Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Urusi yazuia mashambulizi ya Ukraine kwenye mpaka wake- wizara ya ulinzi

Makombora yaliyorushwa katika eneo la Belgorod nchini Urusi yawajeruhi watu wanane huku mashambulio mjini Kyiv yakiwaua watu watatu, maafisa wanasema.

Moja kwa moja

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Hadi kesho kwaheri.

  2. Mzozo wa Sudan: Marekani yawekea vikwazo kampuni nne za Sudan na watu kadhaa

    Marekani imetangaza vikwazo dhidi ya makampuni manne ya Sudan na watu kadhaa kwa kuchochea vita kati ya vikosi vya kijeshi vinavyohasimiana.

    Haya yanajiri huku mazungumzo kati ya wawakilishi wa jeshi na Vikosi Maalum vy akijeshi yakivunjika.

    Siku ya Jumatano takriban raia kumi na wanane waliuawa wakati makundi hasimu yalipokabiliana katika mji mkuu Khartoum.

    Wizara ya Fedha ya Marekani inasema vikwazo hivyo vipya vitakatiza ufadhili muhimu kwa pande hizo mbili zinazopigana vita nchini Sudan.

    Kampuni zilizoorodheshwa ni pamoja na ile inayomiliki migodi ya dhahabu na inadhibitiwa na mkuu wa Rapid Support Forces - Jenerali Dagalo au Hemedti.

    Pia kuna mtengenezaji wa silaha wa mabilioni ya dola ambayo hutoa jeshi.

    Lakini wachunguzi wengi wanatilia shaka ikiwa vikwazo hivyo vya Marekani vitaleta mabadiliko yoyote.

    Sudan imekabiliwa na miaka kadhaa ya vikwazo vilivyowekwa na Marekani hapo awali.

    Jambo la kuogofya ni kwamba hakuna anayeonekana kujua jinsi ya kusimamisha vita hivyo ambavyo siku ya Jumatano vilisasababisha vifo vya raia 18 wakati pande hizo mbili zikipigana huko kusini mwa Khartoum.

    Maelezo zaidi:

  3. Kosovo: Nato tayari kupeleka wanajeshi zaidi baada ya machafuko

    Nato inasema iko tayari kupeleka wanajeshi zaidi Kosovo baada ya machafuko kuzuka kufuatia uteuzi wa mameya wa kabila la Albania katika maeneo ya Waserbia walio wengi.

    Pristina na Belgrade wamelaumiana kwa machafuko hayo, huku kiongozi wa Serbia Aleksandar Vucic akitoa wito wa kuondolewa kwa mameya.

    Marekani pia imekosoa ufungaji wao, ambao ulikuja baada ya wakazi wa Serb kususia uchaguzi wa ndani. Kosovo ilijitangazia uhuru mwaka 2008 lakini Serbia haitambui.

    Nato tayari imetuma vikosi 700 vya kuimarisha Kosovo lakini mkuu wa Nato Jens Stoltenberg alisema vikosi zaidi huenda vikahitajika.Muungano huo tayari una wanajeshi 4,000 huko.

    Mameya hao walichaguliwa baada ya Waserbia kaskazini mwa Kosovo kususia uchaguzi wa serikali za mitaa, na hivyo kudidimiza idadi ya waliojitokeza kufikia takriban 3% na kusababisha wagombea wa kabila la Albania kuchaguliwa. Waandamanaji wa Serb kisha walijaribu kuwazuia kuchukua nyadhifa zao.

    Baadhi ya walinda amani 30 wa Nato na zaidi ya waandamanaji 50 wa Serb walijeruhiwa katika mapigano yaliyofuata. Akizungumza kando ya mkutano wa kilele wa Ulaya mjini Moldova, Bw Vucic alisema kuwaondoa mameya hao itakuwa njia "yenye nguvu zaidi" ya kutuliza mivutano

    Alisisitiza kuwa nchi yake "itajaribu kuwashawishi Waserbia kuandamana kwa utulivu na amani".

    Lakini katika hafla hiyo hiyo Rais wa Kosovan Vjosa Osmani aliilaumu Belgrade kwa ghasia za hivi majuzi, akiishutumu kwa "kuunga mkono magenge ya wahalifu" nchini humo.

    Serbia "inahitaji kukubaliana na siku zake za nyuma", alisema, akiongeza kuwa "tishio halisi kwa kweli linatokana na kukataa kwa Serbia kuwepo kwa taifa huru".

    Marekani, ambayo iliunga mkono uhuru wa Kosovo kutoka kwa Serbia, ilikosoa uamuzi wa Kosovo wa kuwaweka mameya wa kabila la Albania kaskazini mwa Kosovo "kwa njia za kulazimishwa" na kuwafukuza Kosovo kushiriki katika mazoezi ya kijeshi yanayoendelea kuongozwa na Marekani barani Ulaya.

    Mshirika wa Serbia Urusi imetaka haki za Waserbia wa kabila huko Kosovo kuheshimiwa.

  4. Afrika Kusini yafikiria hatua za kuchukua iwapo Putin atahudhuria mkutano wa Brics

    Afrika Kusini bado inazingatia chaguzi zake za kisheria ikiwa Rais wa Urusi Vladimir Putin ataamua kuhudhuria mkutano wa Brics mwezi Agosti, Waziri wa Mambo ya Nje Naledi Pandor amesema, shirika la habari la Reuters linaripoti.

    Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imetoa hati ya kukamatwa kwa Bw Putin kutokana na vita vya Ukraine, na kuiweka Afrika Kusini katika hali ya mkanganyiko inapojiandaa kuandaa mkutano wa kilele wa viongozi wanaounda Brics.

    "Serikali yetu kwa sasa inaangalia chaguzi za kisheria ni zipi kuhusiana na suala hili na nimeonesha ... kwamba ni jambo ambalo rais atakuwa [mtu] bora kuzungumza kuhusu hilo mara tu itakapofikia hitimisho,"

    Reuters inamnukuu Bi Pandor akisema kando ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Brics mjini Cape Town. Shirika hilo la habari pia linamnukuu afisa mmoja ambaye hakutajwa jina akisema kuwa chaguo moja la kupata mvuto miongoni mwa maafisa wa Afrika Kusini ni kuiomba China kuwa mwenyeji wa mkutano huo.

    Shirika la habari la Bloomberg lina ripoti sawa na hiyo, likinukuu vyanzo ambavyo havikutajwa vikisema kwamba Afrika Kusini inafikiria kuomba nchi nyingine, China au nchi jirani ya Msumbiji - kuwa mwenyeji wa mkutano huo. Hata hivyo, msemaji wa Bi Pandor, Lunga Ngqengelele alisema kwamba "kama tunavyofahamu, tumetangaza eneo la mkutano Gauteng, Afrika Kusini", Bloomberg inaripoti. "Hilo ndilo tunalojua kufikia leo," Bw Ngqengelele alisema. Brics inaundwa na Brazil, Urusi, China, India na Afrika Kusini.

    Unaweza kusoma;

  5. Urusi yazuia mashambulizi ya Ukraine kwenye mpaka wake- wizara ya ulinzi

    Mkoa wa Belgorod nchini Urusi umeshambuliwa tena kutoka katika mpaka wa Ukraine, huku takriban watu wanane wakiripotiwa kujeruhiwa kwa kushambuliwa kwa makombora.

    Wizara ya ulinzi ya Urusi inasema imezuia majaribio kadhaa ya vikosi vya Ukraine kuvuka mpaka wake.

    Moscow ilisema ilizuia jaribio la wanajeshi wa Ukraine "kuvamia" eneo lake la kusini magharibi mwa Belgorod, ambalo linapakana na Ukraine.

    Wizara ya ulinzi ilisema ilitumia ndege na mizinga kuzuwia mashambulizi na kuzuia wanajeshi wa Ukraine kuvuka na kuingia Urusi.

    Hapo awali, mamlaka za kikanda zilisema kuwa watu wanane walijeruhiwa katika shambulio dhidi ya eneo la Belgorod lililohusishwa naa wanajeshi wa Ukraine.

    Kyiv bado hajatoa tamko lolote kuhusiana na madai hayo.

    Ikulu ya Kremlin tangu wakati huo imelaani kile kinachosemekana ni ukimya wa jumuiya ya kimataifa kufuatia tukio hilo.

    Maelezo zaidi:

  6. Kiongozi wa Eritrea aitaka Urusi kuchukua jukumu la kihistoria

    Rais wa Eritrea Isaias Afwerki ameitaka Urusi kutekeleza "jukumu lake la kihistoria" la kukuza amani na haki duniani, tovuti ya Wizara ya Habari ya Eritrea, Shabait, imeripoti.

    Bw Isaias alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano na Rais Vladimir Putin mjini Moscow siku ya Jumatano.

    Eritrea ni miongoni mwa nchi chache zinazopinga azimio la Umoja wa Mataifa la kulaani Urusi kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine.

    Ziara yake ya siku nne nchini Urusi inafuatia wiki moja baada ya ziara kama hiyo nchini China, ambapo alifanya mazungumzo na Rais Xi Jinping na maafisa wengine wakuu wa serikali.

    Eritrea ni nchi ya chama kimoja ambapo Bw Isaias amekuwa mamlakani tangu uhuru kutoka kwa Ethiopia mwaka wa 1993.

    • Pia unaweza kusoma:
    • Ni kwanini uvamizi wa Urusi nchini Ukraine bado unaigawanya Afrika?
    • Kwa nini Urusi inalisaidia jeshi la Somalia?
    • Jinsi Urusi inavyochukua nafasi ya Ufaransa katika makoloni yake ya zamani ya Kiafrika
  7. Amazon kulipa $25m kutokana na ukiukaji wa faragha ya watoto

    Amazon italipa $25m (£20m) baada ya madai kwamba ilikiuka haki za faragha za watoto na msaidizi wake wa sauti wa Alexa. Kampuni hiyo ilikubali kuilipa Tume ya Biashara ya Marekani (FTC) baada ya kushutumiwa kwa kushindwa kufuta rekodi za Alexa kwa ombi la wazazi.

    Ilibainika kuwa imehifadhi data nyeti kwa miaka.

    Kitengo cha kamera ya kengele ya mlango ya Amazon pia kitalipa baada ya kuwapa wafanyakazi ufikiaji usio na kikomo wa data ya wateja.

    Kulingana na malalamiko ya FTC kuhusu Alexa, Amazon "iliwahakikishia watumiaji wake mara kwa mara na mara kwa mara kwamba wanaweza kufuta rekodi za sauti zilizokusanywa" na mfumo.

    Lakini kampuni haikufanya hivi, ikiweka data kwa miaka na kuitumia kinyume cha sheria kusaidia kuboresha algorithm yake ya Alexa, nyaraka za malalamiko zilieleza. Katika taarifa, Samuel Levine, Mkurugenzi wa Ofisi ya FTC ya Ulinzi wa Watumiaji, alishutumu Amazon kwa "kupotosha wazazi, kuweka rekodi za watoto kwa muda usiojulikana, na kukiuka maombi ya wazazi kufuta".

    Kampuni hiyo "ilitumia faragha kwa faida", aliongeza. Vile vile, FTC ilisema Amazon iliruhusu "maelfu ya wafanyakazi na wakandarasi" kutazama rekodi za binafsi za wateja. Waliweza kutazama na kupakua data nyeti ya video ya wateja kwa madhumuni yao wenyewe, shirika hilo lilisema.

    Amazon aliiambia BBC katika taarifa yake kwamba ilishughulikia mara moja masuala yaliyokuwepo miaka yake iliyopita, kabla ya FTC kuanza uchunguzi wake". Lakini kulingana na malalamiko hayo, mfanyakazi mmoja alitazama maelfu ya rekodi za video za watumiaji wa kike wa kamera za Ring ambazo "zilichunguza nafasi za karibu katika nyumba zao kama vile bafu au vyumba vyao vya kulala".

    Mfanyikazi huyo alisimamishwa mara tu matendo yao yalipoonekana na mfanyakazi mwenza, ilisema Amazon.

  8. Zimbabwe yapitisha mswada wa kuadhibu 'vitendo visivyo vya kizalendo'

    Bunge la Zimbabwe limepiga kura kuunga mkono mswada wenye utata wa kuwaadhibu raia kwa "vitendo visivyo vya kizalendo", ikiwa ni pamoja na kuwatoza faini kubwa au hata adhabu ya kifo.

    Wakosoaji wametaja hatua hiyo kama pigo kwa demokrasia.

    Mswada huo unaojulikana kama kifungu cha uzalendo cha Sheria ya Jinai kinalenga wale wanaodhuru "maslahi ya kitaifa ya Zimbabwe".

    Inajumuisha raia yeyote anayekutana na mwakilishi wa nchi ya kigeni kwa lengo la kuhimiza vikwazo dhidi ya Zimbabwe au kupindua serikali.

    Maafisa wengi waandamizi wa serikali na makampuni yanayomilikiwa na serikali wako chini ya vikwazo vya Magharibi kwa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu,

    Kwa muda mrefu wamelaumu upinzani kwa hili na wanataka kusitisha mikutano kati ya upinzani na maafisa wa kigeni.

    Bunge lilipiga kura 99 kwa 17 kuunga mkono sheria hiyo - mojawapo ya utata mkubwa wa urais wa Emmerson Mnangagwa.

    Sasa muswada huo utawasilishwa katika bunge la seneti kabla ya kutiwa saini kuwa sheria.

    Wakosoaji wanasema sheria hiyo ni kinyume na katiba kwa vile itakiuka uhuru wa kujumuika na haki ya kujieleza.

    Afisa wa upinzani aliambia BBC kwamba njia ya kukomesha vikwazo ni kuzingatia haki za binadamu, na sio kuharamisha ukosoaji.

    Mabadiliko hayo yenye utata yalipitishwa kama sehemu ya mfululizo wa marekebisho ya Sheria ya Jinai.

    Wabunge pia walipiga kura kuunga mkono hukumu za kima cha chini kwa ubakaji.

  9. Je, ni msikiti gani huu wa kale ambao Waislamu wa China wanapinga usibomolewe?

    Waandamanaji na polisi wa China wamekabiliana katika mji wenye Waislamu wengi katika jimbo la Yunnan, wakipinga kubomolewa kwa msikiti mmoja.

    Video iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha watu wengi wakiwa wamekusanyika katika Msikiti wa karne ya 13 huko Nagyong katika mji wa Nago.

    Mapigano haya yalikuwa kati ya polisi na wakaazi wa eneo hilo, ambao walikuwa wamezingirwa na mamia ya vikosi vya jeshi.

    Yunnan ni mkoa wa tamaduni nyingi ulio kusini mwa Uchina wenye idadi kubwa ya Waislamu.

    China haina dini yake na serikali inasema inatambua uhuru wa kuabudu, lakini watu wanaofuatilia mambo ya nchi hiyo wanasema kuwa uwindaji wa kidini wa jeshi umeongezeka katika miaka ya hivi karibuni na kwamba serikali ya Beijing inajaribu kuwawekea madaraka watu hao.

    Msikiti wa Nagyong huko Nago unaonekana kuwa wa zamani. Minara ya msikiti huo ilijengwa mara kadhaa baada ya upanuzi wa msikiti huo.

    Lakini mnamo mwaka 2020, uamuzi wa mahakama ulitangaza upanuzi wa Msikiti kuwa haramu na kuamuru mnara huo uvunjwe.

    Hatua hizi za kutekeleza agizo hili zinaonekana kusababisha maandamano haya.

  10. Shambulio la roketi laua watu 17 katika soko la Sudan - madaktari

    Takriban watu 17 waliuawa na wengine 106 kujeruhiwa Jumatano baada ya roketi kugonga soko kusini mwa mji mkuu Khartoum, muungano wa madaktari wa Sudan ulisema.

    Hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya watu waliouawa kwa kushambuliwa kwa makombora katika mji mkuu tangu mapigano kati ya jeshi la Sudan na Kikosi Maalum cha RSF kuanza tarehe 15 Aprili.

    Shambulio hilo limekuja huku mazungumzo yaliyokuwa yakisimamiwa na Marekani na Saudi Arabia kumaliza mzozo huo yakiporomoka.

    "Eneo la Mayo [Soko la 6] lilishuhudia mashambulizi makali na ya umwagaji damu mchana huu, ambayo yalisababisha vifo vya watu 17 na zaidi ya 106 kujeruhiwa," Muungano wa Madaktari wa Sudan ulisema katika chapisho kwenye ukurasa wake wa Facebook.

    Inafikisha 883 idadi ya vifo vya raia katika vita hivyo kufikia sasa.

    Maelezo zaidi:

  11. Hakuna mtu atakayetuyumbisha kuhusu sheria dhidi ya mapenzi ya jinsi moja - Museveni

    Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameelea kuhusu upinzani wa jumuiya ya kimataifa dhidi ya sheria ya kupinga mapenzi ya jinsi moja aliyoitia saini wiki hii.

    Bw Museveni alisisitiza kuwa kutiwa saini kwa sheria hiyo ni makubaliano yaliyokamilika, na kukaidi wito wa kutaka ibatilishwe.

    "Utiaji saini wa Muswada wa Kupinga mapenzi ya jinsi moja umekamilika, hakuna mtu atakabadilisha hatua yetu. Tunapaswa kuwa tayari kwa vita," alisema katika taarifa yake baada ya mkutano na wanachama wa chama chake cha National Resistance Movement (NRM).

    "NRM haijawahi kuwa na lugha mbili, tunachokuambia mchana ndicho tutakuambia usiku," aliongeza.

    Hii inakuja huku kukiwa na shutuma kutoka kwa mataifa ya Magharibi na makundi ya haki za binadamu.

    Rais wa Marekani Joe Biden aliikosoa sheria hiyo kama "ukiukaji wa kutisha wa haki za binadamu kwa wote" na akatoa wito ifutwe, akiongeza kuwa Marekani inazingatia vikwazo.

    Umoja wa Ulaya na mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia wamelaani sheria hiyo.

    Sheria hiyo ilitiwa saini baada ya bunge kuipuuza - lakini bado ni miongoni mwa sheria kali zaidi za kupinga LGBTQ duniani.

    Yeyote anayepatikana na hatia ya tendo la ngono ya wapenzi wa jinsi moja anakabiliwa na kifungo cha maisha.

    Sheria pia inatoa hukumu ya kifo kwa "kesi zilizokithiri", ambazo ni pamoja na ubakaji wa mtu aliye na umri wa chini ya miaka 18, au pale ambapo mtu ameambukizwa ugonjwa wa maisha usiopona ikiwa ni pamoja na VVU-UKIMWI.

    Unaweza pia kusoma:

    • Je, sheria ya udhibiti wa mapenzi ya jinsia moja Uganda imepokewaje?
    • Utafungwa maisha gerezani kwa kusema unashiriki mapenzi ya jinsia moja Uganda
  12. Rais Tschisekedi akubali kuongeza muda wa uwepo wa vikosi vya Afrika Mashariki ndani ya DRC

    Wakuu wa nchizaAfrika Mashariki wanaokutana mjini Bujumbura wamesema rais wa DR Congo amekubali kuongeza muda wa vikosi vya umoja huo nchini DRCongo hadi mwezi Septemba.

    Akiwa Botswana mwezi uliopita, Rais wa DR Congo,Felix Tshisekedi alisema vikosi vya Afrika Mashariki vitaondoka nchini humo "ikiwa hawataonyesha matokeo mazuri"kufikia mwisho wa muhula wao leo Juni 1.

    Vikosi vinavyoongozwa na Kenya vilipelekwa katika maeneo ambayo waasi wa M23 walikuwa wakiondoka wakati wakuu wa majimbo wakiendelea na juhudi za amani.

    Viongozi wa DR Congo wanalalamika kuwa vikosi hivyo havikuhusika katika kupambana na waasi.

    Mkutano huo uliofanyika mjini Bujumbura siku ya Jumatano ulisisitiza kuwa ukosefu wa usalama mashariki mwa Congo "unaweza kutatuliwa kwa njia endelevu kupitia mchakato wa amani ya kisiasa na mazungumzo kati ya pande zote".

    Kumekuwa na usitishaji mapigano na utulivu tangu mwezi Machi wakati waasi wa M23 walipokubali kuondoka katika maeneo waliyoyateka ili kukaliwa na vikosi vya kikanda.

    Zaidi ya raia laki tano wameyakimbia makaazi yao katika mkoa wa Kivu Kaskazini kutokana na mapigano kati ya waasi wa M23 na jeshi la DR Congo.

    DR Congo inaituhumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi la M23, jambo ambalo Rwanda imekuwa ikilikanusha mara kwa mara.

    Unaweza pia kusoma:

    • Jumuiya ya Afrika Mashariki, majeshi na mustakabali wa amani DRC
    • Mzozo wa DRC: Je inawezekana kuyamaliza makundi ya wapiganaji Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo?
  13. Wakenya yasherehekea Siku ya Madaraka, huku wakikumbwa na hali ngumu ya uchumi

    Raia wa Kenya wanasherehekea Siku ya Madaraka kuadhimisha miaka 60 tangu waasisi wa taifa hilo walipokabidhiwa madaraka kutoka kwa mkoloni na kuunda Serikali ya kwanza ya Kenya.

    Hatahivyo siku hii inaadhimishwa huku raia wa nchi hiyo wakikumbwa na hali ngumu ya kiuchumi inayotokana na mfumuko mkubwa wa bidhaa muhimu kama vile chakula la mafuta.

    Raia pia wamelalamikia pendekezo la rais wa nchi hiyo William Ruto ya kukatwa kwa mishahara ya wafanyakazi nchini humo kwa 3%, ili kufanikisha utekelezaji wa sera ya serikali ya ujenzi wa makazi kwa raia wenye kipato cha chini.

    Hatahivyo baadhi ya Wakenya wana matumaini ya kuboreka kwa hali ya uchumi.

    Sherehe za kitaifa za Madaraka Day zinafanyika katika Kaunti ya Embu nchini humo, ambako rais William Ruto anatarajiwa kutoa hotuba maalum ya siku hii, huku Wakenya wakisubiri ni nini atakalosema kuhusiana na kupanda kwa gharama ya maisha.

  14. Mpango wa ukomo wa deni: Bunge la Marekani lapitisha muswada kwa wingi wa kura

    Baraza la Wawakilishi limeidhinisha makubaliano ya kuruhusu Marekani kukopa pesa zaidi, siku chache kabla ya nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi duniani kuanza kushindwa kulipa deni lake.

    Bunge lilipitisha muswada huo kwa kura 314-117, licha ya kuwa na kasoro kadhaa.

    Bunge la Seneti la Marekani lazima liupigie kura mswada huo baadaye wiki hii kabla ya Rais Joe Biden kuutia saini kuwa sheria.

    Serikali inatarajia kufikia kikomo chake cha kukopa Jumatatu tarehe 5 Juni.

    Hilo limeacha kiasi kidogo cha makosa huku wabunge wakifanya hima kuepuka Marekani kutolipa deni lake la $31.4tn (£25tn), ambalo ndilo msingi wa mfumo wa kifedha duniani.

    Siku ya Jumatano jioni, Wademocrats 165 walijiunga na Warepublican 149 katika kuidhinisha mswada huo wa kurasa 99 ili kuongeza kiwango cha deni, na kuruhusu Bunge kuupitisha kwa kura nyingi zinazohitajika.

    Huku Warepublican wakidhibiti baraza la chini la Congress na Democrats wakishikilia mamlaka katika Bunge la Seneti na Ikulu ya White House, makubaliano yalikuwa yamethibitika kuwa magumu kwa wiki kadhaa hadi Rais Biden na Spika wa Bunge Kevin McCarthy walipoweka saini makubaliano ya muafaka wa pande mbili mwishoni mwa juma.

  15. Argentina yaruhusu ununuzi wa vidonge vya dharura vya kuzuia mimba kwenye maduka ya madawa

    Wanawake nchini Argentina sasa hawatahitaji tena umaagizo kuhusu matumizi ya uzazi wa mpango wa dharura.

    Serikali ilisema kufanya kidonge cha dharura cha kuzuia mimba kinachofahamika kama - kidonge cha asubuhi (morning-after pill) kwa urahisi zaidi kumeondoa "kizuizi muhimu" kwa wale wanaotaka kuahirisha kupata mimba.

    Hatua hiyo imepokelewa vyema na makundi ya watetezi wa haki za wanawake, ambao wanaona kuwa ni ishara ya maendeleo katika nchi hiyo yenye Wakatoliki wengi.

    Hata hivyo wakosoaji walisema hatua hiyo imeonyesha "kushindwa kuzuia mimba".

    Kundi la Argentina linalounga mkono maisha, DerguiXlaVida, limeitaja hatua hiyo kuwa ya wasiwasi, na kuishutumu serikali kuwa "kimsingi inajielekeza katika kukuza utoaji mimba".

    Ilisema hatua hiyo inaonesha "kushindwa kwa serikali katika uzuiaji wa mimba [na] elimu ya ngono".

    Mnamo 2020, nchi hiyo ilihalalisha utaoaji mimba hadi wiki ya 14 ya ujauzito, hatua iliyopingwa na Kanisa, ambalo lilikuwa limewataka maseneta kuukataa mswada huo.

    Utoaji mimba hapo awali uliruhusiwa tu katika matukio ya ubakaji au wakati afya ya mama inapokuwa hatarini.

    Vidonge vya dharura vya kuzuia mimba - vinavyojulikana kama vidonge vya asubuhi – vinavyomezwa ndani ya saa 120 baada ya kujamiiana bila kinga huzuia mimba kwa kuzuia utungishaji wa yai, kulingana na Shirika la afya Duniani (WHO), ingawa ni bora kumezwa ndani ya saa 12 baada ya kujamiiana.

  16. Vita vya Ukraine: Marekani kutoa msaada wa ziada wa mifumo ya ulinzi wa anga kwa Ukraine

    Marekani inaipatia Ukraine msaada mpya wa kijeshi wenye thamani ya dola milioni 300 utakaojumuisha makombora ya mifumo ya Patriot, Stinger MANPADS na mifumo ya ulinzi ya anga ya Avenger, msemaji wa Ikulu ya White House John Kirby alisema.

    Kama sehemu ya msaada huu, Marekani itaipatia Ukraine makombora ya anga hadi angani yanayoongozwa na rada ya AIM-7 kwa mara ya kwanza.

    Msaada huu pia utajumuisha risasi za drone, ambazo afisa huyo wa Marekani alisema ni risasi kama chokaa ambazo zinaweza kurushwa kutoka kwa ndege zisizo na rubani.

    Kirby alibainisha kuwa huu ni mfuko wa 39 wa msaada kwa Ukraine ulioidhinishwa na utawala wa sasa wa Marekani.

    Hadi sasa, Marekani imetoa zaidi ya dola bilioni 37.6 kama msaada wa kijeshi kwa Ukraine tangu kuanza kwa uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine.

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  17. Sevilla yailaza Roma kwa mikwaju ya penalti kushinda kombe la Yuropa

    Sevilla wameshinda taji la saba la Ligi ya Yuropa lililoongeza rekodiyao kwa kuwashinda Roma kwa mikwaju ya penalti kwenye Uwanja wa Puskas Arena mjini Budapest.

    Gonzalo Montiel, ambaye pia alifunga penalti ya ushindi kwa Argentina katika fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Ufaransa, alirudia hila kwa timu hiyo ya Uhispania kufuatia sare ya 1-1, na mkwaju uliorudiwa baada ya Roger Ibanez na Gianluca Mancini kukosa kwa Roma.

    Timu hiyo ya Uhispania, sasa imeshinda fainali zote saba walizocheza katika shindano hilo huku nahodha Jesus Navas akishiriki katika ushindi wao wa kwanza dhidi ya Middlesbrough mnamo 2006.

    Hatua hii inawafanya kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa msimu ujao licha ya kumaliza nje ya nne bora kwenye La Liga.

    Kutakuwa na hisia kwamba inaweza kuwa tofauti sana kwa Roma na meneja wao Jose Mourinho, ambaye alikuwa ameshinda fainali zote tano za awali za Uropa alizoshiriki na kuiongoza klabu hiyo kuzindua mafanikio ya Ligi ya Europa Conference msimu uliopita.

    Mchezaji wake wa kimataifa wa Montiel, Paulo Dybala aliiweka Roma mbele katika kipindi cha kwanza, akikimbilia pasi ya mlinzi wa Italia Mancini na kuelekeza kwa ustadi kazi ndogo iliyompita kipa wa Sevilla, Yassine Bounou hadi kona ya chini kulia.

    Hata hivyo, timu hiyo ya Serie A, ambayo pia ilimwona Leonardo Spinazzola akimjaribu Bounou kabla ya mapumziko, iliachana na udhibiti wa mchezo huo wa majaribio ambao ulishuhudia wachezaji na makocha 14, akiwemo Mourinho wakifungiwa.

    Nao Sevilla walisawazisha dakika 10 baada ya kipindi cha mapumziko na krosi ya Navas kutoka upande wa kulia,huku wakisukumana mbele mara kwa mara kutafuta bao la kusawazisha.

    Roma bila shaka walipata fursa nzuri zaidi za kushinda shindano hilo katika muda wa kawaida huku Tammy Abraham na Ibanez wakishindwa kucheka na wavu karibu na eneo hatari hukuAndrea Belotti akipangua nje mkwaju wa mpira wa adhabu wa Lorenzo Pellegrini.

  18. Real Madrid na Manchester United zaongoza orodha ya klabu zenye thamani zaidi duniani

    Manchester United ndio klabu yenye thamani kubwa zaidi katika ligi ya Premier, kulingana na orodha iliyotolewa na tovuti ya biashara ya Forbes Jumatano.

    United, yenye thamani ya $6bn (£4.8bn), ni ya pili kwenye orodha nyuma ya Real Madrid ya Uhispania $6.07bn - mara ya kwanza klabu mbili kuwa juu ya $6bn.

    Liverpool, Manchester City, Chelsea, Tottenham Hotspur na Arsenal pia wameingia 10 bora.

    Thamani ya Forbes kwa Manchester United imeongezeka kwa 30% tangu mwaka jana.

    Klabu hiyo ya Old Trafford iliuzwa na familia ya Glazer mwezi Novemba, huku benki ya Qatar Sheikh Jassim bin Hamad Al Thani na Ineos Group ya Sir Jim Ratcliffe wakiwasilisha ombi la kuinunua United.

    Real ilishika nafasi ya kwanza kuanzia 2022 huku ikiongeza thamani yake kwa 19%, huku wapinzani wao Barcelona wakiwa katika nafasi ya tatu wakiwa wameongoza orodha hiyo mwaka 2021.

    Tangu Forbes waanze kuchapisha orodha ya timu zenye thamani kubwa zaidi za kandanda duniani mwaka 2004, ni Real Madrid na Manchester United pekee ndizo zimeorodheshwa katika tano bora kila mwaka.

    Kwingineko, thamani ya Newcastle United imeongezeka kwa 51% hadi $794m kufuatia ununuzi wao unaoungwa mkono na Saudi Arabia na kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

    Nani ameingia 10 bora?

    • Real Madrid - $6.07bn (£4.9bn)
    • Manchester United - $6bn (£4.8bn)
    • Barcelona - $5.51bn (£4.4bn)
    • Liverpool - $5.29bn (£4.2bn)
    • Manchester City - $4.99bn (£4bn)
    • Bayern Munich - $4.86bn (£3.9bn)
    • Paris St-Germain - $4.21bn (£3.4bn)
    • Chelsea - $3.1bn (£2.5bn)
    • Tottenham Hotspur - $2.8bn (£2.2bn)
    • Arsenal - $2.26bn (£1.8bn)

    Wengine waliochaguliwa:

    15. West Ham - $1.03bn (£831m), 20. Crystal Palace - $806m (£650m), 22. Newcastle United - $794m (£640m), 23. Leicester City - $781m (£630m), 24. Aston Villa - $756m (£609m), 25. Everton - $744m (£600m)

  19. Hatuungi mkono mashambulizi ya Ukraine katika ardhi ya Urusi – Marekani

    Katika mahojiano na CNN Msemaji wa Baraza la Usalama la taifa la Marekani John Kirby ameeelezea kuhusu sera ya Ikulu ya Marekani, ambayo haiungi mkono mashambulizi ya jeshi la Ukraine katika ardhi ya Urusi.

    Kirby alisisitiza kuwa Ukraine iliihakikishia Marekani kwamba haitatumia silaha zilizopokelewa kutoka Marekani kwa mashambulizi hayo.

    "Tunakusudia kuendelea kuwapa kile wanachohitaji ili kujilinda na kulinda eneo lao, ardhi ya Ukraine, lakini hatuungi mkono mashambulizi dhidi ya Urusi," Kirby alisema.

    "Tunakubali kwamba Waukraine wana haki ya kujilinda. Katika miezi 15 iliyopita hatujafanya chochote ila kuwasaidia kujilinda na kulinda eneo lao kutokana na uchokozi huu wa Urusi."

    "Tulisema hatutaki kuhimiza au kuwezesha mashambulizi ndani ya Urusi kwa sababu hatutaki vita hivyo kuzidi kuwa ghasia zaidi kuliko zile ambazo tayari yamezipata watu wa Ukraine."

    "Nadhani sote tunaelewa kuwa tukimpa Putin kile anachodai, kwamba hii ni vita na Magharibi, vita na Marekani, vita na NATO, kutakuwa na mateso mengi zaidi katika bara la Ulaya. Hatutaki kuongezeka kwa vita hivi," John Kirby alisema.

    "Sasa angalia, mara tu tunapowasilisha mifumo kwa Waukraine, na hili ni jambo muhimu, wao wenyewe wanaamua nini watafanya nayo. Walituhakikishia kwamba hawatatumia vifaa vyetu kuipiga Urusi. Punde wanapozipokea, ni mali yao," msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa aliiambia CNN.

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  20. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu mubashara ya leo tarehe 01.06.2023