Putin: Mzozo wa Israel ni mbaya - lakini Iran haijahusika
Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema kinachoendelea Israel ni "kibaya", huku akitoa wito kwa pande zote mbili kupunguza mauaji ya raia.
Moja kwa moja
Ambia Hirsi
Weah 'atakubali matokeo ya uchaguzi wa Liberia'
Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, George Weah anagombea muhula wa pili madarakani
Rais wa Liberia, George Weah atakubali matokeo ya uchaguzi mkuu wa Jumanne, afisa kutoka chama chake amesema.
Jefferson Koijee, katibu mkuu wa chama tawala cha Coalition for Democratic Change, aliwaambia waandishi wa habari: "Mtu huyu amesema mara nyingi kwamba amani ya nchi hii ni muhimu kuliko maslahi yake."
Lakini Bw Koijee alipuuzilia mbali uwezekano wa kushindwa kwa Bw Weah, nyota wa zamani wa kandanda mwenye umri wa miaka 57.
Maafisa wa uchaguzi walisema waliojitokeza kupiga kura kwa mara ya nne baada ya vita vya Libeŕia walikuwa wengi.
Kura zinaendelea kuhesabiwa - tume ya uchaguzi itaanza kutoa matokeo saa 16:30 saa za ndani (17:30 BST).
Bw Weah anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Makamu wa Rais wa zamani Joseph Boakai, 78, wa Unite Party.
Bw Boakai alikuwa naibu wa Ellen Johnson Sirleaf alipokuwa rais.
Habari za hivi punde, Tumepokea ripoti ya uvamizi wa anga kutoka Lebanon - Jeshi la Israel
Jeshi la Ulinzi la Israeli linasema kwenye mtandao wa X, ambao zamani ulijulikana kama Twitter, kwamba ilipokea ripoti za tuhuma za uvamizi kutoka Lebanon kwenye anga ya Israel.
Ving'ora zilikuwa zikisikika katika miji mingi kaskazini mwa Israel, kulingana na shirika la habari la Reuters.
Reuters pia ilimnukuu mtangazaji wa Israel Kan akisema makombora yalipiga kaskazini mwa Israel.
Raia wote katika maeneo ambayo ving'ora vilipigwa wanaombwa kuingia kwenye makazi ya kujikinga dhidi ya mashambulizi na kusalia humo hadi ilani nyingine itakapotolewa, IDF ilisema.
Wakati huo huo, ndege ya British Airways kutoka London hadi Tel Aviv imeelekezwa kurudi Uingereza, muda mfupi kabla ya kufika Tel Aviv.
Msemaji wa shirika hilo la ndege alisema kuwa wamechukua uamuzi wa kuirejesha ndege hiyo Heathrow kwa sababu za kiusalama.
Baada ya ndege kuelekezwa kinyume, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ya Israel ilithibitisha kuwa kulikuwa na shambulio la roketi karibu na Tel Aviv lakini "sio karibu na uwanja wa ndege."
Tangu Hamas iliposhambulia Israel siku ya Jumamosi, mashirika mengi ya ndege ya kimataifa yamesitisha safari za kuelekea Tel Aviv.
Uganda:Wabunge wakataa kuruhusu uzazi wa mpango kwa wasichana, 15
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Viongozi wa kidini wenye ushawishi nchini Uganda wanasema vijana wanapaswa kujiepusha na ngono
Wabunge nchini
Uganda wamekataa pendekezo la serikali la kuruhusu wasichana wenye umri wa
miaka 15 kupata tembe za kupanga uzazi ili kupunguza viwango vya juu vya mimba.
Naibu Spika
Thomas Tayebwa aliliita wazo hilo "ushetani", akisema
"litarasimisha unajisi" wa wasichana.
Afisa mkuu
wa wizara ya afya alisema "unyanyapaa" unaowazunguka vijana
wanaotumia uzazi wa mpango unapaswa kukomeshwa.
Takriban
robo ya wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 19 nchini Uganda wana mimba au
tayari ni akina mama, utafiti unasema .
Kiwango
kiliongezeka sana wakati wa Covid wakati shule zilifungwa kwa karibu miaka
miwili .
Wakati wa
mjadala mkali wa bunge siku ya Jumanne, Mbunge Lucy Akello alihoji iwapo umri
wa kuwa na idhini unapunguzwa kutoka miaka 18 ya sasa hadi miaka 15, gazeti la serikali
la New Vision liliripoti.
Alielezea
pendekezo la kutoa uzazi wa mpango kwa wasichana wenye umri wa miaka 15 kama la
"kutisha".
Bi Akello
alisema hakutumia njia za uzazi wa mpango. "Ninatumia njia ya asili,
ambayo Mungu alinipa."
Soma zaidi:
Kwanini jukumu la kupanga uzazi hutwishwa wanawake?
Putin: Mzozo wa Israel ni mbaya - lakini Iran haijahusika
Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, Rais wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema kinachoendelea Israel ni "kibaya", huku akitoa wito kwa pande zote mbili kupunguza vifo vya raia.
Akizungumza katika mkutano mjini Moscow, Putin - ambaye anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Jinai ICC, kuhusu madai ya uhalifu wa kivita unaohusiana na Ukraine - pia aliishutumu Marekani kwa kuchochea hali ya wasiwasi.
"Sielewi kwa nini Marekani inaleta meli ya kivita [katika eneo hilo]", alisema - akimaanisha Marekani kutuma msaada wa ziada wa kijeshi kwa Israel.
Na Putin pia alisema madai kwamba Iran inahusika katika shambulio la Hamas "hayana msingi" - ingawa inafaa kukumbuka kuwa Urusi na Iran zina uhusiano wa karibu, na Iran hata inachukuliwa kuwa mfadhili mkuu wa kijeshi wa Urusi.
Iran imeshangilia shambulio la Hamas dhidi ya Israel lakini kiongozi wake mkuu hapo jana alikanusha kuhusika.
Tehran imekuwa mmoja wa wafadhili wakuu wa Hamas kwa miaka mingi, ikitoa msaada wa kifedha na silaha.
Rais wa Poland amependekeza kuwa Putin anaweza kufaidika na mzozo wa Israel, akitumai huenda ukavuruga vita vya Ukraine - ingawa Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Grant Shapps alisema "hakuna nafasi" ya kupoteza mwelekeo katika vita.
Unaweza pia kusoma:
Mohammed Deif: Mfahamu kiongozi wa Hamas anayewanyima usingizi Israel
Masuala muhimu unayopaswa kujua kuhusu mzozo kati ya Israel na Palestina
Je, ni nini kilichotokea 1967 wakati israel ilipokabiliana kijeshi na mataifa matatu ya kiarabu katika vita vya siku sita?
Fahamu chanzo cha uhasama kati ya Israel na Palestina
Tunachojua kufikia sasa kuhusu raia wa Israel waliotekwa na Hamas
Nigeria yasitisha safari za mahujaji wote wa Kikristo nchini Israel
Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Maelfu ya mahujaji wa Kikristo kutoka Nigeria huzuru maeneo ya kidini nchini Israel kila mwaka.
Nigeria imetangaza kusimamishwa kwa mahujaji wote nchini Israel kufuatia ghasia mbaya zilizozuka mwishoni mwa juma.
Kundi la mahujaji wa Pasaka lilitakiwa kusafiri kuelekea Israel na Jordan siku ya Jumanne, lakini safari hiyo imesitishwa hadi hali itakapotengamaa,
Tume ya Mahujaji wa Kikristo ya serikali inasema.
"Vita hivyo vimezua hali ya kutokuwa na uhakika katika mipango yetu ya Hija kuu mwezi Desemba... tunatumai uhasama utaisha kabla ya mwisho wa mwaka," Sunny Udeh, mkurugenzi wa tume ya uhamasishaji na uhamasishaji, aliiambia BBC.
Kwa wastani, mahujaji wa Kikristo wapatao 18,000 husafiri kutoka Nigeria kuzuru maeneo ya kidini nchini Israel na Jordan kila mwaka.
Tume hiyo ilisema itaendelea kufuatilia hali ya Israel huku usalama wa mahujaji wa Nigeria ukiendelea kuwa muhimu.
Jumamosi iliyopita, kundi la wapiganaji wa Palestina Hamas lilianzisha mashambulizi dhidi ya Israel.
Takriban Waisraeli 1,200 wameuawa katika mapigano hayo yanayoendelea, huku Wapalestina wasiopungua 1,000 wakiuawa kufuatia mashambulizi ya kulipiza kisasi katika Ukanda wa Gaza kutoka Tel Aviv.
Serikali ya Nigeria imetoa wito wa "kupungua kwa uhasama na kusitishwa kwa mapigano" kati ya vikosi vya Israel na wapiganaji wa Hamas, huku ikitetea suluhu la amani la mzozo huo kwa njia ya mazungumzo.
Licha ya machafuko hayo, safari za ndege za kibiashara kuelekea Tel Aviv kutoka Nigeria hazijakatizwa.
Gaza: Watoto walipiga mayowe barabarani tulipokuwa tukikimbia shambulio la anga saa nane usiku
Chanzo cha picha, Reuters
Kiwanda pekee cha kuzalisha umeme cha Gaza kimeishiwa na mafuta, na vifaa vya matibabu na chakula vinapungua, baada ya usiku mwingine ambao ulishuhudia mamia ya watu wakihangaika barabarani kukimbia mashambulizi ya anga.
Saa nane usiku siku ya Jumatano, jirani aligonga mlango wangu na kuniambia niondoke sasa kwa vile gorofa yangu ilikuwa ikilengwa.
Mashambulizi ya anga kutoka kwa ndege za kivita za Israel yameendelea hadi siku ya tano.
Hali kwa watu milioni 2.3 huko Gaza inazidi kuwa mbaya, na hakuna njia ya kuondoka katika eneo hilo dogo.
Kituo pekee cha umeme huko Gaza kiliacha kufanya kazi kabisa Jumatano saa 14:00 kwa saa za ndani (11:00 GMT), mamlaka inasema.
Israel ilikata vifaa muhimu, ikiwa ni pamoja na mafuta, katika eneo lililofungwa Jumatatu kufuatia uvamizi mkali wa wanamgambo wa Hamas.
Ukosefu wa umeme una maana kuwa wakazi wa Gaza wanapaswa kutegemea jenereta kwa ajili ya umeme.Lakini hakuna njia ya kuagiza mafuta kwa jenereta pia.
Sasa kuna matumaini madogo ya kuondoka katika eneo hilo, baada ya vivuko vya Israel kufungwa na Misri kulazimika kufunga kivuko chake pekee na Gaza kutokana na mashambulizi ya anga yaliyo karibu.
Nilijaribu kutoa familia yangu nje, kwa sababu haijulikani nini kinaweza kutokea hapa katika siku zijazo - lakini hiyo haikuwezekana.
Asubuhi na mapema Jumanne, niliwaamsha watoto wangu watatu, tukachukua vifaa vyetu vya dharura na kuelekea hospitali.
Lakini tulipofika huko, mamia ya watu walikuwa wakizuia mlango - wao pia walikuwa wakitafuta mahali pa kujificha usiku kucha.
Watoto waliokuwa hawajalala walipiga mayowe huku wakijikwaa barabarani na roketi zikiruka angani.
Siku ya Jumatano asubuhi, Hamas ilisema watu 30 waliuawa katika shambulio la usiku.Kwa jumla, zaidi ya watu 1,000 wa Gaza wameuawa katika mashambulizi hayo ya kulipiza kisasi.
Wanajeshi wa Israel wamesema wamepiga shabaha 450 katika ukanda wa Gaza katika muda wa saa 24 zilizopita.
Mashambulizi hayo ya angani yalianza baada ya wanamgambo wa Hamas kuvuka na kuingia Israel na kuanzisha wimbi la mashambulizi dhidi ya jamii kote kusini mwa nchi hiyo na kuua takriban Waisrael 1,200.Inakadiriwa watu 150 wamechukuliwa mateka na Hamas.
Uongozi wa kijeshi Niger waamrisha bosi wa UN kuondoka nchini humo ndani ya saa 72
Chanzo cha picha, AFP
Watawala wa kijeshi wa Niger wamemtaka mkuu wa ujumbe wa kidiplomasia wa Umoja wa Mataifa nchini humo kuondoka ndani ya saa 72.
Taarifa kutoka kwa wizara ya mambo ya nje ya taifa hilo la Afrika Magharibi ilishutumu Umoja wa Mataifa kwa kutumia "ujanja ", uliochochewa na Ufaransa, kuzuia Niger kushiriki kikamilifu katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa mwezi uliopita, pamoja na mikutano mingine ya kimataifa.
Kikosi cha kijeshi, ambacho kilimpindua rais wa Niger mwezi Julai, pia kimewatimua wanajeshi wa Ufaransa na balozi wa Ufaransa.
Wabunge wa chama cha CCC wa Zimbabwe wasimamishwa kuhudhuria vikao sita baada ya mapambano na polisi
Chanzo cha picha, Getty Images
Wabunge wote wa chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe wamesimamishwa kwa vikao sita vya bunge na hawatapokea mishahara kwa muda wa miezi miwili ijayo.
Spika Jacob Mudenda alitoa amri hiyo baada ya Chama cha Wananchi (CCC) kufanya maandamano bungeni, kikisema wabunge wake 15 walidanganywa ili kupoteza viti vyao.
Siku ya Jumatatu, mtu aliyejifanya kuwa katibu mkuu wa CCC alimwandikia barua Spika akidai kuwa wabunge hao 15 si wanachama tena.
Chama hakina katibu mkuu na barua ilikuwa imejaa makosa ya kisarufi.
Licha ya kiongozi wa CCC Nelson Chamisa kumtaka apuuze barua hiyo, Spika ambaye ni mbunge wa chama tawala cha Zanu-PF, alitangaza viti 15 viko wazi.
Kutokana na uamuzi huo wa Bw Mudenda, wabunge wa CCC walitatiza shughuli za bunge kwa takriban saa mbili.
Kulingana na wanasiasa wa CCC na vyombo vya habari vya ndani, polisi wa kutuliza ghasia waliitwa bungeni.
“Ni kitendo cha woga cha spika wa bunge la Zanu-PF, Jacob Mudenda, kuita polisi wa kutuliza ghasia na wabunge wetu wapigwe na kujeruhiwa kufuatia kushindwa katika mjadala wa bunge.
"Tabia ya aina hii lazima ikomeshwe ili kuzuia machafuko yanayoweza kutokea katika nchi yetu. Utawala wa Harare haupaswi kukosea tabia yetu ya amani kama udhaifu,"CCC iliandika kwenye Twitter..
Chama cha upinzani kilituma kwenye mtandao wa twitter picha za mapambano hayo bungeni:
Chanzo cha picha, CCC
Kesi hiyo huenda ikazidisha mvutano wa kisiasa, ambao umekuwa ukishuhudiwa katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika tangu uchaguzi wa rais uliokumbwa na utata mwezi Agosti.
Bw Chamisa, 45, alishindwa na rais Emmerson Mnangagwa mwenye umri wa miaka 81 katika kinyang'anyiro ambacho waangalizi wa kimataifa walisema kilikiuka viwango vya kidemokrasia.
Mama wa Gaza: Unajificha wapi wakati kifo kinatoka angani?
Chanzo cha picha, Reuters
Nadiya ni mama wa mvulana wa miaka mitano na mtoto wa miezi mitatu huko Gaza.
Anasema njia pekee ya kumtuliza mwanawe wa kiume, wakati ndege za Israel zikifanya mashambulizi, ni kumwambia "sauti ya mlipuko inakuja muda mfupi baada ya kutokea".
Ni aina ya maarifa ambayo hakuna mtoto wa miaka mitano anayepaswa kutarajiwa kuelewa, lakini kwa Nadiya, ni njia bora ya kukabiliana nayo.
Jumatatu usiku, Nadiya anasema alisikia majirani zake wakikimbia chini kwenye ngazi wakipaza sauti: "Ondoka! Ondoka!"
Mama mdogo alisita kwa sekunde kadhaa. Kisha akabubujikwa na machozi.
Hatimaye, aliondoka kwenye jengo hilo akiwa na watoto wake wawili, lakini akasema hakuweza kutambua ujirani huo kwani majengo karibu na mtaa wake yalikuwa yamesambaratishwa.
Sasa anajaribu kuelekea nyumbani kwa wazazi wake. Lakini, anasema: "Unaweza kujificha wapi wakati kifo kinakuja kutoka mbinguni?"
Mfalme Charles III, Malkia Camilla Kuzuru Kenya Baadaye Mwezi Huu
Chanzo cha picha, EPA
Mfalme wa Uingereza Charles III na mkewe Malkia Camilla watafanya ziara ya kiserikali ya siku nne nchini Kenya kuanzia mwisho wa mwezi huu, Kasri la Buckingham lilitangaza Jumatano.
"Mfalme na Malkia watafanya Ziara ya Kiserikali nchini Kenya, kuanzia Jumanne tarehe 31 Oktoba hadi Ijumaa Novemba 3, 2023, kusherehekea uhusiano mzuri kati ya nchi hizo mbili na ushirikiano thabiti na wenye nguvu wanaoendelea kuuanzisha," ilisema ikulu.
Ziara hiyo inajiri huku Kenya ikijiandaa kusherehekea miaka 60 ya uhuru.
Itakuwa ziara ya kwanza ya Mfalme Charlse katika taifa la Jumuiya ya Madola ikizingatiwa kwamba ni nchi ambayo utawala wa Malkia Elizabeth II ulianza, baada ya kuchukua kiti cha enzi nchini Kenya mnamo Februari 1952.
Mfalme na Malkia wanatarajiwa kuzuru Kaunti ya Jiji la Nairobi, Kaunti ya Mombasa na maeneo jirani.
''Mpango wa Mfalmewao utaakisi njia ambazo Kenya na Uingereza zinafanya kazi pamoja, haswa ili kuimarisha ustawi wa pande zote, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, kukuza fursa na ajira kwa vijana, kuendeleza maendeleo endelevu na kuunda eneo lenye utulivu na usalama zaidi.'' ilisema taarifa rasmi iliyotolewa na tovuti ya serikali ya Uingereza.
Mchapishaji Kenya aondoa kitabu baada ya malalamishi kuhusu picha ya Mtume Muhammad
Maelezo kuhusu taarifa
Author, Wycliffe Muga
Nafasi, BBC News, Nairobi
Chanzo cha picha, AFP
Mchapishaji mmoja nchini Kenya ameondoa kitabu cha shule ambacho kilikuwa na mchoro unaoonyesha Mtume Muhammad kufuatia kilio cha viongozi wa Kiislamu na wazazi.
Walilalamika kwamba ilikuwa ni kufuru kumchora mtume na kuwauliza wanafunzi wachore rangi katika mfano huo.
Kampuni ya Mentor Publishing ilisema inajutia kosa "kubwa" katika kitabu cha masomo ya Kiislamu kwa wanafunzi wa mwaka wa pili wa shule ya msingi.
Takriban 11% ya Wakenya ni Waislamu, kundi la pili kwa ukubwa la kidini.
Picha za Mtume Muhammad zinaweza kusababisha machukizo makubwa kwa Waislamu, huku viongozi wengi wa dini ya Kiislamu wakisema kuwa mila inakataza wazi picha za Mtume Muhammad na Mwenyezi Mungu (Mungu).
Mwanazuoni wa Kiislamu kutoka mji wa pwani wa Mombasa, Sheikh Rishard Rajab Ramadhan, aliambia BBC kwamba kitabu hicho "kinahatarisha" na kilipotosha watoto wadogo.
"Hakuna mtu anayepaswa kufikiria, acha kujaribu kumchora Mtume Muhammad. Hii inaweza kusababisha vita," Bw Ramadhan alisema.
Katika barua kwa jamii ya Kiislamu, mchapishaji huyo alisema imefika katika usikivu wake kwamba yaliyomo katika mojawapo ya vitabu vyake, Mentor Encyclopaedia Grade 2, ni "kukufuru kwa imani ya Kiislamu".
Mchoro huo "uliingizwa bila kukusudia" katika kitabu hicho, na "kutambuliwa kimakosa kama sura ya Mtume Muhammad", alisema mkurugenzi wa Mentor Josephine Wanjuki.
"Tunaomba radhi kwa dhati na kwa moyo wote kwa kosa hilo na tunajitolea kuhakikisha kuwa kosa kama hilo halitajirudia," aliongeza.
Mchapishaji huyo alisema kuwa ataondoa mara moja mchoro huo wa kukera kutoka kwa matoleo yote yajayo na amejitolea kufanya kazi na Baraza la Elimu ya Kiislamu kukagua vitabu vyake vyote.
Walimu wote, wanafunzi na wasimamizi wa shule walio na nakala za kitabu wameshauriwa kuzirejesha kwa mchapishaji.
Bw Ramadhan alikaribisha hatua ya kurudisha nakala za kitabu hicho, lakini akawataka wachapishaji kushauriana na viongozi wa Kiislamu kabla ya kuchapisha vitabu vya Kiislamu.
Masomo ya kidini ni sehemu ya mtaala katika shule za Kenya.
Suala la kumuonyesha Mtume Muhammad (saw) limekuwa gumzo la muda mrefu na limezusha mivutano hasa barani Ulaya.
Mnamo 2020, mwalimu wa shule katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris, Samuel Patywas alikatwa kichwa baada ya kutumia katuni za Mtume Muhammad wakati wa somo kuhusu uhuru wa kujieleza.
Mnamo mwaka wa 2021, mwalimu katika shule moja katika mji wa Batley nchini Uingereza alisimamishwa kazi baada ya maandamano ya wazazi Waislamu kwa kuonyesha katuni "isiyofaa" ya Mtume Muhammad.
Baadaye mwalimu alirudishwa kazini.Uchunguzi uligundua kuwa mwalimu hakukusudia kusababisha kosa kwa kuonyesha picha.
Hakuna marufuku maalum au ya wazi katika Quran, kitabu kitakatifu cha Uislamu, juu ya picha za Mtume Muhammad.
Lakini kuna marejeleo ya kutomuonyesha Mwenyezi Mungu na Waislamu wengi wanaamini kuwa hali hiyo inatumika kwa Mtume Muhammad.
Mkuu wa utawala wa kijeshi wa Mali ajadiliana na Rais wa Urusi
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Haya ni mazungumzo ya tatu kwa simu kati ya viongozi hao wawili katika muda wa miezi kadhaa
Rais wa mpito wa Mali na rais wa Urusi Vladimir Putin wamejadili ushirikiano wa kiuchumi na kiusalama wakati wa mazungumzo ya simu.
“Wakati wa majadiliano ya simu, nilizungumza na Rais Putin kuhusu ushirikiano wetu katika nyanja za kiuchumi, usalama na kukabiliana na ugaidi. Nilitoa shukrani zangu kwa msaada wote ambao Urusi inaipa Mali,” Kanali wa Mali Assimi Goita alisema katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X uliokuwa ukijulikana zamani kama Twitter.
Hayo yameungwa mkono na Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi.
Katika taarifa yake kwenye Telegram, ilisema viongozi hao wawili "walithibitisha dhamira yao ya pamoja ya kuimarisha zaidi uhusiano wa kibiashara na kiuchumi, ushirikiano katika kutoa usalama, na kupambana na ugaidi.Upande wa Mali ulitoa shukrani zake kwa misaada mbalimbali inayotolewa na Urusi".
Haya ni mazungumzo ya tatu kwa simu kati ya viongozi hao wawili katika muda wa miezi kadhaa.
Mamluki wa Urusi kutoka Kundi la Wagner wanachukua nafasi kubwa katika mashambulizi yanayoendelea ya jeshi la Mali dhidi ya waasi wa zamani wa Tuareg katika mji wa Kidal, ikiwa ni pamoja na kuuteka mji wa kimkakati wa Anefis tarehe 6 Oktoba baada ya siku kadhaa za mapigano makali.
Israel inatumia roketi za ardhini kufyatua katika mashambulizi yake dhidi ya Hamas
Maelezo ya picha, Picha ya kizinduzi kilichoshirikiwa na jeshi la Israeli
Jeshi la anga la Israeli linatumia ndege kushambulia maeneo ya Ukanda wa Gaza.
Asubuhi ya leo, walisema walikuwa wamefikia maeneo 450 yanayolengwa katika muda wa saa 24 zilizopita.
Wanajeshi wamesema hivi punde pia wanatumia roketi kwa mashambulizi ya ardhini.
Msemaji Daniel Hagari alisema ilikuwa ni mara ya kwanza kutumia aina hii ya kurusha risasi dhidi ya maeneo ndani ya Gaza tangu mzozo wa 2006.
Afghanistan yakumbwa na tetemeko la ardhi la pili ndani ya siku chache
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Tetemeko la ardhi la Jumamosi limewauwa zaidi ya watu 1,000
Tetemeko jingine
la ardhi limekumba magharibi mwa Afghanistan siku chache tu baada ya matetemeko
mawili makubwa katika eneo hilo kuua zaidi ya watu 1,000.
Tetemeko hilo jipya la kipimo
cha 6.3 lilipiga mwendo wa saa kumi na moja na dakika 10 (00:40 GMT) siku ya
Jumatano, kilomita 28 kaskazini mwa jiji la Herat.
Zaidi ya watu 100 wamejeruhiwa na kupelekwa
hospitalini, maafisa wa afya wamesema.
Athari kubwa bado
haijabainika, lakini wengi walikuwa wamelala nje baada ya nyumba zao kuharibiwa
siku ya Jumamosi.
Mashirika ya misaada yamesema
pia kuna uhaba wa blanketi, chakula na vifaa vingine.
Mtu aliyeshuhudia athari za
tetemeke eneo la kati la Herat, ambako baadhi ya nyumba bado zimesimama,
alisema aliamka akipiga kelele na kukimbia nje ya nyumba yake.
"Nilikuwa katika usingizi
mzito kwa sababu sikuwa nimelala siku zilizopita," aliambia BBC.
"Sijawahi kuhisi karibu
na kifo kama ilivyokuwa sasa," alisema, akiongeza kwamba alikimbia bila
viatu hadi viungani mwa jiji, ambapo wengi wamekuwa wakilala kwenye mahema
tangu tetemeko la kwanza.
Vifusi vilivyosalia kutoka kwa sehemu ndogo ya Titan vyapatikana kwenye bahari ya Atlantiki
Chanzo cha picha, US Coast Guard
Wahandisi wamepata vifusi vilivyosalia na mabaki ya watu wanaodhaniwa kutoka kwenye nyambizi ya Titan ambayo ilipasuka katika ajali mbaya ikielekea katika meli ya Titanic, iliozama Walinzi wa Pwani wa Marekani wanasema.
Chombo hicho kiliharibiwa wakati kilipopiga mbizi kuitazama ajali ya meli ya Titanic mnamo Juni.
Abiria wote watano waliokuwa ndani ya nyambizi hiyo waliuawa.Utafutaji wa nyambizi hiyo ndogo ulizua msako wa kimataifa na kuvutia umma hadi mabaka ya kwanza yalipopatikana siku kadhaa baadaye.
Walinzi wa Pwani walisema Jumanne kwamba sehemu za ziada za boti hiyo zilipatikana kutoka sakafu ya bahari wiki iliyopita na kupelekwa kwenye bandari ya Marekani.
Maafisa wa matibabu watachambua mabaki ya binadamu.Ingawa nyambizi ndogo ya Titan ilielezewa kuwa ya "majaribio" na OceanGate - kampuni iliyoijenga – Titan hiyo ilipiga mbizi mara kadhaa kwenye ajali ya Titanic, ambayo iko mita 3,800 (futi 12,467) chini ya usawa wa bahari katika Bahari ya Atlantiki Kaskazini.
Afisa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo, Stockton Rush, alikuwa ndani ya meli iliyoangamia, ambayo ilizama chini ya shinikizo kubwa la maji.
Abiria wengine wanne waliokufa ndani ya ndege hiyo walikuwa: Mfanyabiashara Mwingereza-Pakistani Shahzada Dawood, 48; mwanawe Suleman, 19; Mfanyabiashara Mwingereza Hamish Harding, 58; na Paul-Henry Nargeolet, 77, mpiga pinnzi wa zamani wa jeshi la wanamaji la Ufaransa.
Bomba la gesi na kebo ya chini ya bahari kati ya Finland na Estonia zimeharibika - Finland yaripoti kwa NATO
Chanzo cha picha, Reuters
Kulingana na mamlaka huko Helsinki, bomba la gesi chini ya bahari kati ya Ufini na Estonia liliharibiwa na usambazaji wa gesi kupitia bomba hilo umesitishwa kwa muda.
Waya ya mawasiliano ya simu iliyowekwa kando ya bomba hilo kati ya nchi hizo pia iliharibiwa.
Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema kuwa Umoja huo unafuatilia kwa karibu hali hiyo na, ikiwa ni lazima, iko tayari kusaidia washirika wake.
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak pia alisema Jumanne kwamba Uingereza iko tayari kuunga mkono Finland na Estonia katika kuchunguza ajali za bomba la gesi hiyo.
"Kama washirika na marafiki wa NATO, tumejitolea kuhakikisha usalama katika Bahari ya Baltic," Sunak aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X, akaunti ya zamani ya Twitter. " Uingereza iko tayari kusaidia katika uchunguzi.
"Bomba la gesi la Balticconnector la kilomita 77, ambalo linapita chini ya Ghuba ya Finland na kuunganisha mji wa Inkoo wa Finland na jiji la Estonia la Paldiski, lilifungwa mapema Jumapili asubuhi kutokana na kushuka kwa kasi kwa shinikizo katika mfumo.
Yaya Toure: Nyota wa zamani wa Manchester City na Barcelona anataka mameneja zaidi weusi kufunza Ulaya
Maelezo ya picha, Yaya Toure
Mchezaji wa zamani wa Ivory Coast Yaya Toure anatumai kuwa yeye na kaka yake Kolo wanaweza kuwasaidia wakufunzi weusi kujiunga na zaidi mchezo wa kulipwa.
Kiungo huyo wa zamani wa Manchester City na Barcelona alikuwa na muda mfupi wa kufundisha nchini Ukraine na Urusi kabla ya kujiunga na Tottenham kama mkufunzi wa Vijana wa timu ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 16 2022.
Toure, 40, aliondoka Spurs mwezi Juni na kuwa kocha msaidizi katika klabu ya Standard Liege ya Ubelgiji.
"Nataka kuona utofauti," Toure aliambia podikasti ya "Meneja Bora wa Afcon" kwenye BBC Mechi Bora ya Siku Afrika."Mara nyingi watu wamehoji ikiwa Waafrika au makocha weusi wataweza kuchukua masomo ipasavyo na kushiriki katika majukumu ya usimamizi.
"Nadhani sasa watapata jibu hivi karibuni."Ndugu yangu alikuwa wa kwanza - alianza [kufundisha], na mimi nilikuwa wa pili. Hebu tuone. Ninajipa changamoto katika kiwango cha juu Ulaya na tutaona kama fursa zitakuja."
Wabunge wa Zimbabwe wapoteza viti kwa sababu ya barua bandia
Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, CCC ililalamikia mbinu za vitisho wakati wa kampeni
Wabunge 15 wa upinzani nchini Zimbabwe
wamewasilisha rufaa mahakamani wakisema walidanganywa ili kupoteza viti vyao
vya ubunge.
Hii imekuja baada ya mtu mmoja
aliyedai kuwa Katibu wa chama hicho kwa uongo kusema kuwa wabunge hao si
wanachama tena.
Alipopokea barua hiyo ya ulaghai, spika wa bunge la Zimbabwe alitangaza kuwa
viti 15 viko wazi.
Matokeo ya uchaguzi mdogo yanaweza kukabidhi chama tawala cha Zanu-PF
idadi kubwa inayohitaji kufanya marekebisho ya katiba.
Barua ya Jumatatu ilitiwa saini na "Sengezo Tshabangu", ambaye
alidai kuwa katibu mkuu wa Citizens Coalition for Change (CCC), chama kikuu cha
upinzani nchini Zimbabwe.
Ilikuwa imejaa makosa ya kisarufi.
Kiongozi wa CCC Nelson Chamisa alimtaka spika Jacob Mudenda kupuuza
barua hiyo akisema chama hicho hakina katibu mkuu na hakijamfukuza wala
kumrudisha mbunge yeyote.
Mzozo wa Israel na Palestina: Kilichojiri saa chache zilizopita huko Israel na Gaza
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Roketi za Hamas zilinaswa na moto wa betri kutoka Iron Dome huko Ashkelon, Israel
Mashambulio ya kulipiza kisasi ya Israel
yameendelea usiku kucha na haya ndiyo tumekuwa tukiripoti katika saa chache
zilizopita:
Makumi ya ndege za kivita za Jeshi la anga
la Israel zimeshambuliazaidi ya shabaha 200 katika
kitongoji cha Al-Furqan huko Gaza, kinachoaminika kuwa kitovu ambacho Hamas hupanga na kutekeleza mashambulizi yao. Jeshi
la Israel linasema kuwa hili ni shambulio la tatu katika eneo hilo katika muda
wa saa 24 zilizopita.
·Idadi ya jumla ya waliofariki imepanda hadi
watu 2,100, huku idadi ya vifo nchini Israel ikiongezeka hadi 1,200 huku
maafisa wa Gaza wakisema watu 900 wamefariki.
Tumekuwa tukisikia kutoka kwa walionusurika katika
maeneo ya Gaza na Israel ambao
wanaelezea ukubwa wa uharibifu kama jambo ambalo
hawajawahi kukumbana nalo katika miongo kadhaa ya migogoro kati ya pande zote
mbili.
Nchini Israel watu wameelezea shambulio la Hamas kuwa ni
"mauaji ya raia". Huko Gaza, mfanyakazi wa kibinadamu aliambia
kipindi cha Newshour cha BBC kwamba hakuna "mahali popote
salama" kwa watu kwenda.
Rais wa Marekani Joe Biden amelaani uvamizi
wa Hamas dhidi ya Israel kama "uovu mtupu". Marekani
inaongeza msaada wa kijeshi kwa Israel - ndege
ya kwanza iliyokuwa imebeba silaha za Marekani iliwasili kusini mwa Israel Jumanne
jioni.
Josep Borrell, Mwakilishi Mkuu wa EU katika Mambo ya Nje, alisema mwitikio wa Israel huko Gaza unaweza kuwa umekiuka sheria za kimataifa . "Israel
ina haki ya kujilinda [yenyewe], lakini inabidi itekelezwe kulingana na haki ya
sheria za kimataifa, sheria za kibinadamu," alisema.
·Marekani inasema inajadiliana na Israel na
Misri kuhusu kujaribu kupata "njia salama" kwa raia wa Gaza.
Mshauri
wa usalama wa taifa wa Marekani Jake Sullivan anasema pande zote
"zimezingatia swali hili" lakini hakufichua maelezo zaidi.
Mkuu wa benki kuu ya Burundi aliyefutwa kazi akamatwa
Chanzo cha picha, Burundi central bank/X
Maelezo ya picha, Dieudonné Murengerantwari aliteuliwa kuwa serikali ya benki kuu mnamo 2022
Gavana wa benki kuu ya Burundi aliyefutwa kazi hivi
majuzi amekamatwa kwa tuhuma za ufisadi.
Dieudonné Murengerantwari ameshutumiwa na wizara ya
sheria kwa "kuhujumu utendakazi mzuri wa uchumi wa taifa, ufisadi wa kimya
kimya, ufujaji wa pesa na ufujaji wa mali ya umma".
Hajajibu tuhuma zinazomkabili.
Siku ya Jumapili, Rais wa Burundi Évariste
Ndayishimiye alimfukuza kazi Bw Murengerantwari na nafasi yake kuchukuliwa na
Édouard Normand Bigendako.
Bw Murengerantwari alikuwa ameteuliwa kuongoza
benki kuu ya Burundi kwa miaka mitano kuanzia Agosti mwaka jana.
Mwanasheria Mkuu Leonard Manirakiza Jumanne alisema
kuwa madai dhidi ya Bw Murengerantwari ni ya muda huku uchunguzi ukiendelea.
Pia alisemautaratibu wa sheria unafuatwa huku Bw
Murengerantwari akiendelea kuzuiliwa.