Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Vita vya Israeli na Hamas: Mapigano ya ardhini yapamba moto huku maelfu wakikimbilia kaskazini

Jeshi la Israel limeendelea kuushambulia ukanda wa Gaza kwa mashambulizi ya anga hii leo, huku wanajeshi wakiendelea na operesheni zao za ardhini dhidi ya Hamas.

Moja kwa moja

Dinah Gahamanyi

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo, tukutane tena hapo kesho majaaliwa.

  2. Picha za hivi karibuni kutoka Ukanda wa Gaza

    Kumekuwa na mashambulizi zaidi ya Israel huko Gaza leo. Hamas inasema watu 13 waliuawa wakati nyumba ilipogongwa huko Khan Younis kusini.

    Israel bado haijatoa maoni.

    Hizi hapa ni baadhi ya picha za hivi punde zinazotufikia kutoka Gaza.

    Unaweza pia kusoma:

    • Hezbollah yaonya vita vya kikanda ikiwa mashambulizi Gaza yataendelea
    • Mtoto mmoja huuawa kila baada ya dakika kumi Gaza
    • Nchi ya Amerika Kusini ambayo ina jamii kubwa zaidi ya Wapalestina nje ya Ulimwengu wa Kiarabu na Israeli
    • 'Ninapiga simu kutoka shirika la ujasusi la Israel.Tunarusha bomu, una saa mbili kuondoka’
    • Vita vya Israel na Gaza: Je, uhalifu wa kivita unatekelezwa?, sheria inasemaje?
  3. Maandamano ya Wapalestina: Makombora yarushwa huku waandamanaji wakiiimba 'warudishe nyumbani!'

    Kundi la takriban waandamanaji 60 wamekabiliana na polisi baada ya kukaribia kundi dogo la waandamanaji wanaounga mkono Palestina kwenye daraja la Lambeth (Lambeth Bridge) mjini London Uingereza.

    Video inaonyesha makombora yakirushwa kuelekea kwa maafisa. Katika video hii fupi waandamanaji walipiga kelele "warudishe nyumbani"

  4. Wanajeshi wa Uganda watimuliwa kazini kwa uoga katika shambulio kwenye kambi ya Bulo Marer Atmis nchini Somalia

      • Author, Joseph Winter
      • Nafasi, Mhariri wa BBC Afrika

    Mahakama ya kijeshi nchini Uganda imewapata maafisa wawili na hatia ya uoga wakati wapiganaji wa Kiislamu walipovamia kambi ya Umoja wa Afrika nchini Somalia mwezi Mei.

    Meja Zadock Abor na John Oluka walikimbia baada ya kushambuliwa na al-Shabab huko Bulo Marer, kusini mwa mji mkuu Mogadishu.

    Takriban wanajeshi 50 wa Uganda waliuawa, maafisa wanasema.

    Uganda ni sehemu ya kikosi cha Umoja wa Afrika kinachoisaidia serikali ya Somalia kupambana na al-Shabab, tawi la al-Qaeda.

    Shambulio dhidi ya Bulo Marer lilikuwa moja ya mauaji mabaya zaidi kwa kikosi cha Umoja wa Afrika, Atmis, tangu kilipoanzisha mashambulizi mapya dhidi ya al-Shabab mwaka jana.

    Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, alikosoa jeshi lake kwa namna lilivyojibu shambulio hilo.

    Mahakama ya kijeshi ya Uganda iliyoketi mjini Mogadishu ilisikia kwamba maafisa hao walikuwa wamepewa onyo kuhusu shambulio lililokuwa likikaribia lakini walishindwa kuchukua hatua za kulizuia.

    Wanamgambo wa al-Shabab walipovamia kambi hiyo, walishindwa kuwakusanya wanajeshi wao na badala yake walikimbilia kambi nyingine.

    Maafisa wote wawili wamefutwa kazi katika jeshi.

    Wanajeshi wengine wanne pia walipatikana na hatia ya kushindwa kulinda zana za kijeshi.

    Kikosi cha wanajeshi 19,000 wa Umoja wa Afrika kilitumwa Somalia mwaka 2007 na kusaidia kuwaondoa al-Shabab katika miji mingi.

    Imepangwa kuwa kikosi hicho kitarejesha majukumu ya usalama kwa vikosi vya serikali ya Somalia na kuondoka nchini mwaka ujao.

    Hata hivyo, mashambulizi dhidi ya al-Shabab yamekwama na kundi hilo bado linadhibiti maeneo mengi ya vijijini nchini humo.

    katika taarifa ya awali mmoja wa maafisa alitambuliwa kuhusika kimakosa. Hili limesahihishwa.

  5. Netanyahu apinga Palestina kuongozwa na chama cha Mahmoud Abbas baada ya vita vya Gaza

      • Author, Paul Adams
      • Nafasi, Mwandishi wa BBC wa masuala ya Diplomasia

    Wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari jana usiku, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema jambo ambalo litakuwa limezua taharuki mjini Washington.

    Alipoulizwa kuhusu utawala wa baadaye wa Ukanda wa Gaza, alisema anapinga kurejeshwa kwa Mamlaka ya Palestina yenye makao yake Ukingo wa Magharibi (PA), inayoongozwa na Rais mzee wa Palestina Mahmoud Abbas.

    "Itabidi kuwe na kitu kingine," alisema.

    "Hakuwezi kuwa na mamlaka ambayo haikulaani mauaji hayo [tarehe 7 Oktoba na Hamas]."

    Pia alirudia msisitizo wake kwamba Israel itadumisha udhibiti wa usalama Gaza. "Sitahatarisha udhibiti wa usalama kwa hali yoyote."

    Wakati wa safari yake ya hivi majuzi katika eneo hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alimwambia Bw Abbas kwamba Washington iinakiona chama chake cha PA kama chama "kitakachochukua jukumu kuu" huko Gaza baada ya kushindwa kwa Hamas.

    Netanyahu ameweka wazi ni nani hataki aitawale Gaza katika siku zijazo: Hamas au PA. Lakini hadi sasa hajatoa njia mbadala.

    Pamoja na kuongezeka kwa wasiwasi wa kimataifa juu ya gharama ya maisha ya Wapalestina ya operesheni ya kijeshi ya Israeli huko Gaza, kukataa kwa Netanyahu jukumu la PA kunamuweka katika hali ya msuguano na mshirika mkuu wa Israeli, Marekani.

    Unaweza pia kusoma:

    • Hezbollah yaonya vita vya kikanda ikiwa mashambulizi Gaza yataendelea
    • Mtoto mmoja huuawa kila baada ya dakika kumi Gaza
    • Nchi ya Amerika Kusini ambayo ina jamii kubwa zaidi ya Wapalestina nje ya Ulimwengu wa Kiarabu na Israeli
    • 'Ninapiga simu kutoka shirika la ujasusi la Israel.Tunarusha bomu, una saa mbili kuondoka’
    • Vita vya Israel na Gaza: Je, uhalifu wa kivita unatekelezwa?, sheria inasemaje?
  6. Papa anatoa wito wa kulindwa kwa raia na kuachiliwa kwa mateka Gaza

    Papa Francis ametoa wito kwa waliojeruhiwa huko Gaza kuhudumiwa mara moja na misaada zaidi ya kibinadamu iruhusiwe kuingia katika eneo hilo.

    Akizungumza kutoka Jiji la Vatican katika sala yake ya kila wiki ya Malaika wa Bwana, Papa alisema fikra zake kila siku zinaelekea katika "mateso" na "hali mbaya" katika Israeli na maeneo ya Palestina.

    "Naomba waliojeruhiwa huko Gaza wasaidiwe mara moja. Raia wanapaswa kulindwa, na misaada zaidi ya kibinadamu inapaswa kuwasilishwa kwa watu hao waliochoka," Papa aliongeza.

    Papa Francis pia alitoa wito mateka waliochukuliwa na Hamas kutoka Israel tarehe 7 Oktoba waachiliwe.

  7. Vita vya Israel na Hamas: Mapigano yachacha kwenye mpaka wa Israel na Lebanon, huku wanajeshi wa UN wakishambuliwa

    Mapigano yanayoendelea kwenye mpaka na Israel na kusini mwa Lebanon, ambako kundi la waislamu Washia wenye silaha Hezbollah lina makao yake makuu.

    Jeshi la Ulinzi la Israel limesema makombora ya vifaru yalirushwa na Hezbollah siku ya Jumapili na kugonga maeneo kadhaa yanayokaliwa na raia ndaniya Israel.

    IDF ilisema ilikuwa inalipiza kisasi kutokana na mashambulizi ya risasi kutoka Lebanon.

    Msemaji wa huduma ya ambulensi nchini Israel ameliambia shirika la habari la Israel N12 News kwamba mtu mmoja amejeruhiwa vibaya na kati ya watatu hadi watano wengine wana majeruhi kutokana na shambulio hilo.

    Picha zilionyesha magari yakiwaka moto kwenye barabara karibu na eneo la wazi.

    Siku ya Jumamosi, kiongozi wa Hezbollah Sayyed Hassan Nasrallah alisema itaendelea kupambana na Israel karibu na mpaka.

    Wakati hayo yakijiri kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, Unifil, kinasema mlinda amani wake mmoja alipigwa risasi kusini mwa Lebanon, karibu na mpaka na Israel, katika kampigano ya usiku kucha.

    Mwanajeshi huyo ambaye hajatambuliwa anapata nafuu na kwa sasa yuko shwari, kikosi hicho kilisema

    Unifil kiliongeza kuwa chanzo cha milio ya risasi hakijajulikana na kwamba uchunguzi unafanyika ili kubaini chanzo chake.

    Kundi la Lebanon la Hezbollah na jeshi la Israel mara kwa mara wamekuwa wakirushiana risasi kwenye mpaka wa Lebanon na Israel.

  8. Raphael Dwamena: Mshambulizi wa Ghana afariki akiwa na umri wa miaka 28 baada ya kuzimia uwanjani

    Mshambuliaji wa Ghana Raphael Dwamena mwenye umri wa miaka 28 amefariki baada ya kuzirai uwanjani wakati wa mchezo wa ligi nchini Albania.

    Dwamena alikuwa anachezea timu ya Egnatia dhidi ya Partizani mnamo Jumamosi.

    "Licha ya kushughulikiwa kwa haraka na madaktari kwa bahati mbaya alifariki," lilisema Shirikisho la kandanda la Albania (AFL).

    Dwamena alikuwa mchezaji anayeongoza katika wingi wa magoli kwenye ligi ya Albania msimu huu akiwa na mabao tisa. Alikuwa ameshiriki michezo tisa ya kuiwakilisha taifa lake na kufunga magoli mawili.

    Mechi ya Jumamosi ilisimamishwa na shirikisho kuahirisha michezo yote iliyokuwa imepangiwa Albania wiki hii.

    "AFL inatoa rambirambi zake kwa familia ya Dwamena na klabu ya Egnatia kwa tukio hili ambalo limeshangaza jamii nzima ya kandanda ya Albania,” shirikisho hilo liliongeza.

    Shirikisho la kandanda la Ghana (GFA) lilisema limetuma "rambirambi kwa familia yake katika wakati huu mgumu".

    "Alitumikia taifa lake vizuri na kuonyesha nidhamu wakati wote alipoiwakilisha Ghana," rais wa GFA Kurt Edwin Simeon Okraku alisema katika taarifa.

    Mwaka 2017, pendekezo la £14m la kuhamia klabu ya Uingereza ya Brighton lilifeli baada ya Dwamena kukosa kufuzu vipimo vya afya. Kisha aliiwakilisha klabu ya Levante katika La Liga na pia kuichezea timu ya Real Zaragoza katika mkopo.

    Mwaka 2021 alizirai nchini Austria katika mechi kati ya klabu yake Blau-Weiss Linz dhidi ya Hartberg, lakini alipona na kuendelea na taaluma yake ya kucheza.

    Anaripotiwa kufanyiwa operesheni ya moyo na kuwekewa kifaa maalum cha kuzuia mshtuko wa moyo.

    "Mawazo yetu yako kwa familia na wapendwa wake katika wakati huu mgumu. Mchango wake kwa klabu yetu hautasahaulika milele," Levante ilisema katika mitandao ya kijamii.

    Zaragoza pia ilitoa taarifa, ikisema: "Tumesikitishwa sana na habari za kuhuzunisha kuhusu mchezaji wetu wa zamani Raphael Dwamena. Milele utasalia kwenye kumbukumbu ya mashabiki wa Zaragoza. Pumzika kwa amani."

  9. Vita vya Gaza: "Kifo kilikuwa karibu sana wakati huu"

      • Author, Rushdi Abualouf
      • Nafasi, Mwandishi wa BBC Gaza

    "Ghafla, mabomu manne yalianguka kwa kasi karibu nasi," alisema Rushdi Abu Al-Ouf, mwandishi wa BBC huko Gaza, alipokuwa akienda kununua vifaa kwa ajili ya watoto wake kutoka kijiji cha Bani Suhaila, mashariki mwa Khan Yunis Gaza.

    Aliongeza kuwa: Nilikuwa nikielekea sokoni na mtu alinialika kunywa chai, na ghafla mabomu yalikuwa yakituangukia, yakirusha mawe na vioo juu ya vichwa vyetu, huku kukiwa na sauti za mayowe katika eneo hilo.

    "Kifo kilikuwa karibu sana wakati huu," Abu Al-Aouf anasema wakati anakimbia kuelekea eneo la bomu, ambalo liliyaharibu majengo 10.

    “Wakati watu wakiwa wametajaa damu na vumbi, mwanamume mmoja alikuwa akipiga kelele, ‘Pigia ambulensi.’ Niliona wanne wakiwa wamekufa na zaidi ya mia moja wamejeruhiwa, na nikasikia sauti za wale walionaswa chini ya kifusi wakipiga kelele wakiomba msaada.

  10. Habari za hivi punde, Mzozo wa Israel na Hamas: Raia wanaripotiwa kupita kwenye kivuko cha Rafah

    Ripoti ya shirika la habari la Reuters inasema kundi la raia leo wamehama Gaza, wakipitia kivuko cha Rafah kuelekea Misri.

    Reuters inavinukuu vyanzo vya usalama vya Misri ambavyo havikutajwa.

    Hii itamaanisha kuwa kivuko hicho takuwa kimefunguliwa mara tatu katika siku tatu.

    Bado hatuna maelezo yoyote kuhusu wahamishwaji hawa.

  11. Ndege za Israel zafanya mashambulizi ndani ya Syria

    Jeshi la Israel limetangaza kwamba ndege zake za kivita zilifanya mashambulizi dhidi ya "miundombinu ya ugaidi" ndani ya Syria, kujibu ufyatuaji wa risasi wa kuvuka mpaka ulioelekezwa kwenye Milima ya Golan.

    Jeshi hilo lilisema kupitia mtandao waTelegram: "Muda mfupi uliopita, katika kujibu mashambulizi kwenye Milima ya Golan jana (Jumamosi), ndege za kivita za jeshi la Israel zilishambulia maeneo ya miundombinu ya magaidi nchini Syria.

    Siku ya Jumamosi, jeshi lilisema kwamba makombora mawili yaliyofyatuliwa kutoka Syria yalianguka katika maeneo yasiyokaliwa na watu huko Kwenye milima ya Golan.

    Israel pia ilishambulia maeneo mbali mbali nchini Syria siku ya Ijumaa, baada ya ndege isiyo na rubani kurusha mabomu kwenye shule iliyopo katika mji wa kusini wa Eilat.

    Israel iliikalia kwa mabavu sehemu kubwa ya Miinuko ya Golan katika Vita vya Siku Sita mwaka 1967, na baadaye ikalichukua katika hatua ambayo haikutambuliwa kamwe na Umoja wa Mataifa.

    Makabiliano ya risasi katika mpaka yametokea pia mara kwa mara kwenye mpaka na Lebanon, wakati Israel inaendelea kuzidisha mashambulizi yake dhidi ya Hamas.

    Unaweza pia kusoma:

    • Hezbollah yaonya vita vya kikanda ikiwa mashambulizi Gaza yataendelea
    • Mtoto mmoja huuawa kila baada ya dakika kumi Gaza
    • Nchi ya Amerika Kusini ambayo ina jamii kubwa zaidi ya Wapalestina nje ya Ulimwengu wa Kiarabu na Israeli
    • 'Ninapiga simu kutoka shirika la ujasusi la Israel.Tunarusha bomu, una saa mbili kuondoka’
    • Vita vya Israel na Gaza: Je, uhalifu wa kivita unatekelezwa?, sheria inasemaje?
  12. Jeshi la Israel lasema litasaidia kuwaondoa watoto wachanga katika hospitali mjini Gaza

    Kuwahamisha watoto kadhaa kutoka ni katika kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU) mchakato mgumu na wa hatari, lakini leo tunaambiwa kuwa utatekelezwa katika hospitali ya Al-Shifa, ambayo sasa ndio kitovu cha mapigano kaskazini mwa Gaza.

    Tunasubiri kuona jinsi mchakato huo utavyofanyika.

    Israel inasema itasaidia kuhamishwa kwa watoto hao lakini wafanyakazi ndani ya hospitali hiyo kubwa zaidi ya Gaza wanaonekana kutoeleweka juu ya maelezo - huku mkuu wa upasuaji akionya kuwa hospitali nyingine katika eneo hilo hazina utaalam au vifaa vya kuwatunza watoto 37 walioripotiwa ambao walikuwa wakitunzwa katika kitengo cha watoto wachanga cha Shifa kabla hakijapoteza umeme.

    Picha zilizotumwa kwa BBC jana usiku – zinazoonyesha zaidi ya watoto 20 - wakionekana kuhitaji matibabu ya oksijeni ni kielelezo tosha cha jinsi wagonjwa hao wachanga zaidi wanafaa kusaidiwa kwa haraka.

    Israel inasisitiza kuwa bado kuna njia salama ya wagonjwa kutoka nje ya hospitali - na wengine ambao walikuwa wametafuta hifadhi huko – ili kuanza safari ya kusini kuelekea Gaza.

    Lakini kutokana na mapigano makali yanayoendelea nje tu ya milango yao ya hospitali wanahisi jaribio kuondoka kwao kwenye hospitali hiyo ni hatari kubwa zaidi.

    Unaweza pia kusoma:

    • Hezbollah yaonya vita vya kikanda ikiwa mashambulizi Gaza yataendelea
    • Mtoto mmoja huuawa kila baada ya dakika kumi Gaza
    • Nchi ya Amerika Kusini ambayo ina jamii kubwa zaidi ya Wapalestina nje ya Ulimwengu wa Kiarabu na Israeli
    • 'Ninapiga simu kutoka shirika la ujasusi la Israel.Tunarusha bomu, una saa mbili kuondoka’
    • Vita vya Israel na Gaza: Je, uhalifu wa kivita unatekelezwa?, sheria inasemaje?
  13. Waziri wa ulinzi wa Israel aionya Hezbollah dhidi ya kuendeleza mashambulizi

    Katika hotuba yake mapema mchana huu Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alionya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran Hezbollah "msifanye makosa hayo na kuanzisha vita".

    Akijibu hotuba ya awali ya mkuu wa Hezbollah Hassan Nasrallah ambayo tumeripoti hivi punde

    Kwa vita vyovyote , Netanyahu alitishia Israel "itaamua hatima ya Lebanon".

    Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant, ambaye alizungumza baada ya Netanyahu, alitumia lugha kali zaidi katika onyo lake kwa Lebanon na Hezbollah.

    Alisema Jeshi la anga la Israeli linaimarisha mikakati yake kwenye mpaka wa Israel-Lebanon, na kuna jeshi kubwa zaidi kwa ajili ya kukabuliana na shambulio lolote kutoka Lebanon.

    ''Raia wa Lebanon wanapaswa kujua kwamba kama Nasrallah atafanya makosa, basi hatima ya Beirut inaweza kuwa kama hatima ya Gaza." anasema Yoav Gallant, Waziri wa ulinzi wa Israel.

  14. Mkuu wa Hezbollah asema mashambulizi yake dhidi ya Israel ni 'uungaji mkono kweney maeneo ya vita'

    Kiongozi mwenye ushawishi mkubwa wa Harakati ya Hezbollah ya Lebanon Hassan Nasrallah, amesema kundi hilo limeongeza mashambulizi yake dhidi ya Israel katika kipindi cha wiki moja iliyopita na kwamba mashambulizi kutoka kusini mwa Lebanon yataendelea, na kuyaelezea kama "usaidizi wa mapigano".

    Akiwahutubia wafuasi wake kwa mara ya pili tangu vita vya Israel na Hamas vianze mapema leo, Nasrallah alisema Hezbollah - ambayo inachukuliwa kuwa shirika la kigaidi na Uingereza, Marekani na wengine - inazidi kupenya ndani ya ardhi ya Israel, ikiwa na silaha ambazo ni pamoja na droni na vilipuzi vyenye uzito wa kati ya kilo 300 na 500.

    Israel na Hezbollah wamekuwa wakikabiliana kwa risasi karibu kila siku katika mpaka wao kwa zaidi ya mwezi mmoja - lakini hadi sasa, mashambulizi mengi yamekomea kwenye maeneo ya kijeshi na maeneo ya wazi.

    Katika hotuba yake ya kwanza wiki iliyopita, Nasrallah alisema Hezbollah tayari inafanya vya kutosha kuisaidia Hamas huko Gaza, kwa kuhakikisha wanajeshi wa Israel wanakuwa na shughuli nyingi kwenye mpaka wa kaskazini mwa nchi hiyo. Kwa wale wanaomtarajia atangaze kuendeleza vita zaidi, alikuwa na ujumbe leo: vitendo vinavyoendelea kwenye maeneo ya vita vitajieleza vyenyewe.

    Katika hotuba yake kwa njia ya televisheni, Nasrallah pia alizungumzia mashambulizi ya hivi karibuni yaliyofanywa na wanamgambo dhidi ya kambi za Marekani nchini Iraq na Syria pamoja na mashambulizi ya waasi wa Houthi nchini Yemen.

    Kama Hezbollah, vikundi hivi ni sehemu ya kile kinachoitwa Axis of Resistance, muungano wa vikosi katika eneo linaloungwa mkono na Iran.

    Tehran, ilisema, iliyapa makundi hayo usaidizi wa kisiasa, kijeshi na kifedha, lakini haikufanya maamuzi kwa niaba yao.

  15. Vita vya Israel na Hamas: Muhtasari wa baadhi ya taarifa zinazojiri hadi sasa

    • Jeshi la Israel linasema limekubali kuwahamisha watoto wagonjwa walio katika hali mbaya katika hospitali kuu iliyoko Gaza leo.
    • Hofu ya madaktari inazidi kuongezeka kuhusu watoto wachanga waliozaliwa hivi karibuni katika hospitali ya Al-Shifa – baada ya kundi moja la madaktari kusema watoto wawili tayari wamefariki kutokana na ukosefu wa umeme.
    • BBC imetumiwa picha za zaidi ya watoto wachanga 20 ambao wamelazwa katika wadi ya upasuaji katika hospitali hiyo. Wamelazwa katika vitanda vya watu wazima, na baadhi wanaonekana kuhitaji matibabu ya oksijeni ambayo hayapo kwa sasa.
    • Jeshi la Israel limeshutumiwa kwa kushambulia Al-Shifa, ambayo imefungwa kutokana na ukosefu wa maji, umeme, wahudumu wa afya na madawa. Jeshi lilikanusha madai ya kuizingira lakini ikakiri kuwa ilishiriki mapigano katika eneo hilo. Ilisema upande wa mashariki wa hospitali hiyo ulikuwa wazi kwa watu wanaotaka kuondoka kwa njia salama.
    • Israel inashutumu Hamas kwa kutumia mahandaki chini ya hospitali hiyo kama kituo kikuu cha operesheni, madai ambayo kundi hilo limekanusha.
    • Shirika la madaktari wasio na mipaka MSF limeonya kuwa hospitali nyingi ndani ya Gaza zimekuwa zikishuhudia ‘mashambulizi yasiyo na kikomo.’
    • Maelfu ya Wapalestina wanaendelea kukimbilia kusini mwa Gaza, wakitumai kupata usalama kutokana na mapigano makali katika upande wa kaskazini mwa ukanda huo.

    Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa mara nyingine tena amekataa wito wa kusitisha mapigano, akisema vita vitaendelea hadi Hamas iangamizwe na mateka kuachiliwa huru.

  16. Katika picha: Vita vya ardhini vyapamba moto huku maelfu wanakimbia kaskazini

    Jeshi la Israel limeendelea kuushambulia ukanda wa Gaza kwa mashambulizi ya anga hii leo, huku wanajeshi wakiendelea na operesheni zao za ardhini dhidi ya Hamas.

    Wakati huo huo, wakati mapigano yakizidi kuzunguka mji wa Gaza, maelfu ya watu wanaendelea kukimbia ghasia na kuhamia kusini.

    Unaweza pia kusoma:

  17. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya mubashara leo ikiwa ni tarehe 12.11.2023