ni kweli kulikuwa na matukio lakini matukio haya hayakuweza kubadilisha matokeo ya uchaguzi wa urais," Bw Muyaya alisema katika mahojiano ya awali na kipindi cha Newsday cha BBC.

    "Ni sawa ikiwa wanataka kutumia njia za kisheria kuwania uchaguzi. Hiyo ni sheria. Wana haki ya kufanya hivyo lakini wakati huohuo wanapaswa kuhakikisha kwamba wanaweza kutoa uthibitisho wa kile wanachobishana,” Bw Muyaya aliongeza.

    Alisema kuwa serikali "haitavumilia machafuko" kutoka kwa wanasiasa wa upinzani wasiofurahishwa na matokeo ya uchaguzi.

  9. Mwanafunzi raia wa China apatikana Marekani baada ya 'kutekwa nyara kwa njia ya mtandao'

    Kai Zhuang anadaiwa kuwa mwathirika wa utekaji nyara mtandaoni

    Chanzo cha picha, RIVERDALE POLICE DEPARTMENT

    Mwanafunzi wa masuala ya biashara ya fedha za kigeni wa China amepatikana akiwa ameganda lakini akiwa hai nchini Marekani baada ya wazazi wake kutapeliwa makumi ya maelfu ya dola katika tukio la "utekaji nyara kwa njia ya mtandao".

    Kai Zhuang aligunduliwa "akiwa amezidiwa na baridi sana na mwenye hofu" katika hema moja katika kijiji cha Utah, Polisi wa Riverdale walisema katika taarifa.

    Kijana huyo mwenye umri wa miaka 17 anaaminika kujitenga baada ya kudanganywa na watekaji nyara.

    Wazazi wake walidanganywa kulipa karibu $80,000 (£62,600).

    Zhuang ni mmoja wa wanafunzi wa kigeni wanaolengwa na wale wanaoitwa watekaji nyara wa mtandaoni nchini Marekani hivi karibuni, Polisi wa Riverdale waliongeza katika taarifa yao.

    Polisi wanaamini kuwa Kai alikuwa akidhibitiwa na watekaji nyara mapema Desemba 20, alipoonekana na maafisa wa Provo, Utah, akiwa amebeba vifaa vya kupigia kambi.

    Maafisa hao walipanga arejeshwe Riverdale, ambako aliishi na familia iliyompokea, kutokana na wasiwasi wa usalama wake. Hata hivyo, hakutaja vitisho vyovyote wakati huo.

    Polisi waliwasiliana mnamo tarehe 28 Desemba na shule aliyokuwa akisoma, ambayo ilikuwa imewasiliana na wazazi wake nchini China.

    Wazazi wa Kai walikuwa wamewaambia maafisa wa shule kuwa wametumwa ombi la fidia na picha ya mtoto wao ikionesha kuwa alitekwa nyara.

    Kulingana na polisi, waathiriwa wa utekaji nyara wa mtandao hushawishiwa kujitenga, na hata kupiga picha zao ili ionekane wanashikiliwa, licha ya watekaji nyara kutokuwepo.

    Badala yake, mwathirika anafuatiliwa kupitia Facetime au Skype.

    Wote mwathiriwa na familia zao basi wanashawishika kuwa mwingine atadhurika ikiwa hawatatii.

    Lakini licha ya watekaji nyara hao kutokuwa na Kai, polisi huko Utah bado wanahofia usalama wake, wakieleza halijoto ya mwezi Disemba ilimaanisha kuwa kuna hatari ya "kuganda hadi kufa usiku kucha".

  10. Moto bado unawaka katika picha za hivi punde kutoka eneo la tukio

    Tumekuwa tukipokea picha zaidi kutoka eneo la tukio kwenye Uwanja wa Ndege wa Haneda - hizi hapa ni baadhi ya picha za hivi punde:

    Lori la zima moto limeketi nyuma ya bawa la ndege, na moshi wa rangi ya chungwa ukijaa angani

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Lori la zima moto likiwa nyuma ya bawa la ndege, na moshi wa rangi ya chungwa ukifuka angani
    Watu wakiendelea kutazama wakiwa kwenye uwanja wa ndege

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Watu wakifuatilia kinachofanyika kwenye uwanja wa ndege
    Shirika la Reuters, ambalo lilitoa picha hii, linasema linaonyesha wazima moto wakifanya kazi katika kuungua kwa ndege ya walinzi wa pwani.

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Shirika la habari la Reuters, ambalo lilitoa picha hii, linasema linaonyesha wazima moto wakihudumia ndege ya walinzi wa pwani.
  11. Tunayojua kuhusu ndege ya Japan iliyowaka moto ikitua mjini Tokyo

    Ni zaidi ya saa moja sasa tangu tulipoanza kupokea picha kutoka Uwanja wa Ndege wa Haneda mjini Tokyo ambapo ndege ya abiria ya Shirika la Ndege la Japan iliwaka moto ilipokuwa ikitua.

    Haya ndio tunayojua kufikia sasa:

    • Watu wote 379 waliokuwa kwenye ndege - abiria na wafanyakazi - wameondolewa salama, kulingana na Shirika la Ndege la Japan.
    • Ndege hiyo nambari 516 inaaminika kuhusika katika mgongano na ndege ya walinzi wa pwani ya Japan ilipokuwa ikitua.
    • Vyombo vya habari vya Japan vinaripoti kuwa mtu mmoja aliyekuwa kwenye ndege ya walinzi wa pwani alitoroka, huku wengine watano wakiwa hawajulikani waliko.
    • Video na picha zilizochapishwa mitandaoni zinaonyesha ndege ya Japan Airlines ikiteketea kwenye barabara ya kurukia ndege, huku picha kutoka ndani ya ndege zikionyesha abiria wakiwa wamezingirwa na moshi mzito.
    • Ndege hiyo ilikuwa safarini kutoka Sapparo kwenye kisiwa cha Hokkaido, kaskazini mwa Japan, na ilitakiwa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Haneda muda mfupi kabla ya 18:00 saa za ndani (09:00 GMT)
    • Mlinzi wa pwani anasema mazingira ya ndege hizo mbili kugongana "inachunguzwa"
    • Safari zote za ndege kutoka Uwanja wa Ndege wa Haneda zimesitishwa
  12. Habari za hivi punde, Watu watano waliokuwa wenye ndege ya walinzi wa pwani ya Japan wafariki

    Watu watano waliokuwa kwenye ndege ya walinzi wa pwani wamefariki, shirika la habari la AFP limemnukuu waziri wa uchukuzi wa Japan akisema.

    Shirika la utangazaji la serikali NHK pia limeripoti watu watano kufariki. Nahodha alifanikiwa kutoka lakini amejeruhiwa vibaya, inaongeza.

    Inaaminika kuwa ndege ya walinzi wa pwani, iliyokuwa ikipeleka chakula katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko kubwa la ardhi siku ya Jumatatu, iligongana na ndege ya Shirika la Ndege la Japan wakati ikitua kwenye njia ya kurukia.

    Muda mfupi uliopita, tulikufahamisha kwamba maafisa walidhani ndege iliyowaka moto mjini Tokyo huenda iligongana na ndege ya walinzi wa pwani ya Japan.

  13. Tazama: Tazama: Picha za moja kwa moja za ndege ikiwaka moto kwenye barabara ya kuruka ndege Tokyo

    Maelezo ya video, Tazama: Picha za kwanza za ndege ikiwaka moto kwenye uwanja wa ndege wa Tokyo

    Shirika la ndege la Japan linasema kuwa abiria na wafanyakazi wote 379 waliokuwa ndani ya ndege hiyo wametolewa, kulingana na shirika la habari la Reuters na NHK.

  14. Habari za hivi punde, Ndege ya Japan yawaka moto ikitua mjini Tokyo

    SCREEN GRAB

    Chanzo cha picha, SCREEN GRAB

    Ndege ya shirika la ndege la Japan Airlines iliwaka moto ilipokuwa ikitua kwenye barabara ya kurukia ndege katika uwanja wa ndege wa Haneda mjini Tokyo Jumanne jioni.

    Picha za shirika la habari la NHK zilionesha miali ya moto ikitoka kwenye madirisha ya ndege na chini yake.

    Njia ya ndege pia iliwaka moto. NHK, ikinukuu mamlaka, ilisema huenda ndege hiyo iligongana na ndege nyingine baada ya kutua Haneda. Kuna abiria kwenye ndege hiyo.

    Taarifa zaidi zinasema ndege hiyo, JAL 516, ilikuwa safarini kutoka Hokkaido.

    Endelea kuwa nasi kwa maelezo zaidi kuhusiana na taarifa hii.

  15. Israel kupunguza wanajeshi wake Gaza

    fdc

    Chanzo cha picha, Getty

    Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Israel wakitayarisha makombora wakati huu vita vikiendelea Gaza

    Jeshi la Israel limezidisha mashambulizi yake huko Gaza licha ya tangazo la mipango ya kuwaondoa maelfu ya wanajeshi wake katika ukanda huo.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, likimnukuu afisa wa Israel aliyesema siku ya Jumatatu kuwa wanajeshi wataondolewa ndani ya Gaza mwezi huu na kuingia kwenye awamu nyingine ya operesheni hiyo.

    Afisa huyo amesema kupunguzwa kwa wanajeshi kutawaruhusu baadhi ya askari wa akiba kurejea katika maisha ya kiraia, kuinua uchumi wa Israel ulioathiriwa na vita na kuwaweka tayari wanajeshi iwapo mzozo wa kaskazini mwa Lebanon na Hezbollah utaongezeka.

    Afisa wa Marekani alisema uamuzi huo unaashiria kuanza kwa mabadiliko ya operesheni za Israel.

    Marekani imekuwa ikiitaka Israel kupunguza makali ya operesheni yake ya kijeshi, huku kukiwa na wito wa kimataifa wa kusitisha mapigano wakati idadi ya vifo ikiongezeka.

    Pia unaweza kusoma:

    • Israel Gaza: Idadi ya vifo vya Gaza inasema nini kuhusu vita
  16. Ethiopia yasaini mkataba na Somaliland ili iweze kutumia bahari

    ethiopia

    Ethiopia imechukua hatua za kwanza za kisheria katika mwelekeo ambao siku moja itaiwezesha nchi hiyo isiyo na bahari kupata ufikiaji wa bahari, serikali yake inasema.

    Nchi hiyo imetia saini kile kinachojulikana kama mkataba wa maelewano (MoU) na jamhuri iliyojitangaza kuwa ya Somaliland, kutumia mojawapo ya bandari zake.

    Awali, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alielezea upatikanaji wa bahari ni suala linalowezekana kwa nchi yake.

    Katika hotuba yake ya mwezi Oktoba ambayo ilizua hofu katika nchi hiyo - wananchi walidhani hatua hiyo itakuwa ni kujaribu kuchukua ardhi kutoka kwa nchi jirani ya Ethiopia, ambayo ni Eritrea.

    Makubaliano yaliyoafikiwa siku ya Jumatatu na Somaliland hayajawekwa wazi lakini taarifa kutoka ofisi ya Abiy ilisema "itafungua njia ili kutimiza azma ya Ethiopia kupata ufikiaji wa bahari".

    Mazungumzo hayo yamelenga bandari ya Somaliland ya Berbera.

    Mshauri wa masuala ya usalama wa taifa, Redwan Hussien alisema kwenye ukurasa wa X kwamba makubaliano hayo yataiwezesha Ethiopia kukodishwa eneo la kijeshi lililopo baharini.

    Mkataba huo haupo kisheria lakini unaashiria ushindi mkubwa wa kidiplomasia kwa Addis Ababa.

    Akizungumza wakati wa utiaji saini, Rais wa Somaliland, Muse Bihdi Abdi alisema makubaliano hayo yanajumuisha Ethiopia kuitambua Somaliland kama nchi huru katika siku zijazo.

    Somaliland imejitenga na Somalia kwa zaidi ya miaka 30 sasa lakini haitambuliwi na Umoja wa Afrika (AU) wala Umoja wa Mataifa kama taifa huru.

    Hapakuwa na majibu kuhusiana na tangazo hilo kutoka Somalia, ambayo inaichukulia Somaliland kama sehemu ya eneo lake. Lakini shirika la utangazaji la kitaifa SNTV limeripoti kuwa kutakuwa na kikao cha dharura cha baraza la mawaziri siku ya Jumanne kujadili suala hilo.

    Ethiopia taifa la watu milioni 100, ni moja ya taifa lenye idadi kubwa ya watu miongoni mwa mataifa yasiyo na bahari.

    Soma zaidi:

    • Uchaguzi wa Somaliland:Je kura itafanya nchi hii itambuliwe?
  17. Waliofariki katika tetemeko la ardhi Japan wafikia 48

    b

    Idadi ya watu waliofariki katika tetemeko kubwa la ardhi nchini Japan lililosababisha nyumba kubomoka na kupelekea onyo la Tsunami sasa wamefikia 30.

    Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani vifo vyote vimetokea katika mkoa wa Ishikawa, kwenye pwani ya kaskazini-magharibi ya Japan, ambapo kilikuwa kitovu cha tetemeko hilo la Jumatatu.

    m

    Chanzo cha picha, Reuters

    m

    Chanzo cha picha, Reuters

    Takribani wanajeshi 1,000 wa nchi hiyo wako katikati juhudi za utafutaji na uokoaji wa watu katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko, Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida amesema.

    Huku onyo la tsunami likiondolewa, Kishida amesema - watajaribu kuanzisha njia za baharini ili kufikia sehemu za mbali za rasi ya kaskazini ya Noto, ambako tetemeko la ardhi lilipiga.

    Pia unaweza kusoma:

    • Nini cha kufanya linapotokea tetemeko la ardhi?
    • Je, tutaweza kutabiri matetemeko ya ardhi?
    • Tetemeko la ardhi Uturuki: Jinsi walionusurika wanavyokabiliana na kiwewe
  18. Mshindi wa Tuzo ya Nobel ahukumiwa kifungo jela

    c

    Chanzo cha picha, EPA

    Mahakama nchini Bangladesh imemhukumu mshindi wa tuzo ya Nobel Muhammad Yunus kifungo cha miezi sita jela kwa kukiuka sheria za kazi za nchi hiyo.

    Wafuasi wa Profesa Yunus wanasema kesi hiyo imechochewa kisiasa.

    Mchumi huyo maarufu na wenzake watatu kutoka kampuni yao ya Grameen Telecom - walipatikana na hatia ya kushindwa kuunda mfuko wa ustawi wa wafanyakazi wao.

    Wote wanne wanakana kufanya makosa yoyote na wamepewa dhamana wakisubiri rufaa.

    "Kama mawakili wangu walivyoeleza mahakamani, hukumu hii dhidi yangu ni kinyume cha sheria na haingii akilini," Prof Yunus alisema katika taarifa iliyotolewa baada ya hukumu hiyo.

    Yunus mwenye umri wa miaka 83, anayejulikana kimataifa kwa kitabu chake "banker to the poor," anasifiwa kwa kuwa muasisi wa mfumo wa mikopo midogo midogo inayosaidia kuondoa mamilioni ya watu kwenye umaskini.

    Prof Yunus na Benki yake ya Grameen walitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa kazi hiyo mwaka wa 2006.

    Pia unaweza kusoma:

    • Tuzo ya amani ya Nobel : Je hawa ndio washindi waliozua utata zaidi?
    • Kwa nini Mtanzania, aliyeshinda Tuzo ya Nobel, Abdulrazak Gurnah hafahamiki sana nyumbani
    • Tuzo ya amani ya Nobel 2021:Maria Ressa na Dmitry Muratov washinda Tuzo ya amani ya Nobel 2021
  19. Lee Jae-myung:Kiongozi wa upinzani Korea Kusini achomwa kisu katika mkutano

    n

    Kiongozi wa upinzani nchini Korea Kusini alichomwa kisu katika mkutano na waandishi wa habari katika mji wa Busan, shirika la habari Yonhap limeripoti.

    Lee Jae-myung, ambaye alikosa nafasi ya urais wakati wa uchaguzi mkuu wa urais mwaka 2022, alichomwa kisu upande wa kushoto wa shingo yake majira ya asubuhi Jumanne.

    Mshambuliaji alikamatwa katika eneo la tukio.

    Bwana Lee alipelekwa hospitali mara tu aliposhambuliwa. Alikuwa katika hali mbaya wakati huo, Yonhap imesema.

    Aliyefanya mashambulizi alikuwa ana kati ya miaka 50 au 60, taarifa zilieleza.Aliripotiwa kuwa alikuwa amemkaribia bwana Lee ili kumuomba saini yake, kabla ya kumchoma kisu.

    Picha za Video zinazoonesha shambulio hilo zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii zikimuonesha bwana Lee akianguka katikati ya mkusanyiko wa watu, wakati baadhi ya watu wakijaribu kumkamata mshambuliaji.

    Picha zinaonesha tukio hilo la bwana Lee lying akiwa amelala chini huku amefumba macho huku mtu mmoja akiwa amemuwekea kitambaa katika shingo.

    Bwana Lee, 59, anayeongoza chama cha Democratic Party of Korea ambaye kwa sasa sio mbunge lakini anatarajiwa kuwania uongozi katika uchaguzi ujao unaotarajia kufanyika mwezi Aprili 2024.

  20. Heri ya Mwaka Mpya 2024!