Israel yasema vita huko Gaza vinatarajiwa kuendelea mwaka mzima wa 2024

Jeshi la Israel limesema linatarajia mzozo wa Gaza kuendelea katika kipindi chote cha 2024.

Moja kwa moja

Esther Namuhisa and Rashid Abdallah

  1. Putin aapa 'kuzidisha' mashambulizi dhidi ya maeneo ya kijeshi ya Ukraine

    Rais wa Urusi Vladimir Putin ametishia kufanya mashambulizi nchini Ukraine kujibu shambulio la Ukraine katika mji wa Belgorod

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais Vladimir Putin ameahidi "kuzidisha" mashambulizi dhidi ya Ukraine, baada ya siku za mashambulizi ya anga ya pande zote mbili katika vita vya muda mrefu.

    Akizungumza katika ziara yake katika hospitali ya kijeshi mjini Moscow, Bw Putin alisema wanajeshi wataendelea kulenga "makampuni ya kijeshi" ya Ukraine.

    Aliita shambulio la anga katika mji wa Belgorod wa Urusi na Ukraine "shambulio la makusudi dhidi ya raia".

    Watu 25 waliuawa katika shambulio la Jumamosi, maafisa wa eneo hilo wanasema.

    Akiongea na wanajeshi wa Urusi siku ya Jumatatu, Bw Putin alisema vita hivyo vinageukia upande wa Moscow na anataka vita viishe haraka, lakini kwa masharti ya Urusi pekee.

    Aliongeza kuwa wafuasi wa nchi za Magharibi wa Ukraine ndio kikwazo kikubwa cha kumaliza mzozo huo, lakini akasema matamshi yao yanaanza kubadilika kwani walianza kutambua hawawezi "kuiangamiza" Urusi.

    Siku ya Jumapili, Bw Putin alitoa ujumbe wake wa jadi wa mwaka mpya ambapo aliwasifu wanajeshi wa Urusi kama "mashujaa" bila kutaja waziwazi vita vya Ukraine.

    Katika hotuba yake ya mwaka mpya, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliahidi ongezeko kubwa la idadi ya silaha ambazo nchi hiyo inazalisha mnamo 2024, akiahidi kuunda takribani droni milioni moja.

  2. Israel yasema vita huko Gaza vinatarajiwa kuendelea mwaka mzima wa 2024

    Zaidi ya watu 21,800 wameuawa huko Gaza,wengi wao wakiwa watoto na wanawake

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Jeshi la Israel limesema linatarajia mzozo wa Gaza kuendelea katika kipindi chote cha 2024.

    Katika ujumbe wa mwaka mpya, msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel Daniel Hagari alisema upelekaji wa wanajeshi unarekebishwa ili kujiandaa kwa "mapigano ya muda mrefu".

    Alisema baadhi ya wanajeshi, hasa askari wa akiba,wataondolewa ili kuwaruhusu kujipanga upya.

    "Marekebisho haya yanalenga kuhakikisha mipango na maandalizi ya kuendeleza vita mwaka wa 2024," alisema.

    "IDF lazima ipange mapema kutokana na kuelewa kwamba kutakuwa na misheni ya ziada na mapigano yataendelea mwaka mzima." Alisema kuwa baadhi ya askari wa akiba wataondoka Gaza " wiki hii" ili kuwaruhusu "kuongeza nguvu kabla ya operesheni zinazokuja".

    Zaidi ya watu 21,800 wameuawa huko Gaza, wengi wao wakiwa watoto na wanawake, wakati wa wiki 11 za mapigano, kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas.

    Vita vya hivi punde zaidi vilichochewa na shambulio la kuvuka mpaka ambalo halijawahi kushuhudiwa na watu wenye silaha wa Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, ambapo watu 1,200 waliuawa, wengi wao wakiwa raia na wengine wapatao 240 walichukuliwa mateka.

  3. Helikopta za Marekani zimewaua wapiganaji wa Houthi wa Yemen

    n

    Chanzo cha picha, Reuters

    Jeshi la Marekani limesema siku ya Jumapili vikosi vyake viliwafyatulia risasi waasi wa Houthi wa Yemen baada ya kushambulia meli ya mizigo katika Bahari Nyekundu, na kuua wapiganaji kadhaa.

    Kwa mujibu wa shirka la habari la AP, Kamandi Kuu ya Marekani imesema boti nne ndogo zilishambulia meli ya mizigo iliyokuwa na bendera ya Singapore mapema Jumapili.

    Helikopta kutoka jeshi la wanamaji la Marekani ziliitikia wito kutoka katika meli hiyo na kutoa onyo kwa washambuliaji, ambao walijibu kwa kushambulia helikopta.

    "Helikopta za Jeshi zilirudisha mapigo na kuzamisha boti tatu kati ya nne na kuwaua watu waliokuwemo wakati boti ya nne ikikimbia eneo hilo,” Kamandi Kuu ya Marekani imesema.

    Wahouthi wamekiri wapiganaji wao 10 wameuawa katika makabiliano hayo na kuonya kuwa italipiza.

  4. Putin amesema nini kwa wanajeshi wa Urusi kwenye hotuba ya Mwaka Mpya?

    d

    Chanzo cha picha, en.kremlin.ru

    Maelezo ya picha, Rais Putin wa Urusi

    Rais wa Urusi Vladimir Putin amelihutubia taifa wakati wa kuukaribisha mwaka mpya 2024.

    Katika hafla hiyo, Putin amesema, "nataka kuzungumza na askari wa Urusi walioko kazini ambao kwa sasa wanapigania ukweli na haki kwenye uwanja wa vita. Nyinyi ni mashujaa wetu. Mioyo yetu iko pamoja nanyi. Salamu kwa ujasiri wenu na tunajivunia.”

    "Ninajua vizuri mumewapeza wapendwa wenu. Ningependa kuwaambia kuwa mamilioni ya raia wa Urusi wako pamoja nanyi.”

    Vilevile amesema, “tumethibitisha huko nyuma tunaweza kukabiliana na changamoto ngumu na hatutopiga goti. Hakuna nguvu inayoweza kututenganisha.”

    Urusi inakabiliwa na vikwazo kutoka nchi za magharibi kutokana na vita vyake nchini Ukraine. Nchi nyingi za magharibi ziko pamoja na Ukraine katika vita vyake dhidi ya Urusi.

    Wanajeshi wa Urusi pia wameuwawa katika vita hivi. Lakini Putin hakutaja idadi katika hotuba yake.

    Urusi na Ukraine zimekuwa kwenye vita tangu Februari 2022 - vita vinavyoendelea kwa miaka miwili sasa.

  5. Onyo la tsunami latolewa Japan baada ya tetemeko la ardhi

    Tokyo Jumatatu, Januari 1, 2024.

    Chanzo cha picha, Reuters

    Msururu wa matetemeko ya ardhi yametokea nchini Japani siku ya kwanza ya mwaka mpya.

    Shirika la Hali ya Hewa la Japan limeripoti matetemeko katika ufuo wa Ishikawa na wilaya za karibu, moja likiwa na nguvu ya 7.6.

    Baada ya matetemeko hayo kutokea, onyo la tsunami limetolewa nchini Japan.

    Kituo cha utangazaji cha umma cha Japani NHK TV kimeonya kuwa mawimbi ya maji yanaweza kufikia urefu wa mita 5 (futi 16.5) na kuwataka watu kukimbilia nchi kavu au juu ya majengo ya karibu haraka iwezekanavyo.

    Soma pia:

    • Majengo yaliyoporomoka ambayo yalikusudiwa kustahimili matetemeko ya ardhi
    • Video ya uharibifu uliotokana na tetemeko Japan
  6. Katika Picha: Maombi,shamrashamra za fataki zatawala sherehe za kuukaribisha mwaka mpya

    Tazama picha zilizopigwa maeneo mbalimbali wakati wa sherehe za mwaka mpya duniani kote:

    kenya

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Waumini wakiwa katika maombi, kukaribisha mwaka mpya Kenya
    n

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Nigeria, mkesha wa Mwaka mpya
    b

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Wengine wakisheherekea kwenye matamasha ya muziki
    n

    Chanzo cha picha, EPA

  7. Malkia wa Denmark atangaza kung’atuka katika kiti chake

    rf

    Chanzo cha picha, AP

    Maelezo ya picha, Malkia wa Denmark Margrethe II

    Malkia wa Denmark Margrethe II ametangaza kujiuzulu nafasi yake katika hotuba mubashara ya Mwaka mpya kupitia televisheni.

    Atajiuzulu rasmi Januari 14, ambapo itakuwa ni miaka 52 tangu awe malkia.

    "Nitamwachia kiti mwanangu, Mwanamfalme Prince Frederik," alitangaza.

    Amebainisha kuwa uamuzi huo umekuja baada ya kufanyiwa upasuaji wa mgongo mapema mwaka 2023.

    "Upasuaji umefanya nifikirie juu ya siku zijazo - wakati umefika wa kuacha jukumu hili kwa kizazi kijacho," alisema.

    "Nimeamua kuwa sasa ni wakati muafaka," aliongeza, na kutoa shukrani zake kwa umma wa Denmark kwa msaada wao kwa miaka mingi.

    Waziri Mkuu Mette Frederiksen alimshukuru Malkia kwa huduma yake.

    "Kwa niaba ya watu wote, ningependa kutoa shukrani za dhati kwa Mtukufu Malkia kwa kujitolea kwake kwa maisha yote na juhudi zake katika Ufalme," alisema.

    Malkia huyo mwenye umri wa miaka 83 ndiye malkia pekee anayetawala duniani katika ufalme uliodumu kwa muda mrefu zaidi barani Ulaya, akichukua kiti cha ufalme baada ya kifo cha baba yake Mfalme Frederik IX mnamo 1972.

  8. Rais Felix Tshisekedi amwagiwa pongezi za ushindi

      • Author, Laillah Mohammed, BBC Swahili
    drc

    Jamii ya kimataifa inaendelea kutuma ujumbe wa pongezi kwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia ushindi wa Rais Felix Tshisekedi kwenye uchaguzi mkuu wa Desemba 20, 2023.

    Kiongozi wa Umoja wa Afrika na Rais wa Comoros Azali Assoumani alikuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kumpongeza rais Tshisekedi kwa ushindi wake wa asilimia 73.34 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi mkuu.

    Kutoka jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais wa Burundi , Evariste Ndayashimiye alituma ujumbe wake wa heri njema kupitia mtandao wa kijamii wa X na kuomba amani kudumu baada ya ushindi huo kutangazwa.

    Katika ujumbe wake, kiongozi huyo wa zamani wa jumuiya ya EAC aliwataka wote wenye kupinga matokeo yaliyotangazwa, ‘kuwasilisha kesi mbele ya mahakama kupitisa njia zinazofuata muongozo wa sheria.’

    Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga naye, amemtakia Rais Tshisekedi kila la kheir anapoanza muhula wake wa pili madarakani.

    ‘Ninamuombea uongozi wake ulete mabadiliko mema na mafanikio katika taifa hilo. Nawatakia raia wa DRC kila la kheri katika juhudi zao kujiinua upya , kuidhibiti na kuendeleza taifa lao,’ alisema Odinga.

    Tshisekedi alishinda uchaguzi huo ulioandaliwa Desemba 20, 2023 kwa kura zaidi ya milioni 13 ambazo ni asilimia 73 ya jumla ya kura zilizopigwa katika uchaguzi huo. Mpinzani wake wa karibu alikuwa Moisee Katumbi aliyepata kura milioni 3 ambazo ni asilimia 18 ya kura zilizopigwa huku Martin Fayulu aliibuka nambari tatu kwa kura laki tisa ambazo ni asilimia tano ya kura zote zilizopigwa.

    Tshishekedi alikuwa anakabiliana na wagombea 19, akiwemo mmoja wa kike, Ifoku Marie-Josee Mputa Mpunga ambaye amekubali kushindwa na kumpa kongole mshindani, Rais Tshisekedi.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye kurasa yake ya mtandao wa kijamii wa X, Marie alisema kwamba, ‘ushindi wake Tshisekedi unaonyesha imani ya raia wa DRC katika uongozi wake.’

    Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, ujumbe wa heri njema kutoka Tanzania, umetumwa Kinshasa huku Rais Samia Suluhu Hassan pia akichapisha salamu zake kwenye mtandano wa kijamii wa X.

    ‘ Nina matumaini kwamba tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na kuboresha uhusiano kati ya mataifa yetu mawili,’ alisema Rais Samia.

    Kiongozi wa upinzani nchini Ufaransa, Marine Le Pen, mbali na kutuma ujumbe wa heri njema na kumpongeza rais Tshiekedi, alitaja pia, ‘ Ninawatumia raia wa DRC heri njema na duah ya amani. Hasa wanaokabiliwa na vita ambavyo vinasahaulika katika jimbo la Kivu,Ufaransa ni sharti isimame na taifa hilo, alisema Le Penn.

    Rais wa Afrika kusini Cyril Ramaphosa katika ujumbe wake wa kumpongeza Rais Tshisekedi, aliwapongeza raia wa DRC kwa kuwa watulivu na kuonyesha umoja wakati walipo subiri matokeo rasmi kutangazwa.

    Aidha, rais huyo amesema kwamba ,’ Ninaomba utulivu hasa ikiwa kunaye kiongozi ambaye atapinga matokeo hay ana kuwataka wote kutumia njia za kisheria kulingana na katiba ya nchi hiyo kuwasilisha malalamishi yao rasmi,’ alisema rais ramaphosa.

    Awali, ujumbe uliotumwa kwenye kurasa ya mtandao wa kijamii wa X ya rais mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta, ukimpongeza rais Tshishekedi, ulifutiiliwa mbali na kutajwa kama usio sawa.

    Katika ujumbe huo, Rais Kenyatta alimtaka yeyote kuwasilisha malalmiko yake kupitia njia za Mahakama huku akitaka amani idumu katika eneo la mashariki mwa DRC.

    Katika ujumbe wake wa mwisho wa mwaka Rais wa Rwanda Paul Kagame aliwaka tu kuwa na hali ya usalama katika taifa jirani na kusema kwamba Rwanda inatizama suala hilo kwa uangalifu.

    Soma zaidi:

    • Uchaguzi DRC 2023: Rais Felix Tshisekedi atangazwa kupata ushindi wa kishindo
  9. Heri ya Mwaka Mpya 2024!