Dharura ya afya ya kimataifa kuhusu Covid-19 imekwisha, WHO yasema

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kwamba Covid-19 sio "dharura ya afya ya kimataifa" tena.

Moja kwa moja

  1. Habari za hivi punde, Mafuriko DRC: Idadi ya waliofariki yafikia 176

    Ramani

    Mamlaka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zinasema idadi ya watu watu wanaosadikiwa kufa kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo imeongezeka na kufikia 176.

    Gavana wa jimbo la Kivu Kusini anasema watu zaidi bado hawajulikani walipo, wanahofiwa kufukiwa chini ya udongo.

    Vijiji vya Bushushu na Nyamukubi - vilisombwa na maji baada ya mito ya mashariki mwa Congo kuvunja kingo zake.

    Pia kumeripotiwa maporomoko makubwa ya udongo ambayo yaliharibu nyumba zilizojengwa kwa mbao na paa za bati.

    Vyombo vya habari vya ndani vinaripoti kwamba katika moja ya vijiji zaidi ya robo tatu ya nyumba zote zimesombwa na maji ikiw ani pamoja na vituo vya afya na shule.

    Upande wa pili wa Ziwa Kivu katika nchi jirani ya Rwanda takriban watu mia moja na thelathini walikufa kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo.

  2. Odinga azuiwa kuingia msitu wa Shakahola

    Raila Odinga

    Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amezuiwa kuingia katika Msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi, ambapo miili ya zaidi ya washiriki 100 wa dhehebu tata la kidini imepatikana.

    Kiongozi wa dhehebu hilo Paul Makenzi anasemekana kuwashawishi wafuasi wake kusali na kufunga hadi kufa "ili waweze kukutana na muundaji wao".

    Bw, Raila alifika eneo hilo akiandamana na viongozi kadhaa wa Pwani wa Munngano wa upinzani wa Azimio la Umoja, One Kenya.

    Waziri Mkuu huyo wa zamani na washirika wake walipokelewa na maafisa wa polisi waliokuwa wakisimamia eneo la tukio na kutembezwa kwa muda mfupi na kupewa maelezo machache kuhusiana operesheni hiyo.

    ''Niliambiwa kwamba siwezi kufika huku na kwamba naweza tu kutembezwa na kuongozwa na wanachama wa kamati ya usalama ya Bunge. Hiyo ni aibu. Sihitaji kuandamana na wabunge, Nalaani kilichotokea hapa leo.'' alisema.

    Huku hayo yakijiri kamanda wa operesheni ya kuchunguza vifo hivyo, Bw Peter Ndung’u, alimtaka Raila kutafuta kibali kutoka kwa Inspekta Jenerali iwapo angetaka kuingia msituni, kulingana na taarifa za vyombo vya habari vya ndani.

    "Nataka kufikia msitu ili niweze kuona makaburi, siwezi kusafiri mwendo mrefu hivi na kurudi bila kufika eneo la tukio," Raila alisema.

    Unaweza kusoma

    • Paul Mackenzie: Ni kipi kinachojulikana kuhusu kiongozi wa dhehebu la kufa njaa nchini Kenya?
    • Kufunga mpaka kufa: 'Mke wangu na watoto sita walimfuata Mchungaji Mackenzie'
  3. Dharura ya afya ya kimataifa kuhusu Covid-19 imekwisha, WHO yasema

    Mkuu wa WHO alisema takribani watu milioni saba walikufa katika janga hilo

    Chanzo cha picha, Reuters

    Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kwamba Covid-19 si "dharura ya afya ya kimataifa" tena.

    Taarifa hiyo inawakilisha hatua kubwa kuelekea kumaliza janga hili na inakuja miaka mitatu baada ya kutangaza kiwango chake cha juu zaidi cha tahadhari kuhusu virusi.

    Viongozi walisema kiwango cha vifo vya virusi hivyo kilipungua kutoka kilele cha zaidi ya watu 100,000 kwa wiki mnamo Januari 2021 hadi zaidi ya 3,500 mnamo 24 Aprili.

    Mkuu wa WHO alisema takribani watu milioni saba walikufa katika janga hilo. Lakini Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema kwamba idadi ya kweli "inawezekana" karibu na vifo milioni 20 - karibu mara tatu ya makadirio rasmi na akaonya kwamba virusi vinasalia tishio kubwa.

    "Jana, Kamati ya Dharura ilikutana kwa mara ya 15 na kupendekeza kwamba nitangaze kusitishwa kwa dharura ya afya ya umma kimataifa. Nimekubali ushauri huo. Kwa hiyo ni matumaini makubwa kwamba ninatangaza Covid-19 kuwa si dharura ya afya ya kimataifa," Dk Tedros alisema.

    Lakini alionya uamuzi wa kuondoa tahadhari ya hali ya juu haimaanishi kwamba hatari imeisha na kusema hali ya dharura inaweza kurejeshwa ikiwa hali itabadilika.

    ''Jambo baya zaidi ambalo nchi yoyote inaweza kufanya sasa ni kutumia habari hii kama sababu ya kuacha macho yake, kubomoa mifumo ambayo imeundwa, au kutuma ujumbe kwa watu wake kwamba Covid-19 sio jambo la kuwa na wasiwasi nalo," alisema.

    Shirika la Afya Ulimwenguni lilitangaza kwa mara ya kwanza kile kinachoitwa dharura ya afya ya umma ya wasiwasi wa kimataifa mnamo Januari 2020.

    Chanjo ilikuwa moja wapo ya mabadiliko makubwa katika janga hilo - ikiruhusu mamilioni ya watu kulindwa dhidi ya ugonjwa mbaya na kifo.

    Marekani na Uingereza, kama nchi nyingine nyingi, tayari zimezungumza juu ya "kuishi na virusi" na kupunguza vipimo vingi na sheria za mchanganyiko wa kijamii. Lakini katika nchi nyingi chanjo hazijawafikia wengi wanaohitaji.

    Dk Mike Ryan, kutoka mpango wa dharura wa afya wa WHO, alisema dharura hiyo inaweza kuwa imeisha, lakini tishio bado lipo.

    "Tunatarajia kabisa kwamba virusi hivi vitaendelea kusambaa na hii ndio historia ya milipuko. "Ilichukua miongo kadhaa kwa utupaji wa mwisho wa virusi vya janga la 1918 kutoweka. "Katika hali nyingi milipuko huisha wakati janga linalofuata linaanza."

  4. Mwanasiasa, mke wahukumiwa kifungo Uingereza baada ya kula njama ya biashara ya viungo vya binadamu

    Seneta Ike Ekweremadu ni mwanasiasa mashuhuri wa Nigeria

    Chanzo cha picha, MET POLICE

    Mwanasiasa tajiri wa Nigeria, mke wake na "mtu wao wa kati" wamefungwa kwa njama ya kusafirisha viungo vya binadamu, baada ya kuleta mwanaume mmoja nchini Uingereza kutoka Lagos.

    Seneta Ike Ekweremadu, 60, na mkewe Beatrice, 56, walitaka kiungo hicho kwa ajili ya binti yao Sonia mwenye umri wa miaka 25, kesi ya wanandoa hao huko Old Bailey ilisikizwa.

    Wawili hao na Dkt Obinna Obeta, 50, walipatikana na hatia hapo awali kwa kula njama ya kupata figo ya mwanaume huyo kwa ajili ya mtoto wao.

    Inasemekana kuwa kesi ya kwanza kama hii chini ya sheria za utumwa mamboleo.

    Ike Ekweremadu, alihukumiwa kifungo cha miaka tisa na miezi minane jela. Dkt Obeta alihukumiwa kifungo cha miaka 10 baada ya hakimu kupata kwamba alikuwa amemlenga mfadhili ambaye alikuwa kijana, maskini na asiye na uwezo.

    Beatrice Ekweremadu alifungwa jela miaka minne na miezi sita kutokana na ushiriki wake.

    "Middleman" Dkt Obinna Obeta na mke wa seneta huyo, Beatrice, pia walipatikana na hatia

    Chanzo cha picha, METROPOLITAN POLICE

    Mwathiriwa, mfanyabiashara maskini wa mitaani huko Lagos, alipelekwa Uingereza kutoa figo kwa binti wa Ekweremadus.

    Jaji Johnson alimtaja mwanasiasa huyo kama mtu wa ofisi ya juu mwenye mali nyingi, wafanyakazi wa ndani, vijakazi, wapishi na madereva ikilinganishwa na mwathiriwa, ambaye hakuweza kumudu tikiti ya pauni 25 ya kusafiri kwenda Abuja.

    Obeta, alisema, aliwadanganya madaktari na kudai kuwa kijana huyo ambaye alitarajiwa kuwa mfadhili alikuwa binamu ya bintiye seneta ambaye alihitaji kupandikizwa kwa haraka.

    Watatu hao walikuwa wamemwacha mfadhili anayetarajiwa kukabiliwa na "athari kubwa na ya muda mrefu katika maisha yake ya kila siku", alisema. "Usafirishaji haramu wa watu kuvuka mipaka ya kimataifa kwa ajili ya kuvuna viungo vya binadamu ni aina ya utumwa," jaji aliongeza.

    Katika taarifa ya binafsi ya mwathiriwa, mfanyabiashara wa soko nchini Nigeria mwenye umri wa miaka 21, ambaye hawezi kutajwa kwa sababu za kisheria, aliiambia mahakama kwamba alikuwa akiomba kila siku ili apewe fursa ya kuingia Uingereza kufanya kazi au kusoma.

  5. Miili 70 yapatikana baada ya mafuriko DRC

      • Author, Caro Robi
      • Nafasi, BBC Swahili
    Mafuriko

    Takriban miili sabini imepatikana baada ya mafuriko makubwa yaliyotokea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Ripoti zinaarifu kuwa tukio la nyumba kusombwa na maporomoko ya ardhi limetokea katika vijiji viwili vya Bushushu na Nyamukubi jimboni Kivu Kusini.

    Gavana wa jimbo hilo ameyataja mafuriko hayo kuwa janga. Katika jimbo jirani la Ituri,mafuriko pia yameharibu zaidi ya makazi elfu moja ambayo yalikuwa yamejengwa kwa ajili ya kuwahifadhi watu wasio na makazi waliokimbia mapigano ya mashariki mwa Congo.

    Shirika la habari la Reuters linaripoti kuwa waandishi wake wameshuhudia wafanyakazi wa kutoa misaada ya kiutu wakitoa miili sabini na mbili kutoka vifusi vya majengo yaliyoporomoka kijijini Bushushu wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

    Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, maafa ya kiwango kama hicho yaliripotiwa katika eneo hilo la mashariki mwa Congo mnamo mwezi Oktoba mwaka 2014 ambapo mvua kubwa ilisababisha mafuriko yaliyoharibu zaidi ya nyumba mia saba na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 130.

  6. Salamu za rambirambi zatolewa Kenya baada ya kifo cha mjane wa Dedan Kimathi

    Bi Kimathi

    Chanzo cha picha, Ikulu Kenya/Twitter

    Wakenya wamekuwa wakitoa heshima zao kwa Mukami Kimathi, mjane wa mwanaharakati wa kupigania uhuru wa Mau Mau nchini Kenya, Dedan Kimathi.

    Familia ya Bi Kimathi iliviambia vyombo vya habari kwamba alipata matatizo ya kupumua Alhamisi usiku na kupelekwa hospitali katika mji mkuu, Nairobi, ambako alifariki muda mfupi baadaye.

    Mumewe, ambaye alikuwa kiongozi wa uasi wa Mau Mau, alitekwa, akahukumiwa na kunyongwa na serikali ya kikoloni ya Uingereza mwaka wa 1956.

    Alizikwa katika gereza la Kamiti nje kidogo ya jiji. Siku ya Ijumaa, Rais wa Kenya William Ruto alitoa pongezi kwa Bi Kimathi kwa "kustahimili ukatili wa ukandamizaji wa wakoloni, kwa kujivunia makovu ya vita na kubeba hasara mbaya za vita kwa ujasiri wa kustaajabisha".

    Naibu Rais Rigathi Gachagua alimtaja kama "mama wa mapambano yetu ya ukombozi na mwanga wa matumaini unaowazunguka wapigania uhuru na vizazi vyao".

    Katika maisha yake, alisukuma mijadala kuhusu ustawi wa wapigania uhuru - ambao hawakufurahia manufaa ya kujitolea kwao kwa ajili ya uhuru wa Kenya. Mnamo Januari, alizuiwa kutoka hospitali alikokuwa amelazwa baada ya familia yake kushindwa kulipa gharama- ambayo ilionekana kama dalili ya umaskini ambao wapigania uhuru walipaswa kuvumilia.

    Aliruhusiwa baadaye baada ya rais kufuta gharama kiasi cha $7,300 (£5,800). Pia alikuwa akishinikiza kufukuliwa kwa mabaki ya mumewe kutoka gerezani ili kuzikwa upya nyumbani kwake.

    Hata hivyo, utafutaji wa miaka mingi wa mahali ambapo alizikwa umeambulia patupu - licha ya Bi Kimathi kueleza nia yake ya kuoneshwa kaburi kabla ya kifo chake.

  7. Viongozi wa Afrika wawasili London kwa sherehe ya kutawazwa kwa Mfalme

    Rais Mnangagwa atakuwa kiongozi wa kwanza wa Zimbabwe kuzuru London kwa zaidi ya miongo miwili

    Chanzo cha picha, The Herald Zimbabwe/Twitter

    Maelezo ya picha, Rais Mnangagwa atakuwa kiongozi wa kwanza wa Zimbabwe kuzuru London kwa zaidi ya miongo miwili

    Viongozi kadhaa wa mataifa ya Afrika, wengi wao kutoka nchi za Jumuiya ya Madola, wamewasili London kwa hafla ya kutawazwa kwa Mfalme Charles siku ya Jumamosi.

    Wale ambao tayari wako Uingereza ni pamoja na Paul Kagame wa Rwanda, Mfalme Mswati III wa Eswatini, Lazarus Chakwera wa Malawi, Hakainde Hichilema wa Zambia, na George Weah wa Liberia miongoni mwa wengine.

    Rais Emmerson Mnangagwa atakuwa kiongozi wa kwanza wa Zimbabwe kuzuru London kwa zaidi ya miongo miwili baada ya Uingereza kuiwekea vikwazo nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

    Bw Mnangagwa alisema "alifurahi" kupokea mwaliko wa kuhudhuria hafla hiyo ya kifalme.

    Baadhi ya wabunge wa Uingereza, hata hivyo, walikosoa mwaliko wake wakitaja madai ya ukiukaji wa haki za binadamu nchini mwake.

    Bado haijabainika iwapo Rais wa Kenya William Ruto atahudhuria hafla hiyo, baada ya kulalamikia kudhulumiwa kwa viongozi wa Afrika wakati wa safari za nje wiki iliyopita.

    Alikuwa akiashiria tukio ambapo marais wa Afrika walipandishwa basi ili kuhudhuria mazishi ya Malkia Elizabeth nchini Uingereza.

    Kutoka nchi zinazozungumza Kifaransa, Rais wa Niger Mohamed Bazoum atahudhuria hafla hiyo ya kifalme huku Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara akiwakilishwa na naibu wake Tiémoko Meyliet Koné.

    Waziri Mkuu wa Cameroon Joseph Dion Ngute atamwakilisha Rais Paul Biya katika hafla hiyo. Nchi hiyo ni koloni la zamani la Uingereza na Ufaransa.

    Mfalme Mswati III wa Eswatini ndiye mfalme wa mwisho kabisa barani Afrika

    Chanzo cha picha, Serikali ya Eswatini/Twitter

    Maelezo ya picha, Mfalme Mswati III wa Eswatini ndiye mfalme wa mwisho kabisa barani Afrika
  8. Rwanda: Mke wangu alikufa na mafuriko na "kuniacha na mtoto wa miezi sita"

    Rwanda

    "Kadiri miaka inavyosonga, nitakuwa nikimleta hapa na kumwambia 'Twende tukamtembelee mama'." Bw Feza Nteziyaremye anasema akimuashiria mtoto wake mchanga baada ya kumzika mkewe ambaye alifariki kwenye mafuriko Jumatano wiki hii kaskazini-magharibi mwa Rwanda.

    Watu 130 walifariki, idadi kubwa zaidi ya waathiriwa wa maafa yanayohusiana na hali ya hewa katika miongo kadhaa nchini Rwanda.

    Maelfu ya watu sasa hawana makazi baada ya nyumba zaidi ya 5,000 kuharibiwa pamoja na barabara na madaraja. Eneo lililoathiriwa linaendelea kukarabatiwa.

    Siku ya Alhamisi watu 13 walizikwa wilayani Rubavu katika tukio moja, wengi wao walifariki baada ya mto Sebeya kufurika na maji yake kusomba vitongoji vya vyake usiku wa Jumanne.

    Bw Nteziyaremye na mkewe Genereuse Mukamanzi, 27, waliamka wakati maji ya mto yalikuwa tayari yamesomba nyumba yao. Alimfunga mgongoni mtoto wao wa miezi sita na kumwomba mke wake ajaribu kujishikilia kwenye kitu chenye nguvu.

    "Hali alipozidi kuwa mbaya, nilimwomba asali na tulipomaliza kusali wimbi zito liligonga dirisha alilokuwa amelishikilia na kumteka", Bw Nteziyaremye aliiambia BBC.

    Rwanda

    Mwili wa mke wake wa Mukamanzi ulipatikana siku ya Jumatano umbali wa kilomita chache, huku Nteziyaremye na mtoto mchanga wakiokolewa na wenyeji baada ya saa kadhaa za kushikilia juu ya mti kwani mto ulikuwa umeharibu na kusomba nyumba yao.

    “Sasa nimefarijika kwa sababu nimemuona na kumzika. Mtoto [aliyemwacha] ana umri wa miezi sita, nitakuwa nikimleta hapa na kumwambia ‘Twende tukamtembelee mama’,” Bw Nteziyaremye aliambia BBC akiwa makaburini.

    Serikali ya Rwanda imeahidi kuimarisha uokoaji na kuwasaidia manusura wa janga la hali ya hewa.

    Papa Francis amesema "anahuzunishwa sana na maafa kupoteza na uharibifu uliotokea" nchini Rwanda na kwamba alikuwa karibu nao kwa maombi "na wale wote wanaoteseka kutokana na janga hili", Vatican News ilimnukuu akisema.

  9. Japan kufadhili vita dhidi ya ugaidi Msumbiji

    Waziri Mkuu wa Japan (katikati) amekuwa akitembelea nchi za Afrika

    Chanzo cha picha, Mozambican Presidency

    Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida anasema nchi yake iko tayari kusaidia Msumbiji katika vita dhidi ya ugaidi.

    Waziri Mkuu wa Japan anazuru Msumbiji kama sehemu ya ziara yake ya siku sita iliyompeleka katika nchi nyingine tatu za Afrika - Ghana, Kenya na Misri.

    Alisema Japan ina nia ya kufadhili mapambano dhidi ya ugaidi kaskazini mwa jimbo la Cabo Delgado, jambo ambalo litaruhusu makampuni ya Japan ambayo ni sehemu ya miungano inayonyonya gesi asilia katika bonde la Rovuma, kufanya kazi katika mazingira salama.

    Mkoa wa kaskazini umezingirwa na waasi wa Kiislamu kwa miaka mingi. Bw Kishida na Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi walizungumza kuhusu hitaji la uwekezaji wa binafsi wa Japan katika "maeneo ya kimuundo" ya uchumi, kwa lengo la kupata matokeo madhubuti katika ushirikiano wa pande mbili. Bw Nyusi aliwataka Wajapani hao kutafuta fursa za uwekezaji katika usafiri, kilimo, viwanda na utalii.

    Unaweza kusoma;

  10. Yevgeny Prigozhin: Mkuu wa Wagner asema ataondoa wanajeshi Bakhmut

    Yevgeny Prigozhin ametoa mfululizo wa taarifa za hasira zilizoelekezwa kwa serikali ya Urusi katika miezi ya hivi karibuni

    Chanzo cha picha, CONCORD PRESS SERVICE

    Kiongozi wa Kundi la Wagner la Urusi ametishia kuwaondoa wanajeshi wake katika mji wa Bakhmut nchini Ukraine ifikapo Jumatano, katika mzozo kuhusu silaha.

    Kauli yake ilikuja baada ya kuchapisha video kwenye mtandao wa kijamii akitembea kati ya miili ya wapiganaji waliokufa, akiwaomba maafisa wa ulinzi vifaa zaidi. Urusi imekuwa ikijaribu kuuteka mji huo kwa miezi kadhaa, licha ya thamani yake ya kimkakati ya kutiliwa shaka.

    "Shoigu! Gerasimov! iko wapi... silaha?... Walikuja hapa kama watu wa kujitolea na kufa kwa ajili yenu ili kujinenepesha katika ofisi zenu za mahogany." Waziri wa Ulinzi Sergei Shoigu na Mkuu wa Wafanyakazi Valery Gerasimov mara nyingi hasira ya Prigozhin imekuwa juu yao.

    Ushawishi wake umeonekana kupungua katika miezi ya hivi karibuni. Hapo awali alitoa vitisho ambavyo hakufuata - na kuvipuuza kama ucheshi wa kijeshi.

    Wiki iliyopita tu alimwambia mwanablogu wa Kirusi anayeunga mkono vita kwamba wapiganaji wa Wagner huko Bakhmut walikuwa wamefikia siku zao za mwisho za usambazaji wa silaha, na walihitaji maelfu ya risasi. Ikiwa uhaba haungeshughulikiwa basi mamluki wake wangelazimika ama kurudi nyuma au kubaki na kufa, alionya: "Basi, bila kujali watendaji wetu wanataka nini, kila kitu kingine kitasambaratika."

    Unaweza kusoma;

  11. Rais Biden aidhinisha vikwazo dhidi ya Sudan

    Mapigano makali yameendelea katika mji mkuu Khartoum na miji inayoungana nayo

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mapigano makali yameendelea katika mji mkuu Khartoum na miji inayoungana nayo

    Rais wa Marekani Joe Biden ametoa agizo la kuidhinishwa kwa vikwazo dhidi ya Sudan, akisema mapigano lazima yaishe.

    Bw Biden ameziita ghasia zinazoendelea nchini Sudan maafa na usaliti kwa watu wa Sudan.

    Amesema ghasia nchini Sudan "ni tisho lisilo la kawaida kwa usalama wa taifa na sera ya kigeni ya Marekani".

    Awali, Mkurugenzi wa shirika la ujasusi la Marekani, Avril Haines, aliiambia kamati ya seneti kwamba mzozo huo unaweza kuendelea kwa muda mrefu, kwani pande zote zinaamini kuwa zinaweza kushinda kijeshi na haziko tayari kwa mazungumo.

    Muda wa usitishaji mapigano wa sasa umeshindwa kuheshimiwa , huku mapigano makali yakiendelea katika mji mkuuKhartoum, pamoja na miji jirani ya Omdurman na Bahri.

    Shirika la mpango wa chakula duniani WFP linakadiria kuwa takriban msaada wa thamani ya dola milioni 13 (£10.3m) wa chakula uliokuwa ukipelekwa Sudan umeporwa tangu mapigano yalipoibuka mwezi uliopita.

    WFP linasema uporaji umekithiri nchini humo.

    Shirika la Umoja wa mataifa la watoto, Unicef, lilionya kuwa hali inaelekea kuwa janga, huku watoto wakiendelea kuuliwa katika mashambulio.

    Unaweza pia kusoma:

    • Mzozo wa Sudan:Mahasimu wa Sudan wakubaliana 'kimsingi' kusitisha mapigano kwa wiki moja
    • Mzozo wa Sudan: Mgogoro wa Sudan unaweza kuisha kwa njia hizi tatu
    • Mzozo wa Sudan: Jeshi na RSF zalaumiana kwa kutoheshimu makubaliano ya kusistisha vita
  12. Shambulio la pili la risasi lawauwa 8 Serbia

    f

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Vikosi vya usalama vikifanya operesheni kwenye kituo cha ukaguzi baada ya ufyatuaji risasi katika kijiji cha Dubona.

    Watu kadhaa wameuawa na wengine wapatao 10 wamejeruhiwa katika tukio la ufyatuaji risasi nyingi nchini Serbia wa siku nyingi.

    Mtu mwenye silaha ameripotiwa kufyatua silaha inayofyatua risasi moja kwa moja kutoka kwenye gari karibu na kijiji kilichopo km60 (maili 37) kusini mwa mji wa Belgrade.

    Ripoti ambazo hazijathibitishwa zinasema kuwa mshukiwa bado hajakamatwa na haijajulikana aliko.

    Mapema wiki hii, mvulana mwenye umri wa miaka 13, aliwauwa wanafunzi wanane katika shule iliyopo mjini Belgrade katika tukio baya zaidi la ufyatuaji risasi kuwahi kushuhudiwa nchini Serbia kwa miaka.

    Ijumaa asubuhi, vyombo vya habari vya Serbia vilisema kwamba kikosi maalumu cha polisi kimewasili katika vijiji vya Mladenovac na Dubona, ambako mauaji ya hivi karibuni yalitokea.

    Picha kutoka katika eneo la tukio zinaonyesha maafisa wa polisi wakisimamisha magari kwenye vituo vya ukaguzi kujaribu kumpata mshukiwa. Helikopta, droni na polisi wengi wanafanya doria pia kumsaka mshukiwa katika maeneo ya kijiji cha Dubona.

    Taarifa za vyombo vya habari zinasema kuwa mwanaume mwenye umri wa miaka 20, alianza kuwafyatulia risasi watu kwa kutumia silaha inayomimina risasi moja kwa moja baada ya kuwa na mapishano na afisa wa polisi katika bustan iliyopo Dubona Alhamisi jioni.

    Baadaye mwanaume huyo anasemekana aliendelea kuwapiga risasi watu kutoka kwenye gari, akawauwa watu wanane na kuwajeruhi wengine zaidi.

  13. Urusi haina nguvu ya 'Mashambulizi Makubwa' mwaka huu - Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Rais Joe Biden wa Marekani na mwenzake wa Uruso Vladmir Putin

    Mkurugenzi wa Ujasusi wa Kitaifa Avril Haynes alizungumza kwenye kikao mbele ya Kamati ya Seneti ya Huduma za Silaha. Na, alisema, Urusi - bila kujali uwezo wa Urusi na mafanikio yake - "pengine haitaweza kutekeleza mashambulizi makubwa mwaka huu."

    Kulingana na Haynes, Urusi haina wanajeshi wa kutosha waliofunzwa na silaha kuanzisha shambulio kubwa

    Hii ina maana, anasema Haynes, kwamba Urusi itaelekeza nguvu zake zote kutetea maeneo yanayokaliwa na hivyo kufanya iwe vigumu iwezekanavyo kwa Ukraine kujiunga na NATO.

    Akijibu swali kuhusu uwezekano wa matumizi ya silaha za nyuklia na Urusi, Haynes alisema kuwa Marekani inaona uwezekano huo kama "usiowezekana".

  14. Umoja wa Mataifa unatahadharisha kuhusu rasilimali za wakimbizi Sudan Kusini

    v
    Maelezo ya picha, Renk kwa sasa inawapokea maelfu ya wakimbizi kutoka Sudan

    Waandishi wa BBC wamewasili katika kituo cha muda cha kuwapokea wakimbizi kilichopo Renk nchini Sudan Kusini, ambako wahudumu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa wanasema wana ukosefu wa rasilimali zinazohitajika kwa ajili ya kuwasaidia wale wanaokimbia wakivuka mpaka na kuingia kutoka Sudan.

    Waliiambia BBC kuwa walipanga operesheni ya msaada kuanzia mwanzo, ingawa huduma kama maji, chakula na mahema vinatolewa.

    Renk iko karibu na mpaka na Sudan, ambako zaidi ya watu 4,000 wanaishi baada ya kukimbia mzozo ambao uliibuka karibu wiki tatu zilizopita.

    g

    Takriban watu 30,000 kwa ujumla wamekuja Sudan Kusini kutoka Sudan katika kipindi hicho – wengi wakiwa ni raia wa Sudan Kusini, lakini baadhi ni Wasudan na mataifa mengine.

    Wengi wanaishi na familia au jamii za eneo hilo, wengine wamefanikiwa kufika katika mji mkuu Juba.

    Hapa katika eneo la Renk makundi ya familia na marafiki, baadhi yao wakiwa ni watoto wadogo wanaishi katika mahema ya wazi huku wengine wakipiga kambi nje katika majengo yaliyotelekezwa kaika Chuo kikuu kikuu cha zamani.

    Sudan Kusini tayari iliathiriwa na mzozo wa miaka mingi, na inahangaika kiuchumi kutoa usaidizi kwa wale wanaokuja kwa kuvuka mpaka.

    Biashara na Sudan tayari imesitishwa kutokana na mzozo huku mawaziri wa serikali wakionya kuhusu athari za muda mrefu kama mapigano ya Sudan yataendelea.

    Unaweza pia kusoma:

    • Mzozo wa Sudan:Mahasimu wa Sudan wakubaliana 'kimsingi' kusitisha mapigano kwa wiki moja
    • Mzozo wa Sudan: Mgogoro wa Sudan unaweza kuisha kwa njia hizi tatu
    • Mzozo wa Sudan: Jeshi na RSF zalaumiana kwa kutoheshimu makubaliano ya kusistisha vita
  15. Napoli wanyakua taji la kwanza la Serie A ndani ya miaka 33

    w

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Napoli washinda taji lao la kwanza la Serie A kwa miaka 33 walipotoka sare na Udinese kwenye uwanja wa Dacia Arena na kuibua shangwe kubwa huko Naples.

    Walishinda ligi mara ya mwisho mwaka wa 1990 huku timu iliyoongozwa na Diego Maradona ikiongeza taji lao la kwanza miaka mitatu nyuma.

    Victor Osimhen alifunga bao la kusawazisha dakika ya 52 baada ya Sandi Lovric kuipatia Udinese bao la kuongoza. Na Napoli walishikilia hatua waliyohitaji kushinda taji lao la tatu la Serie A zikiwa zimesalia mechi tano.

    "Kuona wana Napoli wakiwa na furaha inatosha kukupa hisia ya furaha wanayohisi," bosi wa Napoli Luciano Spalletti aliiambia DAZN.

    "Watu hawa wataangalia wakati huu ambapo maisha yatakuwa magumu, wana haki ya kusherehekea hivi. "Unajisikia utulivu zaidi ukijua kuwa umewapa wakati huu wa furaha."

    Napoli inamaliza miongo mitatu ya maumivu Mataji mawili ya awali ya Napoli yalikuja katika siku za nguli wa Argentina Maradona - ambaye uwanja wao sasa unaitwa - mnamo 1987 na 1990. Kufuatia siku hizo za utukufu klabu ilianguka katika mdororo wa kifedha, kushuka daraja na kufilisika; ikicheza Serie C hivi majuzi mwaka 2006.

  16. Vita vya Ukraine: Ukraine yaidungua droni yake yenyewe katikati ya Kyiv

    Maelezo ya video, Ukraine: Droni ikidunguliwa juu ya anga la ya Kyiv na kuungua angani

    Vikosi vya Ukraine vimeidungua ndege yake isiyokuwa na rubani ambayo ilisema kuwa ilikuwa imepoteza udhibiti juu ya eneo la katikati mwa mji mkuu Kyiv.

    Kulikuwa ni milipuko ya dakika 15 hadi 20 siku ya Alhamisi jioni huku mifumo ya ulinzi ya anga ikijaribu kuidungua katika eneo lililopokaribu na ofisi ya rais.

    Mkuu wa wafanyakazi wa ofisi ya rais nchini Ukraine Andriy Yermak awali alisema kuwa ilikuwa ni droni ya adui ambayo ilidunguliwa.

    Lakini jeshi baadaye lilikiri kuwa ilikuwa ni droni ya Ukraine na iliangamizwa ili kuepuka "hali zisizohitajika".

    Katika taarifa yake, ilisema Bayraktar TB2 UAV [chombo cha anga kinachojiongoza] kilikuwa kimepoteza udhibiti majira ya saa mbili usiku kwa saa za eneo(17:00 GMT) katika jimbo la Kyiv , wakati wa safari iliyopangwa.

    Iliongeza kuwa ilichukua uamuzi wa kuidungua "kwani uwepo wa UAVs kwenye anga la mji mkuu bila udhibiti inaweza kusababisha athari zisizohitajika".

    Hapakuwa na wahanga au majeruhi kutokana na kuangua kwa droni, ilisema taarifa.

    Unaweza pia kusoma:

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  17. Vita vya Ukraine: Marekani yakanusha kupanga shambulio la droni la Moscow

    g

    Marekani imekanusha madai kwamba ilipanga shambulio la ndege isiyokuwa na rubani inayodaiwa kuishambulia Kremlin siku ya Jumatano kwa lengo la kumuua Rais Vradimir Putin.

    Siku moja baada ya kuishutumu Ukraine kwa kutekeleza shambulio hilo, msemaji wa Bw Putin amesema lilifanywa kwa usaidizi wa Washington.

    Msemaji wa Usalama wa taifa nchini Marekani John Kirby ameyaita "madai ya kejeli".

    Ukraine imesema haihusiki na shambulio linalodaiwa. Bw Putin hakuwepo katika katika jengo la Kremlin wakati huo.

    Ukraine imeishutumu Moscow kupanga tukio hilo ili kuendeleza vita zaidi.

    Licha ya kwamba mashambulio ya Urusi yameendelea bilakupungua – watu 21 waliuawa Jumatanokatika jimbo la Kherson lililopo kusini mwa Ukraine – bado hakuna dalili kwa upande wa Urusi ya kufanya mashambulizi makali.

    Jumapili jioni ndege isiyokuwa na rubani ilidunguliwa katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, katika eneo ambalo sio mbali sana na ofisi ya rais.

    Maafisa baadaye walikiri kuwa ilikuwa ni droni ya Ukraine ambayo ilikuwa "imepoteza udhibiti" na kwamba iliharibiwa ili kuepusha "athari mbaya".

    Unaweza pia kusoma:

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  18. Hujambo na karibu tena kwa matangazo yetu ya mubashara leo ikiwa ni Ijumaa tarehe 05.05.2023