Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uasi nchini Urusi unaonyesha 'mpasuko' katika mamlaka ya Putin-Marekani
Yevgeny Prigozhin na askari wake hawatashtakiwa, inasema Kremlin. Wapiganaji wa Wagner wameripotiwa kuanza kuondoka katika mji wa kusini wa Rostov-on-Don
Moja kwa moja
Yusuf Jumah
Dhana iliyojengwa ya Putin kama mtu 'mkali' imevunjwa na Prigozhin
Matukio ya wikendi hii yanaangazia "udhaifu halisi katika utawala wa Putin," mhariri wa BBC wa masuala ya ulimwengu anasema.
Akiongea na BBC Radio 5 Live, John Simpson anasema kwa miaka 20 Putin ameweza - pamoja na misukosuko kadhaa - kila mara kujionyesha kama 'bosi mkuu'
"Unakumbuka picha zake zote akiwa amepanda farasi akiwa bila shati na kupigana mieleka," anakumbuka Simpson.
Lakini kuibuka kwa mkuu wa Wagner Yevgeny Prigozhin kumepinga hilo.
"Muundo mzima wa Putin unaanza kushuka kama matokeo ya uasi wa Wagner"
Mshauri wa zamani wa Putin anakubali "mgogoro fulani" katika serikali ya Urusi
Je viongozi kisiasa wa Urusi wanachukuliaje uasi wa jana wa kundi la mamluki la Wagner?
Maoni ya Sergei Markov, mwanasayansi wa siasa wa Urusi na mshauri wa zamani wa Rais Putin, ni dalili moja.
Aliambia kipindi cha BBC Radio 4's Broadcasting House kwamba matukio hayo yalikuwa "kiashiria cha baadhi ya mgogoro katika serikali ya Urusi", ambayo haidhibiti kikamilifu sehemu za jeshi la Urusi.
"Kwa hivyo Vladimir Putin itabidi abadili sera yake na, chini ya matakwa ya jamii ya Urusi, na sehemu ya jeshi la Urusi, kufanya sera [kali zaidi] kwa vita vya ushindi nchini Ukraine," alisema.
Alisema kuwa uasi wa Wagner uliunda "hali mbaya" kwa Putin na kwa Urusi kwa ujumla, na ungeweza kusababisha "vita vikubwa vya wenyewe kwa wenyewe".
Alisema Putin alifanya "makosa", lakini kubwa zaidi ni "kwamba anawaamini sana wanasiasa wa Magharibi".Kuanzia sasa, Putin anaweza kutegemea tu "nguvu za kijeshi", alisema.
Uasi wa Wagner ulikuwa 'pingamizi ya moja kwa moja kwa mamlaka ya Putin' - Marekani
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amekuwa akizungumza kuhusu hali nchini Urusi.
Blinken anasema uasi wa muda mfupi kutoka kwa mamluki wa Wagner unaonyesha "mpasuko halisi" katika mamlaka ya Putin, kulingana na shirika la habari la AFP.
Uasi wa kundi la kibinafsi la mamluki na kiongozi wake Yevgeny Prigozhin mwishoni mwa juma ulikuwa "pingamizi ya moja kwa moja kwa mamlaka ya Putin", Blinken amesema.
"Kwa hivyo hii inazua maswali mazito, inaonyesha mpasuko halisi," Blinken aliambia kipindi cha mazungumzo cha CBS News 'Face the Nation'.
Ni mapema mno kusema nini mustakabali wa kundi la mamluki la Wagner walioasi jana, Blinken anasema.
Kama tumekuwa tukiripoti, Kremlin imesema haitowafungulia mashtaka wanajeshi wa Wagner ambao waliasi jana, licha ya kuwashutumu mapema kwa uasi wa kutumia silaha.
Unaweza pia kusoma
'Mwanzo wa mwisho kwa Putin' - Waziri Mkuu wa zamani wa Urusi Kasyanov
Mikhail Kasyanov alikuwa waziri mkuu wa Urusi chini ya Putin kuanzia 2000-04.Lakini tangu afutwe kazi, amekuwa mmoja wa wakosoaji wakuu wa rais.
Alipoulizwa na BBC ambako anadhani Prigozhin atakwenda, alisema: "Nadhani kwanza ataenda Belarus, lakini nadhani atatoka Belarus hadi Afrika na kuwa mahali fulani katika msitu au kitu kama hicho.
"Bwana Putin hawezi kumsamehe kwa hili."
Prigozhin, anasema, ameharibu utulivu wa Putin - na maisha yake yatakuwa chini ya "swali kubwa" kama matokeo.
Kwa Putin, anasema Kasyanov, huu ni "mwanzo wa mwisho ... yuko katika matatizo makubwa sana hivi sasa."
Urusi na Ukraine zote zinadai mafanikio katika uwanja wa vita
Mbali na maasi, mapigano makali yanaendelea nchini Ukraine.
Katika ripoti yake ya hivi punde, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema kuwa vikosi vya jeshi la nchi hiyo vilizuia mashambulizi mengi ya vikosi vya Ukraine mashariki na kati mwa Ukraine.
Inasema kuwa katika eneo moja pekee - karibu na mji wa mashariki wa Bakhmut unaokaliwa na Urusi - mashambulio 10 ya Kiukreni yalizuiwa katika masaa 24 yaliyopita.
Jumamosi jioni, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Hanna Maliar alisema wanajeshi wa Ukraine walifanikiwa kusonga mbele karibu na Bakhmut na maeneo ya karibu.
Madai ya pande zinazopigana hayajathibitishwa kwa njia huru
Unaweza pia kusoma
Putin yuko wapi? - Tunachojua
Lakini vipi kuhusu Rais wa Urusi Vladimir Putin?
Kweli, sawa - hatujui, ni jibu la kuaminika
Siku ya Jumamosi asubuhi, kiongozi wa Kremlin alilaani uasi wa Wagner katika hotuba ya televisheni, lakini haijulikani ikiwa hayo yalikuwa matangazo ya moja kwa moja au yalirekodiwa mapema.
Baadaye mchana, ripoti za vyombo vya habari zilisema ndege ya rais ambayo Putin hutumia kawaida iliondoka katika mji mkuu wa Moscow, kuelekea kaskazini-magharibi.
Kisha ikatoweka kwenye rada katika eneo karibu na Tver.
Kufuatilia data kwenye tovuti ya flighradar24 inaonekana kuthibitisha habari hii - lakini hatujui kama Putin alikuwa kwenye ndege hiyo.
Hii ilikuja huku kukiwa na uvumi wa vyombo vya habari kwamba rais alikuwa akienda kwenye moja ya vyumba vyake vya chini ya ardhi katika eneo hilo, wakati mamluki wa Wagner walikuwa wakiandamana kwenda Moscow.
Lakini msemaji wa rais Dmitry Peskov alipuuza ripoti hizi, akisema Putin alikuwa akifanya kazi katika makazi yake ya Kremlin.
Baadaye Jumamosi - baada ya mpango wa kumaliza uasi kuripotiwa kupitishwa - Peskov alisema kuwa hakuna hotuba mpya ya rais iliyokuwa ikipangwa katika siku za usoni.
Sio kawaida kwa Putin kuwaachilia wanajeshi wa Wagner - Rainsford
Kauli ya Kremlin kwamba hakuna mashtaka yataletwa dhidi ya kiongozi wa Wagner Yevgeny Prigozhin au wanajeshi wake kwa uasi wao "inashangaza sana", mwandishi wa BBC wa Ulaya Mashariki Sarah Rainsford anasema.
Sio tabia ya Putin"kurudi nyuma namna hiyo kwa njia ya ajabu" baada ya kumshutumu Prigozhin kwa kumsaliti na 'kumchoma kisu mgongoni', anasema.
Rainsford anaongeza kuwa maswali mengi bado hayajajibiwa, bila kujali uhuru na usalama wa Prigozhin, ambayo inaweza kutegemea kile anachofanya huko Belarus.
Ana uwezekano wa kutaka kuendesha trekta au kuchimba viazi, anasema.
Putin, huenda akajibu matukio ya jana kwa ukandamizaji zaidi na kumsaka yeyote anayehusishwa na uasi huo.
Pia atajaribu kuangazia tena kile anachokichukulia kama tishio kwa Urusi kutoka Magharibi na Ukraine, Rainsford anaongeza.
Unaweza pia kusoma
Yuko wapi kiongozi wa Wagner Prigozhin sasa?
Kuna maswali mengi ambayo hayajajibiwa kuhusu mpango ambao kiongozi wa Wagner Yevgeny Prigozhin ili kukomesha uasi, na kuhusu nini kitafuata.
Moja ya mambo ambayo hatujui ni aliko Prigozhin sasa hivi.
Alionekana mara ya mwisho kwenye gari akiondoka Rostov-on-Don Jumamosi jioni - mji ulioko kusini mwa Urusi aliodai kuudhibiti kwa siku moja.
Alitabasamu huku akiwasalimu wakazi wa eneo hilo waliokuwa wakishangilia.
Alifaa kuelekea Belarus, kufuatia makubaliano yaliyoripotiwa kusimamiwa na kiongozi wa nchi hiyo Alexander Lukashenko, mshirika mkuu wa Rais Vladimir Putin.
Lakini Prigozhin tangu wakati huo hajasema juu ya ratiba yake.
Amri ya kutopaa ndege kwa sasa inatekelezwa kusini-magharibi mwa Urusi, ikimaanisha kuwa viwanja vya ndege vya karibu zaidi vya Rostov viko Volgograd na Sochi - lakini kila kimoja kiko umbali wa kilomita 400 (maili 250).
Prigozhin anaweza, kusafiri kwa gari au gari moshi - lakini ni njia ndefu hadi Belarusi, kwani lazima aipite Ukraine.
Unaweza pia kusoma
Putin atachukua hatua gani ifuatayo?
Hakika atajibu kwa kuonyesha nguvu - amekuwa akifanya hivyo kila wakati.
Hii inaweza kuwa kubana zaidi uhuru wa ndani na hata udhibiti mkubwa zaidi wa nyanja ya vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na Telegram yenye ushawishi.
Au Putin anaweza kufanya kampeini nyingine ya kijeshi katika eneo la Ukraine.
Au labda zote mbili.
Jambo moja ni wazi - ikiwa Ukraine itavunja ngome za Urusi kwenye mstari wa mbele wiki ijayo, bila shaka Moscow itaimlaumu Wagner na kile kinachojulikana kama usaliti.
Uasi wa Prigozhin unapinga taswira ya umoja na utulivu ambayo Putin na vyombo vya habari vya serikali walikuwa wakijaribu kuionyesha kwa miaka mingi.
Baadhi viongozi wa kisiasa waliogopa.Huduma za rada za ndege zilisababisha ndege kadhaa za kibinafsi kuondoka Moscow.
Lakini haikuwa mgogoro wa kimfumo.
Magavana wa mikoa walikuwa wepesi na kwa kauli moja katika kuahidi utiifu kwa Moscow.
Matukio haya yalikuwa tofauti sana na 1991 - jaribio lingine la mapinduzi ya kijeshi.Hapo zamani, baadhi ya viongozi wa kanda waliungana haraka na waasi.Hatukuona chochote kinachokaribiana na hali hiyo hapo jana.
Wakati huo huo, sura ya Putin imefunguliwa wazi na udhaifu wake kuanikwa.
Unaweza pia kusoma
Marekani ilijua kuwa mkuu wa Wagner alikuwa akipanga kuchukua hatua kabla ya uasi wake - ripoti
Wakati maasi ya Prigozhin yalionekana kuipata Kremlin kwa ghafla mashirika ya kijasusi ya Marekani yalikuwa tayari yamepata ishara kwamba alikuwa akipanga kuchukua hatua na yalikuwa yamemjulisha Rais Biden pamoja na viongozi wakuu wa bunge mapema wiki hii, vyombo vya habari vya Marekani viliripoti.
Habari za kijasusi za Marekani ziligundua kuwa kiongozi wa kundi la mamluki alikuwa akikusanya silaha, risasi na vifaa vingine karibu na mpaka na Urusi, CNN iliripoti.
Gazeti la New York Times linaripoti kuwa Rais Biden alizungumza na viongozi wa Ufaransa, Ujerumani na Uingereza kwa sababu ya wasiwasi kwamba udhibiti wa Putin wa silaha kubwa za nyuklia za Urusi ungeweza kumponyoka katikati ya machafuko hayo.
Wakuu wa kijasusi wa Marekani walikuwa wakifuatilia uhusiano unaozidi kuzorota kati ya Prigozhin na maafisa wa ulinzi wa Urusi kwa miezi kadhaa na ujasusi ulibaini kuwa ni ishara kwamba vita vya Ukraine vinakwenda vibaya kwa Wagner na wanajeshi wa kawaida, gazeti hilo linasema.
Unaweza pia kusoma
Ni nini kilitokea nchini Urusi?
Kwa wale wanaojiunga nasi, haya ndio mambo mambo muhimu ya ya kujua kuhusu kilichotokea Urusi:
- Rais wa Urusi Vladimir Putin amenusurika vitisho vya ghafla kwa mamlaka yake baada ya kiongozi wa kundi la mamluki la Wagner kukubali kukomesha uasi wake dhidi ya jeshi la Urusi.
- Yevgeny Prigozhin- pichani juu - alisitisha msafara wa wanajeshi wake wa Wagner kuelekea Moscow Jumamosi usiku baada ya mazungumzo na mshirika wa Putin na kiongozi wa Belarus Alexander Lukashenko.
- Pia alikubali kuondoka Urusi kuelekea Belarus, na Kremlin imesema haitafuata adhabu dhidi yake au wapiganaji wa Wagner.
- Mkataba huo unapunguza mzozo mkubwa wa usalama kwa Urusi
- Putin hata alionya kuhusu vita vya wenyewe kwa wenyewe siku ya Jumamosi katika hotuba yake ya kitaifa, akilaumu vitendo vya Prigozhin kama "usaliti" na "uhaini"
- Lakini kufikia Jumapili asubuhi,wanajeshi wa Wagner walikuwa wametoka nje ya Rostov-on-Don, Makao ya jeshi la kusini mwa nchi ambalo walikuwa wameiteka Jumamosi.
- Rais wa Ukraine Zelensky anasema uasi huo umefichua "machafuko kamili" nchini Urusi na kwamba "Viongozi wa Urusi hawadhibiti chochote"
- Viongozi wa Marekani, Uingereza na EU wanasema wanafuatilia kwa karibu hali hiyo
- Washington iliripotiwa kuarifiwa kuhusu mipango ya uasi mapema Jumatano, vyombo vya habari vya Marekani vinaripoti
Kwa nini mkuu wa Wagner alifanya uasi?
Mkuu wa Kundi la Wagner Yevgeny Prigozhin huenda alicheza kamari ili kupata waasi katika jeshi la Urusi, lakini alipandisha sana uwezo na ushawishi wake mwenyewe, Taasisi ya Uchunguzi wa Vita (ISW) inasema.
Wachambuzi wanaamini uasi ulioshindwa wa Prigozhin ulikuwa ni jitihada ya kuhifadhi uhuru wa jeshi lake la mamluki., haswa baada ya kupewa makataa ya wakuu wa jeshi la Urusi tarehe ya 1 Julai kuiweka Wagner chini ya udhibiti wao.
Makubaliano hayo yaliyosimamiwa na kiongozi wa Belarus Alexander Lukashenko yanampokonya Prigozhin udhibiti wa Kundi la Wagner katika hali yake ya sasa na badala yake kumfutia mashtaka ya jinai.
"Walakini, haijulikani ikiwa vikosi vya Wagner vitashirikiana kwa hiari katika ujumuishaji wao chini ya Wizara ya Ulinzi ya Urusi, au ikiwa jeshi la Urusi litahudumu kwa hiari pamoja na wafanyikazi wa Wagner Group katika siku zijazo," wanaandika.
Hatutamwona Putin akizungumza leo
Baada ya masaa 24 ya ghasia za uasi nchini Urusi, mzozo unaonekana kuisha.Eneo linalofuata la bosi wa kundi la Wagner Yevgeny Prigozhin linaripotiwa kuwa Belarus baada ya kufikiwa makubaliano na kiongozi wa nchi hiyo, Alexander Lukashenko.
Kuhusu Rais wa Urusi Vladimir Putin: Kweli, anaonekana kunusurika moja ya changamoto kubwa zaidi kwa utawala wake wa kimabavu katika miaka ya hivi karibuni.
Lakini watazamaji kadhaa wa Kremlin - nchini Urusi na nje ya nchi - wanasema Putin amejeruhiwa vibaya na mvutano wa hadharani na Prigozhin, ambaye wakati mmoja alikuwa mfuasi mwaminifu sana na hata alipewa jina la utani "mpishi wa Putin" kwa mikataba ya upishi aliyopewa na Moscow.
Na Putin sasa pia amepoteza uwezo wake wake wa kutumia nguvu: Hili lilionyeshwa wazi kabisa na Prigozhin alipochukua udhibiti wa maeneo ya kijeshi katika miji miwili mikubwa ya Urusi.
Siku ya Jumamosi asubuhi, Putin alitoa hotuba ya televisheni, akimshutumu Prigozhin kwa "usaliti" na uhaini.
Putin hajaonekana hadharani tangu wakati huo, na Jumamosi jioni msemaji wake Dmitry Peskov alisema hakuna hotuba mpya ya rais inayopangwa katika siku za usoni.
Unaweza pia kusoma
Tunajua nini kuhusu alichopata Prigozhin katika makubalino ya kumaliza uasi?
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Abdujalil Abdurasulov
- Nafasi, BBC News, Kyiv
Tunajua kuwa kama matokeo ya mazungumzo ambayo yalidumu kwa siku nzima, Yevegeny Prigozhin alikubali kupunguza mzozo wa uasi wake kufikia jana usiku.
Rais wa Belaras Aleksander Lukashenko - mshirika wa karibu wa Putin - ndiye aliyefanya mazungumzo na Prigozhin siku ya Jumamosi.
Kama sehemu ya mpango huo, Prigozhin ameruhusiwa kwenda Belarus na Kremlin imesema itaondoa mashtaka yote dhidi yake.
Mazungumzo hayo yalifanyika kwa makubaliano ya Putin, huduma ya vyombo vya habari ya Lukashenko ilisema.
Kama sehemu ya makubaliano, Kremlin ilikubali kufuta mashtaka dhidi ya kiongozi wa kundi la Wagner na pia kuwapa wapiganaji wa Wagner hakikisho la usalama.
Kingine kilichotolewa kwa Prigozhin na mamluki bado hakijulikani wazi.
Urusi imekuwa ikitumia eneo la Belarus kuanzisha mashambulizi dhidi ya Ukraine tangu mwanzo wa uvamizi huo, na hivyo kufuta mamlaka au uhuru wa Belarus.
Dalili zozote zinazoonyesha kudhoofika kwa Putin madarakani zilitishia utawala wa Lukasenko huko Minsk, ambao unategemea sana Moscow.
Belarus iko wapi haswa?
Makubaliano ya kumaliza uasi, kulingana na Kremlin, yatampeleka kiongozi wa Wagner Yevgeny Prigozhin nchini Belarus.
Mpango huo ulisimamiwa na kiongozi wa Belarus Alexander Lukashenko.
Belarus iko katikati mwa Ulaya na inapakana na Urusi, Ukraine, Poland, Lithuania na Latvia.
Lukasjenko ametawala kimabavu tangu 1994. Wapinzani wanakabiliwa na adhabu kali kwa kuandaa maandamano.
Mnamo 2005, Belarus iliorodheshwa na Marekani kama "nchi pekee ya dhuluma" barani Ulaya.
Katika miaka ya baada ya vita vya Soviet, Belarusi ikawa moja ya sehemu zilizofanikiwa zaidi za USSR, lakini baada ya uhuru uchumi ulidorora.
Inategemea sana Urusi kwa usambazaji wake wa nishati.
Unaweza pia kusoma
Je,huu ni wakati wa Putin kubadili mwelekeo?
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Steve Rosenberg
- Nafasi, Mhariri wa BBC Russia huko Moscow
Uasi wa Wagner umezua kipindi cha hali tofauti sana nchini Urusi , wakati hatari sana kwa Vladimir Putin.
Ukiwa madarakani kwa muda mrefu kiasi hicho unafikiri huwezi kushindwa, unaweza kustahimili chochote.
Miezi kumi na sita iliyopita, Putin alizindua "operesheni yake maalum ya kijeshi" huko Ukraine "kuifanya Urusi kuwa salama".
Lakini katika miezi ya hivi karibuni kumekuwa na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwenye Kremlin na makombora katika eneo la Magharibi mwa Urusi.
Na sasa: uasi wa silaha wa mamluki ambao walikuwa wakienda Moscow, wakitaka kuondolewa kwa waziri wa ulinzi aliyeteuliwa na Vladimir Putin, kabla ya kuamua kujiondoa.Je,hatua hizi zote zinamaanisha nini kwa mustakabali wa Urusi na rais wake Vladmir Putin.Baada ya matukio hayo ya Wagner ,Putin yuko salama au ana hakikisho la nguvu zake katika Urusi?
Nguvu na mamlaka ya Putin
Ilikuwa ni saa 24 za kushangaza ambapo Vladimir Putin alikabiliwa na changamoto kubwa zaidi kwa mamlaka yake tangu aingie madarakani zaidi ya miongo miwili iliyopita.
Uasi umekwisha - baada ya makubaliano kati ya Kremlin na kundi la mamluki la Wagner.Wapiganaji wa Wagner wanaweza kurudi kwenye kambi zao na hawatashtakiwa, lakini kiongozi wao Yevgeny Prigozhin lazima aondoke Urusi na kuhamia Belarus.
Kuhusu Rais Putin, hatoki katika matukio haya akionekana kuwa na nguvu.
Angalia kile kilichotokea huko Rostov - Wagner, jeshi la kibinafsi, liliweza kuchukua udhibiti wa vifaa vya kijeshi katika mojawapo ya miji mikubwa ya Urusi kwa urahisi, kisha kuanza safari kaskazini kuelekea Moscow.
Na aliyehusika na uasi, Prigozhin,yuko huru.Licha ya ukweli kwamba alijaribu kupindua uongozi wa kijeshi wa Urusi, shtaka dhidi yake la uasi wa kutumia silaha limefutwa.
Unaweza pia kusoma
Saa 24 za jaribio la uasi Urusi
Kwa usiku mmoja mrefu wa Juni , kiongozi wa mamluki wa Urusi Yevgeny Prigozhin alianzisha uasi, na kutuma msafara wa kivita kuelekea Moscow na kuibua maswali juu ya mamlaka na nguvu za Vladimir Putin madarakani.
Lakini mwisho wa Jumamosi, Prigozhin alikuwa amebadilisha mwelekeo huo kuwaamuru wapiganaji wake kurejea kambini .
Kwa miezi kadhaa amekuwa akitekeleza jukumu muhimu katika kampeni ya kijeshi ya Urusi nchini Ukraine, akiandikisha maelfu ya watu kwa kundi lake la mamluki la Wagner, haswa kutoka jela za Urusi.
Kwa muda mrefu amekuwa katika mzozo wa hadharani na wakuu wa kijeshi wanaoendesha vita, lakini hilo liligeuka kuwa uasi wa wazi walipokuwa wakitafuta kuweka majeshi yake chini udhibiti wao ifikapo tarehe 1 Julai.
Prigozhin alisisitiza haya yalikuwa "maandamano ya haki", sio mapinduzi.Vyovyote ilivyokuwa, yaliisha haraka sana.
Saa ishirini na nne za ghasia, na mengi sana ambayo hatujui.
Huu ni muhtasari wa matukio hayo:
Katika muda wa siku moja tu, matukio yaliongezeka na kisha yakapungua haraka kama mamluki wa Wagner walipoanzisha uasi na kisha kuukomesha haraka.
Ijumaa
- Bosi wa Wagner Yevgeny Prigozhin atoa cheche za maneno ya kumlaumu Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu kwa vita vya Ukraine, akidai alifanya hivyo ili kupata heshima ya kijeshi.
- Prigozhin baadaye aliapa "kuandamana kwa ajili ya haki" na kuishutumu Kremlin kwa kuwashambulia wanajeshi wake kwa shambulio la kombora siku ya Ijumaa.
- Usalama uliimarishwa mjini Moscow siku ya Ijumaa baada ya Prigozhin kutoa wito wa uasi wa kutumia silaha
Jumamosi
- Prigozhin atangaza wanajeshi wake 25,000 wamevuka mpaka kutoka Ukraine mapema asubuhi.
- Meya wa Moscow atangaza hatua za kupambana na ugaidi zinachukuliwa ili kuimarisha usalama na huko Rostov-on-Don, karibu na mpaka wa Ukraine, wakaazi wanaambiwa kukaa ndani.
- Muda mfupi kabla ya 06:00 BST video inaonekana mtandaoni inayoonyesha Prigozhin ndani ya makao makuu ya kijeshi ya kusini mwa Urusi.
- Rais wa Urusi Vladimir Putin anashutumu "matukio ya uhalifu" na kuonya juu ya adhabu katika hotuba ya TV karibu 08:00.
- Kwa muda wa siku hiyo, vikosi vya Wagner vinasonga mbele kwenye barabara ya M4 kuelekea Moscow, pamoja na kukamata vifaa vya kijeshi huko Voronezh.
- Kabla ya 18:30, Prigozhin anasema kwenye chaneli yake ya Telegraph kwamba amekubali "kusimamisha" harakati za wanajeshi wake.
- Belarus inaonyesha kiongozi wake, Alexander Lukashenko, alikuwa akifanya mazungumzo na Prigozhin na Putin alikubali mazungumzo hayo.
- Karibu 21:00 vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vinaripoti kwamba Prigozhin ataondoka kwenda Belarusi, na kwamba mashtaka ya uhalifu dhidi yake na askari wake yatafutwa.
Unaweza pia kusoma
Mkuu wa Wagner kuhamia Belarus baada ya kuachana na uasi
Na tunaanzia huko nchini Urusi ambapo matukio mengi yamefanyika ndani ya saa 24 zilizopita tangu kiongozi wa Wagner Yevgeny Prigozhin kuitisha uasi dhidi ya jeshi la Urusi na kisha baadaye kusitisha harakati zake kuelekea Moscow.
Mkuu wa kundi la mamluki la Wagner amepigwa picha na shirika la habari la Reuters akiondoka katika mji wa Rostov-on-Don, ambao wapiganaji wake waliudhibiti mapema jana.
Yevgeny Prigozhin alikuwa akiendesha gari kutoka makao makuu ya jeshi ya wilaya jijini, shirika hilo linasema.
Kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya Urusi, Progozhin ataondoka Urusi kuelekea Belarus na mashtaka yote dhidi yake na vikosi vyake vya Wagner yatafutwa na mamlaka ili kuepusha "umwagaji damu".
Yevgeny Prigozhin na askari wake hawatashtakiwa, inasema Kremlin. Wapiganaji wa Wagner wameripotiwa kuanza kuondoka katika mji wa kusini wa Rostov-on-Don ambako uasi wao ulianza. Prigozhin alitoa wito wa uasi dhidi ya jeshi la Urusi - na vikosi vyake vilikamata Rostov, kituo kikuu cha kijeshi.
Wenyeji wa Rostov wawashangilia kuunga mkono wapiganaji wa Wagner
Wakati wapiganaji wa Wagner wakiondoka katika makao makuu ya kijeshi huko Rostov-on-Don, wakazi wa jiji hilo wamekuwa wakiimba "Wagner! Wagner!" katika onyesho dhahiri la kuunga mkono mamluki.
Usiku ulipoingia, watu kadhaa wa eneo hilo walikusanyika kuwaonyesha wapiganaji hao uungwaji mkono kulingana na picha kutoka jiji hilo.
Haijabainika iwapo walikuwa wakionyesha kuunga mkono hatua za wapiganaji hao nchini Ukraine au uasi uliozuiliwa.
Je, huu ndio mwisho wa Prigozhin na Wagner?
Yevgeny Prigozhin kuhamia Belarus na wapiganaji wa Wagner kuingizwa katika jeshi la Urusi kunaweza kumaanisha mwisho kundi hilo la mamluki, mtaalam ameiambia BBC.
Andrew D'Anieri, kutoka taasisi ya wataalam ya Baraza la Atlantiki yenye makao yake nchini Marekani, anasema ni vigumu kusema nini hasa kitakachotokea, kutokana na hali ya mkanganyiko na isiyoeleweka ya taarifa zinazotoka Urusi.
Lakini pia anasema kuanguka kwa kwa Wagner haimaanishi kwamba makampuni yote ya kijeshi ya kibinafsi nchini Urusi "yako nje pia".
"Ingawa kiufundi ni kinyume cha sheria nchini Urusi, tumeona ongezeko la makundi hayo katika kipindi cha miezi 12 hivi."
D'Anieri anasema imekuwa wazi katika siku ya mwisho "ni kiasi gani kundi la kufanya maamuzi ni ndogo huko Moscow" na jinsi mamlaka ya Vladimir Putin ni dhaifu.
‘Ikiwa uliwafuata waenezaji wa propaganda wa Kremlin kwa karibu ... kulikuwa na ukimya mwingi na bila kujua la kufanya, kwa sababu kwa kweli hapakutolewa uamuzi uliofanywa kuhusu jinsi ya kujibu."
Unaweza pia kusoma
Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja leo Jumapili tarehe 25 Juni 2023.