Vita vya Ukraine: Urusi yafanya shambulio kubwa la anga huko Ukraine na kuua 19

Ni shambulio la kwanza kubwa zaidi kufanyika katika kipindi cha miezi miwili iliyopita

Moja kwa moja

  1. Vietnam yawakamata watu 65 kwa kusafirisha dawa za kulevya kwenye mirija ya dawa ya meno

    w

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Polisi wamewakamata watu 65 kwa kusafirisha kilo 50 za dawa za kulevya - zingine zikiwa zimefichwa kwenye mirija ya dawa za meno - hadi Vietnam.

    Tukio hili Iinafuatia kukamatwa mwezi uliopita kwa wafanyakazi wanne wa shirika la ndege la Vietnam waliokutwa na mirija kwenye mifuko ya kubebea baada ya safari ya ndege kutoka Paris kuelekea Ho Chi Minh City.

    Walisema waliajiriwa kusafirisha kilo 60 za dawa ya meno lakini hawakujua ni ecstasy, ketamine na cocaine.

    Vietnam ni kitovu kikuu cha biashara ya dawa za kulevya licha ya kuwa na sheria kali zaidi za dawa za kulevya ulimwenguni.

    Takriban nusu ya mirija 327 ya dawa za meno ambayo wahudumu wa ndege walikuwa wakisafirisha ilikuwa na dawa za kulevya.

    Wachunguzi walisema wanawake hao hawakujua yaliyomo - kwa sasa wako nje kwa dhamana.

    Polisi walisema wiki hii kwamba washukiwa hao 65 walikamatwa baada ya kugundua shehena nyingine sita za mihadarati zikisafirishwa kwenda Vietnam kupitia njia hiyo hiyo.

    Inadaiwa walielekezwa na kisa hicho cha magendo ambacho kilikodi wahudumu wa ndege hiyo.

    Washukiwa hao 65 wanachunguzwa kwa makosa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kununua, kuuza, kusafirisha na kuhifadhi mihadarati, vyombo vya habari nchini viliripoti.

    Polisi wanashuku kundi moja mara nyingi hutumia raia wa Vietnam wanaosoma na wanaoishi Ufaransa kuleta dawa za kulevya nchini humo.

    Wale waliopatikana na hatia nchini Vietnam kwa kumiliki au kusafirisha zaidi ya gramu 600 za heroini au zaidi ya kilo 2.5 za methamphetamine wanakabiliwa na hukumu ya kifo.

    Uzalishaji au uuzaji wa dawa za kulevya zaidi ya kiasi fulani pia huadhibiwa kwa kifo.

  2. Mamlaka zawasaka Wabakaji wawili walitoroka jela Afrika Kusini

    Jela

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mamlaka ya Afrika Kusini inawasaka wabakaji wawili waliokutwa na hatia ya kubaka ambao wametoroka jela katika jimbo la Eastern Cape.

    Siyabulela Khohliso na Athini Mzingelwa wanasemekana kutoroka wakiwa katika uwanja wa michezo wa Jela ya Ngqeleni Alhamisi alasiri.

    "Uchunguzi kuhusu tukio hili tayari umeanza. Lakini muhimu katika hatua hii ni kukamatwa tena kwa wahalifu hao wawili," Idara ya Huduma za Urekebishaji (DCS) ilisema katika taarifa yake.

    Idara hiyo inawataka wananchi kuwasiliana na kituo chao cha polisi kilicho karibu nao haraka iwapo watakutana na yeyote kati ya hao waliotoroka.

    Haya yanakuja huku kukiwa na uchunguzi mkali wa vyombo vya habari kuhusu kutoroka jela kwa mtu mwingine, Thabo Bester, ambaye alidanganya kifo chake hapo mwaka jana kabla ya kukamatwa nchini Tanzania mwezi huu.

  3. Putin atia saini amri ya kufukuzwa kwa watu ambao hawatachukua uraia wa Urusi maeneo yaliyonyakuliwa

    h

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Urusi Vladimir Putin siku ya Ijumaa alitia saini amri inayowapa watu wanaoishi katika sehemu za Ukrainia chini ya udhibiti wa Moscow njia ya kupata uraia wa Urusi lakini inamaanisha wale wanaokataa au ambao hawaidhinishi hadhi yao wanakabiliwa na uwezekano wa kufukuzwa.

    Amri hiyo inaenea hadi maeneo manne ya Ukrain ambayo Urusi imedai kuwa chini yake na inadhibiti kwa kiasi: Donetsk, Luhansk, Kherson na Zaporizhzhia.

    Kyiv inasema itachukua tena maeneo yote manne na imeishutumu Moscow kwa kujaribu kuwashawishi raia wake kukubali uraia wa Urusi.

    Amri mpya inaweka njia ambazo raia wa Ukraine au wale walio na hati za kusafiria zilizotolewa na jamhuri zilizojitenga zinazoungwa mkono na Urusi, na wanaoishi katika mikoa minne, wanaweza kuanza mchakato wa kuwa raia wa Urusi au kuhalalisha hali yao kwa mamlaka ya Urusi.

    Lakini pia inasema kuwa yeyote ambaye hatachukua hatua hiyo ifikapo Julai 1 mwaka ujao atachukuliwa kuwa raia wa kigeni, jambo ambalo litawaacha katika hatari ya kufukuzwa kutoka eneo ambalo Urusi inaona ni lake.

    Agizo hilo pia linaruhusu mamlaka kuwatimua watu kutoka maeneo hayo manne ikiwa wanachukuliwa kuwa tishio kwa usalama wa taifa la Urusi au kushiriki katika kile ambacho amri hiyo inarejelea kuwa maandamano yasiyoidhinishwa.

  4. Zanzibar yapiga marufuku rangi za upinde kwa kuhusishwa na 'harakati za wapenzi wa jinsia moja'

    w

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri wa Elimu Visiwani Zanzibar Bi. Lela Muhamed Mussa, amepiga marufuku matumizi ya rangi za upinde (Rainbow) katika shule kwa kuhusisha rangi hizo harakati za wapenzi wa jinsia moja.

    ‘’Busara tumeona ni vyema kuondoa rangi ya upinde katika shule zote za serikali na binafsi, tubadilishe zile nembo, kwasababu hao wenzetu ambao wapo katika mrengo huo wamekua wakizitumia, ili kuwanusuru vijana wetu’’ anasema Bi Lela.

    Waziri huyo alibanisha marufuku hiyo wakati akitoa taarifa ya uchunguzi kuhusiana na kamati iliyoundwa kuchunguza tuhuma za shule moja kujihusisha na mafunzo ya wapenzi wa jinsia moja.

    Amesema Wizara imejiridhisha kutokuwepo na vitendo vinavyoashiria tuhuma hizo ndani ya Shule hiyo baada ya kufanya uchunguzi kuanzia umiliki wa shule, vifaa vinavyotumika, taaluma za walimu pamoja na njia wanazotumia katika kufundishia na kuona hakuna dalili ya tuhuma zilizotolewa.

    Miezi michache iliyopita serikali ya Tanzania ilipiga marufuku vitabu 16 vya mfululizo wa vitabu vya watoto kutumika shuleni kwa madai ya kutetea haki za wapenzi wa jinsia moja -LGBTQ.

    Mfululizo wa Diary of a Wimpy Kid unasemekana kukiuka mila, desturi na tamaduni za nchi.

    Waziri wa Elimu Adolf Mkenda alisema kuwa vitabu hivyo vinahatarisha ubora wa elimu kwa watoto.

    Shule zinazotumia vitabu hivyo zitachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria, ikiwa ni pamoja na kufutiwa usajili wao, mamlaka ilisema.

    Vitabu vilivyopigwa marufuku ni:

    ·Diary of a Wimpy Kid: Rodrick Rules

    ·Diary of a Wimpy Kid: The Last Straw,

    ·Diary of a Wimpy Kid: The Ugly Truth

    ·Diary of a Wimpy Kid: Cabin Fever.

    ·Diary of a Wimpy Kid: The Third Wheel

    ·Diary of a Wimpy Kid: Hard Luck

    ·Diary of a Wimpy Kid: The Long Haul

    ·Diary of a Wimpy Kid: Old School

    ·Diary of a Wimpy Kid: Double Down

    ·Diary of a Wimpy Kid: The Gateway

    “Hii ni orodha ya kwanza, baada ya kuhakiki na kuthibitisha kuwa vitabu hivi vinakiuka mila na desturi, yaliyomo ndani yake si mazuri kwa malezi ya Watanzania, uhakiki unaendelea,” alisema Prof Mkenda.

  5. Ndege ya Uturuki yashambuliwa huko Sudan

    Turkey

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ndege ya Uturuki iliyokuwa ikitua katika kambi ya anga nje ya mji mkuu wa Sudan, Khartoum, imeshambuliwa, wizara ya ulinzi ya Uturuki imethibitisha.

    Hakuna aliyejeruhiwa na ilitua salama Wadi Seidna, ambako ilikuwa ikikaguliwa. Jeshi la Sudan limewalaumu wapiganaji wa RSF kwa kufanya shambulio hilo na kuharibu mfumo wake wa mafuta.

    Vikosi vya RSF vinavyopambana na Jeshi la serikali vilikanusha madai hayo, vikisema kuwa vimejitolea katika kulinda haki za kibinadamu.

    Muda wa kusitisha mapigano Sudan umerefushwa lakini mapigano yanaendelea

    Taarifa kutoka Sudan, na kwingineko barani zinasema makundi hasimu ya kijeshi yalikubali kurefusha muda wa kusitisha mapigano usiku wa manane saa za huko (Saa 22:00 GMT siku ya Alhamisi) kwa siku tatu zaidi.

    Makubaliano ya awali yaliruhusu maelfu ya watu kujaribu kuondoka kwa usalama nchini humo, huku mataifa kadhaa yakipanga kuondoa raia wao.

    Waziri wa ulinzi wa Uturuki amesema juhudi zitaendelea kuwaokoa raia wa Uturuki kutoka Wadi Seidna na mji wa Port Sudan kwenye pwani ya Bahari Nyekundu.

    Tangu mapigano hayo yaanze siku 14 zilizopita, mamia ya watu wameuawa na makumi ya maelfu kulazimishwa kuyakimbia makazi yao.

  6. Mahakama yaambiwa waliokufa kwenye Kanisa la mchungaji Ezekiel walizikwa Shakahola kwa Mackenzie.

    Odera

    Chanzo cha picha, Nation

    Maafisa upelelezi nchini Kenya wanadai kuwa wana ushahidi wa kuaminika kwamba baadhi ya watu waliofariki katika kanisa la Odero walizikwa huko Shakahola katika eneo linalomilikiwa na kiongozi wa madhehebu ya Kilifi Paul Mackenzie.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari Kenya, Mhubiri mwenye utata Ezekiel Odero na kiongozi wa madhehebu ya Kilifi Paul Mackenzie ni watu wanaofahamiana, mahakama ya Shanzu ilielezwa leo Ijumaa.

    Chombo cha Nation kunaripoti kuwa Maafisa wa upelelezi wamegundua uwepo wa uhusiano wa karibu kati ya Odero wa Kanisa la New Life lenye makao yake Mavueni na Mackenzie ambaye anadaiwa kuwashawishi wafuasi wake kufunga mpaka kufa ili kukutana na Mungu.

    Wafuasi zaidi ya 100 wanadaiwa kupoteza maisha kwa ibada hiyo ya ‘kufunga mpaka kufa’.

    Maafisa wa upelelezi pia walisema wamefuatilia miamala ya fedha na kubaini kuwepo kwa muamala wa Sh3 milioni katika miamala ya kifedha kati ya Odero na Mackenzie inayotajwa ni kwa ajili ya kuuzia kituo cha TV.

    Odero alikiri kununua kituo hicho cha TV kutoka kwa Mackenzie lakini akasema biashara hiyo haipaswi kuhusishwa na vifo vya Shakahola.

    Odero anatuhumiwa kwa mauaji, kusaidia watu kujiua, utekaji nyara, itikadi kali, mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya ubinadamu, ukatili wa watoto, ulaghai, utakatishaji fedha na kusaidia uhalifu, mahakama kesi ikisikilizwa Mahakamani.

    th
  7. Urusi yaua 19 kwa shambulio kubwa zaidi la anga huko Ukraine katika miezi miwili iliyopita

    Ukraine

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Urusi imerusha makombora katika miji kote nchini Ukraini Ijumaa na kuua takriban watu 19 katika mashambulio makubwa ya kwanza ya anga katika kipindi cha karibu miezi miwili.

    Mashambulizi haya ya asubuhi yalitekelezwa wakati Kyiv inajiandaa kufanya mashambulizi ya kujaribu kulirejesha tena eneo lililokaliwa na Urusi.

    Katika jiji la kati la Uman, wazima moto walipambana na moto mkali katika jengo la makazi ambalo lilikuwa limeshambuliwa kwenye ghorofa ya juu. Takriban watu 10 waliuawa, wakiwemo watoto wawili, na tisa walipelekwa hospitalini, gavana wa mkoa Ihor Taburets alisema.

    Mwanaume mtu mzima aliyevalia barakoa aliliakwa uchungu, na mwanamke akaja kumliwaza. "Mwanzoni madirisha yalilipuliwa, kisha mlipuko mkubwa ukatokea," mkazi wa jengo hilo la ghorofa ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Olga alisema wakati waokoaji wakiendelea kufukua vifusi. "Kila kitu kilirushwa nje."

  8. Mzozo wa Sudan: Uingereza yamhamishia balozi wake wa Sudan, Ethiopia

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Zaidi ya Waingereza 500 wamekwisha okolewa hadi sasa kutoka Sudan

    Uingereza inasema Giles Lever, balozi wake nchini Sudan, amehamishiwa katika nchi jirani ya Ethiopia baada ya kufungwa kwa ubalozi wake kwa muda, kulikosababishwa na mzozo katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

    ‘’Kutoka Addis Ababa, ataongoza juhudi za kidiplomasia katika kanda hiyo ili kumaliza vita nchini Sudan", Wizara ya mambo yan je ya uingereza ilisema katika taarifa.

    Hadi sasa, Waingereza 536 wamekwisha okolewa kutoka Sudan, mamlaka za Uingereza zimesema.

    Lakini kumekuwa na ukosoaji wa kuzorota kwa uokoaji wa serikali ukilinganishwa na nchi nyingine za Magharibi.

    Jeshi la Sudan na kikundi cha jeshi la dharura - Rapid Support Forces (RSF) wamekubaliana kuongeza muda wa mkataba wa usitishaji kwa saa nyingine 72 zaidi.

    Unaweza pia kusoma:

    • Sudan: Kikosi cha kukabiliana na dharura RSF ni kikosi cha aina gani?
    • Sudan: Jinsi vikosi hasimu vya jeshi Sudan vinavyotoa madai ya ushindi yanayopingana
    • Mgogoro wa Sudan: Majenerali wanaopigania hatima ya Sudan
  9. Afisa wa chama tawala wa jimbo la Amhara nchini Ethiopia auawa

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mauaji yanakuja wiki kadhaa baada ya kuvunjwa kwa kikundi cha wanajeshi wa kijimbo jambo lililoibua ghasia katika Amhara.

    Mkuu wa chama cha Prosperity nchini katika jimbo la Ethiopia la Amhara amepigwa risasi na kufa, pamoja na maafisa wengine wa usalama, wamesema maafisa.

    Girma Yeshitla alikuwa akirudi kutoka kwenye ziara rasmi wakati alipopigwa risasi yapata kilomita 250 (maili 155 ) kaskazini mwa mji mkuu Addis Ababa, kulingana na taarifa iliyotolewa na afisa mawasiliano wa jimbo.

    Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ameyaita mauaji hayo ya "aibu nay a kutisha" na akawalaumu "watu wenye itikadi kali za ghasia" ambão hakuwataja ambao alisema walichagua kumaliza tofauti kwa bunduki kuliko mazungumzo.

    Mauaji hayo yanakuja baada ya serikali kuu yakutangaza kuvunja kikosi cha jimbo, jambo lililoibua ghasia na maandamano katika Amhara.

    Bw Girma alikabiliwa na ukosoaji kutoka kwa wanaopinga kuvunjwa kwa kikosi, ambao walimuona kama watu waliopanga hatua hiyo.

    Mauaji ya maafisa wa ngazi ya juu wa kisiasa katika jimbo la Amhara sio jambo geni. Katika mwaka 2019, kiongozi wa kikanda na maafisa wengine wa kisiasa waliuliwa katika kile kilichoelezwa kama jaribio la mapinduzi lililoshindwa.

    Unaweza pia kusoma:

    • 'Kiongozi wa mapinduzi' Amhara, Ethiopia auawa na polisi
  10. Je unaweza kushiriki chakula cha jioni ukiwa uchi na watu 40 usiowafahamu?

    g

    Je unaweza kushiriki chakula cha jioni ukiwa uchi na watu 40 usiowafahamu?... wakati ukitafakari hayo. nchini Marekani upo mgahawa unaowapokea wateja wanaopenda kupata mlo wakiwa watupu.

    "The Füde Breathwork Experience" mjini New York City ni hafla ya chakula cha jioni ambapo washiriki hula chakula huku wakiwa uchi wa myama.

    Gharama ya kiingilio ni kuanzia $44 hadi $88 (£35-£70), ambazo zijtakuwezesha kushiriki pia mazoezi ya kupumua na hatimayekula mlo usiokuwa na nyama yaani chakula kitokanacho na mimea…huku nyote mkiwa uchi wa mnyama.

    Wateja kwenye mgahawa huo, mara nyingi huwa ni watu ambao hawafahamiani, lakini huketi pamoja na kula chakula.

    Lengo la hafla ya ya Füde ni kuwasaidia watu kuungana na 'uhalisia wao sahihi, na nafsi halisi'.

  11. Rwanda: Watu 6 waliofunikwa na udongo kwenye ‘mgodi wa ajabu’ wasakwa kwa siku ya 8 sasa

    g

    Chanzo cha picha, RADIOHUYE/RBA

    Maelezo ya picha, Mashine zikifukua kwenye eneo la machimbo kuwasaka watu sita waliofunikwa na udongo

    Ni zaidi ya wiki moja sasa tangu watu sita wakiwemo wanafunzi watatu wa Shule ya sekondari- Groupe Scolaire Kinazi katika wilaya ya Kinazi – jimbo la kusini la Huye wangukiwa na udongo wakati walipokuwa wakichimba mgodi. Shughuli ya kuwasaka hadi sasa haijaweza kuzaa matunda.

    Msako wa watu hao iliendelea Alhamisi baada ya kusitishwa Juamatano baada ya sehemu nyingine ya udongo kuporoka katika eneo hilo, Jean Marie Ntakiyimana, mkazi wa eneo la Kinazi aliyepo katika eneo la tukio, aliimbia BBC.

    Maporomoko ya udongo kwenye'mgodi' huo yalitokea Jumatano wiki iliyopita, huku baadhi ya wenyeji wakidai kuwa hawakuwa na habari kuhusu kuwepo kwa mgodi wa madini.

    Maafisa wa serikali wanasema kuwa machimbo hayo hayatambuliki na haikubaliki kisheria kuanzisha machimbo ya madini bila idhini ya serikali.

    g
    Maelezo ya picha, Ramani ya eneo la tukio

    ‘Machimbo ya ajabu’

    Hakujawahi kuwa na uvumbuzi wowote wa madini katika wilaya ya Huye iliyopo kusini mwa Rwanda.

    Taasisi ya inayohusika na ‘’uchimbaji wa madini’’ nchini rwandailitoa tangazo Jumatano kwamba machimbo haya “hayakubaliki kisheria”, na kuongeza kuwa yapo “mahala pasipokubalika”, wanaoyatumia “hawajulikani” na kwamba uchunguzi unafanyika ili “kuwawajibisha wahusika”.

  12. Vita vya Ukraine: 12 wafariki wakati makombora ya Urusi yakipiga miji

    g

    Chanzo cha picha, SOCIAL MEDIA

    Maelezo ya picha, Picha zinasambazwa kwenye mitandao ya kijamii za uharibifu wa jengo katika mji wa Uman

    Mashambulizi ya anga ya Urusi yameshambulia miji kote Ukraine, ukiwemo mji mkuu wa Kyiv, na kuua takriban watu 12.

    Watu kumi walikufa katikati mwa jiji la Uman baada ya makombora kugonga majengo ya makazi, maafisa walisema.

    Na mwanamke na binti yake wa miaka mitatu waliuawa katika jiji la Dnipro, kulingana na meya wa eneo hilo.

    Kulikuwa pia na milipuko katika miji ya Kremenchuk na Poltava, kulingana na shirika la habari la Interfax.

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema majengo 10 ya makazi yameharibiwa huko Uman na kusema mashambulizi hayo yanaonyesha hatua zaidi za kimataifa zinahitajika kuchukuliwa dhidi ya Urusi.

    "Uovu unaweza kuzuiwa na silaha - watetezi wetu wanafanya hivyo. Na unaweza kuzuiwa kwa vikwazo - vikwazo vya kimataifa lazima viimarishwe," alisema katika Twitter

    Mkuu wa utawala wa kijeshi wa mji wa Kyiv alisema hilo lilikuwa shambulio la kwanza la kombora la Urusi kwenye mji mkuu katika muda wa siku 51.Hakuna ripoti za mara moja za vifo vya raia katika mji mkuu.

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  13. Gough Island: Wafanyakazi waliopata ajira katika moja ya maeneo yaliyo mbali zaidi kufikiwa duniani

    j

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Kisiwa cha Gough ni tegemezi kwa Tristan da Cunha – ambacho ni eneo la Uingereza lililopo kusini mwa Atlantiki

    Kikundi cha wanayamapori cha Uingereza kinamtafuta mtu wa kufanya kazi katika mojawapo ya visiwa vilivyo mbali zaidi kufikiwa duniani kwa ajili ya kufanya kazi kwa miezi 13 .

    Kisiwa cha Gough au Gough Island, ambacho ni shehemu ya nchi ya Uingereza kinapatikana ndani ya Bahari ya Atlantic na hakina wakazi wa kudumu.

    Kiko karibu umbali wa maili 1,500 (2,400km) kutoka eneo la bara la Afrika - na kutokana na kwamba hakina uwanja wa ndege, kufika Gough unahitaji kusafiri kwa boti kwa siku saba kutoka Afrika Kusini.

    g

    Chanzo cha picha, ANTJE STEINFURTH

    Maelezo ya picha, Lucy na Rebekah katika Gough

    Ni safari ambayo tayari imekamilishwa na Rebekah Goodwill - na Lucy Dorman, ambao kwa sasa wanafanya kazi katika Gough.

    Ni miongoni mwa wafanyakazi saba wenye ajira ya kudumu- wakiishi na ndege milioni nane - ambao wanakiita Kisiwa cha Gough nyumbani.

  14. Mzozo wa Sudan: Muda wa kusitisha mapigano umeongezwa lakini mapigano yanaendelea

    n

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Watu wametumia muda mfupi wa usitishaji mapigano Kwenda nje ya nyumba zao

    Makundi ya kijeshi yanayohasimiana yamekubaliana kuongeza upya siku tatu za usitishaji mapigano, muda mfupi kabla ya kipindi cha awali kumalizika.

    Kuongezwa- kwa muda wa saa 72 – kunafuatia juhudi kubwa za kudiplomasia za nchi Jirani, pamoja na Marekani, Uingereza na Umoja wa Mataifa.

    Lakini kumekuwa na ripoti za kuendelea kwa mapigano makali katika mji mkuu Khartoum.

    Mkataba wa awali uliwaruhusu maelfu ya watu kujaribu kukimbia , huku makumi kadhaa ya nchi zikijaribu kuwaokoa watu wake.

    Mapigano ya wiki takriban mbili kati ya jeshi na kikundi hasimu cha kijeshi yamewauwa watu mamia kadhaa.

    Muda wa kusitisha mapigano ulitarajiwa kuisha usiku, saa nne kwa saa za eneo(22:00 GMT).

    Alhamisi usiku jeshi la Sudan lilikubali kuongezwa kwa muda huo, na baadaye mahasimu wao wa kikosi cha dharura- Rapid Support Forces (RSF) wakakubali kufanya hivyo.

    Sudan Kusini imejitolea kupokea mazungumzo ya amani, na jeshi limekubali kutuma wawakilishi wake kwenye mazungumzo.

    Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken samesema kuwa Washington ina "inafanya kazi kubwa" kuhakikisha kunakuwepo na mkataba wa usitishaji mapigano, na kuongeza kuwa licha ya kwamba sio mkamilifu umepunguza ghasia.

    Lakini msemaji wa White House Karine Jean-Pierre baadaye alisema kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi wakati wowote.

    Wakati huo huo kundi RSF na mashahidi wanasema kuwa jeshi likipoteza maeneo yake katika mjini Khartoum.

    Mapigano yamekuwa yakiripojtiwa katika jimbo la magharibi la Darfur na majimbo mengine.

    Takriban watu 512 wameuawa katika mapigano huku 4,200 wakijeruhiwa, licha ya kwamba idadi halisi ya vifo inaweza kuwa kubwa zaidi.

    Unaweza pia kusoma:

    • Sudan: Kikosi cha kukabiliana na dharura RSF ni kikosi cha aina gani?
    • Sudan: Jinsi vikosi hasimu vya jeshi Sudan vinavyotoa madai ya ushindi yanayopingana
    • Mgogoro wa Sudan: Majenerali wanaopigania hatima ya Sudan
  15. Hujambo na karibu tena kwa matangazo yetu ya moja kwa moja, leo ikiwa ni tarehe 28.04.2023