Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mamia ya wanajihadi wawaua wanajeshi nchini Niger
Mamia ya wanamgambo wa Kiislamu waliokuwa wakiendesha pikipiki wameshambulia mji wa kusini-magharibi mwa Niger na kuua wanajeshi 12, wizara ya ulinzi imesema.
Moja kwa moja
Mbwa alaumiwa kwa kumnyima Mkenya ushindi katika marathon
Seneta mmoja nchini Kenya amekosoa mashirika ya michezo ya kushindwa kuchukua hatua baada ya mbwa kumfukuza mwanariadha Robert Kimutai Ng’eno wakati wa mashindano ya riadhaa ya Buenos Aires wiki iliyopita.
Ripoti zinasema mwanariadha huyo alionekana akiongoza akiwa amesalia na kilomita 4 kukamilisha mbio hizo, wakati mbwa alipojitokeza na kuanza kumfukuza.
Licha ya juhudi za baadhi ya watazamaji kumfukuza mbwa huyo, tukio hilo lilionekana kumfanya Ng’eno kupoteza mweleko na hatimaye kumalizia katika nafasi ya tatu kwenye mbio hizo.
Raia wenzake wa Kenya Cornelius Kiplagat na Paul Kipngetich Tanui waliibuka katika nafasi ya kwanza na ya pili mtawalia.
Picha inayoonyesha mbwa akimfukuza Ng’eno imesambaa sana katika mitandao ya kijamii na baadhi wameuliza kwanini juhudi zaidi hazikuchukuliwa kumlinda wanariadha.
“Mwanariadha hakupewa heshima yake na kukabiliwa na kejeli,” alisema Seneta Samson Cherargei kwenye mtandao wa X (zamani uliokuwa ukijulikana kama Twitter).
Alisema kwamba Waziri wa Michezo wa Kenya Ababu Namwamba na shirika la wanariadha la Kenya hawakusimama na mwanariadha huyo, huku akiongeza kwamba “hawajachukua hatua kwa kueleza malalmishi yao au kutoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi na mamlaka za Argetina.
Pia unaweza kusoma:
- Tetesi za soka Ulaya Ijumaa 29.09.2023
Mke wa rais wa Gabon ashtakiwa kwa utakatishaji fedha
Sylvia Bongo, mke wa Rais aliyeondolewa madarakani wa Gabon, Ali Bongo, ameshtakiwa kwa utakatishaji fedha, kupokea mali ya wizi, kughushi.
Mwendesha mashtaka wa umma Andre Patrick Roponat alitangaza Ijumaa kuwa kesi ya Sylvia Bongo ilifikishwa mbele ya hakimu anayechunguza kesi siku moja kabla.
Pia alisema amri yake ya kukamatwa nyumbani ilikuwa ikifikiriwa.
Mashtaka hayo yanajiri baada ya wiki kadha ya sintofahamu kuhusu wapi alipo mke wa rais Bongo, baada ya kuzuiliwa kuondoka nyumbani mnamo Agosti 30 wakati jeshi lililopompindua mume wake.
Uamuzi wa kumshtaki mke huyo wa rais wa zamani unafanyika kufuatia mtoto wake wa kiume Noureddin Bongo pia kushtakiwa kwa tuhuma za ufisadi na kuiba mali ya umma.
Mtoto huyo bado anazuiliwa akisubiri kufikishwa mahakamani.
Hata hivyo, rais aliyeng’olewa madarakani Ali Bongo ambaye utawala wake ulighubikwa na ufisadi ameachiliwa huru na serikali ya kijeshi na kukubaliwa kusafiri nje ya nchi kupata matibabu kama alivyo kuwa ameomba awali.
Pia unaweza kusoma:
- Familia moja iliyoiongoza Gabon kwa miaka 56. Je mapinduzi haya ndio mwisho wake?
Mamia ya wanajihadi wawaua wanajeshi nchini Niger
Mamia ya wanamgambo wa Kiislamu waliokuwa wakiendesha pikipiki wameshambulia mji wa kusini-magharibi mwa Niger na kuua wanajeshi 12, wizara ya ulinzi imesema.
Wanajeshi saba wameuawa katika mapigano, na wengine watano wamefariki katika ajali ya barabarani kujibu shambulio hilo.
Waziri wa ulinzi alisema zaidi ya wanamgambo 100 wameuawa katika shambulio la kukabili.
Mashambulio ya wanajihadi dhidi ya jeshi yameongezeka tangu jeshi lilipochukua mamlaka mnamo mwezi Julai.
Jeshi lilisema lilifanya mapinduzi hayo ili kuweza kupambana vyema na wanamgambo hao ambao baadhi yao wanahusishwa na al-Qaeda na kundi la Islamic State.
Utawala wa kijeshi umeamuru wanajeshi wa Ufaransa walioko nchini humo kusaidia kupambana na wanajihadi kuondoka na wiki iliyopita, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikubali kuwaondoa.
Balozi wa Ufaransa aliondoka Niger mapema wiki hii baada ya kuishi chini ya amri ya watawala wa kijeshi kwa wiki kadhaa katika ubalozi huo.
Sasa amerudi Paris, Sylvain Itté aliiambia TV ya Ufaransa kuwa lengo lilikuwa "kunivunja moyo".
Ripoti zinasema wanajeshi kutoka maeneo mbali mbali ya nchi wameitwa kwenda mji mkuu, Niamey kulinda viongozi wa mapinduzi, na hivyo kuyaacha maeneo mengi katika hatari ya kushambuliwa na makundi yaliojihami.
Takribani wanajeshi 17 waliuliwa mwezi uliyopita kwenye shambulio lingine kwenye mpaka na Burkina Faso.
Shambulio hilo ndio baya zaidi kuwahi kutokea tangu kufanyika kwa mapinduzi.
Waziri wa Ulinzi wa Niger Salifou Mody alisema shambulio liliotokea siku ta Alhamisi lilitekelezwa na “mamia ya magaidi waliokuwa wakiendesha pikipiki” wakielekea mji wa Kandadji.
“Oparesheni ya kuwatafuta na kuwaangamiza magaidi sasa imeanzishwa ili kumkamata adui,” Waziri huyo alisema.
Bado haijabainika nani alikuwa nyuma ya shambulio hilo.
Soma zaidi:
- 'Ufaransa inatuchukulia kama wajinga' - Ndani ya Niger iliyokumbwa na mapinduzi
- Mapinduzi Niger: Historia ya mapinduzi manne Niger tangu uhuru
Marekani yaomba hatua za haraka kuchukuliwa Ethiopia
Marekani imeelezea wasi wasi wake kuhusu mzozo unaondelea katika majimbo ya Ethiopia ya Amhara na Oromia, na imetoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo ya kisiasa ili kutatua mzozo huo.
Akizungumza kwa njia ya simu na Wazri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, Waziri wa masuala ya kigeni wa Marekani Antony Blinken aliomba kulindwa kwa haki za kibinadamu.
Kulingana na shirika moja la kibinafsi linalofuatilia mzozo huo, Ethiopia Peace Observatory, katika wiki mbili ziliopita kumetokea makabiliano 26 katika maeneo tofauti tofuati kwenye jimbo la Amhara kati ya makundi ya kujihami na wanajeshi wa serikali.
Operesheni ya kuvunja jeshi la kikanda imepingwa vikali, na kusababisha ghasia kuenea.
Huko Oromia kumezuka ghasia zaidi kati ya wanajeshi na waasi wa Oromo Liberation Army.
Katika wito wake na waziri mkuu wa Ethiopia, Bw Blinken pia alizungumzia uwezekano wa kurejesha msaada wa chakula kwa Ethiopia.
Marekani na Umoja wa Mataifa ziliisimamisha miezi mitano iliyopita kutokana na tuhuma za wizi.
Kumekuwa na ripoti za mamia ya watu kufariki kutokana na njaa katika eneo la Tigray kaskazini.
Kuzima kwa mtandao kunaoendelea katika maeneo yenye migogoro nchini Ethiopia kumefanya kuwa vigumu kupata taarifa za wakati halisi.
Pia unaweza kusoma:
- Mzozo wa Tigray, Ethiopia: Kwa nini ulimwengu mzima una wasiwasi na mzozo huu?
Marekani yamuwekea vikwazo waziri wa zamani wa Sudan kwa 'kutatiza amani'
Marekani imemuwekea vikwazo Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Sudan Ali Karti na makampuni mawili - moja yenye makao yake makuu nchini Urusi - inayowashutumu kwa kuhujumu amani nchini Sudan.
Bw Karti, ambaye alihudumu katika serikali ya rais aliyepinduliwa Omar al-Bashir, ndiye kiongozi wa Vuguvugu la Kiislamu la Sudan lenye kuungwa mkono na jeshi.
"[Karti] na maafisa wengine wa zamani wa serikali sasa wanatatiza juhudi za kufikia usitishaji vita kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na kundi la Rapid Support Forces (RSF)," Wizara ya fedha imesema katika taarifa yake.
Vuguvugu la Kiislamu la Sudan limejibu kwa kuelezea vikwazo hivyo kama "ishara ya heshima", limesema shirika la habari la Reuters.
Pia mwingine aliyewekewa vikwazo ni kampuni ya GSK Advance, yenye makao yake nchini Sudan ambayo Wizara hiyo ilisema imetumika "kama njia ya kufanyika kwa manunuzi ya kundi la RSF".
Marekani inasema GSK ilifanya kazi na Aviatrade LLC, kampuni ya usambazaji wa kijeshi yenye makao yake nchini Urusi, "kupanga ununuzi wa vifaa".
"Tutaendelea kuwalenga wahusika wanaoendeleza mzozo huu kwa manufaa ya kibinafsi," iliongeza wizara hiyo.
Mapema mwezi huu, Marekani iliweka vikwazo vya kifedha kwa naibu kiongozi wa RSF Abdel Rahim Dagalo na kupiga marufuku kusafiri kwa kamanda wa kundi hilo katika jimbo la Darfur Magharibi, Jenerali Abdul Rahman Juma, kwa madai ya ukiukaji wa haki za binadamu.
Wawili hao walikanusha shutuma za Marekani.
Mwezi Juni, Marekani pia iliweka vikwazo kwa makampuni yanayomilikiwa na makundi yanayopigana ya kijeshi ya Sudan.
pia unaweza kusoma:
Putin akutana na kamanda wa zamani wa Wagner Troshev
Rais wa Urusi Vladimir Putin amekutana na mmoja wa makamanda wakuu wa zamani wa kundi la mamluki la Wagner, ambaye Kremlin inasema sasa anafanya kazi katika wizara ya ulinzi.
Andrei Troshev ni msaidizi wa zamani wa kiongozi marehemu Wagner Yevgeny Prigozhin, ambaye aliuawa katika ajali ya ndege mwezi Agosti.
Kifo chake kilikuja miezi miwili baada ya wanajeshi wa Wagner kuandamana kwa muda mfupi kuelekea Moscow.
Rais Putin alimwomba Bw Troshev kusimamia vitengo vya wapiganaji wa kujitolea nchini Ukraine, Kremlin ilisema.
Akizungumza na Bw Troshev, rais alisema anaweza kushirikiana kwa karibu na "vitengo vya kujitolea vinavyoweza kufanya kazi mbalimbali katika mapigano, zaidi ya yote, bila shaka, katika eneo la operesheni maalum ya kijeshi", akimaanisha Ukraine.
"Unajua kuhusu masuala ambayo yanahitaji kutatuliwa mapema ili mipangilio katika eneo la mapigano iende kwa njia bora na yenye mafanikio," Bw Putin aliongeza.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliambia shirika la habari la RIA kwamba Bw Troshev "sasa anafanya kazi katika wizara ya ulinzi".
Mkutano huo unawadia wakati Bw Putin akijaribu kuhakikishia mamlaka yake kufuatia maasi ya Wagner mwezi Juni.
Katika muda wa saa 24 tu, Prigozhin ilifanya uasi, na kutuma wanajeshi katika mji wa kusini wa Rostov, kisha zaidi kuelekea Moscow, kabla ya kurudi nyuma.
Ilikuwa changamoto kubwa zaidi kwa mamlaka ya Bw Putin katika miongo miwili.
Mwezi uliopita, rais alitoa wito kwa wafanyikazi wote wa Wagner na wakandarasi wengine wa kijeshi wa kibinafsi wa Urusi kula kiapo cha utii kwa serikali ya Urusi.
Soma zaidi:
- Vita nchini Ukraine: Je, Ukraine imevunja ngome za ulinzi mkali za Urusi?
Victor Osimhen: Napoli 'haikuwa na nia ya kumuudhi au kumkejeli' mshambuliaji lakini hawakuomba msamaha kwa TikTok
Napoli walisema "hawakuwa na nia ya kumuudhi au kumkejeli" Victor Osimhen katika chapisho la mtandao wa kijamii lakini hawakumuomba msamaha hadharani.
Klabu hiyo ilishirikisha umma video kwenye akaunti yao ya TikTok ya Osimhen wa Nigeria akikosa penalti, iliyopewa jina la sauti ya juu ikisema ''Nipatie penati tafadhali''-"gimme penalty please".
Wakala wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 ametishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya klabu hiyo.
Taarifa ya Napoli ilisema "kamwe haikuwa nia ya klabu kumkasirisha Victor" ikiwa "iwapo ameona hivyo".
Chapisho la mitandao ya kijamii limefutwa.
Napoli inaeleza kuwa haikuwahi kumuudhi au kumkejeli Victor Osimhen, ambaye ni kiungo muhimu wa kiufundi wa klabu ," ilisema taarifa kwenye tovuti ya klabu hiyo.
"Ushahidi wa hili ni ukweli kwamba klabu ilikataa kwa dhati ofa zote ilizopokea za uhamisho wa mshambuliaji nje ya nchi."
Mkufunzi wa Napoli Rudi Garciaalisema Osimhen ''amewekeza 100%katika klabu hiyo ya Serie A baada ya kufunga bao katika ushindi wa 4-1 dhidi ya Udinese Jumatano - mechi ya kwanza tangu tukio hilo.
Osimhen aliifungia timu yake bao la pili katika ushindi mnono lakini hakujaribu kushangilia kabla ya kuwindwa na wachezaji wenzake.
Habari za hivi punde, Mlipuko nchini Pakistan wasababisha vifo vya watu 50
Takriban watu 50 wameuawa na zaidi ya 50 kujeruhiwa katika mlipuko uliotokea Pakistan, polisi wameiambia BBC.
Mlipuko huo ulitokea karibu na msikiti mmoja katika mkoa wa kusini magharibi wa Balochistan siku ya Ijumaa wakati watu walipokusanyika kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume Muhammad.
Polisi wanashuku lilikuwa shambulio la kujitoa mhanga lililolengwa katika mkusanyiko wa kidini katika mji wa Mastung.
Maafisa wametangaza hali ya hatari.
Majeruhi wanasafirishwa hadi hospitali mbili, polisi wamesema.
Maafisa wawili wa polisi wa mji wa Mastung walithibitisha hesabu ya vifo kwa BBC News.
Waziri wa Mambo ya Ndani Sarfraz Bugti aliutaja mlipuko huo kuwa "kitendo cha kuchukiza sana".
Video nyingi kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha majeruhi wakiokolewa na wahudumu wa dharura na wenyeji.
Hadi kufikia sasa, hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo.
Mamia ya wanamgambo wa Jihadi wafanya mashambulizi katika mji wa Niger
Serikali nchini Niger imesema takriban wanajeshi 12 wamefariki baada ya kushambuliwa na watu wanaoshukiwa kuwa wananmgambo wa jihadi kusini-magharibi mwa nchi hiyo.
Wizara ya ulinzi imesema wanajeshi saba waliuawa katika mapigano, wakati kikosi chao kiliposhambuliwa na mamia ya waasi waliokuwa kwenye pikipiki katika mji wa Kandadji.
Wengine watano walifariki katika ajali ya barabarani walipokuwa wakijaribu kuja kusaidia kitengo hicho.
Washirika wa ndani wa al-Qaeda na kundi la Islamic State wanafanya kazi katika eneo hilo - ambalo liko karibu na mpaka wa Mali na Burkina Faso
Putin afanya mazungumzo na kiongozi wa mashariki mwa Libya
Rais Vladimir Putin wa Urusi amefanya mazungumzo na kiongozi wa kijeshi wa mashariki mwa Libya, Khalifa Haftar mjini Moscow.
Vikosi vya Jenerali Haftar vilitegemea zaidi mamluki wa Urusi Wagner - ambao wengi wao bado wako mashariki mwa Libya - wakati wa shambulio lake ambalo halikufanikiwa mjini Tripoli miaka minne iliyopita.
Msemaji wa Kremlin alisema walijadili hali ya Libya na eneo hilo.
Vikosi vya Jenerali Haftar vinatawala mashariki mwa nchi hiyo, huku serikali inayotambulika kimataifa yenye makao yake makuu mjini Tripoli ikidhibitiwa na baadhi ya nchi za magharibi.
Urusi kwa muda mrefu imekuwa ikitafuta kuongeza ushawishi wake barani Afrika.
Unaweza pia kusoma:
- Wagner Afrika: Mustakabali usioeleweka baada ya kifo cha Prigozhin
- Mkutano wa Urusi na Afrika: Putin anataka kuongeza ushawishi
Itachukua miezi 6 hadi hali ya umeme kutengamaa Tanzania
Mkuu mpya wa kampuni ya umeme inayomilikiwa na serikali ya Tanzania, Gissima Nyamo-Hanga, amepewa muda na Rais Samia Suluhu kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi.
Kampuni ya umeme inayomilikiwa na serikali nchini Tanzania (Tanesco) imesema ukame unaosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na masuala ya matengenezo ndio chanzo cha uhaba mkubwa wa umeme unaotarajiwa kudumu hadi mwezi Machi mwaka ujao.
Wiki iliyopita, hatua za mgao zilianzishwa kote nchini.
Rais Samia Suluhu Hassan amesema ifikapo Machi hataki kusikia mgawo wa umeme.
Bw Nyamo-Hanga amesema mitambo ya taifa inakabiliwa na uharibifu wa miundombinu katika vituo vya umeme vinavyotumia gesi na kupungua kwa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme.
Hivi karibuni uwezo huo utapata nguvu kubwa kwani bwawa katika mbuga ya wanyama, ambalo lilikabiliwa na ukosoaji mwingi kutoka kwa wanamazingira, sasa linakaribia kukamilika.
Pia kuna miradi muhimu ya jua imo njiani kukamilika.
Chini ya nusu ya Watanzania wote wana umeme nyumbani na kwa ongezeko kubwa la watu itakuwa ni changamoto kumudu mahitaji ya umeme yanayoongezeka.
Unaweza pia kusoma:
- Uhaba wa maji: Ni wakati wa jiji la Dar es salaam kufunga mkanda?
- Uhaba wa maji: Ni wakati wa jiji la Dar es salaam kufunga mkanda?
Kiatu cha zamani zaidi chapatikana katika pango la popo Uhispania
Wanasayansi wanasema wametambua viatu vikongwe zaidi barani Ulaya, viatu vilivyofumwa kwa nyasi vinavyodhaniwa kuwa na umri wa miaka 6,000 hivi.
Vilikuwa miongoni mwa vitu vya kale vilivyogunduliwa katika pango la popo nchini Uhispania baada ya kuporwa na wachimba migodi katika Karne ya 19, lakini vilichambuliwa katika utafiti mpya.
Unyevu mdogo na upepo wa baridi kwenye pango ulivifanya vihifadhiwe vizuri isivyo kawaida.
Watafiti pia walichambua vikapu na seti ya zana.
Vitu hivyo ni seti ya zamani zaidi na iliyohifadhiwa zaidi ya nyenzo za nyuzi za mmea kusini mwa Ulaya inayojulikana hadi sasa." mwandishi mwenza wa utafiti huo María Herrero Otal alisema.
"Anuwai za kiteknolojia na jinsi malighafi zilizoandikwa zinaonyesha ustadi wa jamii zilizoishi kabla ya historia," aliongeza.
Mbinu mpya za kutafuta terehe zilizotumika zilionyesha kuwa mkusanyiko wa vitu 76 vilivyopatikana kwenye pango hilo vilikuwa na umri wa miaka 2,000 kuliko ilivyofikiriwa hapo awali.
Baadhi ya vitu katika mkusanyika huo vina zaidi ya miaka 9,000.
Viatu vilivyochambuliwa vilitumia aina tofauti za nyasi katika muundo wao, watafiti walisema, lakini pia ni pamoja na vifaa vingine kama vile ngozi na chokaa.
Shambulio la risasi Rotterdam: Mshambuliaji akamatwa baada ya kuua watu watatu
Polisi wa Uholanzi wamemkamata mtu aliyejihami kwa bunduki ambaye aliwaua takriban watu watatu katika matukio mawili ya ufyatuaji wa risasi katika mji wa Rotterdam.
Wanasema mshambuliaji huyo wa kiume, 32, alifyatua risasi katika nyumba moja kabla ya kuiteketeza, kisha akavamia kituo cha matibabu cha Erasmus cha jiji hilo siku ya Alhamisi.
Alikuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Erasmus, ambacho kina uhusiano na hospitali hiyo.
Mwanamke, mwenye umri wa miaka 39, na binti yake mwenye umri wa miaka 14 waliuawa katika shambulio la kwanza. Mhadhiri wa kiume, mwenye umri wa 43, aliuawa pia kwa kupigwa risasi hospitalini.
Picha zimeibuka zikimuonyesha mwanaume aliyevalia mavazi ya siri akichukuliwa kutoka kwenye jengo la hospitali akiwa amefungwa pingu. Sababu za shambulio hilo hazikujulikana mara moja.
Mlinzi ambaye anasema kuwa alikuwa wa kwanza kwenye eneo la tukio aliiambia BBC kuwa ilikuwa siku "ya kushtua".
"Ilikuwa mbaya, mbaya," alisema, akionekana kuchanganyikiwa na hakutaka kutaja jina lake.
Alisema kuwa mtu mwenye bunduki hakuwa ameingia katika kituo cha matibabu kupitia lango kuu.
Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte aliandikakwenye mtandao wa kijamii: "Mawazo yangu yanaenda kwa waathiriwa wa ghasia, wapendwa wao na watu wote ambao wamekuwa na hofu kubwa."
Marubani wa Ukraine wameanza mafunzo ya silaha nchini Marekani huku wakifunzwa Kiingereza - Pentagon
Msemaji wa Pentagon Sabrina Singh amesema kuwa marubani wa Ukraine ambao wataendesha ndege za kivita za F-16 tayari wameanza mazoezi nchini Marekani.
Kulingana na Singh, wanajeshi hao wa Ukraine kwanza huchukua kozi za lugha, ambazo ni muhimu ili kupata ujuzi wa kuendesha ndege za Magharibi.
Singh amesema urefu wa mafunzo ya lugha hutegemea kiwango cha elimu ya marubani, hivyo haijulikani yatachukua muda gani.
Katikati ya mwezi Septemba, mkuu wa Walinzi wa Kitaifa jeshi la anga Merika, Michael Law, alisema kuwa mafunzo ya marubani wa Ukraine yataendelea kwa miezi mitatu hadi tisa, kulingana na kiwango cha ujuzi.
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, jeshi la Ukraine linatarajia kuanza safari za ndege za kivita na F-16 kufikia Februari 2024 - tarehe hizi kwa ujumla zinathibitishwa na makadirio ya Michael Law.
Nchi za Magharibi ziliahidi kuipatia Ukraine takriban wapiganaji 50 mafunzo ya matumizi ya silaha ya F-16.
Vita vya Ukraine: Soma zaidi
- MOJA KWA MOJA:Biden amuonya Putin: ''Madikteta watagharamika
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
Rais wa Rwanda amteua jenerali mshukiwa kuwa waziri
Rais wa Rwanda Paul Kagame amemteua afisa mkuu wa kijeshi kuwa waziri wa nchi kwa ushirikiano wa kikanda licha ya kwamba anashutumiwa kufanya kazi kwa karibu na kundi la waasi la Kongo.
Jenerali James Kabarebe, ambaye kwa miongo kadhaa amekuwa mshirika wa karibu wa Bw Kagame, alistaafu kutoka jeshi mwezi uliopita.
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa walichapisha ripoti mwezi Juni wakimtuhumu Jenerali Kabarebe kwa kuwa na jukumu kubwa katika kuratibu operesheni za kundi la waasi la M23 mashariki mwa DR Congo. Rwanda imekanusha kuwa jeshi lake limeunga mkono kundi la M23.
Tangu kundi hilo lianzishe tena uasi karibu miaka miwili iliyopita, mamia ya maelfu ya raia wamelazimika kuyahama makazi yao.
DR Congo inaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono M23 - madai ambayo yamekanushwa mjini Kigali.
Unaweza pia kusoma:
- Fahamu baadhi ya makundi ya waasi yanayoyumbisha amani ya DR Congo
- Mzozo wa DRC: Je inawezekana kuyamaliza makundi ya wapiganaji Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo
Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya mubashara leo ikiwa ni Ijumaa tarehe 29.09.2023