Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Putin aunga mkono uanachama kamili wa G20 na nafaka kwa Afrika

Anatumai uanacha wa Afrika katika G20 unaweza kuidhinishwa mwezi Septemba na kusema Urusi inaweza kuchukua nafasi ya mauzo ya nafaka ya Ukraine.

Moja kwa moja

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Hadi kesho kwaheri.

  2. Putin amzawadia rais wa Zimbabwe helikopta - Wizara

    Rais wa Urusi Vladimir Putin amemzawadia mwenzake wa Zimbabwe helikopta ya rais, kulingana na wizara ya habari ya Zimbabwe.

    Zawadi hiyo itatolewa hivi karibuni, taarifa hiyo iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii ilisema.

    Rais Emmerson Mnangagwa anahudhuria Mkutano wa Viongozi wa Urusi na Afrika huko St Petersburg pamoja na viongozi wengine wa Afrika.

    Urusi pia iliahidi kutoa nafaka bure kwa Zimbabwe na nchi nyingine tano za Afrika.

    Zimbabwe ina uhusiano wa muda mrefu na Urusi kuanzia vita vya ukombozi dhidi ya utawala wa wazungu wachache.

    Ni miongoni mwa nchi za Kiafrika ambazo zimeshikilia msimamo wa kutoegemea upande wowote katika vita vya Ukraine, zikikataa kulaani Urusi kwa uvamizi huo.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Myanmar: Aung San Suu Kyi aondolewa jela na kuwekwa katika kuzuizi cha nyumbani

    Kiongozi wa kiraia aliyeondolewa madarakani wa Myanmar Aung San Suu Kyi amehamishwa hadi kwenye kifungo cha nyumbani baada ya jeshi kumzuilia kufuatia mapinduzi ya Februari 2021.

    Bi Suu Kyi alipelekwa katika jengo la serikali huko Nay Pyi Taw siku ya Jumatatu, vyanzo vya magereza viliiambia BBC Burma.

    Alikaa mwaka mmoja katika kifungo cha peke yake. Mama huyo mwenye umri wa miaka 78 anatumikia kifungo cha miaka 33, baada ya kufungwa jela katika kesi zinazoendeshwa na jeshi.

    Hakuna habari yoyote iliyoibuka kuhusu hali yake kwa zaidi ya miaka miwili.

    Hakujawa na uthibitisho kutoka kwa jeshi kuhusu uhamisho wake kutoka jela, lakini hatua ya kuzuiliwa nyumbani inaweza kuwa ishara chanya kutoka kwa mamlaka, ambao wamekabiliwa na miito mingi ya kumwachilia kiongozi huyo aliyechaguliwa kidemokrasia nchini humo.

    Bi Suu Kyi alivumishwa kuwa alikuwa mgonjwa, lakini jeshi limekanusha taarifa hizo.

    Mapema wiki hii chanzo kutoka katika gereza la Nay Pyi Taw alikokuwa akishikiliwa kiliiambia BBC Burma kwamba yuko katika hali nzuri kiafya.

    Waziri wa mambo ya nje wa Thailand pia alifichua mwezi huu kwamba alimtembelea Bi Suu Kyi - hata hivyo hakufichua maelezo zaidi.

    Jeshi limepanga mkutano kati ya Bi Suu Kyi na T Khun Myat, Spika wa baraza la chini la bunge, BBC Burma iliripoti.

    Hata hivyo jeshi limekanusha kuwa kuna mazungumzo kama hayo yanayofanyika.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Kenya: Simba Jesse afia Maasai Mara baada ya kushambuliwa na mpinzani wake

    Wakenya wanaomboleza kifo cha simba wa kuhamahama, Jesse, aliyefariki baada ya mapigano ya kimaeneo na mpinzani wake huko Maasai Mara.

    "Alikuwa simba mzuri," lilisema shirika la Mara Predator Conservation Programme (MCPC) katika kutoa heshima zake kwenye Facebook.

    Taarifa za kusikitisha za simba aliyejeruhiwa vibaya awali zilitolewa na Shirika la Hifadhi ya Mara Kaskazini (MNC).

    Licha ya usaidizi wa haraka, Jesse ambaye alikuwa na umri wa miaka 12, hakuweza kunusurika katika shambulio hilo na alikufa kutokana na majeraha yake.

    Alizaliwa ndani ya MNC mapema 2011, Jesse na kaka yake Frank.

    Mnamo 2014, ndugu hao waliachana na kuchukua uongozi katika kundi jingine la simba.

    Wakati wao kama viongozi, Jesse na Frank walikuwa na watoto kadhaa.

    Ingawa wana wao wamekufa au wamepotea, binti zao wanasemekana "kuendeleza jamii yao."

    Mnamo mwaka wa 2016, Frank alipotea na Jesse akaanza maisha ya kuhamahama na ya kujitenga zaidi ingawa bado alikuwa akionekana katika hifadhi mbalimbali mara kwa mara.

    Jesse alirejea MNC mapema 2023, hata hivyo eneo ambalo aliwahi kutawala na kaka yake lilikuwa na viongozi wapya - wanaume wa Engoyanai.

    Ugomvi mbaya na wao ulisababisha kifo chake cha ghafla mnamo 24 Julai.

    Muda wa wastani wa maisha wa simba ni takriban miaka 13 porini, ingawa wanaweza kuishi muda mrefu zaidi wakiwa wanatunzwa mahali pamoja.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Kenya yathibitisha kushambaliwa kwa jukwa la serikali la E-citizen

    Serikali ya Kenya imethibitisha kuwa kulikuwa na shambulio la mtandao kwenye jukwaa la serikali mtandaoni.

    Tovuti ya E-citizen hutumiwa na umma kupata huduma zaidi ya 5000 za serikali ambazo ni pamoja na maombi ya pasipoti, leseni za kuendesha gari, kadi za utambulisho na rekodi za afya za kitaifa.

    Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Kidijitali nchini Eliud Owalo amethibitisha kuwa wadukuzi walishambulia tovuti ya E-citizen.

    "Walijaribu kuvuruga mfumo kwa kufanya maombi zaidi ya kawaida kwenye mfumo.

    Ilianza kwa kupunguza kasi ya mfumo.’ ‘Hakuna data iliyofikiwa.

    Data ya N0 imepotea.’ Ingawa haijathibitishwa kivyake, akaunti ya telegram chini ya jina Anonymous Sudan inadai kuhusika na shambulio hilo.

    Kufuatia shambulizi hili, huduma mbalimbali za benki kwa njia ya simu za mkononi nchini Kenya zimekuwa zikivuma kwenye Twitter na Wakenya wanaelezea wasiwasi wao kwa nini mifumo hiyo haifanyi kazi.

    Hii si mara ya kwanza kwa huduma za serikali ya Kenya kuvamiwa.

    Mnamo 2019 iliripotiwa kuwa mitandao mbalimbali ya serikali ya Kenya iliathirika ikiwa ni pamoja na wizara ya fedha, ofisi ya rais na shirika la kijasusi.

  6. Uchambuzi: Mapinduzi pigo kubwa kwa eneo la Afrika Magharibi

    Tangazo la mapinduzi nchini Niger inakuja kama pigo kubwa kwa uongozi wa Jumuiya ya Kanda ya Afrika Magharibi, Ecowas, na kupeleka migogoro ya kikatiba katika kanda hiyo kwenye ngazi mpya.

    Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, wanajeshi wamewapindua marais wa Mali, Guinea na Burkina Faso. Na kama ilivyokuwa kwa nchi hizi, wanajeshi nchini Niger wametaja kuzorota kwa hali ya usalama na utawala mbaya kuwa chanzo cha wao kuchukua mamlaka ya serikali ya nchi hiyo.

    Lakini maswali yanaulizwa ikiwa kuna ushawishi kutoka nje unaochochea mapinduzi haya ya kijeshi katika makoloni ya zamani ya Ufaransa.

    Wiki mbili zilizopita mwenyekiti wa Ecowas Rais Bola Tinubu alionya kwamba ugaidi na mtindo unaoibuka wa mapinduzi Afrika Magharibi umefikia viwango vya kutisha na kutaka hatua za haraka na za pamoja.

    Rais Tinubu sasa amemtuma Rais wa Benin Patrice Talon kuwa mpatanishi katika hali inayoendelea nchini Niger.

  7. Putin aunga mkono uanachama kamili wa G20 na nafaka kwa Afrika

    Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema anatazamia kuona Umoja wa Afrika (AU) unakuwa mwanachama kamili wa mataifa ya G20, akizungumza wakati wa kuanza kwa mkutano wa viongozi wa Afrika mjini St Petersburg.

    "Tunatumai kuwa uamuzi huu utafikiwa mwanzoni mwa Septemba, wakati wa mkutano wa kilele wa G20 huko New Delhi," Bw Putin alisema.

    "Kama hapo awali, Urusi iko tayari kufanya kila linalowezekana kukuza uimarishaji wa uhuru wa mataifa ya Afrika, kusaidia kuifanya Afrika kuwa moja ya washirika muhimu katika mfumo mpya wa mpangilio wa ulimwengu wa pande nyingi," aliongeza.

    Akihutubia uamuzi wa Urusi kujiondoa kwenye mkataba ulioidhinishwa na Umoja wa Mataifa wa kuruhusu usafirishaji wa nafaka kutoka bandari za kusini mwa Ukraine, na hatimaye kuelekea Afrika, Bw Putin alisema kuwa Urusi inaweza kuziba pengo hilo.

    Aliongeza kuwa Urusi itaweza kutoa nafaka bure kwa nchi sita za Afrika katika miezi michache ijayo.

    Viongozi wachache wa Kiafrika wanashiriki katika mkutano huo ikilinganishwa na tukio la lililopita kama hilo, kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

  8. Singapore kumnyonga mwanamke wa kwanza katika kipindi cha miaka 20

    Singapore inajiandaa kutekeleza hukumu ya kifo dhidi ya mwanamke kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 20, watetezi wa haki za binadamu wanasema.

    Raia wa Singapore Saridewi Djamani, 45, alipatikana na hatia ya kusafirisha gramu 30 (1.06oz) za dawa ya kulevya aina ya heroin mnamo 2018.

    Atakuwa mfungwa wa pili wa dawa za kulevya kunyongwa ndani ya siku tatu, baada ya raia mwenzake wa Singapore Mohd Aziz bin Hussain, na wa 15 tangu Machi 2022.

    Singapore ina baadhi ya sheria kali zaidi za kupambana na dawa za kulevya, ambayo inasema ni muhimu kulinda jamii.

    Aziz alipatikana na hatia ya kusafirisha gramu 50 za heroin.

    Chini ya sheria ya Singapore, hukumu ya kifo inaweza kutumika kwa usafirishaji wa zaidi ya gramu15 ya heroin na zaidi ya gramu 500 ya bangi.

    Ofisi kuu ya Madawa ya Kulevya ya Singapore (CNB) ilisema Aziz alipewa "utaratibu kamili", na kwamba rufaa yake dhidi ya kukutwa na hatia na hukumu ilitupiliwa mbali mwaka wa 2018.

    Mnamo Aprili, raia mwingine wa Singapore, Tangaraju Suppiah, aliuawa kwa kusafirisha kilo 1 (oz 35) ya bangi ambayo hakuwahi kuigusa.

    Mamlaka zinasema aliratibu uuzaji huo kupitia simu ya rununu.

    CNB ilikataa kutoa maoni kuhusu kesi ya Saridewi Djamani ilipowasiliana na BBC.

    Bilionea wa Uingereza Sir Richard Branson, ameikosoa tena Singapore kwa kunyongwa kwake, akisema hukumu ya kifo sio kizuizi dhidi ya uhalifu.

    "Walanguzi wadogo wa dawa za kulevya wanahitaji usaidizi, kwani wengi wao hudhulumiwa kutokana na hali zao," Bw Branson alisema kwenye Twitter, akiongeza kuwa bado haijachelewa kukomesha kunyongwa kwa Saridewi Djamani, alisema.

    Yeye ni mmoja wa wanawake wawili wanaosubiri kunyongwa nchini Singapore, kulingana na Transformative Justice Collective, kikundi cha kutetea haki za binadamu chenye makao yake nchini Singapore.

    Atakuwa mwanamke wa kwanza kunyongwa na jimbo hilo tangu msusi Yen May Woen mwaka 2004, kundi hilo lilisema. Yen pia alipatikana na hatia ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

    Maelezo zaidi:

    • Hukumu ya kifo: Ni nchi ngapi ambazo bado zinatekeleza hukumu ya kifo?
    • Zifahamu haki walizonazo wanaohukumiwa kifo duniani
    • Vyakula vya mwisho kuagizwa na wafungwa waliohukumiwa kunyongwa Marekani
  9. Demokrasia italindwa - rais wa Niger

    Rais wa Niger Mohamed Bazoum amesema "mafanikio magumu ya nchi hiyo yatalindwa" baada ya wanajeshi kutangaza mapinduzi kwenye televisheni ya taifa.

    "Waniger wote wanaopenda demokrasia na uhuru wataona hilo," kulingana na taarifa kwenye akaunti ya kiongozi huyo anayeshikiliwa kwenye mtandao wa kijamii wa X, ambao zamani ulijulikana kama Twitter.

    Waziri wa mambo ya nje alichapisha kwenye jukwaa moja akitoa wito kwa wanademokrasia na wazalendo wote kufanya juhudi ili kushinda "matukio haya hatari".

    Hassoumi Massoudou pia alinukuliwa na shirika la habari la AFP akiiambia France24 kwamba serikali iliyochaguliwa ndiyo "mamlaka halali na ya kisheria".

    Waziri huyo aliambia kituo cha televisheni kuwa rais huyo, ambaye amekuwa akishikiliwa na walinzi wake tangu Jumatano, "alikuwa na afya njema".

    Wanajeshi walisema kwenye televisheni ya taifa siku ya Jumatano kwamba wamefanya mapinduzi, kuvunja katiba, kusimamisha taasisi zote na kufunga mipaka ya taifa.

    Hatua hiyo imelaaniwa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa na viongozi wengine wa kimataifa.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Korea Kaskazini: Kim Jong Un amuonyesha mkuu wa ulinzi wa Urusi Shoigu makombora

    Kim Jong Un amemuonyesha silaha za kisasa zaidi za Korea Kaskazini mkuu wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu.

    Utawala wa Pyongyang uliualika ujumbe wa Urusi unaoongozwa na Bw Shoigu, pamoja na maafisa wa China.

    Watahudhuria sherehe za Pyongyang za kumbukumbu ya miaka 70 ya uwekaji silaha wa Vita vya Korea, inayoadhimishwa kwa gwaride kubwa la kijeshi.

    Silaha zilizoonyeshwa ni pamoja na kombora la balestiki la Hwasong intercontinental (ICBM).

    Silaha hii ilijaribiwa kwa ufanisi mwezi wa Aprili, na inaaminika kuwa ina uwezo wa kurushwa kwa haraka kulenga eneo lililokusudiwa.

    Pia kwenye onyesho hilo kulikuwa na miundo miwili mipya ya ndege zisizo na rubani, ikiwa ni pamoja na moja inayofanana na ndege isiyo na rubani ya msingi inayotumiwa na Jeshi la Wanahewa la Marekani, kulingana na NK News, tovuti maalum inayoangazia Korea Kaskazini.

    Ziara hiyo ya kirafiki inajiri huku kukiwa na shutuma kwamba Pyongyang inaipatia Urusi silaha kwa ajili ya matumizi katika vita vyake nchini Ukraine - madai ambayo Pyongyang na Moscow zinakanusha.

    Korea Kaskazini ilisema Bw Kim na Bw Shoigu walijadili "mambo ya kuheshimiana" katika nyanja za ulinzi wa taifa na mazingira ya usalama wa kimataifa.

    Ziara ya wajumbe hao kwa ajili ya Siku ya Ushindi ya Korea Kaskazini - kama vile mwisho wa uhasama wa 1953 inavyoitwa Kaskazini - inatarajiwa kukamilika siku ya Alhamisi kwa gwaride kubwa la kijeshi. Kitaalam Korea bado wako vitani kwa sababu hakuna makubaliano ya amani yaliyofikiwa mzozo ulipoisha.

  11. Tazama: Moto ukiteketeza sanamu ya Buddha kubwa zaidi nchini Uchina

    Sanamu kubwa ya Buddha imeharibiwa na moto katika mkoa wa Gansu kaskazini magharibi mwa China.

    Video zilizoshirikiwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha sanamu hiyo katika Hekalu Kuu la Buddha la Kaunti ya Shandan ikiwa imezingirwa na miali ya moto asubuhi ya Jumatatu.

    Baada ya moto kuzimwa, sanamu hiyo ilionekana kusalia kwa kiasi, lakini sehemu kadhaa za hekalu ziliharibiwa.

    Sanamu hiyo ilijengwa mnamo 1998 kama nakala ya asili ambayo inadhaniwa kuwa ya zamani karibu 425 AD.

    Hakuna majeruhi walioripotiwa kufikia sasa na uchunguzi kuhusu chanzo cha moto huo unaendelea

  12. Marekani: Seneta Mitch McConnell asema "yuko sawa" baada ya kushindwa kuzungumza kwenye mkutano

    Seneta mwandamizi wa chama cha Republican Mitch McConnell amesema "yuko sawa" baada ya kuonekana kushindwa kuzungumza katikati ya sentensi wakati wa mkutano na wanahabari siku ya Jumatano.

    Kiongozi huyo wa walio wachache katika Seneti ya Marekani aliacha ghafla kuzungumza wakati wa kikao cha kila wiki cha viongozi wa chama cha Republican kabla ya kuongozwa na wenzake.

    Bw McConnell baadaye alirejea kwenye mkutano na kusema yuko sawa.

    Mnamo Machi, mzee huyo wa miaka 81 alipelekwa hospitalini kwa mtikiso baada ya kuanguka katika hoteli mjini Washington DC.

    Bw McConnell aliwasalimia wanahabari kwenye mkutano wa kila wiki wa viongozi wa chama cha Republican kabla ya kukushindwa kuzunguza katikati ya sentensi na kunyamaza, akitazama mbele kwa takriban sekunde 20.

    Wenzake wa chama cha Republican wanasikika wakimuuliza ikiwa yuko sawa.

    "Uko sawa, Mitch?" aliuliza Seneta John Barrasso wa Wyoming, daktari wa upasuaji wa mifupa wa zamani. "Unataka kusema kitu kingine au nikusindikize ofisini kwako?" aliongeza.

    Lakini baadaye Mitch McConnell alirudi kujibu maswali.

    Bw McConnell alipatwa na mtikiso na kuvunjika mbavu kidogo baada ya kuanguka wakati wa tukio mwezi Machi. Aliruhusiwa kutoka hospitalini baadaye mwezi huo na kurejea katika baraza la Congress katikati ya Aprili.

  13. Mwanaume aliyefungwa jela kwa ubakaji kimakosa

    Mwanamume ambaye hukumu yake ya ubakaji imebatilishwa baada ya mapambano ya kisheria ya miaka 20 amesema miongo miwili iliyopita alihisi kama "ametekwa nyara na serikali".

    Andrew Malkinson alifungwa mwaka 2004 kwa shambulio la ubakaji dhidi ya mwanamke mkazi wa jiji la Salford Uingereza.

    Alifungwa gerezani miaka 17 jela kwa kosa ambalo alisema siku zote hakulifanya.

    Kesi yake ilipelekwa katika Mahakama ya Rufaa mwezi Januari baada ya ushahidi mpya kuonyesha kuwa kulikuwa na mshukiwa mwingine anayetarajiwa.

    Bw Malkinson, 57, alisema: "Sikuwa na hatia na hatimaye walisikiliza."

    "Lakini nimekuwa sina hatia wakati wote, kwa miaka 20 iliyopita kabla ya leo," alisema.

    "Imechukua karibu miaka 20 kuwashawishi watekaji nyara wangu kuniachilia."

    Akibatilisha hukumu yake, Jaji Holroyd alisema Bw Malkinson anaweza "kuondoka huru mahakamani na hatakuwa chini ya masharti ya leseni tena".

    Polisi pia waliomba radhi kwa kile walichokitaja kuwa "ukosefu mkubwa wa haki".

    Mara ya kwanza Bw Malkinson kujua kuhusu ubakaji huo ni pale alipokamatwa katika mji alikozaliwa wa Grimsby, wiki mbili baada ya shambulio hilo ambapo pia alishutumiwa kwa kujaribu kuua huko Salford.

    Alikuwa katika eneo la tukio wakati huo, akifanya kazi kwa muda kama mlinzi.

  14. Vita vya Ukraine: NATO kuimarisha uchunguzi wa Bahari Nyeusi

    Taarifa kutoka katika muungano wa NATO imesema kwamba vikosi vya muungano vitaongeza ufuatiliaji wa eneo la Bahari Nyeusi baada ya kujiondoa kwa Urusi kwenye makubaliano ya nafaka, ambayo yalihakikisha usafirishaji salama wa nafaka za Ukraine katika Bahari Nyeusi.

    Haya yanajiri baada ya mkutano wa Baraza la NATO linalohusika na masuala ya vita vya Ukraine.

    "NATO na washirika wanaongeza uchunguzi na upelelezi katika eneo la Bahari Nyeusi, ikiwa ni pamoja na ndege za doria za baharini na ndege zisizo na rubani," huduma ya vyombo vya habari ya NATO ilisema katika taarifa.

    Kama ilivyosisitizwa katika taarifa hiyo, hali ya sasa imezua hatari mpya katika eneo hilo na inaleta vikwazo vikubwa dhidi ya uhuru wa urambazaji.Kituo cha habari cha kijeshi

    Kituo cha habari za kijeshi cha Ukraine hapo awali (kituo cha vyombo vya habari kilichoratibiwa na Wizara ya Ulinzi ya Ukraine) kiliripoti kwamba meli za Urusi katika Bahari Nyeusi zinafanya kazi kikamilifu kuzuia maeneo ya bahari, kugundua na uharibifu wa meli.

    Pia, mfumo wa ulinzi wa Crimea unaendelea kuboreka huko, hususan katika maeneo ya barabara inayoelekea Armenia na Perekop.

    Vita vya Ukraine: Taarifa zaidi:

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  15. Marekani inatumaini viongozi wa Afrika watamuuliza Putin kwanini alizuia usambazaji wa nafaka kutoka Ukraine

    Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken amesema anatumai kuwa katika mkutano wa kilele na viongozi wa Afrika utakaofunguliwa mjini St.Petersburg.

    "Wanajua hasa ni nani wa kulaumiwa kwa hali ya sasa," alisema Blinken, ambaye anazuru New Zealand. "Natarajia Urusi itasikia hili wazi kutoka kwa washirika wetu wa Kiafrika."

    Tangu Julai 17, wakati Urusi ilisimamisha ushiriki katika mpango wa nafaka wa Ukraine, ambao ulihakikisha usafirishaji salama wa chakula kutoka kwa bandari za Ukraine bei ya ngano kwenye Soko la Hisa la Chicago imepanda kwa 20%.

    "Sio tu kutoka nje ya mpango huo. Wamefanya nini tangu waondoke? Walipiga mabomu mara kwa mara katika bandari za Odessa. Walipandikiza mabomu ya ardhini katika Bahari Nyeusi. Walitishia usafirishaji waziwazi. Inatuma ujumbe wazi kabisa," Blinken alisema.

    Urusi iliripoti kuwa mkutano huo utahudhuriwa na wajumbe kutoka nchi 49 za Afrika, lakini ni wakuu wa nchi 17 pekee watakaohudhuria. Mnamo 2019, katika hafla kama hiyo ya mwisho, kulikuwa na wakuu wa nchi 45.

    Vita vya Ukraine: Taarifa zaidi:

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  16. Wanajeshi wa Niger watangaza mapinduzi kwenye televisheni ya taifa

    Wanajeshi katika nchi ya Afrika Magharibi ya Niger wametangaza mapinduzi kwenye televisheni ya taifa.

    Walisema wamevunja katiba, wamesimamisha taasisi zote na kufunga mipaka ya taifa.

    Rais wa Niger Mohamed Bazoum amekuwa akishikiliwa na wanajeshi kutoka kwa kikosi cha walinzi wa rais tangu mapema Jumatano.

    Aliahidiwa "uungwaji mkono usioyumba" wa Washington kwa simu kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken.

    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia alisema amezungumza na rais na kumpa uungaji mkono kamili wa Umoja wa Mataifa.

    Bw Bazoum ni mshirika mkuu wa Magharibi katika vita dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu katika Afrika Magharibi.

    Nchi mbili jirani, Mali na Burkina Faso, zimekumbwa na mapinduzi yaliyochochewa na maasi ya makundi ya Jihadi katika miaka ya hivi karibuni.

    Katika nchi zote mbili viongozi wapya wa kijeshi wametofautiana na Ufaransa, koloni la zamani, ambalo pia liliitawala Niger.

    Katika tangazo la TV siku ya Jumatano, Kanali Maj Amadou Abdramane, pamoja na askari wengine tisa waliovalia sare nyuma yake, walisema: "Sisi, vikosi vya ulinzi na usalama... tumeamua kukomesha utawala unaoujua.

    "Hii inafuatia kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama, na utawala mbovu wa kiuchumi na kijamii."

    Pia alisema taasisi zote nchini zimesimamishwa kazi na wakuu wa wizara watasimamia shughuli za kila siku.

    Jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi Ecowas imesema "inalaani kwa maneno makali jaribio la kunyakua mamlaka kwa nguvu".

    Unaweza pia kusoma:

    • Wanajeshi 20 wauawa Niger
    • Ufaransa kutuma wanajeshi Niger
    • Kiongozi wa Upinzani Niger ahukumiwa kifungo gerezani
  17. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu mubashara ya leo tarehe 27.07.2023