Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Rais wa Niger aiomba Marekani msaada baada ya mapinduzi

Mohamed Bazoum anaonya kuwa eneo hilo linaweza kuathiriwa na ushawishi wa Urusi kupitia kundi la Wagner.

Moja kwa moja

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo yetu ya mubashara leo tukutane tena hapo kesho majaaliwa

  2. Niger yavunja uhusiano na Nigeria, Togo, Marekani na Ufaransa

    Utawala wa kijeshi wa Niger umevunja uhusiano na Nigeria, Togo, Marekani na Ufaransa mkoloni wake wa zamani, baada ya kushindwa kwa mazungumzo na ujumbe wa Jumuiya ya Kikanda, ECOWAS yenye lengo la kutatua mzozo wa kisiasa uliomuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum wiki iliyopita.

    Katika hotuba ya runinga ya serikali ya Niger (RTN), Kanali Amadou Abdramane mwanachama wa utawala huo, alitangaza amri kadhaa zilizoamriwa na viongozi wa mapinduzi.

    "Kazi za mabalozi wa Jamhuri ya Niger nchini Ufaransa, Nigeria, Togo na Marekani zimesitishwa. Misimamo yote ya awali ambayo ni tofauti na amri hii inafutwa," Kanali Abdramane amesema.

    Ujumbe unaoongozwa na mkuu wa zamani wa jeshi la Nigeria, Jenerali Abdulsalami Abubakar, ulikutana na baadhi ya wanachama wa utawala wa kijeshi siku ya Alhamisi, lakini waliondoka baada ya saa chache tu bila dalili yoyote ya mafanikio.

    Serikali ya Nigeria na mkuu wa ECOWAS, Rais Bola Tinubu bado hajajibu hatua hii.

    Siku ya Ijumaa, Wakuu wa Ulinzi wa Afrika Magharibi, walihitimisha mkutano wa siku tatu huko Abuja, mji mkuu wa Nigeria ambapo majadiliano juu ya uwezekano wa kuingilia kijeshi yalifanyika, ikiwa diplomasia itashindwa.

    Soma zaidi:

    • Mapinduzi ya Niger: Viongozi wa Afrika Magharibi watishia kuingilia kijeshi
    • Mapinduzi Niger: 'Kwa nini naitaka Urusi na si Ufaransa'
    • Mapinduzi Niger: Je ni nchi gani zimekuwa na mapinduzi mengi zaidi Afrika?
  3. Kenya: Amnesty International yasema watu zaidi ya 11 waliuawa Kisumu, Kisii Mnamo Julai

    Ripoti mpya ya shirika la Amnesty International imefichua kuwa takriban watu 11 waliawa katika kauni za Kisumu na Kisii wakati wa maandamano ya upinzani dhidi ya serikali majuma mawili yaliyopita.

    Ripoti hiyo iliyotolewa kwa ushirikiano na Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK) na Chama cha Madaktari Kenya (KMA) siku ya Ijumaa, yanaonyesha kuwa polisi walitumia nguvu kupita kiasi kuwatawanya waandamanaji wakati wa ghasia hizo.

    "Kati ya tarehe 28-30 Julai 2023, Amnesty International Kenya, Chama cha Wanasheria wa Kenya na Chama cha Madaktari cha Kenya zilitembelea Kaunti za Kisumu na Kisii," mashirika hayo matatu yalibainisha katika taarifa ya pamoja.

    Matokeo ya ripoti hiyo pia yalibainisha kuwa katika kipindi hicho, kesi 107 za shambulio la polisi zilirekodiwa katika mikoa hiyo miwili, huku 47 kati ya hizo zikihusiana na risasi.

  4. Habari za hivi punde, Alexei Navalny: Kiongozi wa upinzani nchini Urusi ahukumiwa kifungo cha miaka 19 zaidi jela

    Kiongozi wa upinzani wa Urusi aliyefungwa jela Alexei Navalny amehukumiwa kifungo cha miaka 19 jela, katika kesi iliyofanyika katika gereza la mbali la wafungwa wanaoishi uhamishoni.

    Bw Navalny alipatikana na hatia ya kuanzisha na kufadhili shirika nashughuli zenye itikadi kali. Anakanusha mashtaka.

    Tayari anatumikia kifungo cha miaka tisa kwa ukiukaji wa msamaha, udanganyifu na kudharau mahakama. Mashitaka hayo yanatazamwa na watu wengi kuwa yenye uchochezi wa kisiasa.

    Tangu kufungwa kwake mwaka wa 2021, Bw Navalny amekuwa akishikiliwa gereza la mbali la wafungwa wanaoishi uhamishoni.

    Ukumbi gereza wa Penal Colony No 6 huko Melekhovo, lililoko kilomita 240 (maili 150) mashariki mwa Moscow, uligeuzwa kuwa chumba cha mahakama cha muda kwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Kremlin. Kesi hiyo ilifanyika faraghani.

    Waendesha mashitaka wa serikali ya Urusi walikuwa wamemuombea kifungo cha miaka 20 jela Bw Navalny katika "gereza maalumu la serikali" lenye vizuizi zaidi. Kwa kawaida magereza hayo huwekwa kwa ajili ya wahalifu hatari zaidi nchini Urusi.

    Katika ujumbe uliotumwa kwenye mitandao ya kijamii kabla ya hukumu hiyo, Bw Navalny alielezea kuwa anaamini atapewa kifungo cha mtu anayeunga mkono sugu wa Usoviet "Stalinist" gerezani kilichoundwa ili kuwatia hofu wapinzani wengine.

    Bw Navalny bado anaweza kukabiliwa na mashtaka zaidi. Anasema kuwa wachunguzi wamemwambia kutarajia kesi nyingine kuhusu mashtaka ya ugaidi.

    Kwa zaidi ya muongo mmoja, Bw Navalny alitaka kufichua ufisadi katika kiini cha mamlaka ya Urusi. Uchunguzi wake wa video umepata makumi ya mamilioni ya maoni mtandaoni.

  5. Mapinduzi ya Niger: Mgogoro kati ya rais wa Niger na jeshi

    Viongozi wa mapinduzi nchini Niger wamesema kuendelea kukosekana kwa usalama nchini humo kuwa moja ya sababu zilizowafanya kumpindua Rais Mohamed Bazoum wiki iliyopita.

    Lakini mtafaruku kati ya baadhi ya wanajeshi na rais umekuwa ukiongezeka, kulingana na mtaalam akizungumza kwenye BBC.

    Olayinka Ajala, kutoka Chuo Kikuu cha Leeds Beckett, alisema kuwa kuna mwelekeo wa kikabila katika mzozo wa madaraka pamoja na kuongezeka kwa hasira ya kuwepo kwa wanajeshi wa kigeni nchini humo.

    Rais Bazoum anatoka katika kabila la Waarabu walio wachache nchini humo na alionekana na baadhi ya watu kuwa na asili ya kigeni, Dkt Ajala aliambia BBC.

    "Hii haikukaa vyema ndani ya duru ya kijeshi, ambayo inaundwa na makabila makubwa," mtaalamu huyo ameandika.

    Dk Ajala pia alisema kuwa uhamisho wa wanajeshi wa Ufaransa kwenda Niger baada ya kufurushwa kutoka Mali mwaka jana na kuwekwa kwa vituo vya ndege zisizo na rubani za Marekani na Ufaransa nchini humo kumezidi kuwa vigumu kwa baadhi ya wanajeshi wa Niger.

    David Kampmann kutoka BBC Monitoring pia alisema kuwa kumekuwa na ripoti kwamba mtu aliyeongoza mapinduzi hayo, Jenerali Abdourahmane Tchiani, alikuwa karibu kubadilishwa na Bw Bazoum kama mkuu wa walinzi wa rais kama sehemu ya mageuzi ya vyombo vya usalama.

    Kisha akatangulia mbele ya haki kwa kumuondoa rais madarakani.

    Lakini hizi ni tetesi ambazo hazijathibitishwa, Bw Kampmann anasema.

    Maelezo zaidi:

    • Mapinduzi ya Niger: Viongozi wa Afrika Magharibi watishia kuingilia kijeshi
    • Mapinduzi ya Niger mtihani wa demokrasia Afrika Magharibi
    • Mapinduzi Niger: 'Kwa nini naitaka Urusi na si Ufaransa'
  6. Marekani yawakamata wanajeshi wawili wanaoshukiwa kutoa siri za kijeshi kwa China

    Wanajeshi wa kikosi cha wanamaji cha Marekani wamekamatwa kwa tuhuma za kutoa ujasusi wa kijeshi kwa China, maafisa wa Marekani wamesema.

    Jinchao Wei Thomas, 22, raia wa Marekani mwenye uraia, anatuhumiwa na Marekani kwa kula njama ya kupitisha taarifa za siri za ulinzi kwa mawakala wa China.

    Koplo mwingine wa jeshi la wanamaji wa Marekani, Wenheng Zhao Patrick, alikamatwa na Marekani kwa kupokea pesa badala ya picha na video muhimu.

    Haijabainika iwapo wakala huyo huyo wa China aliwasiliana na watu hao wawili.

    Wawili hao walikamatwa jimboni California siku ya Jumatano.

    Wei Jinchao alikamatwa akielekea kazini katika Kituo cha Wanamaji cha San Diego.

    Waendesha mashitaka wa California walifichua mashitaka hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini San Diego siku ya Alhamisi.

    Wei Jinchao, ambaye alifanya kazi kama mekanika kwenye meli ya mashambulizi ya amphibious USS Essex, ana kibali cha usalama cha kuweza kupata taarifa muhimu kuhusu meli ya kivita, walisema.

  7. Habari za hivi punde, Vita vya Ukraine: Meli ya Urusi yagongwa na droni kwenye Bahari Nyeusi, vyanzo vya Ukraine vinasema

    Meli ya jeshi la wanamaji la Urusi imeharibiwa katika shambulio la ndege isiyo na rubani ya jeshi la wanamaji la Ukraine katika Bahari Nyeusi, duru za Ukraine zimesema.

    Shambulio hilo limeripotiwa kutokea karibu na bandari ya Urusi ya Novorossiysk, ambayo ni kitovu kikuu cha usafirishaji wa bidhaa za Urusi.

    Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema imezima shambulio la Ukraine kwenye kambi yake ya jeshi la wanamaji lililohusisha ndege mbili zisizo na rubani za baharini, lakini haikukubali kuwa kulikuwa na uharibifu wowote.

    Lakini vyanzo vya usalama vya Ukraine vinasema kuwa Olenegorsky Gornyak ilipigwa na kuharibiwa vibaya.

    Waliiambia BBC kuwa ndege isiyo na rubani ilikuwa imebeba kilo 450 (lb 992) za baruti ilipoigonga meli hiyo.

    Urusi haikutaja uharibifu wowote katika ripoti yake ya tukio hilo.

    Ndege zisizo na rubani za baharini ni vyombo vidogo visivyo na rubani vinavyofanya kazi juu au chini ya uso wa maji.

    Video iliyotumwa kwa BBC na chanzo cha idara ya usalama ya Ukraine inaonekana kuonyesha ndege hiyo isiyo na rubani ikikaribia meli inayodhaniwa kuwa ni Olenegorsky Gornyak.

    Picha inaonyesha meli ikisafiri kabla ya picha kukatika, inaonekana kutokana na athari.

    Video nyingine ambayo haijathibitishwa inadhaniwa kuonyesha meli hiyo upande mmoja.

    Olenegorsky Gornyak ni meli , iliyoundwa kuzindua vikosi vya amphibious vilivyopo haribu na ufuo lakini pia kutia nanga na kupakua mizigo haraka bandarini.

    Uharibifu wowote kwake unaweza kuathiri juhudi za Urusi za kurudisha nyuma vikosi vinavyopigana katika eneo la kusini mwa Ukraine.

    Bandari ya Novorossiysk ilisimamisha shughuli zake kwa muda kufuatia shambulio hilo, kulingana na Caspian Pipeline Consortium, kampuni ambayo ambayo hupakia mafuta kwenye meli za mafuta kwenye bandari.

  8. Tazama: Jeti za RAF zinavyozuia ndege za kijeshi za Urusi wakati wa mashambulio ya Baltic

    RAF imetoa picha za ndege za kivita kutoka RAF Lossiemouth zikizuia ndege za Urusi.

    Wafanyakazi wa jeshi la anga walitumwa Estonia kusaidia doria katika anga ya Nato kwa muda wa miezi minne, ambapo walinasa ndege 50 za Urusi.

    Wafanyikazi wa RAF walitumia "zombie" kama neno la siri kwa ndege ya Urusi inayofanya kazi kwa kutia shaka.

    Ujumbe huo unaoitwa Operesheni Azotie, ulikuja huku kukiwa na mvutano mkali kati ya nchi wanachama wa Nato na Urusi kufuatia uvamizi wa Ukraine.

  9. DRC: Rais Tshisekedi azindua kumbukumbu ya mauaji ya kimbari

    Rais Felix Tshisekedi ameanzisha kumbukumbu ya mauaji ya kimbari yaliyofanywa dhidi ya watu katika katika Jamuhuri ya kidemokrasi ya Congo,

    Katika tukio hilo lililofanyaika jana katika mji mkuu Kinshasa, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, RDC, alitaka kukumbuka utu wa watu wote wa Congo ambao waliuawa bila sababu faida binafsi za watu binafsi kwasababu ya utajiri, kama ilivyoripotiwa na Radio ya Umoja wa Mataifa - Okapi.

    Ofisi ya Rais iliwataka wote kusimama kidete kupambana dhidi ya nchi za kigeni zilizoishambulia DRC.

    Rais Tshisekedi alizungumza alisema: "Ni kwa uchungu na huzuni, lakini pia kwa hamu na subira, kwa sababu ya tishio la kuwepo kwetu, kwamba ninazungumza; na kwa sababu ya kile ninachopaswa kufanya na kile ninachowajibika, kama mwakilishi wa nchi, katika kuanzisha amani kukumbuka Mauaji ya Kimbari nchini Kongo (GENOCOS), kuwakumbuka mamilioni ya watu waliouawa katika zaidi ya miaka 20 ya vitendo vya kikatili."

  10. Kocha wa Zambia Mwape anatuhumiwa kwa unyanyasaji wa kingono

    Fifa inachunguza malalamiko rasmi kwamba kocha mkuu wa Zambia Bruce Mwape alimnyanyasa kingono mchezaji katika Kombe la Dunia la Wanawake.

    Mwape anashutumiwa kwa kutomasa kifua cha mmoja wa wachezaji wake wakati wa mazoezi huko New Zealand mnamo 29 Julai.

    "Malalamiko yamepokelewa," msemaji wa Fifa alisema.

    Lakini Chama cha Soka cha Zambia (FAZ) kilisema "hakijapokea malalamiko kama hayo" na ilikuwa "mshangao" kwake.

    Tukio hilo linalodaiwa kuwa lilitokea wakati wa mazoezi siku mbili kabla ya mechi yao ya mwisho ya kundi dhidi ya Costa Rica, ambayo Zambia ilishinda 3-1 kwa ushindi wao wa kwanza kwenye Kombe la Dunia.

    Msemaji wa Fifa aliongeza: "Fifa inachukulia tuhuma zozote za utovu wa nidhamu kwa uzito mkubwa na ina mchakato wazi kwa yeyote katika soka ambaye anataka kuripoti tukio."

    Zambia imerejea nyumbani, baada ya kuondolewa baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu katika Kundi C.

  11. Habari za hivi punde, Axel Disasi: Chelsea imemsajili beki wa Ufaransa kwa mkataba wa miaka sita

    Beki wa kimataifa wa Ufaransa Axel Disasi amejiunga na Chelsea kutoka AS Monaco kwa mkataba wa miaka sita kwa Euro 45m (£38.57m).

    Disasi, 25, anatoa ulinzi katika uwanja wa Stamford Bridge baada ya jeraha la goti alilopataWsley Fofana.

    Alicheza katika michezo yote 38 ya Monaco ya Ligue 1 msimu uliopita.

    "Ninajivunia sana kuweza kuwa sehemu ya familia hii kubwa," Disasi aliambia tovuti ya Chelsea.

    "Natumai kupata mambo makubwa sana hapa. Kushinda mataji. Nitafanya kila niwezalo kufikia malengo hayo. Nina matarajio makubwa."

  12. Ethiopia kutangaza hali ya dharura Amhara

    Baraza la mawaziri la Ethiopia limepitisha uamuzi wa kutangaza hali ya dharura katika eneo lenye machafuko la Amhara kufuatia siku kadhaa za mapigano kati ya wanamgambo wa eneo hilo na jeshi.

    Hatua hiyo inajiri siku moja baada ya mkuu wa mkoa wa Amhara Yilkal Kefale kuitaka serikali ya muungano kuingilia kati suala la usalama katika eneo hilo kuwa "vigumu kudhibiti ndani ya mifumo ya kawaida ya utekelezaji wa sheria."

    Wanamgambo wa eneo hilo, wanaojulikana kama Fano, wamepata udhibiti wa miji na vijiji kadhaa pamoja na miji mikubwa zaidi.

    Safari za ndege zimesitishwa katika miji miwili ya eneo hilo na mtandao wa simu za mkononi umepotea.

    Taarifa iliyochapishwa na ofisi ya waziri mkuu ilisema agizo la katiba liko chini ya tishio katika eneo hilo linaloelezea hitaji la amri ya hali ya hatari.

    Uamuzi huo bado unapaswa kuidhinishwa na bunge ili kuwa na ufanisi.

  13. Boti zisizo na nahodha zashambulia kambi ya jeshi la wanamaji wa Urusi

    Milipuko imeripotiwa usiku kucha karibu na bandari ya Urusi ya Novorossiysk kwenye Bahari Nyeusi.

    Kanda zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii siku ya Ijumaa zilionekana kuonyesha milipuko mikubwa kwenye bandari hiyo, ambayo ni kitovu kikuu cha usafirishaji wa Urusi.

    Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema imezima shambulio la Ukraine kwenye kambi yake ya jeshi la wanamaji kwa kutumia boti mbili zisizo na nahodha.

    Ilisema boti hizo zisizo na nahodha zimepatikana na kuharibiwa na meli za Urusi zinazolinda bandari ya nje ya kituo cha jeshi la wanamaji.

    Bandari hiyo ilisimamisha kwa muda shughuli zake, kulingana na Caspian Pipeline Consortium ambayo hupakia mafuta kwenye meli za mafuta kwenye bandari.

    Ni boti ndogo zisizo na mshika usukani. Tofauti na ndege zisizo na rubani, hizi hufanya kazi juu au chini ya maji.

    Huduma za dharura katika eneo hilo zilithibitisha ripoti za milipuko na huduma za usalama zimefahamishwa, vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vinasema.

    Novorossiysk ni moja ya bandari kubwa katika Bahari Nyeusi.

    Utafiti wa BBC Verify unaonyesha kuwa Ukraine imefanya karivu mashambulizi 10 kwa boti zisizo na nahodha- zikilenga meli za kijeshi na kambi ya jeshi la wanamaji la Urusi huko Sevastopol, pamoja na bandari ya Novorossiysk katika shambulio la awali.

    Vyanzo vya ulinzi vya Ukraine vimeiambia CNN kwamba boti zisizo na rubani pia zilitumika katika shambulio kwenye daraja la Kerch hadi Crimea mwezi Julai.

    Ukraine haijatoa tamko lolote hadharani kuhusiana na mashambulizi hayo yaliyoripotiwa.

    Makabiliano baharini yameongezeka katika wiki za hivi karibuni, baada ya Urusi kujiondoa kwenye mpango wa usafirishaji nafaka kwa meli kati ya Urusi na Ukraine.

    Mapema wiki hii, Urusi ilifanya mashambulizi dhidi ya bandari za Odesa na Chornomorsk kwenye Bahari Nyeusi ambapo mamlaka ilisema tani 60,000 za nafaka ziliharibiwa.

    Soma:

  14. Utafiti: Ugunduzi wa bahati utakavyosaidia kupambana na malaria

    Wanasayansi wamegundua aina ya asili ya bakteria ambayo inaweza kusaidia kuzuia maambukizi ya malaria kutoka kwa mbu kwenda kwa wanadamu.

    Waliipata kwa bahati, baada ya kundi la mbu katika jaribio moja kutokuza vimelea vya malaria.

    Watafiti hao wanasema bakteria hao wanaweza kuwa chombo kipya cha kupambana na moja ya magonjwa kongwe zaidi duniani, ambayo huua watu 600,000 kila mwaka.

    Majaribio ya kutathmini usalama wake katika ulimwengu halisi sasa yanafanyika. Wanasayansi katika kituo cha utafiti nchini Uhispania, kinachoendeshwa na kampuni ya dawa ya GSK, walifanya utaifti huo baada ya kugundua kuwa kundi la mbu wanaotumiwa kutengeneza dawa hawana tena viini vya malaria.

    "Kiwango cha maambukizi katika mbu kilianza kupungua na hivyo kufikia mwisho wa mwaka mbu hawangeambukizwa vimelea vya malaria," anasema Dk Janneth Rodrigues, ambaye aliongoza mpango huo.

    Watafiti hao waligandisha sampuli kutoka kwa jaribio lao la 2014 na kuzirudia miaka miwili baadaye ili kuchunguza kile kilichotokea.

    Maelezo zaidi:

  15. Ujumbe wa ECOWAS waanza mazungumzo ya kutatua mzozo wa Niger

    Wajumbe kutoka Jumuiya ya Afrika Magharibi, ECOWAS wameanza mazungumzo ya kutatua mzozo wa kisiasa nchini Niger kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum wiki iliyopita.

    Rais wa Nigeria na mkuu wa jumuiya ya kikanda, Bola Tinubu alikuwa amewapa wajumbe jukumu la kuhakikisha "azimio la kirafiki" linafikiwa walipokuwa wakianzisha mazungumzo nchini Niger na maeneo mengine ya kanda.

    Ujumbe mmoja unaoongozwa na mkuu wa zamani wa jeshi la Nigeria, Jenerali Abdulsalami Abubakar unakutana na viongozi wa mapinduzi huko Niamey, mji mkuu wa Niger.

    Ujumbe wa pili unaongozwa na Balozi Baba Gana Kingibe, mwanadiplomasia wa Nigeria na Katibu wa zamani wa Serikali unatarajiwa kuzungumza na viongozi wa Libya na Algeria.

    Marekani pia imetoa wito wa kutafuta upatanishi wa amani nchini Niger.

    "Kwa sasa, tunaangazia diplomasia, tunaamini bado kuna nafasi ya kufikia hilo," msemaji wa Katibu wa Kitaifa wa White House, John Kirby aliambia mkutano mfupi, Alhamisi.

    ECOWAS ilikuwa imetoa msururu wa vikwazo, ikiwa ni pamoja na makataa ya siku 7 kulitaka jeshi nchini Niger kumrejesha madarakani Rais Bazoum aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, ambaye bado anashikiliwa na utawala huo.

    Ijumaa, Wakuu wa Ulinzi wa Afrika Magharibi Ijumaa, watahitimisha mkutano wa siku 3 huko Abuja, Nigeria ambapo majadiliano juu ya uwezekano wa kuingilia kijeshi yatafanyika, ikiwa diplomasia itashindwa.

    Soma zaidi:

    • Mapinduzi ya Niger: Viongozi wa Afrika Magharibi watishia kuingilia kijeshi
    • Mapinduzi Niger: 'Kwa nini naitaka Urusi na si Ufaransa'
    • Mapinduzi Niger: Je ni nchi gani zimekuwa na mapinduzi mengi zaidi Afrika?
  16. Trump akana mashtaka ya uchaguzi wa 2020

    Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amekana mashtaka ya kula njama ya kutengua uchaguzi wa 2020 katika mahakama ya Washington DC.

    Wakati wa kesi ambayo ilichukuwa muda mfupi, alizungumza kwa upole ili kuthibitisha ombi lake la kutokuwa na hatia, jina, umri na kwamba hakuwa chini ya ushawishi wa kilevi.

    Baadaye aliwaambia waandishi wa habari kesi hiyo ilikuwa "mateso kwa mpinzani wa kisiasa".

    Rais huyo wa zamani alionekana kwa mara ya tatu ndani ya miezi minne kama mshtakiwa wa uhalifu.

    Bw Trump aliingia kwenye mlango wa nyuma wa mahakama siku ya Alhamisi alasiri katikati mwa mji mkuu wa taifa hilo, mwendo mfupi kutoka eneo la ghasia katika bunge la Marekani ambalo ni msingi wa kesi ya mwendesha mashtaka.

    Takriban washtakiwa 1,000 walioshtakiwa kwa kushiriki katika shambulio dhidi ya Bunge la Marekani mnamo Januari 6, 2021 pia wamefikishwa katika mahakama hiyo.

    Hakimu Moxila Upadhyaya alimwambia rais huyo wa zamani asiwasiliane kuhusu kesi hiyo na kumuonya kwamba asipotii agizo hilo hati ya kukamtwa kwake itatolewa, masharti ya kuachiliwa itabatilishwa kwa kupuuza amri ya mahakama.

    Waendesha mashtaka waliomba kesi hiyo kusikilizwa kwa haraka.

    Lakini wakili wa Trump John Lauro alisema watahitaji muda zaidi kujiandaa.

    Alisema muda wa upande wa mashtaka ulikuwa wa "kushangaza" kutokana na kwamba uchunguzi wenyewe umechukua miaka mitatu.

    Madai hayo yaliyowekwa Jumanne katika hati ya mashtaka, ni pamoja na hesabu ya "njama ya kudhoofisha, kuzuia, na kuvuruga shuguli za serikali kwa kutumia ulaghai na udanganyifu".

    Bw Trump alishindwa katika uchaguzi wa 2020 na mpinzani wake wa chama cha Democratic, Joe Biden, lakini alikataa kukubali na kuongeza changamoto za wiki kadhaa katika majimbo kadhaa ya Marekani.

    Kwa sasa anawania kupeperusha bendera ya Republican katika kinyang'anyiro cha kuongia Ikulu ya White House 2024 na huenda akachuana tena na Biden katika uchaguzi ujao.

    Soma zaidi:

    • Trump kukabiliwa na kesi ya kula njama ya kubatilisha uchaguzi mahakamani
    • Trump ashtakiwa kwa jaribio la kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa 2020
    • Je, Donald Trump anakabiliwa na mashtaka gani ya jinai kuhusu nyaraka za siri?
    • Mashitaka ya Donald Trump: Rais wa zamani wa Marekani kushtakiwa kwa kutoa pesa kununua kimya cha muigizaji wa filamu za utupu
    • ‘Trump alijua wafuasi wake walikuwa wamejihami na aliwataka wavamie bunge’
  17. Niger: Rais wa Niger aiomba Marekani msaada baada ya mapinduzi

    Rais wa Niger aliyetimuliwa ameitaka Marekani na "jumuiya nzima ya kimataifa" kusaidia "kurejesha... utaratibu wa kikatiba" baada ya mapinduzi ya wiki iliyopita.

    Katika maoni kwenye gazeti la Washington Post, Rais Mohamed Bazoum alisema alikuwa akiandika "kama mateka".

    Machafuko yamezuka katika taifa hilo la Afrika Magharibi tangu alipoondolewa madarakani.

    Siku ya Alhamisi, viongozi hao wa mapinduzi walitangaza kuwa wanawaondoa mabalozi wa nchi hiyo kutoka Ufaransa, Marekani, Nigeria na Togo.

    Katika taarifa iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa, walisema kazi za mabalozi wanne "zimekatishwa".

    Saa chache tu kabla, balozi wa Niger nchini Marekani, Kiari Liman-Tinguiri, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba wanajeshi "lazima wafikirie" na "kutambua kwamba jambo hili haliwezi kufanikiwa".

    Niger ni mzalishaji mkubwa wa uranium - mafuta ambayo ni muhimu kwa nishati ya nyuklia - na iko kwenye njia kuu ya uhamiaji kwenda Afrika Kaskazini na Mediterania.

    Maelezo zaidi:

  18. Karibu katika matangazo ya moja kwa moja leo Ijumaa 04/08/2023