Hamas wanataka kuiangamiza Israel - Blinken
"Yeyote anayetaka amani na haki lazima alaani utawala wa kigaidi wa Hamas," Blinken alisema.
Moja kwa moja
Dinah Gahamanyi
Ndege ya Kenya Airways iliyokuwa ikielekea London Heathrow yaelekezwa Stansted kwa kuhofia usalama

Chanzo cha picha, PA Media
Maelezo ya picha, Kenya Airways Boeing 787 ilielekezwa Stansted kabla ya saa 15:45 BST. Ndege ya Kenya Airways iliyokuwa ikielekea London Heathrow imeelekezwa kwengine kotokana na kile kilichotajwa kuwa ''tishio la kiusalama''.
Msemaji wa Wizara ya Usalama alisema: "Ndege za kivita za RAF Typhoon kutoka kitengo cha RAF Coningsby zilitumika kama tahadhari mchana wa leo kufuatilia ndege ya raia iliyokuwa ikikaribia Uingereza.
"Ndege hiyo ilisindikizwa hadi sehemu ya maegesho ya mbali na shughuli za kawaida za ndege zikiendelea," alisema. Ndege ilielekezwa kwa Stansted kabla ya saa 15:45 BST.
Msemaji wa London Stansted alisema ndege ya Kenya Airways Boeing 787 "ilitua salama huku polisi wa Essex wakiihudumia".
"Ndege iliyokuwa ikisafiri kutoka Nairobi hadi Heathrow ilielekezwa Stansted mchana huu. Uwanja wa ndege bado upo wazi."
Ndege hiyo iko ardhini baada ya kutua Stansted, lakini polisi hawakusema ikiwa kulikuwa na tishio lolote linaloendelea, au ikiwa abiria walikuwa bado ndani.
Msemaji wa shirika la ndege la Kenya alisema "Kenya Airways plc (KQ) inathibitisha kwamba Alhamisi tarehe 12 Oktoba 2023, mwendo wa saa 10:30 BST, makao makuu yake yalipokea arifa kuhusu tishio la usalama kwenye ndege ya KQ100 iliyokuwa ikisafiri kutoka Nairobi hadi London Heathrow.
“Usimamizi wa KQ kwa kushirikiana na mamlaka za usalama za Serikali ya Kenya na Uingereza zilifanya tathmini ya kina ya hatari ya tishio hilo.
"Wafanyakazi waliokuwemo walipewa taarifa, na tahadhari zote za kiusalama zilichukuliwa ili kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wetu na abiria waliokuwemo."
DR Congo yawashtumu waasi na Rwanda kwa kupanga njama ya kuvuruga uchaguzi
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Ian Wafula
- Nafasi, BBC News, Nairobi

Chanzo cha picha, AFP
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaonya kuwa karibu wapiga kura milioni 1.5 wanaoishi katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa M23 hawataweza kushiriki katika uchaguzi mwezi Desemba.
Msemaji wa serikali Patrick Muyaya alisema wako katika harakati ya kuwapa makazi watu wengine milioni moja waliokimbia makwao kutokana na migogoro katika eneo hilo.
Aliongeza kuwa inaweza kuwa vigumu kwa tume ya uchaguzi kufikia maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa "M23 na Rwanda" akiongeza kuwa kusitisha uchaguzi sio suluhisho.
Awali DR Congo iliishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi la waasi la M23 - madai ambayo Rwanda imekuwa ikikanusha.
Kundi la M23 kwa kiasi kikubwa linaundwa na Watutsi, kundi moja ambalo linatawala serikali ya Rwanda.
Kundi la M23 linadhibiti eneo la Rutshuru na sehemu za Masisi katika jimbo la Kivu Kaskazini.
Inadai inataka kuwalinda Watutsi dhidi ya makundi ya wapiganaji wa Kihutu, ikiwa ni pamoja na Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR).
Msemaji wa Rwanda Yolande Makolo aliiambia BBC kwamba Rwanda haiwezi kulaumiwa kwa uamuzi wa DR Congo wa kuvipa silaha, kufadhili na kujumuisha vikundi haramu vyenye silaha vilivyoidhinishwa kwenye jeshi lao - akiashiria FDLR.
Aliongeza kuwa tatizo kubwa lilikuwa ni DR Congo kushindwa kutawala na kuwashutumu kwa kuendelea kukiuka taratibu za amani za kikanda zilizofikiwa.
Pia unaweza kusoma:
- Ipi nafasi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutatua mvutano wa Congo na Rwanda?
Watanzania wawili waliotoweka Israel bado hawajulikani walipo- Balozi
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Alfred Lasteck
- Nafasi, BBC News, Dar es Salaam

Chanzo cha picha, Getty Images
Balozi wa Tanzania nchini Israel ameiambia BBC kuwa bado hawajui walipo wanafunzi wawili kutoka Tanzania ambao walipoteza mawasiliano nao toka nchi hiyo iliposhambuliwa na kundi la Hamas mwishoni mwa wiki.
“Sisi kama ubalozi tumetumia kila namna tunavyoweza kutafuta ukweli wa hawa ndugu zetu (wanafunzi wawili wa kitanzania walipo Israel kimasomo). Wako wapi au nini kimetokea hivyo tutakapopata taarifa sahihi tutazitoa,“ amesema Balozi wa Tanzania nchini Israel, Alex Kallua.
Kauli hiyo inakuja siku kadhaa za sintofahamu ya raia wawili wa nchi hiyo ambao wanaishi eneo la kusini ambalo Jumamosi iliyopita limeshuhudia mapambano baina ya wanamgambo wa wa Kipalestina wa Hamas pamoja na jeshi la Israeli.
Balozi Kallua aliimbia BBC kuwa wanaendelea kufuatilia hali ilivyo katika maeneo mbalimbali na kuhakikisha watanzania wote wako salama ikiwemo kubaini walipo raia hao wawili.
“Hatuwezi kutoa taarifa za kukisia na tunaendelea kufuatilia kwa mamlaka za Israel ili kupata taarifa sahihi…
“…sisi tuko hapa ‘on the ground‘ tunafuatilia watanzania wote waliopo hapa, kuhakikisha usalama wao,“ alisema balozi huyo.
Jumatatu ya wiki hii, ubalozi wa Tanzania uliileza BBC kuwa hawana mawasiliano na wanafunzi hao wawili wanaosoma masomo ya kilimo nchini humo huku ikibainisha kuwa ina mawasiliano na wanafunzi wengine zaidi ya 260 waliopo nchini humo.
Israel yashambulia viwanja vya ndege vya Damascus na Aleppo - ripoti
Vyombo vya habari vya serikali nchini Syria vinasema kuwa Israel imeshambuia viwanja vya ndege katika mji mkuu wake Damascus na mji wa Aleppo.
Shirika la habari la serikali Sana liliripoti kwamba "milipuko ya makombora" ilisababisha uharibifu wa sehemu za kutua za viwanja vya ndege na kulemaza huduma.
Vyombo vya habari vya ndani pia vinasema kwamba ulinzi wa anga wa Syria ulizinduliwa kujibu mashambulizi.
Wachunguzi wa vita wenye makao yake nchini Uingereza Shirika la Kufuatilia Haki za Kibinadamu la Syria (SOHR) liliripoti milipuko kadhaa huko Aleppo.
BBC haijaweza kuthibitisha kikamilifu mashambulizi yaliyoripotiwa.
Mashambulizi hayo ya anga yameripotiwa siku moja kabla ya waziri wa mambo ya nje wa Iran kuzuru Syria.
Nchi zote mbili ni mahasimu wa Israeli, na Iran imekuwa ikiunga mkono Hamas kwa muda mrefu. I
srael mara kwa mara hushambulia kwa mabomu maeneo maalum nchini Syria yenye uhusiano na Iran na kundi la wanamgambo wa Lebanon Hezbollah, lakini ni nadra sana kukubali kuhusika na mashambulizi hayo.

Wakulima wapoteza kesi dhidi ya chakula cha GMO nchini Kenya

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Mahindi ni chakula kikuu nchini Kenya Kundi linalowakilisha wakulima wadogo nchini Kenya limeshindwa katika ombi lake la kusitisha chakula cha GMo kuagizwa kutoka nje au kukuzwa nchini humo.
Jaji aliamua kwamba kulikuwa na ukosefu wa ushahidi kuonyesha kwamba teknolojia ya GM ilidhuru wanadamu au mazingira, na akasema kwamba Kenya "imeweka mfumo thabiti na miundo iliyojengwa" ili kuwaweka watu salama.
Kesi hiyo ilikuwa imewasilishwa na wakili Mkenya Paul Mwangi na kundi la kushawishi, Ligi ya Wakulima ya Kenya. Mwaka jana, Kenya iliondoa marufuku ya miaka 10 ya mahindi, huku kukiwa na upinzani kutoka kwa wakulima na vikundi vya kampeni.
Ilimaanisha wakulima sasa wangeweza kulima kwa uwazi mazao ya GM, ikiwa ni pamoja na mahindi kuu, pamoja na kuagiza chakula kinachozalishwa na GM na mifugo.
Hatua hiyo hata hivyo ilisitishwa kufuatia kesi mahakamani kwa misingi kuwa marufuku hiyo haikuwa ya kitaratibu na kinyume cha sheria.
Walalamishi hao pia waliteta kuwa bidhaa za GM zilihatarisha afya ya Wakenya, haswa maskini.
Soma:
Paul Mackenzie kuendelea kuzuiliwa baada ya kesi yake kuahirishwa tena

Chanzo cha picha, PAUL MAKENZIE
Mahakama mjini Mombasa pwani ya Kenya imeahirisha uamuzi wake kwa ombi la waendesha mashtaka wa serikali kuongeza muda wa kuzuiliwa kwa kiongozi wa madhehemu tata Paul Mackenzie Nthenge kwa miezi sita zaidi, hadi Ijumaa, Oktoba 19.
Wakili wa utetezi Wycliffe Makasembo aliiambia mahakama kuwa alikuwa mgonjwa na alihitaji muda wa kupata nafuu.
Pia aliambia mahakama kuwa mteja wake, Mackenzie hatafika mbele ya kamati ya Seneti hadi uamuzi wa mwisho utakapotolewa.
Kamati ya maalum ya Seneti inayochunguza kuenea kwa mashirika ya kidini nchini Kenya imemwita mwinjilisti mwingine maarufu wa televisheni, Mchungaji Ezekiel Odero kufika mbele yake Ijumaa saa 10 asubuhi saa za Afrika Mashariki.
Kamati hiyo inachunguza hali iliyopelekea vifo vya wafuasi wa mhubiri mwenye utata wa Kanisa la Good News International Paul Mackenzie, ambaye kwa sasa yuko chini ya ulinzi wa polisi.
Waendesha mashtaka wanasema wanahitaji muda zaidi kukamilisha uchunguzi, ikiwa ni pamoja na kuhitimisha uchunguzi wa maiti kwa madai ya uhalifu uliofanywa na kanisa la Good News International la Mackenzie.
Mackenzie na washirika wake walikamatwa mwezi wa Aprili na wanadaiwa kuwaua kwa njaa takriban watu 429 kwa ahadi kwamba wangeenda mbinguni.
Pia unaweza kusoma:
- Paul Mackenzie: Ni kipi kinachojulikana kuhusu kiongozi wa dhehebu la kufa njaa nchini Kenya?
- Paul Makenzi:Mhubiri huyu alianzaje safari tata ya kuwashawishi watu kufunga hadi kufa?
- Madhehebu ni nini na kwa nini watu hujiunga nayo?
Zaidi ya familia 95 zilizoshikwa mateka zimearifiwa jamaa zao wako Gaza - Israel

Chanzo cha picha, Reuters
Taarifa kutoka kwa Jeshi la Ulinzi la Israel:
Zaidi ya familia 95 zilizoshikwa mateka zimeambiwa jamaa zao wamepelekwa Gaza.
Zaidi ya makombora 5,000 yamerushwa ndani ya Israel kutoka Gaza tangu Jumamosi
Israeli imelenga zaidi ya maeneo 2,600 huko Gaza
Takriban Waisraeli 1,200 wameuawa na zaidi ya 3,000 kujeruhiwa na mashambulizi ya mwishoni mwa juma ya Hamas.
Soma zaidi:
Hamas wanataka kuiangamiza Israel - Blinken

Chanzo cha picha, US Pool
Mwanadiplomasia mkuu wa Marekani Antony Blinken amekuwa akitoa hotuba yake nchini Israel, akiwa amesimama bega kwa bega na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
"Yeyote anayetaka amani na haki lazima alaani utawala wa kigaidi wa Hamas," Blinken anasema.
"Hamas ina ajenda moja tu - kuharibu Israeli na kuwaua Wayahudi."
Hata hivyo, anaonya kuwa tahadhari lazima zichukuliwe ili kuepuka kuwadhuru raia wa oande zote.
"Ndiyo maana ni muhimu sana kuchukua tahadhari zote zinazowezekana ili kuepuka kuwadhuru raia, na ndiyo sababu tunasikitika kupoteza maisha ya kila raia," Blinken anasema, "raia wa kila imani, kila taifa wameuawa."
Walinda amani wa UN wasimamishwa kazi kwa madai ya unyanyasaji wa kingono nchini DR Congo

Chanzo cha picha, UN
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo unasema kuwa umewasimamisha kazi baadhi ya walinda amani wake kutokana na ripoti za utovu wa nidhamu.
Ilisema ina sera ya kutovumilia kabisa unyonyaji na unyanyasaji wa kingono.
Shirika la habari la AFP linaripoti kuwa shutuma hizo ni dhidi ya walinda amani wanane wa Afrika Kusini.
Ujumbe wa Monusco umekabiliwa na shutuma za hapo awali za unyanyasaji wa kijinsia.
Ina zaidi ya wanajeshi 14,000 mashariki mwa DR Congo.
Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na maandamano kadhaa dhidi ya Umoja wa Mataifa ambayo inashutumiwa kwa kushindwa kuwalinda raia dhidi ya mashambulizi ya makundi yenye silaha.
Mke wa rais aliyeondolewa madarakani Gabon afungwa jela - ripoti

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Rais aliyeondolewa madarakani wa Gabon, Ali Bongo Odimba na mkewe Sylvia Bongo Mke wa Rais aliyeondolewa madarakani wa Gabon, Ali Bongo Odimba, amefungwa jela, wakili wake ameliambia shirika la habari la AFP.
Sylvia Bongo, ambaye alikuwa chini ya kifungo cha nyumbani, alituhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha za umma.
Mumewe alilazimishwa kuondokai tarehe 30 Agosti.
Wakili Francois Zimeray aliliambia shirika la habari la AFP kwamba kufungwa kwake siku ya Jumatano ni hatua ya "kiholela" na "utaratibu usio halali".
Bi Bongo mwezi uliopita alishtakiwa kwa utakatishaji fedha, kupokea mali ya wizi, kughushi nyaraka.
Mwanawe Noureddin Bongo Valentin pia amefunguliwa mashtaka ya rushwa, ubadhirifu wa fedha na kuwekwa kizuizini kabla ya kesi yake kuanza kusikilizwa.
Jeshi lilichukua mamlaka mara baada ya Ali Bongo kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa Gabon.
Alikuwa ofisini tangu 2009 alipomrithi babake ambaye alitawala nchi hiyo kwa miaka 41.
Maelezo zaidi:
Kansela wa Ujerumani achukua hatua huku vifo vya Israel vikisherehekewa Berlin

Chanzo cha picha, Re
Maelezo ya picha, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameliambia bunge asubuhi ya leo kwamba mtu yeyote anayeitukuza Hamas, kuunga mkono mauaji au kuchoma bendera za Israel atakabiliwa na mashtaka ya jinai.
Alisema kundi linalounga mkono Palestina liitwalo Samidoun litapigwa marufuku.
Aliwashutumu wanachama wake kwa kuingia katika mitaa ya eneo la Neukölln mjini Berlin siku ya Jumamosi kusherehekea mauaji ya raia wa Israel kwa kuwagawia pipi wapita njia.
"Hii ni mbaya, huu ni unyama," aliiambia Bundestag. "Hatukubalia chuki na uchochezi. Hatutavumilia chuki dhidi ya Wayahudi."
Scholz pia alitangaza kupiga marufuku shughuli zote za Hamas nchini Ujerumani.
Tayari imetambuliwa kama kundi la kigaidi katika Umoja wa Ulaya, Uingereza na Marekani na Hamas haina shirika rasmi nchini Ujerumani - lakini kansela huyo alisema marufuku itajumuisha vyama na shughuli zote.
Rais wa Iran aishutumu Israel kwa 'mauaji ya halaiki'

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Rais wa Iran Ebrahim Raisi Huku Israel ikiendelea kushambulia ngome za Hamas mjini Gaza, rais wa Iran ameishutumu Israel kwa kufanya "mauaji ya halaiki".
Ebrahim Raisi pia alisema kuzingirwa kwa Gaza - ambapo huduma za maji, umeme na mafuta zimekatwa - kunavunja mikataba yote ya kimataifa.
Iran inajulikana kufadhili na kuiwezesha Hamas huko Gaza.
Lakini siku ya Jumanne, Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei alisema nchi yake haiko nyuma ya mashambulizi mabaya ya wikendi dhidi ya Israel.
Hata hivyo, alisema "tunabusu mkono" wa wale waliopanga mashambulizi.
'Walifyatua risasi mfululizo. Haikuwa moja baada ya nyingine kama katika sinema'

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Katchakorn Pudtason, aliyeketi kwenye kiti cha magurudumu, muathiriwa wa mashambulizi ya wanamgambo wa Hamas Kundi la kwanza la raia wa Thailand waliookolewa kutoka Israel wamewasili Thailand mapema leo.
Mmoja wao, Katchakorn Pudtason, ambaye alikuwa akizungumza huku ameketi kwenye kiti cha magurudumu, alielezea shambulio la Hamas Jumamosi asubuhi, wakati alipopigwa risasi kwenye goti.
"Wao [wanamgambo] walipiga risasi kutoka barabarani. Nilikuwa nyuma ya gari na nilikuwa wa kwanza kupigwa risasi kwenye goti," alisema Katchakorn.
“Tuliendesha gari lakini waliendelea kutupiga risasi, rafiki yangu mmoja alijificha nyuma ya injini ya gari lakini risasi ikapita.
"Walifyatua risasi mfululizo. Haikuwa moja baada ya nyingine kama kwenye sinema. Nilidhani singepona."
Petr Pavlensky: Hukumu ya miezi sita yatolewa kwa Mrusi aliyechapisha video ya ngono ya mshirika wa Macron

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Petr Pavlensky Mwanaharakati wa Urusi Petr Pavlensky amehukumiwa kifungo cha miezi sita na mahakama ya Ufaransa kwa kuhusika katika kashfa ya kanda ya ngono iliyomhusisha mshirika wa kisiasa wa Rais Macron.
Pavlensky, ambaye alihamia Ufaransa mwaka 2017, atatumikia kifungo chake nje ya gereza.
Mshirika wake pia atatumikia kifungo cha miezi sita kilichosimamishwa.
Walitoa video ambayo ilimharibia sifa na kumnyima fursa mgombea Benjamin Griveaux ya meya wa Paris mnamo 2020.
Wote wawili wameagizwa kulipa €15,000 (£12,950) kama fidia kwa Bw Griveaux, pamoja na €5,000 ili kulipia ada za kisheria.
Alexandra de Taddeo, mwenzi wa Pavlensky, alikuwa na uhusiano na Bwana Griveaux mnamo 2018.
Video ilitumwa kwenye tovuti mnamo 2020, ikifichua picha za skrini za jumbe zilizotumiwa kati ya wawili hao na mwanamume akifanya tendo la ndoa na mwanamke mchanga.
Kufuatia kuachiliwa kwake, Bi Taddeo alikamatwa kwa madai ya kuvamia faragha na kusambaza picha za kibinafsi bila idhini.
Habari za hivi punde, Mzozo wa Israel na Palestina: Blinken awasili Israel
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amewasili nchini Israel.
Katika ziara yake hiyo fupi, Blinken atakutana na viongozi wa Israel na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas.
Ni muhimu kukumbuka kuwa Abbas anaishi Ukingo wa Magharibi, na ni mpinzani wa kisiasa wa Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Habari za hivi punde, Hakuna umeme, maji, au mafuta kwa Gaza hadi mateka waachiliwe - Israel
Waziri wa Nishati wa Israel, Israel Katz anasema Israeli haitaacha kuizingira Gaza hadi mateka wa Israel waachiliwe.
Katika chapisho la mitandao ya kijami Katz alisema hakuna "swichi ya umeme itawashwa, hakuna bomba la maji litakalofunguliwa na hakuna lori la mafuta litakaloingia" hadi "mateka" wawe huru.
Israel ilisimamisha usambazaji wa bidhaa kwa Ukanda wa Gaza baada ya mashambulizi ya Hamas siku ya Jumamosi.
Hali ya kibinadamu ya Gaza inazidi kuwa mbaya, huku Israel ikitarajiwa kuanza mashambulizi ya ardhini
Huku Gaza sasa ikiwa imezingirwa kikamilifu na wanajeshi wa Israel na baada ya siku tano za mashambulizi ya mabomu, hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya.
Umeme ulikatika leo baada ya kituo pekee cha umeme katika eneo hilo kukosa mafuta. Hospitali, ambazo zimejaa maelfu ya majeruhi, zinasema zinakosa dawa.
Umoja wa Mataifa unasema watu nusu milioni wa Gaza hawajapata mgao wao wa chakula tangu Jumamosi. Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuanzishwa eneo la kibinadamu. Afisa mmoja wa Misri aliiambia BBC kwamba serikali mjini Cairo ilikuwa katika majadiliano na pande zote kujaribu kuruhusu msaada kuingia Gaza kupitia Misri hata kama ni kwa saa chache tu.
Wakati huo huo, kuna matarajio makubwa kwamba Israel hivi karibuni itaimarisha zaidi operesheni yake kwa mashambulizi ya ardhini.
Msemaji wa Israel alisema vikosi, ikiwa ni pamoja na askari wa akiba 300,000, walikuwa karibu na mpaka wakijitayarisha kwa kwa mashambulizi, ili kuhakikisha kwamba kunakuwa na "mwisho wa vita hivi Hamas hawana tena uwezo wowote wa kijeshi".
Kwa idadi ya watu waliouawa na Hamas mwishoni mwa juma ambayo sasa inajulikana kuwa zaidi ya 1,200, ujumbe huo utakuwa na uungwaji mkono mkubwa wa umma wa Israeli.
Lebanon: Israel yawashambulia kwa makombora wapiganaji baada ya kuvuka mpaka

Maelezo ya picha, Mashambulio ya Hezbollah ndani ya Israel Israel inasema imeimarisha eneo lake la kaskazini na maelfu ya wanajeshi wa ziada baada kukabiliana kwa makombora na Lebanon.
Jeshi lake lilishambulia maeneo ya wapiganaji nchini Lebanon baada ya makombora mawili kurushwa katika kituo cha kijeshi cha Israel karibu na mpaka usio rasmi.
Watu watatu walijeruhiwa katika shambulizi hilo lililopiga miji na vijiji kadhaa, vyombo vya habari vya serikali ya Lebanon vilisema.
Hezbollah ilisema kuwa makombora hayo ni jibu la mauaji ya wapiganaji wake watatu siku ya Jumatatu.
Makabiliano hayo yamekuja wakati Israel ikiishambulia kwa mabomu Gaza ili kulipiza kisasi kwa kundi la wanamgambo wa Palestina Hamas.
Kikosi cha Ulinzi cha Israel (IDF) kimesema kombora la kifaru lilirushwa kutoka Lebanon kuelekea kituo cha kijeshi cha Israel karibu na kijiji cha Arab al-Aramshe, ambacho kiko kusini mwa Mji wa Blue Line uliotengwa na Umoja wa Mataifa - mpaka usio rasmi unaotenganisha Israel na Lebanon.
Hezbollah ilisema ilifanya mashambulio hayo "katika kulipiza kisasi kwa uchokozi wa Wazayuni siku ya Jumatatu". Ilidai kuwa kombora hilo lilisababisha majeruhi kadhaa wa Israel.
Unaweza pia kusoma:
- Mohammed Deif: Mfahamu kiongozi wa Hamas anayewanyima usingizi Israel
- Masuala muhimu unayopaswa kujua kuhusu mzozo kati ya Israel na Palestina
- Je, ni nini kilichotokea 1967 wakati israel ilipokabiliana kijeshi na mataifa matatu ya kiarabu katika vita vya siku sita?
- Fahamu chanzo cha uhasama kati ya Israel na Palestina
- Tunachojua kufikia sasa kuhusu raia wa Israel waliotekwa na Hamas
Wanariadha watatu wa Kiafrika walioteuliwa kuwania tuzo ya riadha ya kifahari

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Faith Kipyegon yuko tayari kutwaa tuzo hiyo baada ya kuwa wa kwanza kuvunja rekodi zaidi ya moja ya dunia katika msimu mmoja. Shirikisho la riadha la kimataifa la Riadha Duniani limewateua wanariadha watatu wa Afrika kuwania tuzo ya Mwanariadha Bora wa Dunia kwa Wanawake mwaka huu.
Faith Kipyegon wa Kenya na Tigist Assefa na Gudaf Tsegay, wote Muethiopia, ni miongoni mwa wanariadha 11 wa kike walioteuliwa kuwania tuzo za mwaka huu, baada ya kuonyesha utendaji mzuri katika msimu wa riadha wa mwaka huu.
Tigist alishinda mbio za masafa marefu -Berlin marathon mwezi Septemba, na kuweka rekodi mpya ya dunia ya mbio za marathon za wanawake.
Gudaf pia alishinda mbio za dunia mita 10,000 na Diamond League miya 5,000, ambapo aliweka rekodi ya dunia.
Wachanganuzi wa riadha wanamuunga mkono Bi Kipyegon kama mtu anayepewa nafasi kubwa kushinda tuzo ya mwaka huu baada ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 kuweka rekodi tatu mpya za dunia.
Kulingana na Wanda Diamond League, msimu wa kuvunja rekodi wa Bi Kipyegon umemweka kama "mwanariadha wa kwanza katika historia ya Diamond League kuvunja rekodi ya ulimwengu katika mbio nyingi na wa kwanza kuvunja rekodi zaidi ya moja ya ulimwengu katika msimu mmoja".
Winfred Yavi mzaliwa wa Kenya, ambaye alibadili uraia wake na kuwakilisha Bahrain, pia yuko katika kinyang'anyiro cha tuzo hiyo ya kifahari.
Washindi watatangazwa tarehe 11 Disemba baada ya kujumlisha kura zilizopigwa na mashabiki na maafisa wa Riadha wa Dunia.

