Takriban watu sita waripotiwa kuuawa katika maandamano nchini Kenya
Watu watatu kati ya waliofariki waliuawa kwa kupigwa risasi karibu na Kituo cha Tozo cha Barabara ya Express Way.
Moja kwa moja
Ukraine: Jenerali wa Urusi aripotiwa kuuawa katika shambulio kwenye hoteli ya Berdyansk

Chanzo cha picha, MILITARY INFORMANT/TELEGRAM
Jenerali mkuu wa Urusi ameuawa katika shambulizi la kombora nchini Ukraine, duru za Urusi zimesema.
Luteni Jenerali Oleg Tsokov anasemekana kufariki dunia katika shambulio kwenye hoteli yenye makamanda wa kijeshi wa Urusi huko Berdyansk, kwenye pwani ya kusini inayokaliwa na Ukraine.
Wizara ya ulinzi ya Urusi haijathibitisha rasmi kifo chake.Lakini kilitangazwa sana na vituo vya vita vya Urusi kwenye programu ya kutuma ujumbe ya Telegram.
Mtangazaji wa TV Olga Skabeyeva alisema "vyombo vyote vya habari" vilikuwa vikiripoti.
Luteni Jenerali Tsokov alikuwa naibu kamanda wa wilaya ya kijeshi ya kusini mwa Urusi.Bi Skabeyeva ambaye anawasilisha kipindi cha mazungumzo kwenye chaneli ya serikali ya Rossiya-1 alisema aliuawa kwa kombora la Storm Shadow lililotolewa na Uingereza.
Andrei Gurulyov, mbunge na jenerali mstaafu ambaye alionekana kwenye kipindi chake maarufu cha 60 Minutes siku ya Jumanne, alisema jenerali huyo alirejea Ukraine licha ya kujeruhiwa vibaya mapema katika mzozo huo.
Takriban watu sita wameuawa katika maandamano nchini Kenya

Chanzo cha picha, AFP
Mamlaka nchini Kenya imethibitisha kuwa watu sita wamefariki wakati wa maandamano ya nchi nzima kupinga gharama ya juu ya maisha siku ya Jumatano.
Mashirika ya haki za binadamu hata hivyo yameweka idadi ya waliofariki kuwa 12, huku wengine wengi wakijeruhiwa, katika mojawapo ya maandamano mabaya zaidi yaliyoshuhudiwa nchini Kenya katika siku za hivi karibuni.
Maandamano hayo yalikuwa yametangazwa kuwa kinyume cha sheria na polisi.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekosoa mamlaka kwa kile wanachokiona kuwa ni matumizi ya nguvu kupita kiasi ya polisi, ikiwa ni pamoja na kuwarushia vitoa machozi watoto 53 wa shule.
Maelezo ya video, Jinsi polisi walivyokabiliana na waandamanaji nchini Kenya Katika kukabiliana na maandamano hayo, mamlaka nchini Kenya imeeleza nia yao ya kuwakamata waandalizi hao ambao ni viongozi wa upinzani Raila Odinga na Martha Karua.
Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa, Prof Kithure Kindiki, alilaani vikali matukio ya Jumatano, akiitaja kuwa "siku ya uporaji usio na aibu na usio na sababu, kizuizi haramu cha shughuli za kiuchumi, na uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu ya umma inayofadhiliwa na ushuru wa serikali'.
Alisema ili kukabiliana na hali hiyo, Serikali itatumia vyombo vya sheria na taasisi za makosa ya jinai nchini kufanya uchunguzi, kuwakamata na kuwafungulia mashtaka waliohusika kupanga na kutekeleza uhalifu huo.
Hii inajumuisha watu binafsi ambao walifadhili au kusaidia na kufanikisha maandamano hayo
Unaweza pia kusoma
Mpatanishi wa EAC, Uhuru Kenyatta yuko DRC kuhuduria mkutano wa kutafuta amani

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa zamani Kenya, Uhuru Kenyatta yuko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kuhudhuria mkutano wa pili wa timu ya Ushauri.
Kenyatta, ambaye ndiye mpatanishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), katika mchakato wa utafutaji amani alipokelewa mjini Goma na Waziri anayeshughulikia Ushirikiano wa Kikanda Mbusa Nyamwisi.
Wengine waliohudhuria mkutano huo ni Naibu Waziri Mkuu wa DRC na Waziri wa Ulinzi Jean Pierre Bemba, Mwakilishi Maalum wa Rais Félix Tshisekedi Prof. Serge Tshibangu Kabeya, pamoja na Gavana wa Kivu Kaskazini Jenerali Ndima Kongba.
Wadau mbalimbali na mashirika ya kimataifa yanayotaka kujadiliana kuhusu masuala muhimu yanayolenga kuimarisha mchakato wa amani wa Luanda na Nairobi pia yapo.
Wakati wa mkutano mjini Nairobi mwishoni mwa mwezi uliopita na washikadau mbalimbali kuhusu masuala ya jimbo la Kivu Kaskazini mashariki mwa DRC, Kenyatta aliwataka wajumbe wanaozozana kuzingatia midahalo ya wazi ya mashauriano katika jitihada za kukabiliana na uhasama katika eneo hilo.
Uingereza yaiwekea vikwazo majeshi hasimu ya Sudan

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Majenerali wapinzani Mohamed Hamdan "Hemedti" Dagalo (kushoto) na Abdel Fattah al-Burhan wanaonekana hapa miezi kadhaa kabla ya mapigano kuzuka. Uingereza imetangaza vikwazo dhidi ya makampuni yanayohusishwa na makundi hasimu ya kijeshi katika mzozo unaozidi kuleta maafa nchini Sudan.
Waziri wa serikali ya Uingereza, Andrew Mitchell, alisema jeshi la Sudan na wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) wameiingiza nchi yao kwenye vita visivyokuwa na msingi wowote.
Vikwazo hivyo vinalenga kusitishwa kwa mali ya biashara tatu zinazohusishwa na kila upande katika mapigano.
Washington iliweka vikwazo mwanzoni mwa Juni. Tangu mapigano nchini Sudan yalipuke miezi mitatu iliyopita, inadhaniwa maelfu ya watu wameuawa.
Mamilioni ya watu wamelazimika kutoroka makwao.
Unaweza pia kusoma:
- Wagner: Mamluki wa Urusi wamekuwa wakifanya nini Sudan?
- Mgogoro wa Sudan: Kwa nini Misri ipo katika njia panda juu ya mapigano Sudan?
Tanzania yanufaika na mradi mkakati wa miaka 5 utakaonufaisha sekta ya kilimo
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Aboubakar Famau
- Nafasi, BBC News, Dodoma

Wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo wameshuhudia uzinduzi wa mpango mkakati wa miaka mitano wenye lengo la kuchochea mabadiliko ya kilimo.
Hivyo mkakati wa sasa wa miaka mitano wenye thamani ya takriban dola milioni sitini, umejikita zaidi katika kuangalia maeneo manne.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa ni waziri mkuu mstaafu Mizengo Pinda ambae ametaka kuwepo kwa kilimo cha kisasa na cha umwagiliaji ambacho kitaweza kuwatoa wakulima katika umaskini.
Kwa upande wao, baadhi wa wadau wa sekta hiyo, walionyesha shauku ya kutaka utekelezwaji wa mkakati huo kufanyika kwa ufanisi ili uweze kuleta tija.
Uzinduzi wa mkakati huu, unakuja wakati ripoti ya Umoja wa Mataifa ikionyesha wasiwasi wa kutofikiwa kwa baadhi ya malengo ya Maendeleo Endelevu ya dunia kufikia mwaka 2030. Hivyo uzinduzi wa mkakati huu, unaweza kuleta matumaini ya kufikiwa kwa baadhi ya malengo hayo.
Hata hivyo, baadhi ya wadau hao waliohudhuria uzinduzi huo uliofanyika jijini Dodoma wamesema, mabadiliko yanaweza kupatikana iwapo tu utekelezaji wa mikakati hiyo utafanyika kwa ufanisi.
Huu ni mkakati wa tatu kuzinduliwa nchini, ambapo tofauti na ile iliyopita ambayo ilijikita zaidi katika kujenga mifumo ikiwemo utengezaji wa mbegu bora pamoja na kutoa elimu kwa wakulima.
Watoto wa shule 'warushiwa vitoa machozi' wakati wa maandamano ya upinzani Kenya

Chanzo cha picha, AFP
Watoto 53 wa shule wamekimbizwa hospitali baada kitoa machozi kuripotiwa kuanguka darasani mwao wakati wa maandamano ya upinzani yanayoendelea nchini Kenya.
Daktari Aron Shikuku, mmiliki wa hospitali ya Eagle Nursing Home, ameithibitishia BBC, kwamba watoto hao wamehudumiwa na kwa sasa wako chini ya uangalizi wa kimatibabu.
“Wamekuwa hospitalini kwa takriban saa nne wakitibiwa kwa mshtuko baada ya kuzidiwa na moshi wa mabomu ya machozi. Hakuna majeruhi aliyeripotiwa.”, alisema Dk Shikuku.
Maelezo ya video, Jinsi polisi walivyokabiliana na waandamanaji nchini Kenya Tukio hili lilitokea wakati wa maandamano ya kitaifa ya kupinga kupanda kwa gharama ya maisha, ambayo yamesababisha hasara kubwa.
Visa viwili vya vifo vimeripotiwa huku waandamanaji wakivamia kituo cha polisi na kukichoma moto katika kaunti inayopakana na Mji Mkuu wa Nairobi, na mtu mwingine kupoteza maisha baada ya gari la polisi kuchomwa moto kando ya Barabara ya Nairobi Expressway huko Mlolongo nje kidogo ya jiji la Nairobi.
Kutokana na wasiwasi kuhusu kile alichokiita kuongezeka kwa ghasia kutoka kwa mamlaka, kiongozi wa Upinzani Raila Odinga amesitisha mkutano uliopangwa kufanyika katika uwanja wa Kamukunji viungani mwa jiji la Nairobi..
Kaunti mbali mbali zimeathiriwa baada ya huduma za usafiri na biashara kukatizwa, huku waandamanaji wakiamua kuwasha moto barabarani kujihusisha na shughuli kama vile michezo ya soka kwenye vituo vya mabasi.
Hali bado ni tete na video zinazonasa matukio haya zimesambazwa sana mtandaoni.
Unaweza pia kusoma
Eto'o akabiliwa na wito wa kujiuzulu kama mkuu wa FA wa Cameroon

Maelezo ya picha, Samuel Eto'o, ambaye ameongoza FA ya Cameroon tangu Desemba 2021, amekosolewa kwa baadhi ya maamuzi yake ya hivi majuzi. Kundi linalowakilisha vilabu vya wachezaji soka wa ridhaa nchini Cameroon limemtaka mchezaji maarufu wa zamani Samuel Eto'o kujiuzulu wadhifa wake kama rais wa shirikisho la soka la nchi hiyo, kwa sababu ya "ukiukwaji mkubwa" katika shirika hilo.
Wiki iliyopita, Chama cha Vilabu vya Wachezaji wa Ridhaa nchini Cameroon (ACFAC) kilipiga kura 11-1 kuunga mkono kumtaka Mwanasoka Bora wa Afrika mara nne ajiuzulu.
Kilisema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 42, ambaye alichezea vilabu kadhaa vikubwa barani Ulaya, anapaswa kujiuzulu "ikiwa bado anapenda soka ya Cameroon, kama ambavyo amekuwa akidai kila mara".
ACFAC ilitoa wito kwa waziri wa michezo wa Cameroon kuingilia kati, na kutaja uwezekano wa kumtaka rais wa Fifa Gianni Infantino kufanya hivyo.
Miongoni mwa yale yanayolalamikiwa na, ACFAC n pamoja na uamuzi wa kubadilisha mamlaka ya rais wa Fecafoot kutoka miaka minne hadi saba ulikuwa kinyume na sheria na kinyume cha sheria.
Pia ilionyesha ukosefu wa uchapishaji wa sheria mpya zilizopitishwa Agosti iliyopita.
Zimbabwe: Mshirika wa karibu wa Mugabe azuiwa kuwania urais

Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Saviour Kasukuwere, pichani mwaka 2013, amezuiwa na mahakama ya Zimbabwe kugombea Urais. Waziri wa zamani wa serikali ya Zimbabwe Saviour Kasukuwere, ambaye alitaka kumpinga rais Emmerson Mnangagwa katika uchaguzi ujao, amezuiwa kugombea.
Jaji wa mahakama kuu ya Harare amebatilisha ombi la Bw Kasukuwere la kugombea kama mgombea huru wiki chache tu baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe kukubali karatasi zake za usajili.
Wakili Lovedale Mangwana alipinga uamuzi wa chombo hicho mahakamani, akisema kuwa Bw Kasukuwere si mpiga kura aliyesajiliwa tena - kigezo cha mgombea - kwa vile alikuwa ameishi nje ya Zimbabwe kwa zaidi ya miezi 18.
Bw Kasukuwere ni mfuasi mkuu wa Mugabe ambaye aliwahi kuwa kamishna wa kisiasa wa Zanu-PF na waziri wa vijana na wazawa katika serikali ya rais wa zamani.
Aliikimbia nchi baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomuingiza Rais Emmerson Mnangagwa madarakani mwaka 2017.
Alirejea kwa muda mfupi mwaka wa 2018, lakini akakimbilia tena Afrika Kusini akihofia mateso ya kisiasa.
Uchaguzi mkuu wa Zimbabwe utafanyika tarehe 23 Agosti.
Pia unaweza kusoma:
Afrika Kusini yatajwa kuwa nchi bora zaidi duniani kutembelea

Chanzo cha picha, Getty Images
Wasomaji waliohojiwa na gazeti la Telegraph la Uingereza wanasema Afrika Kusini ndio kivutio bora zaidi cha watalii duniani.
Gazeti hilo limesfia uzuri wa Cape Town, ikiliita jiji hilo kuwa "mwanamitindo bora chini ya Mlima wa meza".
Pia inasifu "mazao mazuri" ya mvinyo wa Afrika Kusini na kuita Njia ya Bustani "utepe wa nirvana ".
Kenya na Botswana pia ziko katika 10 bora kwenye orodha hiyo ya Telegraph, katika nambari saba na 10 mtawalia.
Mtu mmoja auawa huku waandamanaji wakikabiliana na polisi Kenya

Chanzo cha picha, AFP
Mwanamume mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi wakati wa maandamano katika mji wa Emali nchini Kenya, takriban kilomita 100 kutoka mji mkuu wa Nairobi, kulingana na ripoti nyingi katika vyombo vya habari vya ndani.
Gazeti la Daily Nation linasema kuwa polisi waliwafyatulia risasi waandamanaji ambao inasemekana walichoma gari la polisi na kurushia mawe benki moja ya eneo hilo.
Emali ipo kwenye barabara kuu ya Nairobi hadi Mombasa.Tovuti ya K24 inaripoti kuwa mamia ya waandamanaji huko walifunga barabara Jumatano asubuhi,na kuzuia magari kupita.
Maandamano hayo ya upinzani yameendelea licha ya polisi kutangaza kuwa ni kinyume cha sheria.
Polisi na viongozi wa eneo hawajatoa maelezo kuhusu kifo cha mtu huyo.
Huku maandamano yaliyopigwa marufuku yakiendelea nchini Kenya , polisi wamerusha vitoa machozi kwa umati wa watu waliokusanyika katika viwanja vya Kamukunji katika mji mkuu, Nairobi, ambapo kiongozi wa upinzani Raila Odinga alitarajiwa kuhutubia wafuasi wake.
Video iliyopeperushwa moja kwa moja kwenye uwanja huo inaonyesha mafundi jukwaani wakihangaika kutafuta vifaa vyao.
Sehemu ya barabara kuu ya Nairobi yenye thamani ya mamilioni ya dola imefungwa kutokana na maandamano, kampuni inayoisimamia inasema.
Video kwenye mitandao ya kijamii zinaonekana kuonyesha kundi la watu wakiharibu barabara.
Ruka X ujumbeRuhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya njeMkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Maelezo ya video, Jinsi polisi walivyokabiliana na waandamanaji nchini Kenya Unaweza pia kusoma
Wasia uliokutwa katika sofa la Aretha Franklin ni halali – Baraza la Mahakama

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Aretha Franklin Baraza la Mahakama ya Michigan limeamua kwamba hati ya wasia wa mali ya mamilioni ya dola, iliopatikana mwaka 2014 katika sofa la Aretha Franklin baada ya kifo chake ni halali.
Kesi ya siku mbili iliwashindanisha watoto wa marehemu kuhusua hati mbili za wasia zilizoandikwa kama matakwa ya mwisho ya mwimbaji huyo.
Mawakili wa watoto wawili wa kiume wa Franklin wa kuwazaa walidai kaka yao wa kambo Ted White anataka kuwanyima urithi. Uamuzi wa Jumanne unamaliza takriban miaka mitano ya ugomvi wa kisheria wa familia hiyo.
Franklin alipofariki kutokana na saratani mnamo Agosti 2018, iliaminika hakuwa ametayarisha wasia wa mali zake za takribani dola za kimarekani milioni 6; kwa mali isiyohamishika, pesa taslimu, albamu zake za dhahabu na hakimiliki za muziki wake.
Miezi tisa baadaye, mpwa wake Sabrina Owens - msimamizi wa mirathi wakati huo – aligundua hati mbili tofauti zilizoandikwa kwa mkono nyumbani kwa mwimbaji huyo huko Detroit.
Wasia ulioandikwa Juni 2010, ulilipatikana ndani ya droo, pamoja na mikataba na nyaraka zingine. Wasia ulioandikwa Machi 2014, ulipatikana ndani ya daftari dogo chini ya sofa la sebule.
Chini ya wasia wa 2014, wana watatu watagawana mirabaha yake ya muziki na fedha za benki, huku mtoto wake mdogo Kecalf na wajukuu zake watarithi makazi yake ya awali na jumba la kifahari.
Wakati wasia ya 2010 unamtaka Kecalf na mwana mwingine Edward, lazima wakajifunze masomo ya biashara na kupata cheti au digrii ili kufaidika na mali za Franklin.
Aretha Louise Franklin alikuwa ni mwanamuziki, mtunzi wa muziki na mpiga kinanda. Alijuulikana kama ‘malkia wa roho,’ akiuza zaidi ya rikodi milioni 75 na kutambulika kama mmoja wa wasanii waliouza sana kazi za muziki.
Habari za hivi punde, Maandamano yafanyika Kenya licha ya marufuku ya polisi

Chanzo cha picha, Raila Odinga facebook
Maelezo ya picha, Raila Odinga akiongoza maandamano ya siku ya Saba Saba Maandamano ya upinzani yameanza nchini Kenya, licha ya kutangazwa na polisi kuwa haramu, na kusababisha matumizi ya vitoa machozi na vyombo vya sheria kuwatawanya waandamanaji katika miji mbalimbali.
Inspekta Jenerali wa Polisi alisema kuwa "mamlaka hawana lingine ila kuchukua hatua zinazohitajika kutawanya maandamano hayo haramu", kama ilivyotajwa katika taarifa aliyoitoa Jumanne jioni.
Barabara kuu za Nairobi, Kisii, Kisumu na Nyeri zina msongamano mdogo, na video za mtandaoni zinaonyesha barabara zilizofungwa katika maeneo kadhaa.
Biashara nyingi zimesalia kufungwa, na usafiri umesimama.
Ijumaa iliyopita, makabiliano kati ya waandamanaji wa upinzani na polisi yalisababisha vifo vya watu sita katika miji mingi.
Wahudumu wa magari ya utumishi wa umma katika miji kadhaa wamejiunga na maandamano hayo, na kusitisha shughuli zao kupinga kupanda kwa gharama ya mafuta.
Madereva wa programu zinazotumia njia za kidijitali pia wamejiunga na maandamano, wakielezea wasiwasi wao kuhusu gharama za mafuta, ukosefu wa marekebisho ya bei na masuala ya usalama.
Waandalizi hao wanahimiza ushiriki mkubwa kote nchini Kenya, wakitaka kufutwa kwa sheria mpya ya fedha inayoongeza ushuru wa mafuta maradufu na kuweka ushuru wa nyumba wa 1.5% kwa wafanyikazi.
Rais wa Kenya, William Ruto, anatetea sheria ya fedha iliyositishwa kwa muda, akisema kuwa itashughulikia masuala ya ulipaji wa madeni na kuunda nafasi za kazi kwa vijana wasio na ajira.
Anashutumu upinzani kwa kuhujumu mustakabali wa mamilioni ya vijana wasio na ajira na kuapa kuzuia kupoteza maisha kutokana na maandamano.
Mahakama kuu jijini Nairobi imesitisha utekelezwaji wa sheria ya fedha, ikitaja wasiwasi mkubwa wa kikatiba.
Ruka X ujumbeRuhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya njeMkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Tazama jinsi mafuriko yanavyosababisha hasara kubwa nchini India
Maelezo ya video, Tazama: Mvua kubwa na mafuriko katika eneo la Himachal Pradesh ya India Jimbo la kaskazini mwa India la Himachal Pradesh limekuwa likishuhudia mvua kubwa katika siku chache zilizopita na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi katika eneo la milima.
Maji yanayotiririka yanafagia madaraja, nyumba na magari, na kusababisha uharibifu mkubwa katika jimbo hilo.
Jimbo jirani la Uttarakhand liko katika hali sawa na viwango vya maji vya mito kadhaa katika eneo hilo vimevuka alama ya hatari.
Zaidi ya watu kumi na mbili wamekufa katika siku tatu zilizopita kaskazini mwa India kutokana na ugonjwa huo
Korea Kaskazini yarusha kombora la masafa marefu baada ya kuitishia Marekani

Chanzo cha picha, Reuters
Korea Kaskazini imerusha kombora linalosadikiwa kuwa la masafa marefu (ICBM), maafisa wa Japan na Korea Kusini wameripoti.
Kombora hilo la masafa marefu lilipaa kwa zaidi ya saa moja kabla ya kutua karibu na maji ya Japan Jumatano asubuhi.
Urushaji huo umekuja baada ya Pyongyang kutishia kulipiza kisasi dhidi ya kile ilichosema ni uvamizi wa hivi karibuni wa ndege za kijasusi za Marekani katika eneo lake. Mapema wiki hii ilitishia kutungua ndege hizo.
Washington imepuuzilia mbali shutuma hizo ikisema kuwa doria zake za kijeshi zinazingatia sheria za kimataifa.
Wasiwasi wa usalama umeongezeka katika rasi hiyo mwaka huu baada ya Korea Kaskazini kufanya majaribio ya silaha mpya. Nchi hiyo pia iliongeza urushaji wa makombora mwaka 2022 ikiwa ni pamoja na yale yenye uwezo wa kufikia ardhi ya Marekani.
Kwa kujibu, Marekani na Korea Kusini zimeongeza mazoezi yao ya kijeshi ya pamoja katika peninsula hiyo.
Pyongyang imeendelea na urushaji wa makombora yake - ikifanyia majaribio ya ICBM mpya mwezi Aprili, kombora linalotajwa ni "lenye nguvu zaidi" hadi sasa. Pia ilijaribu kurusha satelaiti ya kijasusi mwezi Mei ambayo haikufaulu.
Rais Ruto amkaribisha Mwenzake wa Iran Ebrahim Raisi

Chanzo cha picha, Ikulu ya Rais Kenya
Maelezo ya picha, Rais Ruto akimkaribisha mwenzake wa Iran Rais wa Iran, Ebrahim Raisi, ameanza ziara ya kihistoria barani Afrika, akianzia na Kenya, ambapo amepata mapokezi makubwa ya saluti 21 na gwaride la kijeshi katika Ziara yake ya Kiserikali.
Kuwasili kwa Rais Raisi nchini Kenya kunaashiria kuanza kwa ziara yake muhimu ya mataifa matatu barani Afrika, na ziara zilizofuata zimepangwa nchini Uganda na Zimbabwe.
Ziara hii ina umuhimu mkubwa kwani ni mara ya kwanza katika kipindi cha muongo mmoja kwa kiongozi wa Iran kuzuru bara hilo.
Rais Raisi ambaye alizungumza na waandishi wa habari alipokuwa akiondoka Tehran Jumanne Julai 11, alisisitiza umuhimu wa kufufua uhusiano na mataifa ya Afrika, akikiri kwamba uhusiano huo ulikwama katika muongo mmoja uliopita.
Ameelezea shauku ya Iran ya kushirikiana na Bara la Afrika na kuashiria uwezekano wa kunufaishana na kushirikiana katika sekta mbalimbali.
Wachambuzi wa mambo wanasema, ingawa juhudi hizo ni sehemu ya mkakati wa Rais Raisi wa kuimarisha uhusiano na nchi za Kusini mwa Dunia na kukabiliana na kutengwa kwa Iran kutokana na vikwazo vya nchi za Magharibi, ni muhimu kuzingatia sifa za muda mrefu za Iran, zikiwemo mielekeo yake ya kimapinduzi na kupenda kujitanua, kuyumbisha uthabiti kikanda, ufadhili, na masuala ya haki za binadamu.
Kuendelezwa kwa mipango ya Iran ya nyuklia na makombora ya balistiki pia kunaendelea kuzusha wasiwasi miongoni mwa Marekani, washirika wake, na maslahi ya kikanda.
Rais Raisi anapotaka kupanua uhusiano wa kiuchumi wa Iran, nchi za Magharibi kwa hakika zitazingatia kwa karibu muktadha mpana na athari zinazoweza kujitokeza kisera na shughuli za kigeni za Iran barani Afrika.
Safari hiyo ya siku tatu pia inajumuisha Uganda na Zimbabwe na itakuwa ya kwanza kwa rais wa Iran kuzuru barani Afrika katika kipindi cha miaka 11
Wamiliki wa magari Kenya waingia Tanzania kununua mafuta ya bei rahisi

Chanzo cha picha, AFP
Maelfu ya wamiliki wa magari pamoja na waendesha boda boda katika mji wa mpakani wa Namanga wanaendelea kuingia nchini Tanzania ili kununua mafuta ya bei rahisi kulingana na gazeti la Nation.
Tarehe Mosi mwezi julai shirika la kudhibiti bei ya mafuta nchini Kenya EPRA liliongeza bei ya mafuta kwa mujibu wa sheria ya fedha ya 2023, ambayo iliongeza VAT kutoka asilimia 8 hadi kumi na sita
Mjini Nairobi na kaunti ya Kajiado lita moja ya petroli inauzwa kwa shilingi 195.5 za Kenya huku nchini Tanzania ikiuzwa kwa shilingi 2,781 za Tanzania ambazo ni shilingi 160 za Kenya.
Hii ina maana kwamba lita moja ya mafuta ya petroli iko chini kwa shilingi 35 za Kenya nchini Tanzania.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti la Nation Media, umebaini kwamba wengi waliokuwa wakinunua mafuta katika kituo cha mafuta cha Admire Filling Station kilichopo kilomita moja kutoka mpakani ni raia wa Kenya.
Kulingana na gazeti hilo, bei ya mafuta imekuwa ikishuka nchini Tanzania katika kipindi cha miezi miwili iliopita huku ikipanda nchini Kenya.
Maandamano dhidi ya Serikali Kenya, Rais William Ruto atoa onyo

Chanzo cha picha, BBC News
Maelezo ya picha, Rais William Ruto Rais William Ruto ametoa onyo kali kuhusu maandamano ya Azimio yaliyopangwa kufanyika siku ya Jumatano.
Akizungumza mjini Ruai Jumanne, Rais alithibitisha kwamba hataruhusu maisha ya Mkenya yeyote kupotea kutokana na maandamano.
"Walifanya maandamano, na Wakenya wasita wakapoteza maisha yao. Mnataka maandamano ifanyike, maisha mengine yapotezwe? Haitatokea," Ruto alisema.
Ili kujiepusha, Ruto alisema kuwa hataruhusu kifo chochote kutokana na kuridhika kwa mtu kisiasa.
Kiongozi huyo aliambia upinzani kukubali matokeo ya uchaguzi wa Agosti 2022 na kuendelea.
"Iwapo unataka uchaguzi mwingine, subiri ratiba ya IEBC kuhusu lini uchaguzi mkuu ujao utafanyika. Ni wakati wa kufanya kazi," aliongeza.
Kinara wa upinzani Raila Odinga aliapa kuwaongoza wafuasi wake barabarani kwa maandamano dhidi ya serikali siku ya Jumatano.
Maandamano hayo yanatarajiwa kufanyika katika miji mikuu ya nchi huku Raila akiwa tayari amewatuma wanachama wakuu wa muungano wa Azimio kuongoza maandamano hayo katika ngazi za mashinani.
Maandamano ya Saba Saba ya siku ya Ijumaa iliyopita yalishika kasi huku sehemu mbalimbali za nchi zikiwemo Kisumu, Mombasa, Kisii, Kakamega, Kirinyaga, Machakos na Nyahururu zikishiriki.
Katika taarifa iliyotolewa Jumanne jioni, Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome alisema viongozi wa muungano wa Azimio unaoongozwa na Raila Odinga hawajawasilisha taarifa yoyote rasmi kwa polisi kuhusu maandamano yaliopangwa, kwa hivyo mikusanyiko hiyo itachukuliwa kuwa haramu.
Kwa hivyo IG ya Polisi imeapa kutumia "njia zote halali" kutawanya mikusanyiko yoyote ambayo itafanyika Jumatano.
Maandamano hayo, kwa mujibu wa muungano wa Azimio, ni sehemu ya kushinikiza Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua kuondoka afisini kwa msingi kuwa wameshindwa kutanguliza masaibu ya Wakenya na badala yake kutunga sheria za kutoza ushuru.
Odinga ambaye alifanya mkutano wa mazungumzo ya umma katika soko la Kenyatta jijini Nairobi siku ya Jumanne amewataka Wakenya bila kujali itikadi zao za kisiasa kujitokeza kwa wingi Jumatano na kujiunga na maandamano.
Madereva wa utumishi wa umma na kibiashara walikuwa wametoa notisi ya mgomo hapo awali, uliopangwa kuanza leo. Hata hivyo, mgomo huu umesitishwa kufuatia uamuzi wa serikali kusitisha upimaji upya wa madereva wa utumishi wa umma na kibiashara hadi Septemba 1.
Madereva hao walikuwa wametaka kusitishwa kwa upimaji mpya , kutatuliwa kwa ada za ziada za kufuata sheria, suluhu za kufurika kwa waendeshaji "wa kigeni", na kujumuishwa kwa madereva katika vyombo vya kufanya maamuzi vinavyosimamia biashara yao.
Mgomo huo ungeenda sambamba na maandamano ya nchi nzima dhidi ya serikali yaliyoandaliwa na upinzani na asasi za kiraia wakiwemo baadhi ya watumishi wa umma na mashirika mengine ya kitaaluma.
Aidha, madereva wa teksi wanaohusishwa na mashirika ya waendeshaji pia wametishia mgomo wa kitaifa, ambao unaweza kusababisha usumbufu mkubwa kote nchini Kenya hii leo.
Mkutano wa Nato: Wanachama wakataa kuipa Ukraine muda wa kujiunga

Chanzo cha picha, BBC News
Maelezo ya picha, Rais Zelensky katika mkutano wa Nato Vilnius Mataifa ya Nato yamesema Ukraine inaweza kujunga na muungano huo wa Kijeshi , wakati wanachama watakubaliana na masharti kuafikiwa baada ya Zelensky kukosoa ucheleweshaji wa nchi yake kujiunga na Muungano huo.
Katika Taarifa yake , Nato ilisema inatambua umuhimu wa kuharakisha lakini haitatoa muda sahihi .
Mapema bwana Zelensky alisema kwamba inaonekana utayariya kuialika Ukraine kujiunga na Nato amba hata kuifanya kuwa mwanachama wa Muungano huo.
Hivi sasa yuko katika mji mkuu wa Lithuania Vilnius , ambapomkutano huo unafanyika.
Ukraine inakubali kwamba haiwezi kujiunga na Nato wakati ambapo ipo katika vita na Urusi lakini inataka kujiunga na Muungano huo mara moja vita vitakapoisha.
Lakini bwana Zelensky katika ujumbe wake wa Twitter alisema kwamba ukosefu wa muda sahihi wa kujiunga na Muungano huo kunamaanisha taifa lake huenda likajiunga na Muungano huo baada ya masharti kadhaa.
"Dirisha la fursa linaachwa ili kujadili uanachama wa Ukraine katika Nato katika mazungumzo na Urusi. kutokuwa na uhakika ni udhaifu," alisema.
Nato inaweza kuwa haijasema lini na jinsi Ukraine inaweza kujiunga na muungano huo. Lakini wanadiplomasia walisisitiza kwamba walikuwa wameweka njia wazi zaidi ya uanachama, na mchakato mgumu wa maombi umefupishwa kwa kiasi kikubwa.
Muungano huo ulikuwa umetambua kuwa jeshi la Ukraine lilikuwa linazidi "kushirikiana" na "kuunganishwa kisiasa" zaidi na vikosi vya Nato na ungeendelea kuunga mkono mageuzi ya sekta ya demokrasia na usalama ya Ukraine.
Natumai Hujambo

