Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wapiganaji wa Wagner wanaweza kujiunga na jeshi la Urusi au kuhamia Belarus - Putin
Putin aliwaambia Warusi kwamba wale walioandaa "maasi" walitaka Urusi ipoteze "na jamii yetu kuzama kwenye damu, lakini walikosea".
Moja kwa moja
Wapiganaji wa Wagner wanaweza kujiunga na jeshi la Urusi au kuhamia Belarus - Putin
Rais wa Urusi Vladimir Putin amehutubia taifa kupitia video kwenye runinga ya serikali.
Amesema wapiganaji wa Wagner wana chaguo la kujiunga na jeshi la Urusi,kwenda nyumbani kwa familia zao wau kuhamia nchini Belarus.
Ameapa kutekeleza ahadi yake kuhusiana na mpango wa kundi hilo la kiongozi wake kuhamia Belarus .
Amesema idadi kubwa "ya wapiganaji wa kampuni ya Wagner ni wazalendo wa Urusi.
"Kwa kurudi nyuma waliepuka umwagaji damu zaidi," Putin anaongeza.
Uasi ungekandamizwa – Putin
Katika hotuba yake, Putin pia anasema maamuzi yote muhimu ya kupunguza tishio yalichukuliwa mwanzoni kabisa.
Uasi huo ungekandamizwa hata hivyo na waandaaji waligundua kuwa vitendo vyao vilikuwa vya uhalifu, anaongeza.
Kupitia hotuba yake alimshukuru kiongozi wa Belarus Alexander Lukashenko kwa juhudi zake za kutatua hali hiyo kwa amani, lakini alisema ni umoja wa jamii ndio uliochukua jukumu kuu.
Wale ambao hawakumwaga damu wanaweza kusaini mkataba au kuhamia Belarus - Putin
Aliendelea kushukuru idara zote za usalama "ambao walibaki waaminifu kwa kiapo chao" pamoja na marubani waliofariki.
Aliongeza kuwa hatua zilichukuliwa ili kuepusha umwagaji mkubwa wa damu, "lakini ilichukua muda".
"Nawashukuru askari na makamanda wa Wagner ambao hawakumwaga damu - wanaweza kusaini mkataba na Wizara ya Ulinzi, au kuhamia Belarus," alisema.
Unaweza pia kusoma
Eid ul Adha:Yote unayofaa kujua kuhusu Eid Ul Adha na Hajj
Waislamu kote ulimwenguni wameanza kusherehekea sikukuu ya kila mwaka ya Eid al-Adha - Sikukuu ya kutoa au sadaka - ambayo huangukia siku ya 10 ya Dhul Hijjah, mwezi wa 12 na wa mwisho wa kalenda ya mwandamo ya mwezi wa kiislamu.
Eid al-Adha ni sikukuu ya pili kuu ya Waislamu baada ya Eid al-Fitr, ambayo inaadhimisha mwisho wa Ramadhani, mwezi wa mfungo.Haya hapa yote unayofaa kujua kuhusu Eid Ul Adha na Hajj;
Habari za hivi punde, Prigozhin azungumza kwa mara ya kwanza baada ya kukomesha uasi
Kiongozi wa kundi la Wagner Yevgeny Prigozhin ameshirikisha mtandaoni ujumbe wa sauti wa dakika 11 ambapo anasema hakuna aliyekubali kusaini mkataba na wizara ya ulinzi na kwamba kampuni yake ya mamluki ingevunjwa kufikia tarehe 1 Julai.
Prigozhin pia amesema hakumlenga Putin alipotangaza kwamba wapiganaji wake wangeandamana mjini Moscow, akisema: "Hatukuandamana kuupindua utawala wa Urusi."
Katika ujumbe huo, anasema: "Lengo la maandamano hayo lilikuwa kuepusha kuvunjwa kwa Wagner na kuwawajibisha maafisa ambao kwa vitendo vyao visivyo vya kitaalamu wamefanya makosa mengi".
Anasema Wagner anasikitika "ilibidi waishambulie ndege ya Urusi" na kubadili nia ya uasi" ili kuzuia umwagaji wa damu ya wanajeshi wa Urusi."
Prigozhin anasema hakuandamana kupindua uongozi wa Urusi
Kiongozi wa Wagner Yevgeny Prigozhin ameweka wazi kuwa hakumlenga Putin alipotangaza kuwa wanajeshi wake wangeandamana hadi mjini Moscow akisema: "Hatukuandamana kuupindua uongozi wa Urusi."
Katika ujumbe wake wa sauti wa dakika 11, anasema: "Lengo la maandamano hayo lilikuwa kuepusha uharibifu wa Wagner na kuwawajibisha maafisa ambao kwa vitendo vyao visivyo vya kitaalamu wamefanya makosa mengi".
Akizungumzia kuhusu masharti ya makubaliano ambayo yaliripotiwa kufanywa ili kukomesha uasi wa Wagner mwishoni mwa juma, Prigozhin anadai Makamanda walikataa ombi la kutia saini mikataba na wizara ya ulinzi ya Urusi.
Kwa kubadilishana, anadai karibu watu wake 30 "waliuawa na mashambulizi ya Urusi" - BBC haijathibitisha dai hili.
Prigozhin pia anasema kuwa kiongozi wa Belarus Alexander Lukashenko alihusika katika mpango huo, akisema kwamba Lukasjenko "alinyoosha mkono wake na kujitolea kutafuta njia za Wagner kuendelea na kazi yake kisheria" - bila kutoa maelezo zaidi.
Prigozhin hakufichua alipokuwa katika ujumbe wa video alioshiriki kwenye Telegram. Imeripotiwa kuwa kama sehemu ya mpango huo, Prigozhin alikuwa amekubali kwenda Belarus.
Prigozhin asema vita vya Ukraine vingemalizika mapema zaidi chini ya Wagner
Yevgeny Prigozhin anakosoa sana vikosi vya usalama vya Urusi katika ujumbe wake wa hivi punde wa sauti.
Alisema maandamano yake huko Moscow siku ya Jumamosi yalifichua "matatizo makubwa zaidi ya usalama katika nchi nzima," akidai kwamba vitengo vyake viliweza kuzuia "vitengo vyote" vya kijeshi vya Urusi na viwanja vya ndege kwenye njia yao.
Prigozhin anadai kundi la mamluki la Wagner lilikuwa na uungwaji mkono katika miji ambayo lilipitia wakati wa uasi wake wa muda mfupi.
Pia anadai kuwa vikosi vyake vilisafiri kilomita 780 (maili 484) katika maandamano yao kuelekea Moscow kutoka kusini - sawa na umbali ambao majeshi ya Urusi yalichukua tarehe 24 Februari mwaka jana (walipoanza uvamizi wao nchini Ukraine) kutoka mpaka wa Ukraine hadi Kyiv, na kuingia Uzhgorod, jiji lililo mbali magharibi mwa Ukraine kwenye mpaka wa Hungary na Slovakia.
Anasema iwapo wanajeshi Wagner wangefanya shambulio hilo la kwanza, "operesheni maalum ya kijeshi nchini Ukraine" ingemalizika mapema zaidi.
Lukashenko alitoa njia kwa Wagner kuendelea kufanya kazi - Prigozhin
Akizungumzia kuhusu masharti ya makubaliano ambayo yaliripotiwa kufanywa ili kukomesha uasi wa Wagner mwishoni mwa juma, Prigozhin anadai kundi hilo "lilikuwa kinyume kabisa na uamuzi wa kufunga Wagner mnamo 1 Julai 2023 na kuijumuisha katika wizara ya ulinzi. ".
Makamanda walikataa kukubali ombi la kutia saini mikataba na wizara ya ulinzi ya Urusi, anaongeza.Anadai karibu watu wake 30 "waliuawa na mashambulizi ya Urusi" - BBC haijathibitisha dai hili.
Prigozhin pia anasema kuwa kiongozi wa Belarus Alexander Lukashenko alihusika katika mpango huo, akisema kwamba Lukasjenko "alinyoosha mkono wake na kujitolea kutafuta njia za Wagner kuendelea na kazi yake kisheria" - bila kutoa maelezo zaidi.
Prigozhin hakufichua alipokuwa katika ujumbe wa video alioshiriki kwenye Telegram.Imeripotiwa kuwa kama sehemu ya mpango huo, Prigozhin alikuwa amekubali kwenda Belarus.
Unaweza pia kusoma
Wapiganaji wa Wagner wataendelea kuhudumu barani Afrika - Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov, anasema operesheni za kundi la Wagner zitaendelea nchini Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati, huku kukiwa na sintofahamu kuhusu mustakabali wa kundi hilo la mamluki.
Wanachama wa Wagner "wanafanya kazi huko kama wakufunzi" na kazi hii itaendelea, Lavrov alisema katika mahojiano na shirika la utangazaji la Urusi RT, akiongeza kuwa uasi wa Wagner wa wikendi hii hautaathiri uhusiano wa Moscow na "washirika wake".
Kauli ya Lavrov imeongeza hali ya ati ati kuhusu uwazi juu ya mustakabali wa kundi hilo, haswa baada ya Urusi mapema mwezi huu kutangaza kwamba "makundi ya kujitolea" yatahitajika kutia saini kandarasi ili kuziunganisha na wizara ya ulinzi - jambo ambalo kiongozi wa Wagner Yevgeny Prigozhin alikosoa vikali.
Mswada huo ulitoa makataa kwa "makundi ya kujitolea" hadi tarehe 1 Julai kutii na kutia saini kandarasi, na ingawa tangazo hilo halikutaja Wagner moja kwa moja, lilizingatiwa sana kuwa sehemu ya juhudi za kupunguza ushawishi wa kundi hilo - hasa kiongozi wake Prigozhin.
Bado haijabainika uasi wa wikendi utaathiri vipi mipango hii ya ujumuishaji.
Huku hayo yakijiri, Bw Lavrov amesema mamlaka ya Urusi inachunguza ikiwa nchi za Magharibi zilihusika katika maasi ya Wagner siku ya Jumamosi, shirika la habari la Tass linaripoti.
Lavrov pia anasema balozi wa Marekani mjini Moscow "alitoa ishara" kwamba nchi yao haikuhusika, akiongeza kuwa kilichofanyika ni mambo ya ndani ya Urusi.
Soma zaidi:
- Yuko wapi kiongozi wa Wagner Prigozhin sasa?
- Saa 24 za jaribio la uasi Urusi
- Mkuu wa Wagner kuhamia Belarus baada ya kuachana na uasi
- Je, haya ni mapinduzi? Prigozhin anafanya nini nchini Urusi?
- Kiongozi wa kundi la Wagner aapa kuwapindua viongozi wa kijeshi wa Urusi
- Tazama: Mamluki wa Wagner wenye silaha katika mitaa ya Rostov
Sudan Kusini yawapokea wakimbizi 10,000 wanaokimbia Sudan
Zaidi ya watu 10,000 wamejiandikisha kuwa wakimbizi nchini Sudan Kusini baada ya kukimbia mzozo nchini Sudan, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (Ocha), imesema.
Kwa ujumla, watu 130,000 wamekimbilia Sudan Kusini tangu mapigano yalipoanza mwezi Aprili, wengi wao walikuwa raia wa Sudan Kusini wanaorejea nyumbani.
Ocha ilisema mmiminiko wa hivi punde unaendelea kuzidisha hali mbaya kwani idadi ya wanaowasili inakadiriwa kuendelea kuongezeka huku mapigano yakiendelea.
Miongoni mwa wanaowasili ni pamoja na watoto waliotenganishwa na wazzi wao, wazee, watu wenye ulemavu, walio na mahitaji ya dharura ya matibabu, nyumba zinazoongozwa na mwanamke mmoja au wanawake wajawazito, Ocha aliongeza.
Wengi waliofika wameshuhudia, au kufanyiwa vurugu na dhulma kama vile unyang'anyi na uporaji, hasa wakati wa safari yao ya Sudan Kusini.
Majirani wengine wa Sudan, Misri - yenye 255,000 - na Chad - yenye 120,000 - wamechukua sehemu kubwa ya watu wanaokimbia ghasia.
Uchaguzi wa Sierra Leone: Julius Maada Bio na Samura Kamara wadai ushindi
Matokeo rasmi ya uchaguzi mkuu wa Sierra Leone uliofanyika Jumamosi bado hayajatangazwa, lakini Rais Julius Maada Bio na mpinzani wake mkuu Samura Kamara wanadai ushindi.
Kampeni ya kuelekea uchaguzi huo ilikuwa kuwa kali na iliyogubikwa na vurugu.
Bw Kamara anasema risasi zilifyatuliwa katika makao makuu ya chama chake alipokuwa na kikao na wanahabari Jumapili.
Mwanamke mmoja aliripotiwa kujeruhiwa na kuna hofu maisha yake yako hatarini.
Uchaguzi huo wa Jumamosi ilishuhudia idadi kubwa ya watu waliojitokeza kupiga kura, huku wapiga kura wakiambia BBC kuwa mchakato huo ulikuwa rahisi licha ya upigaji kura kuchelewa katika baadhi ya maeneo.
Kumekuwa na wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuzuka kwa ghasia wakati wa maandalizi ya uchaguzi huo.
Mnamo Jumatano, chama cha All People's Congress (APC) cha Bw Kamara kilidai kuwa mmoja wa wafuasi wake aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi, jambo ambalo polisi wamekanusha.
Wafuasi wa vyama vikuu viwili wametuhumiwa kushambulia wapinzani.
Shutuma za makosa ya uchaguzi pia zilikuwa zikitupwa siku ya Jumamosi, baada ya Bw Kamara kudai kuwa shughuli ya upigaji kura ilikumbwa na ukandamizaji katika baadhi ya maeneo nchini humo.
Hata hivyo, katika mkutano na waandishi wa habari mapema wiki hii Tume ya Uchaguzi imesisitiza, kwamba ilikuwa na utaratibu wa kuhakikisha uchaguzi wa haki.
Vyombo vya habari vya ndani vinaripoti kwamba watu walikamatwa.
Hatua ya kupandisha kodi Kenya ni 'kosa' - Upinzani
Upinzani nchini Kenya umeelezea nyongeza ya ushuru iliyotiwa saini na Rais William Ruto kama "kosa", shirika la habari la AFP linaripoti.
Tayari upinzani umefanya maandamano ya kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha mwaka huu na unatishia kuafanya maandamano zaidi "Msimamo wetu unasalia kuwa mswada huo ni makosa na mzigo ambao Wakenya hawawezi kuumudu," msemaji wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga amenukuliwa na AFP akisema.
"Tulitumai kuwa Ruto angeweza kuitisha ukaguzi wake kabla ya kuutia saini."
Miongoni mwa mabadiliko yaliyokubaliwa na bunge wiki iliyopita ni pamoja na kuongezeka maradufu ushuru wa mauzo ya mafuta, kutoka 8% hadi 16%, na ushuru mpya wa nyumba.
Hatua hizo mpya zimewakasirisha baadhi ya wafuasi wa rais, ambaye wakati wa kampeni zake za uchaguzi zilizofaulu alijidhihirisha kama mtu ambaye angejali masilahi ya maskini.
Bw Ruto ametetea mabadiliko hayo akisema yanastahili kufanywa ili kushughulikia tatizo la deni la nchi na kama njia ya kuwekeza katika mipango ambayo itawanufaisha wasio na uwezo.
Maelezo zaidi:
- Mswada wa Fedha 2023 uliozua utata watiwa saini kuwa sheria
- Jinsi muswada tata wa fedha 2023 utakavyoathiri maisha ya Mkenya
- Wabunge Kenya wapitisha Mswada wa Fedha
Picha mpya zinaonyesha puto za kijasusi za China juu ya Asia
Ushahidi mpya wa mpango wa puto za kijasusi wa China - ikiwa ni pamoja na safari za ndege juu ya Japan na Taiwan - umefichuliwa na BBC Panorama.
Japan imethibitisha kuwa puto zimeruka katika eneo lake na kusema iko tayari kuziangusha katika siku zijazo.
China haijajibu moja kwa moja kuhusu ushahidi uliowasilishwa na BBC.
Uhusiano kati ya Marekani na China ulitumbukia katika msukosuko mapema mwaka huu, wakati puto linalodaiwa kuwa la kijasusi la China lilipotunguliwa kwenye pwani ya Marekani.
China ilidai puto lililoonekana kaskazini-magharibi mwa Marekani mwishoni mwa Januari lilikuwa la kiraia, kwa matumizi ya utafiti wa kisayansi kama vile hali ya hewa - na kwamba lilikuwa tukio lisilotarajiwa na la kipekee.
John Culver - mchambuzi wa zamani wa Asia Mashariki wa CIA - aliiambia Panorama kwamba hii "haikuwa tu ya mara moja, lakini jitihada zinazoendelea za takriban miaka mitano."Alisema puto za Uchina "ziliundwa mahsusi kwa misheni hii ya masafa marefu" na zingine "zimezunguka ulimwengu".
Putin atoa hotuba ya kwanza tangu uasi wa Wagner
Rais wa Urusi Vladimir Putin ametoa kauli yake ya kwanza tangu uasi wa kundi la Wagner mwishoni mwa juma, akionekana kwenye video ya Kremlin akiwahutubia washiriki katika kongamano la viwanda.
Akihutubia watu katika kongamano lililoitwa "Wahandisi wa siku zijazo", Putin alisifu makampuni kwa kuhakikisha "uendeshaji thabiti" wa sekta mbali mbali za nchi "katika kukabiliana na changamoto kali za nje", kulingana na nukuu zilizotajwa na shirika la habari la AFP.
Haijulikani ni lini au wapi Putin alipokuwa aliporekodi taarifa hiyo.Hakutaja mpango ambao Prigozhin alikubali kusimamisha askari wake na kuhamia Belarusi.
Katika hotuba nyingine siku ya Jumamosi, Putin alishutumu mamluki wa Wagner kwa uhaini, na kuyataja matendo yao kuwa "usaliti."
Ujumbe wa hivi punde zaidi wa video wa Rais Vladimir Putin unamaanisha kuwa shughuli zinaendelea kama kawaida kwa Kremlin: anawapongeza wahandisi wachanga wanaohudhuria kongamano hilo.
Hotuba hiyo imejaa maneno ya kizalendo.Putin anawasifu "vijana, wataalam wenye uzoefu, vikundi katika biashara zetu", akisema wamepata ukuaji wa uzalishaji katika sekta muhimu zaidi kwa maisha ya nchi - kiraia na kijeshi.
Jambo la kushangaza ni kwamba kongamano la viwanda linafanyika Tula, jiji lililo kusini mwa Moscow ambalo kwa jadi ni kituo cha utengenezaji wa silaha.Na Tula ilikuwa kwenye njia ya kaskazini kuelekea Moscow ambayo wanajeshi wa Wagner wa Yevgeny Prigozhin walitumia wikendi - ingawa waligeuka na kurejea nyuma kabla ya kuchukua udhibiti wa Tula.
Lazima tuungane nyuma ya Putin - Waziri Mkuu wa Urusi
Waziri Mkuu wa Urusi Mikhail Mishustin anasema Urusi imekabiliwa na "changamoto kwa uthabiti wake", na lazima ibaki na umoja nyuma ya Rais Vladimir Putin katika maoni yaliyotolewa wakati wa mkutano wa serikali ulioonyeshwa kwenye televisheni.
Katika kikao kilichopeperushwa na shirika la habari linalomilikiwa na serikali Tass, Mishustin alisema kwamba "chini ya uongozi wa rais" maafisa wa serikali walifanya kazi "kwa umoja" ili kuhakikisha utulivu baada ya maasi.
"Jambo kuu katika hali hizi ni kuhakikisha uhuru wa nchi yetu, usalama na ustawi wa raia," alisema, akitoa wito kwa watu 'kusimama na rais rais".
Soma zaidi:
Je, kiongozi wa Belarus Lukashenko ni mwokozi wa Putin?
Kitu kimoja cha ajabu cha msukosuko wa wikendi nchini Urusi ni jukumu la upatanishi la kiongozi wa Belarus Alexander Lukashenko.
Kulingana na Kremlin, bosi wa mamluki wa Wagner Yevgeny Prigozhin alikubali kurudi nyuma , wanajeshi wake waliachana na maandamano yao kuelekea Moscow, na akakubali kuhamia Belarusi baada ya kufanya mazungumzo moja kwa moja na Lukashenko.
Lakini kumkaribisha kiongozi wa Wagner Belarus kunaweza kuwa hatari kwa Lukasjenko.
Belarus ilikuwa moja ya njia za kurushia makombora ya Urusi dhidi ya Ukraine na makombora ya Urusi yamerushwa kutoka anga ya Belarus, lakini hadi sasa Lukashenko ameepuka kuwaingiza wanajeshi wa Belarus vitani.
Sasa Lukasjenko anaweza kupata ugumu wa kukwepa kuburutwa kwenye vita au katika machafuko ya kisiasa ya Urusi.
Ikiwa Prigozhin atatokea Belarusi inamaanisha yuko nje ya nchi lakini anaweza kufikia Urusi kwa urahisi.
Hii pia inaweza kuonekana kama wakati wa malipo kwa Kremlin.Ahadi ya Putin ya kuimarisha polisi ilisaidia kumweka Lukasjenko madarakani mwaka wa 2020, wakati maandamano makubwa ya kupinga kuchaguliwa tena kwa Lukasjenko.
Kwa hivyo hatima ya Lukasjenko inaonekana kuhusishwa kwa karibu na Putin- ni mmoja wa viongozi wachache wa kigeni ambao Putin anaweza kutegemea, na Belarusi, kama Urusi, iko chini ya vikwazo vikubwa vya Magharibi.
Utawala mkali wa kimabavu wa Lukashenko, wa miongo kadhaa, ni sawa na wa Putin.Wote wawili wanajifananisha na uhafidhina usio na uvumilivu na kijeshi wa enzi ya Soviet.
Lakini "ndugu mdogo" Belarusi anayesaidia "ndugu mkubwa" Urusi katika saa yake ya mahitaji inaonekana ni taswira inayomfedhehesha Putin.
Hatua ya Prigozhin kwenda Belarus itaongeza msukosuko - kiongozi wa upinzani
Kiongozi wa upinzani wa Belarus aliye uhamishoni Svetlana Tikhanovskaya anasema kuhamia nchini humo kwa kiongozi wa Wagner Yevgeny Prigozhin "kunaongeza hali nyingine ya ukosefu wa utulivu" nchini humo.
Akimtaja Prigozhin kama "mhalifu wa kivita", Tikhanovskaya alisema katika maoni yaliyonukuliwa na tovuti huru ya habari ya Belarus Zerkalo kwamba nchi yake haihitaji "wahalifu zaidi na majambazi".
Maoni yake yamekuja baada ya kutangazwa kuwa Prigozhin atakwenda Belarus baada ya uasi wake wa muda mfupi nchini Urusi mwishoni mwa juma kusitishwa, kufuatia mpango uliosimamiwa na kiongozi wa Belarus Alexander Lukashenko.
Tikhanovskaya pia alimkosoa Lukashenko, akisema kwamba ameifanya Belarusi "mateka kwa michezo na vita vya watu wengine".
Tikhanovskaya alikimbia Belarus mnamo 2020 baada ya kugombea uchaguzi dhidi ya Lukashenko, ambao anafikiriwa kuwa alishinda.Baadaye alihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela bila kuwepo mahakamani na mahakama ya Belarus.
Soma zaidi:
Mwanamume auawa na genge la watu kaskazini mwa Nigeria kwa madai ya kukufuru
Mtu mmoja ameuawa kaskazini mwa Nigeria na kundi la watu kwa madai ya kukufuru.
Usman Buda, ambaye alifanya kazi kama mchinjaji katika kichinjio cha jiji la Sokoto, "alivamiwa na kushambuliwa na baadhi ya waumini wa Kiislamu [ambao] walimjeruhi vibaya", msemaji wa polisi wa jimbo la Sokoto Ahmad Rufa'i amenukuliwa na shirika la habari la AFP akisema .
Polisi walipofika kwenye eneo la tukio, "kundi la watu lilitoroka na kumwacha mwathiriwa akiwa amepoteza fahamu", aliongeza, ripoti ya Premium Times.
Bw Buda alipelekwa kwa matibabu na polisi walipoenda kumuokoa lakini alithibitishwa amefariki hospitalini.
Mamlaka sasa inawasaka wanaodaiwa kuwa wahusika.
Shirika la habari la AFP Linaripoti kuwa Bw Buda aliuawa kufuatia mabishano kuhusu baadhi ya watoto ombaomba waliokuwa wameomba pesa. AFP inamnukuu shuhuda mmoja akisema kwamba alijipata katika mzozo baada ya kuwakaripia watoto hao. Kisha akatoa matamshi yanayodaiwa kuwa ya kukufuru kuhusu Mtume Muhammad.
Video ya kutisha inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha umati ukimpura mwanamume kwa mawe huku akijikwaa na kuanguka.
Akijibu, Gavana wa jimbo la Sokoto Ahmed Aliyu "alitoa wito kwa watu wa jimbo hilo kuwa watulivu na kuzingatia sheria wakati wote", lakini akaongeza kuwa watu hawapaswi kufanya chochote ambacho kinaweza kumdhalilisha Mtume Muhammad.
Mnamo Mei mwaka jana, mwanafunzi wa kike alivamiwa katika chuo chake huko Sokoto, na wanafunzi Waislamu ambao walimuua na kuuchoma moto mwili wake.
Alikuwa ameshtakiwa kwa kukufuru
Mwanamke wa Marekani ampiga risasi dereva wa Uber aliyedhani anamteka nyara
Mwanamke mmoja nchini Marekani amefunguliwa mashtaka ya mauaji baada ya kumpiga risasi dereva wa Uber ambaye alidhani alikuwa akimteka nyara, polisi wanasema.
Kulingana na polisi katika mji wa mpaka wa El Paso, Texas, Phoebe Copas alifikiria alikuwa akipelekwa Mexico.
Na hapo ndipo akampiga risasi dereva Daniel Piedra Garcia, mamlaka ilisema katika taarifa.
Dereva huyo mwenye umri wa miaka 52 alifariki hospitalini baada ya siku kadhaa.
Akiwa ndani ya gari,Copas aliona alama za trafiki zilizoandikwa Juarez, Mexico, kulingana na hati za polisi.
Miji hiyo miwili iko pande zote mbili za mpaka wa Marekani na Mexico.
Hati za polisi pia zinaeleza kwamba baada ya kufikiria kuwa alikuwa akitekwa nyara, Copas alichomoa bunduki kutoka kwa mkoba wake na kumpiga dereva kichwani.
Baada ya hapo gari liligonga vizuizi vya barabarani kabla ya kusimama. Copas - ambaye anatoka Kentucky lakini alikuwa akimtembelea mpenzi wake - anadaiwa kupiga simu nambari ya dharura 911, kumpiga picha ya dereva na kumtumia mpenzi wake.
"Uchunguzi haujathibitisha kwamba utekaji nyara ulifanyika au kwamba Piedra alikuwa akikwepa kutoka kwa kituo cha Copas," taarifa ya polisi ya El Paso ilisema.
Félix Tshisekedi aonya mtafaruku wa maaskofu unahatarisha umoja wa kitaifa kabla ya uchaguzi wa rais
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Félix Tshisekedi ameonya "mtafaruku" katika kanisa katoliki ambao unahatarisha umoja wa kitaifa kabla ya uchaguzi wa rais.
Wiki iliyopita, maaskofu wa DRC waliwataka watu wa Congo kuwa macho kwa ajili ya uchaguzi wa kuaminika.
Akijubu maaskofu moja kwa moja, Bw Tshisekedi alisema kuwa katika uongozi wa kanisa la eneo kuna “mtafaruku ambao ningeuelezea kuwa hatari, haswa katika mwaka huu wa uchaguzi."
"Miongoni mwenu, kwa bahati mbaya kuna watu wachache ambao wamechukua mwelekeo hatari ambao unaweza kuligawa taifa letu ... siwezi kukubaliana na jambo kama hilo", aliongeza baada ya misa ya Jumapili katika maadhimisho ya miaka 50 ya Askofu wa Mbuji-Mayi Emmanuel-Bernard Kasanda katikati ya Congo.
Katika taarifa yao wiki iliyopita, maaskofu wa kanisa katoliki DRC walisema, "hali ya kisiasa ni ya wasiwasi" na kuchukiza, "ukandamizaji mbaya zaidi wa upinzani, vikwazo vya uhuru, ukandamizaji wa haki na watu kukamatwa kiholela" tangu Bw Tshisekedi achukue hatamu mwaka wa 2019.
"Kwa uchaguzi wa kuaminika, watu wa Congo, kuweni macho!”, Maaskofu waliwaambia wenzao.
Soma zaidi:
Je kuna ishara yoyote ya utumiaji nguvu upande wa Urusi?
Tangazo la ziara ya Waziri wa Ulinzi Sergei Shoigu linaweza kuwa onyesho kutumia nguvu la Urusi, na jaribio la kusisitiza bado linalenga kile kinachoitwa "operesheni maalum ya kijeshi" nchini Ukraine.
Kufuatia tangazo la kuondoka kwa mkuu wa kundi la Wagner Yevgeny Prigozhin mwishoni mwa juma, kumekuwa na uvumi kama angejaribu kushambulia eneo la Ukraine kutoka Belarus.
Kujibu hili, mkuu wa majeshi ya Ukraine alisema hakuna ushahidi wa ongezeko la wanajeshi wa kigeni au vifaa katika mpaka wa kaskazini, na kwamba hali huko iliendelea kuwa shwari.
Licha ya hayo, aliongeza kuwa vikosi vya Ukraine vimeimarisha ulinzi wao kaskazini na kwamba jaribio lolote la kufanya mashambulizi huko litakuwa kama "kujimaliza" kwa upande wa Urusi.
Soma zaidi:
Tazama video ya waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu akiwatembelea wanajeshi wa Urusi baada ya uasi wa Wagner
Tazama video ya Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu, iliyoonekana kwa mara ya kwanza tangu uasi wa kundi la Wagner uliokomeshwa wikendi.
Mkuu Wagner Yevgeny Prigozhin alidai Shoigu aondolewe alipoanzisha uasi wake - lakini video hii inamuonyesha bado yuko kazini.
Hatujui ilirekodiwa lini.Lakini tunaweza kusoma ujumbe unaokusudiwa katika video hii: kwamba, kwa sasa angalau, Vladimir Putin anamlinda waziri wake - sio kumfukuza kazi, kama Yevgeny Prigozhin alivyotaka alipoanzisha uasi wake mwishoni mwa wiki.
Shoigu, ambaye amekuwa mshirika wa karibu na rafiki wa Putin kwa miaka mingi, anarekodiwa akiangalia ramani na kushauriana na majenerali wake .
Anabainisha hata mafanikio yao yanayodhaniwa kuwa kwenye uwanja wa vita.Ni onyesho la wazi la utulivu na udhibiti wa Kremlin baada ya uasi wa kutumia silaha ambao ulimwacha Putin akionekana dhaifu;mamlaka yake yalipungua vibaya.
Hata alilazimika kufuta mashtaka ya uhalifu dhidi ya Prigozhin - mtu ambaye alikuwa amemtaja hadharani kuwa msaliti, saa chache kabla.
Soma zaidi:
Mfanyakazi wa uwanja wa ndege wa Texas afariki baada ya 'kufyonzwa' ndani ya injini ya ndege ya Delta
Mfanyakazi wa uwanja wa ndege amefariki baada ya kuingia kwenye injini ya ndege ya abiria huko Texas.
Mfanyikazi huyo "alifyonzwa" ndani ya injini ya ndege ya Delta iliyokuwa ikielekea katika eneo lake la kuegeshwa huku injini moja ikiwashwa, maafisa walisema.
Waajiri wa mfanyakazi huyo wanasema uchunguzi wa awali unaonyesha tukio hilo halihusiani na taratibu za usalama, lakini bado haijafahamika jinsi lilivyotokea.
Uchunguzi pia unafanywa na wakala wa serikali.
Bodi ya Kitaifa ya Usalama wa Usafiri ilisema imekuwa ikiwasiliana na Delta Air Lines na ilikuwa "katika mchakato wa kukusanya habari wakati huo."
Ndege hiyo aina ya Airbus A319, iliwasili San Antonio Ijumaa usiku kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Los Angeles.
Maafisa bado hawajamtaja mfanyikazi huyo wa Unifi Aviation, ambaye Delta Air Lines inaweka kandarasi kwa shughuli za wafanyakazi wa ardhini.
"Tangu uchunguzi wetu wa awali, tukio hili halikuhusiana na michakato ya uendeshaji ya Unifi, taratibu za usalama na sera," kampuni hiyo ilisema.
Msemaji wa Delta alisema shirika hilo la ndege "lilivunjika moyo" kwa kuhuzunishwa na "maisha ya mwanafamilia huyo wa anga".
"Mioyo yetu na msaada kamili uko pamoja na familia zao, marafiki na wapendwa wao wakati huu mgumu."
Shirika hilo la ndege pia liliambia mtangazaji wa eneo hilo Kens 5 kwamba lilikuwa likishirikiana na mamlaka "wanapoanza uchunguzi wao".
Siku ya Jumatano, shirika la ndege la eneo la Piedmont lilitozwa faini ya $15,625 (£12,285) na Utawala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa kifo cha mfanyakazi wa uwanja wa ndege miezi sita iliopita katika tukio kama hilo huko Alabama.
"Mafunzo sahihi na utekelezaji wa taratibu za usalama ungeweza kuzuia janga hili," OSHA ilisema.
Mswada uliozua utata wa Fedha 2023 watiwa saini kuwa sheria
Rais wa Kenya William Ruto ametia saini na kuufanya kuwa sheria mswada uliozua utata wa Fedha 2023, huku upinzani ukijitayarisha kuchukua hatua ya kukabiliana na hilo.
Kutia saini mswada huo Jumatatu, kunafungua njia ya kuanza kutekelezwa kwa utozaji kodi ya nyumba iliyoanzishwa na utawala wa Kenya Kwanza.
Mswada huo unajumuisha kodi ya ongezeko la thamani ya asilimia 16 kwa mafuta na kodi ya nyumba ambazo zimepangiwa kuanza kutekelezwa Julai 1, 2023.
Soma zaidi:
Wanajeshi wa Kenya kuongeza muda wa kukaa Somalia ili wasipotezi kile walichofanikiwa kupata
Rais William Ruto amedokeza kwamba wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Kenya nchini Somalia huenda wakasalia huko kwa muda mrefu zaidi hata baada ya ratiba kufungwa.
Ruto alisema mataifa yaliyo vitani - Kenya, Uganda, na Ethiopia- wameamua kusalia na kuendeleza masuala ya ulinzi zaidi ya muda uliowekwa ili wasipoteze mafanikio yaliyopatikana hadi sasa.
"Tumeamua kama mataifa yaliyovitani - Uganda, Kenya, Sudan- kwamba tutabaki kuendeleza hili na ikiwa ni lazima na tunadhani ni muhimu tutakaa zaidi ya ratiba iliyopunguzwa ili tusipoteze kile tumefanikiwa kupata kwa sababu tu tumetoka kwenye hali fulani na kuwaruhusu al Shabaab kurudi tena kwenye maeneo hayo.”
Alisema kundi la kigaidi la al Shabaab linajaribu kujipanga upya baada ya kuanza kwa kuondolewa kwa wanajeshi wa Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) ili kujenga hisia kwamba watachukua eneo hilo.
Ruto aliyasema hayo katika mahojiano na France 24 na kuapa kuwa watakabiliana na kundi hilo la kigaidi.
"Changamoto ya al Shabaab inabidi tukabiliane nayo. Tuna nia na tuna kila nafasi ya kuwashinda al Shabaab,” Ruto alisema.
Soma zaidi:
Fentanyl: Watu wengi zaidi wanajidunga dawa za kulevya duniani kote - UN
Watu wengi zaidi wanajidunga dawa za kulevya kuliko ilivyofikiriwa hapo awali, inasema ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu matumizi ya dawa za kulevya duniani kote.
Kwa ujumla, watu milioni 13.2 walijidunga dawa mwaka 2021, 18% zaidi ya ilivyokadiriwa hapo awali, ilisema Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) yenye makao yake Vienna.
Dutu za syntetisk kama vile fentanyl na methamphetamine sasa zinatawala masoko haramu ya dawa za kulevya, Umoja wa Mataifa unasema.
Ulimwenguni, watumiaji wa dawa za kulevya waliongezeka kwa 23% na shida zinazohusiana na dawa za kulevya ziliongezeka kwa 45% katika muongo mmoja hadi karibu milioni 40.
Watu wenye matatizo ya afya ya akili, wale wanaotoka katika jamii zenye uchumi wa chini na vijana walikuwa hatarini zaidi, ripoti hiyo ilisema.
Ulaya Mashariki na Amerika Kaskazini zilionekana kuwa na kiwango kikubwa cha watu wanaojidunga sindano kuliko katika Mashariki na Kusini-Mashariki mwa Asia.
Fentanyl imebadilisha soko la opioid huko Amerika Kaskazini na athari zake ni mbaya zaidi, ripoti iligundua.
Kwa msingi wa takwimu kutoka nchi 18, ilisema wanaume wana uwezekano mara tano zaidi kuliko wanawake kujidunga dawa na kuwatambulisha wenzi wao wa kike tabia hiyo.
Bado, ni mtu mmoja tu kati ya watano anayeweza kupata matibabu, unasema Umoja wa Mataifa, huku wanawake hasa wakikabiliwa na vikwazo.
Sababu ni nyingi na zinafungamana: Covid-19, lakini pia hofu ya vikwazo vya kisheria, unyanyapaa wa kijamii, ukosefu wa malezi ya watoto na hofu ya kupoteza malezi ya watoto wao.
Ghada Waly, mkuu wa UNODC, alisema kuwa katika matukio mengi, matibabu yanashindikina kwa wale wanaohitaji.
"Tunahitaji kuongeza hatua za kukabiliana na biashara haramu ya dawa za kulevya ambazo zinatumia migogoro na matatizo ya kimataifa kupanua kilimo na uzalishaji haramu wa dawa za kulevya, hasa dawa za syntetisk, kuchochea masoko haramu na kusababisha madhara makubwa kwa watu na jamii," Bi Waly alisema.