Marekani inachukua hatua kuhakikisha ndege isiyo na rubani haitaangukia mikononi mwa adui zake - Kirby

Msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa Ikulu John Kirby ameambia CNN kwamba Marekani "imechukua hatua" kuzuia ndege isiyo na rubani ya MQ-9 Reaper iliyoanguka kwenye Bahari Nyeusi Jumanne kupatikana na watu wenye nia mbaya.

Moja kwa moja

  1. Na kufikia hapo ndio tumekamilisha matangazo yetu kwa leo.

  2. Sudan Kusini:Waandishi habari waachiliwa huru baada ya kuhusishwa na video inayoonesha rais akitokwa na haja ndogo

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Video ya Bw Kiir ilirekodiwa Desemba mwaka jana

    Wanahabari wawili kati ya wanne waliozuiliwa mwezi Januari baada ya video inayomuonyesha rais wa Sudan Kusini akilowesha suruali yake kwenye hafla ya hadhara wameachiliwa.

    Muungano wa chama cha Wanahabari Sudan Kusini (UJOSS) umesema katika taarifa yake kwamba unafurahishwa na kuachiliwa kwa Victor Ladu na Mustapha Osman.

    Mnamo mwezi Desemba mwaka jana, video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ilionekana kumuonyesha Bw Kiir akijikojolea huku wimbo wa taifa ukipigwa kwenye hafla.

    Wafanyikazi sita kutoka shirika la utangazaji la serikali walikamatwa baadaye, lakini wawili bado wanazuiliwa.

    "[Tunaitaka] serikali kuwaachilia huru Garang John na Jacob Benjamin au ikiwa wana kesi ya kujibu, wanapaswa kuwasilishwa katika mahakama ya sheria," taarifa ya UJOSS ilisema.

    Kukamatwa huko kumeshutumiwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu ikiwa ni pamoja na Kamati ya Kulinda Wanahabari (CPJ).

    Kukamatwa kwa watu hao kunalingana na "mtindo wa maafisa wa usalama kuzuia wat kiholela wakati maafisa wanaona kuwa utangazaji wao haufai", alisema mwakilishi wa CPJ Kusini mwa Jangwa la Sahara, Muthoki Mumo alisema wakati huo.

    Soma zaidi:

  3. Marekani inachukua hatua kuhakikisha ndege isiyo na rubani haitaangukia mikononi mwa wenye nia mbaya - Kirby

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa Ikulu John Kirby ameambia CNN kwamba Marekani "imechukua hatua" kuzuia ndege isiyo na rubani ya MQ-9 Reaper iliyoanguka kwenye Bahari Nyeusi Jumanne kupatikana na watu wenye nia mbaya.

    "Hakika hatutaki mtu yeyote ila sisi tu kuipata ndege hiyo," Kirby alisema.

    Hapo awali, Brigedia Jenerali Patrick Ryder, msemaji wa Wizara ya Ulinzi nchini Marekani, alisema kuwa ndege hiyo isiyo na rubani iliyoanguka haikuwa mikononi mwa wanajeshi wa Urusi.

    Awali, rekodi ya sauti ilionekana kwenye chaneli za televisheni zinazounga mkono jeshi la Urusi, ambapo unaweza kusikia jinsi watu wengine wanajadiliana kwa Kirusi kuhusu kuinua baadhi ya mabaki ya ndege isiyo na rubani iliyoanguka kutoka chini.

    Inadaiwa kuwa inawezekana kuinua "injini ya ndani" ya ndege hiyo ingawa taarifa hizi bado hazijathibitishwa rasmi.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Mpiga gitaa maarufu wa Congo Lokassa ya Mbongo amefariki dunia nchini Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mpiga gitaa wa Congo Denis Lokassa Kasiya, almaarufu Lokassa ya Mbongo, amefariki dunia Jumanne usiku nchini Marekani baada ya kuugua kwa muda mrefu.

    Lokassa, ambaye hivi majuzi alifikisha umri wa miaka 80, alikuwa kiongozi wa bendi maarufu ya Soukous Stars, iliyokuwa na makao yake mjini Paris.

    Hapo awali, aliwahi kutamba na bendi ya Tabu Ley Rochereau ya Afrisa International na baadaye bendi ya All African Stars.

    Alikuwa akiuguwa ugonjwa wa kisukari wakati huo huo, akipata nafuu kutokana na ugonjwa wa kiharusi uliokuwa kiwango cha wastani aliopata miaka michache iliyopita.

    Mwanamuziki mwenzake wa Congo anayeishi Marekani, Mekanisi Modero alisema alikuwa amefahamishwa kuhusu kifo cha Lokassa na muuguzi ambaye amekuwa akimhudumia.

    Alisema alikuwa na matatizo ya kupumua kabla ya kuzimia na kufariki huko Nashua, New Hamsphire.

    Mwanamuziki mwingine wa Congo Ngouma Lokito, anayeishi New York, alitoa habari hiyo ya kusikitisha kwa mashabiki wake kupitia ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa Facebook.

    Lokassa, mpiga gitaa na mtunzi, atakumbukwa kwa baadhi ya nyimbo zake maarufu kama vile "Bonne Annee", "Monica", "Marie-Josse" na "Assitou".

    Inasemekana alikuwa mmoja wa wapiga gitaa bora zaidi wa miondoko kutoka Congo, baada ya kutumbuiza na bendi ya Tabu Ley Rochereau ya Afrisa International kuanzia 1970 hadi 1978.

    Katika kipindi chake akiwa Afrisa, alicheza muziki pamoja na waimbaji Pepe Ndombe, Sam Mangwana na Michelino Mavatiku Visi.

    Hata hivyo, Lokassa alitumia sehemu kubwa taaluma yake ya muziki akiwa nje ya DR Congo.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Wanajeshi wa Ukraine: Ndege ya kijeshi ya Urusi imedunguliwa karibu na Bakhmut

    .

    Chanzo cha picha, 93 brigade

    Maelezo ya picha, Picha ya ndege ya Urusi iliodunguliwa karibu na Bakhmut

    Andriy Yermak, mkuu wa ofisi ya Rais wa Ukraine, anadai kuwa jeshi la Ukraine liliidungua ndege ya Urusi aina ya Su-24 karibu na Bakhmut.

    Yerman alichapisha video inayoonyesha mlipuko, na vile vile, huku rubani akijaribu kutoka katika ndege hiyo. Hatma ya rubani huyo haijulikani.

    Afisa wa vyombo vya habari wa brigedi ya 93 alithibitisha kwa waandishi wa habari kwamba ndege hiyo ilikuwa imetunguliwa.

    Su-24 ni ndege ya kijeshi ya mstari wa mbele wa vita iliyoundwa na Ofisi ya Usanifu wa Sukhoi (kampuni ya Sukhoi, sehemu ya Shirika la Ndege la Umoja) na iliyoundwa kurusha mashambulio ya makombora na mabomu katika hali nzuri na mbaya ya hewa , mchana na usiku, ikijumuisha kuruka chini chini kwa lengo la shabaha za ardhini. Ilianza kufanya kazi 1975. Wafanyakazi wake ni watu wawili.

    Urusi haijatoa maoni kwa njia yoyote juu ya ripoti za uwezekano wa upotezaji wa Su-24.

  6. Ndege za kivita za Uingereza na Ujerumani zazuia ndege za Urusi karibu na Estonia

    .

    Chanzo cha picha, RAF

    Maelezo ya picha, Ndege ya kivita

    Kulingana na waandishi wa BBC, ndege za kivita za Uingereza na Ujerumani zaizuia ndege ya Urusi karibu na anga ya Estonia.

    Usafiri wa anga wa Magharibi huzizuia ndege za kijeshi za Urusi mara nyingi, lakini hii ni operesheni ya kwanza ya pamoja ya vikosi vya anga vya Uingereza na Ujerumani.

    Ndege mbili za kijeshi zilifanikiwa kuizuia ndege ya kijeshi ya Il-78 (kulingana na uainishaji wa NATO ikwa jina Midas), iliyokuwa ikiruka kati ya St. Petersburg na Kaliningrad. Inaarifiwa kuwa ndege hiyo ya Urusi haikuwasiliana na wadhibiti wa trafiki wa anga nchini Estonia.

    Baada ya ndege hizo za kivita kuisindikiza ndege hiyo ya Il-78, zilielekezwa kuizuia ndege ya An-148, ambayo pia inasemekana iliruka karibu na anga ya Estonia.

    Wanajeshi wa angani wa Uingereza na Ujerumani hufanya kazi ya zamu katika anga ya nchi za NATO

  7. Urusi yaikabidhi Iran sampuli za silaha za Marekani zilizokamatwa nchini Ukraine - CNN

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mifumo ya kukabiliana na mashambulizi ya angani wa Marekani kwa jina javelin

    Urusi inatuma silaha za Marekani zilizokamatwa nchini Ukraine nchini Iran, ambako, kulingana na Washington, zinafanyiwa uchunguzi wa kina na wataalamu wa Iran, inaripoti CNN, ikinukuu vyanzo vya Pentagon.

    Hasa, mamlaka za Marekani zinajua kwa hakika kwamba sampuli za mifumo ya makombora ya kivita ya Marekani imeishia mikononi mwa Tehran.

    Mitambo kadhaa ya Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine ililazimishwa kuondoka kwenye uwanja wa vita.

    Vyanzo vya CNN vinaamini kuwa kwa makubaliano kama haya kati ya Moscow na Tehran, viongozi wa Iran wana nia kubwa ya kuendelea na uhasama na wataiunga mkono Urusi katika vita kwa njia zote zinazowezekana.

    Bado haijafahamika iwapo Iran imefanikiwa kunakili silaha zozote za Marekani zilizokamatwa nchini Ukraine, lakini imekuwa na rekodi ya mafanikio katika siku za nyuma katika kujenga mifumo ya silaha kwa kuzingatia miundo ya Marekani iliyoangukia mikononi mwa Wairani.

    Moja ya hatua kuu zilizopigwa na Irani, kombora la kuongozwa na kifaru cha la Toophan, lililoundwa katika miaka ya 1970 kutokana na kombora la Marekani la BGM-71 TOW.

    Mnamo mwaka wa 2011, Wairani pia walikamata ndege isiyo na rubani ya Lockheed Martin RQ-170 "Sentinel" iliyotengenezwa na Marekani na kuinakili, na kuunda ndege yao isiyo na rubani, ambayo mnamo 2018 iliweza kuvuka anga ya Israeli kabla ya kuangushwa.

    Pentagon inasema kwamba wakati wa kufanya maamuzi juu ya usambazaji wa silaha kwa nchi za tatu, hatari kama hizo huzingatiwa na hakuna sababu za wasiwasi mwingi.

  8. GPT-4:Programu ya akili bandia inayozungumza na kusaidia katika kazi nyingi yazinduliwa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kampuni ya OpenAI imetoa programu ya kompyuta ya akili bandia iitwayo GPT-4, toleo la kisasa zaidi yenye kuzungumza ambayo ni maarufu sana.

    Programu hii mpya inaweza kujibu picha - kutoa mapendekezo ya mapishi kutoka kwa picha za viungo pamoja na kuandika maelezo ya picha.

    Inaweza pia kuchakata hadi maneno 25,000, takriban mara nane ya ile roboti ya ChatGPT iliyokuwa mtangulizi wake.

    Mamilioni ya watu wametumia programu ya ChatGPT tangu ilipozinduliwa mnamo Novemba 2022.

    Maombi ambayo yamekuwa maarufu ni pamoja na kuandika nyimbo, mashairi, nakala ya uuzaji, msimbo wa kompyuta, na kusaidia katika masomo ya ziada nyumbani - ingawa walimu wanasema wanafunzi hawapaswi kuitumia.

    ChatGPT hujibu maswali kwa kutumia lugha asilia inayofanana na binadamu, na inaweza pia kuiga mitindo mingine ya uandishi kama vile watunzi wa nyimbo na waandishi, kwa kutumia mtandao kama ilivyokuwa mwaka wa 2021 kama hifadhidata yake ya maarifa.

    Kuna wasiwasi kwamba siku moja programu hiyo inaweza kuchukua kazi nyingi zinazofanywa na wanadamu kwa sasa.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Marubani wa Urusi walikua wazembe katika kuendesha droni iliyogongwa - Marekani

    g

    Chanzo cha picha, EPA

    Marekani imeishutumu Urusi kwatabia ya uzembe baada ya ndege isiyokuwa na rubani ya Marekani kuanguka ndani ya Bahari Nyeusi kufuatia kugongana na ndege za mapigano za Urusi.

    Kabla ya kugongana, ndege za mapigano aina ya jet za Urusi zinasemekana kumwaga mafuta katika njia ya droni , ambayo marekani inasema ilikuwa ni njia ya safari za anga za kimataifa.

    Droni ya MQ-9 Reaper iliangushwa Jumanne baada ya makabiliano yaliyodumu kwa muda wa dakika kati ya 30-40, Marekani ilisema.

    Urusi inakanusha kwamba ndege zake mbili za mapigano aina ya jet Su-27 zilizofanya mawasiliano.

    Swali muhimu ni iwapo mgongano ulikua ni jaribio tu la Urusi la kuvuruga droni ya Marekani na kazi yake- au iwapo lilikuwa ni jaribio la kuiangusha chini.

    Maafisa wa kijeshi wa marekani wanasema tukio hillo lilitokea saa moja na dakika 3(06:03 GMT) Jumanne.

    Mara kadhaa kabla ya mgongano, jest za kivita ziliangusha mafuta kwenye droni"kiuzembe, bila kujali mazingira na kwa uzembe , bila maadili ya kitaaluma", ilisema taarifa hiyo.

    Iliongeza kuwa : "ndege zetu za MQ-9 ilikuwa katika operesheni yake ya kwaida katika anga la kimataifa ilipopigwa na ndege ya Urusi, na kusababisha kuanguka na kupotea kabisa kwa MQ-9."

    Katika jibu lake kwa Marekani, Wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema kuwa droni ilianguka baada ya "kukwepa kwa ujanja" na kuongeza kuwa droni ya MQ-9 Reaper ilikuwa inasafiri huku Transponders zake zikiwa zimezimwa. Transponders ni vifaa vya mawasiliano vinavyoruhusu ndege kufuatiliwa.

  10. Wanajeshi miongoni mwa waliotoweka katika kimbunga Malawi

    Malawi

    Chanzo cha picha, AFP

    Wanajeshi wawili wa Malawi walitoweka baada ya mashua yao ya uokoaji kusombwa na maji siku ya Jumanne katika eneo la Mulanje kusini

    Gazeti la New York Times linamnukuu msemaji wa jeshi akisema kuwa ujumbe huo ulitatizwa na mto uliojaa.

    Askari hao walikuwa ni sehemu ya wafanyakazi sita waliokwenda kuokoa watu waliokwama baada ya Kimbunga cha Tropiki Freddy kukumba eneo hilo, Waziri wa Serikali ya Mtaa Richard Chimwendo Banda aliambia chombo cha habari cha eneo hilo.

    Wanajeshi wengine wawili na raia mmoja walifanikiwa kuogelea na kujiokoa baada ya boti yao kukumbwa na hitilafu ilipokuwa njiani kuelekea kazi ya uokoaji, waziri aliiambia Zodiak Online.

    Bw Banda alisema mmoja wa askari waliotoweka alionekana kwenye mti na juhudi za kumwokoa zinaendelea.

    Kumbunga Freddy, dhoruba iliyovunja rekodi ambayo ilitua katika taifa hilo lisilo na bandari kusini-mashariki mwa Afrika mwishoni mwa juma, imesababisha vifo vya zaidi ya watu 200.

    Kituo cha kibiashara cha Malawi, Blantyre, kimeshuhudia vifo vingi, ikiwa ni pamoja na makumi ya watoto. Mamlaka imechelewesha kufunguliwa kwa shule hadi Ijumaa na kutangaza hali ya dharura katika wilaya 10 za kusini ambazo zimeathiriwa zaidi na kimbunga hicho.

  11. Marekani itaendeleza juhudi za kuwalinda wapenzi wa jinsia moja

    G

    Chanzo cha picha, William Samoei Ruto PHD/Twitter

    Maelezo ya picha, Balozi wa Marekani nchini Kenya Meg Whitman

    Balozi wa Marekani nchini Kenya Meg Whitman anasema Marekani itaendelea kuzilinda haki za wapenzi wa jinsia moja na jamii ya LGBTQI+ kwa ujumla.

    Katika ujumbe wake kupitia mtandao wa Twitter Balozi White alisema: “Katika kipindi cha wiki moja iliyopita mimi na timu yangu tulikutana watu wa makundi ya LGBTQI+ na wadau kusaidia haki za kibinadamu za watu LGBTQI+ . Marekani inajivunia kuendeleza juhudi za kuwalinda LGBTQI+ dhidi ya ubaguzi na unyanyasaji na itaendelea kutetea haki za binadamu na usawa,” BaloziWhitman alisema.

    Ruka X ujumbe
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe

    Taarifa ya Whitman inakuja wakati rais wa Kenya William Ruto pamoja na viongozi wa kidini nchini humo wakiwa tayari wamepinga hadharani uamuzi wa mahakama ya juu zaidi ulioruhusu usajiri wa mashirika ya LGBTQI+ nchini humo.

    Hatahivyo, Balozi Whitman amesema kwamba Marekani haitaingilia msimamo wa Kenya kuhusu suala la wapenzi wa jinsia moja (LGBTQI+) , akisema kuwa kila nchi ina uhuru wa kufanya maamuzi yake kuhusu jinsi ya kushughulia suala la haki za wapenzi wa jinsia moja.

  12. Mbunge atimuliwa bungeni kwa kutohuria vikao vya bunge tangu achaguliwe

    g

    Chanzo cha picha, GAASYY/YOUTUBE

    Mbunge wa bunge la seneti nchini Japan ametimuliwa kazini baada ya kutohudhuria kikao chochote cha bunge kwa mieza saba.

    Mwanaume huyo ambaye ni maarufu sana katika mtandao wa You Tube – amekuwa mbunge wa kwanza kufutwa kazi bila kuwahi hata siku moja kuingia bungeni tangu achaguliwe

    Maseneta walimfuta kazi Seneta Yoshikazu Higashitani Jumanne kwa kutohudhuria vikao vya bunge.

    Tangu achaguliwe miezi saba iloyopita, hajawahi kuhudhuria hata kikao kimoja cha bunge.

    Ni mtumiaji wa You Tube maarufu

    Mwezi Julai 2022, Bw Higashitani alichaguliwa kama seneta

    Seneta huyo anayefahamika kwa jina maarufu kama 'GaaSyy' kwenye YouTube ambako ni maarufu sana kwa video zake maarufu – amekuwa ni senet awa kwanza kuwahi kufukuzwa kazini kwa kukataa kuhudhuria vikao.

    Kufutwa kazi ndio adhabu kubwa zaidi ambayo mbunge anaweza kupewa nchini Japan.

    Taarifa zinasema kuwa mbunge huyo anaishi katika Milki za Kiarabu

    Vyombo vya habari vya Japan vilisema kuwa alikataa kuhudhuria vikao vya bunge kwa hofu ya kukamatwa kwa shutuma za wizi na kumtusi mtu mashuhuri.

  13. Usiku wa mafanikio kwa Halaand huku Manchester city wakifuzu kuingia robo fainali

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Erling Haaland ameandikisha upya historia kwa kufunga mabao mara tano , huku Manchester City wakiwafagia na kuwaweka kando RB Leipzig ili kufika robo fainali katika Championi Ligi.

    Haaland anakuwa ndiye mchezaji mwenye kasi zaidi na mwenye umri mdogo kufikia maggoli 20 katika shindano hilo la Ulaya.

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Pia ni mchezaji mwenye umri mdogo zaidikufunga mara tano katika mecho moja ya Championi Ligi, akijiunga na mchezaji nyota wa Argentina Lionel Messi na mshambuliaji Mbrazil Brazil Luiz Adriano kama wachezaji pekee waliofanikiwa kufanya hivyo.

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Halaand mwenye umri wa miaka 22 amekwishafunga mabao 39 tayari katika msimu huu katika mashindano yote, akiwa ndiye mchezaji pekee wa City kufikia idadi hiyo mabao katika msimu mmoja.

    Soma zaidi:

    • Kwanini Haaland anaweza kuipaisha Manchester City?
    • Tetesi za Soka Ulaya Jumatano 15.03.2023
  14. Daktari aliyefichua siri ya serikali ya China kuhusu janga la Sars afariki akiwa na miaka 91

    Jiang Yanyong aliyefichua kuhusu kesi za siri za mamlaka ya Uchina za Sars

    Chanzo cha picha, ge

    Jiang Yanyong, daktari wa zamani wa kijeshi wa upasuaji ambaye alifichua mamlaka ya China kuhusu janga la Sars la mwaka 2003 amefariki akiwa na umri wa miaka 91.

    Alikufa kwa tatizo la homa ya mapafu siku ya Jumamosi huko Beijing, marafiki wa familia na vyombo vya habari vya lugha ya Kichina huko Hong Kong viliripoti.

    Dkt Jiang alisifiwa kwa kuokoa maisha baada ya kuandika barua katika hatua ya awali ya mzozo wa Sars ambayo ilifichua kuwa maafisa walikuwa wakipuuza tishio hilo.

    Lakini alistahimili kifungo cha nyumbani wakati fulani kwa kusema kwake bila kuyumbayumba.

    Daktari huyo mkuu alikuwa akifanya kazi katika hospitali ya Beijing mnamo Aprili 2003, wakati alishtuka kusikia Waziri wa Afya wa China akiuambia umma kulikuwa na kesi chache tu za ugonjwa mpya mbaya wa kupumua.

    Dkt. Jiang alisema anafahamu zaidi ya watu 100 walio na Sars katika hospitali za kijeshi pekee. Alituma barua kufichua uwongo huo katika simulizi rasmi kwa watangazaji wa serikali ya China, ambao walipuuza.

    Lakini barua hiyo ilivujishwa kwa vyombo vya habari vya kigeni ambavyo vilichapisha kwa ukamilifu.

    Ufichuzi wake uliilazimu serikali ya China kukiri kuwa ilikuwa imetoa habari za uwongo kuhusu janga hilo, na kulichochea Shirika la Afya Ulimwenguni kuchukua hatua.

    Hatua kali za kuzuia ziliwekwa mara moja, ambazo zilisaidia kudhibiti kuenea kwa virusi. Vitendo vyake pia vilisababisha kufutwa kazi kwa waziri wa afya wa China na meya wa Beijing wakati huo.

    "Nilihisi ni lazima nifichue kilichokuwa kikifanyika, sio tu kuokoa China, lakini kuokoa ulimwengu," alisema.

  15. Mwanamke afungwa kwa madai ya uongo ya kubakwa aliyoyatoa

    g

    Chanzo cha picha, CUMBRIA CONSTABULARY

    Maelezo ya picha, Williams alidai wafanya biashara haramu walimshambulia kwa nyundo, lakini picha zavideo ya CCTV zinaonyesha akinunua nyundo mwenyewe.

    Mwanamke aliyetoa madai ya udanganyifu kwamba alibakwa na wanaume wengi na kusafirishwa kiharamu na genge la wanaume wanaopewa mafunzo Asia amefungwa gerezani kifungo cha miaka minane na nusu.

    Eleanor Williams alisababisha maandamano ya umma katika mji Barrow nchini Uingereza anakoishi baada ya kutuma picha kwenye mitandao ya kijamii za majerehaambayo alisema yalisababishwa na kipigo alichopata.

    Lakini mahakama ya Preston Crown Court ilibaini kuwa alijisababishia majeraha mwenyewe.

    Williams, 22, alipatikana na hatia ya kupotosha njia ya haki.

    Katika hukumu iliyosomwa kwa muda wa siku mbili, mahakama iliambiwa kuwa wanaume watatu ambao Bi Williams aliwashutumu kwa uongo kwa kipindi cha miaka mitatu walijaribu kujiua baada ya kulengwa na waliishi"maisha magumu duniani ".

    Mmoja wao - Jordan Trengove – alifungwa siku 73 gerezani, katika mahabusu ya watu wenye makosa ya kingono baada ya kushitakiwakutokana na madai ya Bi Williams.

    Wanaume hao walikuwa wametoka kutembea usiku machi 2019 wakati alipopelekwa nyumbani baada ya kulewa.

    Baadaye Williams alidai kuwa Bw Trengove alikuwa amembaka usiku ule, halafu mara mbili, alidai alimshambulia na kutishia maisha yake kwa kisu.

  16. Blinken awasili Ethiopia, kuzungumza na serikali na maafisa wa AU

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken, amewasili katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa wakati akianza ziara ya mataifa mawili ya Afrika.

    Alipokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Mesganu Agra alipowasili.

    Wakati wa kukaa kwake Addis, Bw Blinken anatarajiwa kukutana na maafisa wakuu wa Ethiopia na Umoja wa Afrika.

    Jambo kuu la majadiliano litakuwa utekelezaji wa makubaliano ya amani ya kihistoria yaliyofikiwa Novemba mwaka jana kati ya serikali ya shirikisho ya Ethiopia na wapiganaji kutoka eneo la Tigray nchini humo ili kumaliza vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka miwili.

    Mashirika ya utetezi yamemtaka Waziri wa Mambo ya nje kuweka haki za binadamu na uwajibikaji kwa uhalifu uliofanywa wakati wa vita kwenye ajenda yake.

    Bw. Blinken atasafiri hadi Niger baada ya Ethiopia ambako atajadili kuongezeka kwa harakati za wanajihadi katika eneo la Sahel.

  17. Wanawake wa Nigeria waliosafirishwa kwenda Libya waokolewa Niger

      • Author, Chris Ewokor
      • Nafasi, BBC News, Abuja
    Maelezo ya waathiriwa yalionesha kuwa wanatoka zaidi kusini mwa Nigeria

    Shirika la kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu nchini Nigeria linasema kuwa linachunguza hali iliyosababisha ulanguzi wa wanawake kumi na mmoja wa Nigeria kutoka nchini humo.

    Waathiriwa waliokolewa katika nchi jirani ya Niger walipokuwa wakisafirishwa kuelekea Libya na kitengo cha biashara ya binadamu.

    Waathiriwa ambao wote walikuwa vijana, walirejeshwa nchini Nigeria na kukabidhiwa kwa Wakala wa Kitaifa wa Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu, (NAPTIP), huko Sokoto, kaskazini magharibi mwa Nigeria.

    Kamanda wa NAPTIP Kanda ya Sokoto, Abubakar Tabra aliiambia BBC kwamba waathiriwa walipokelewa kutoka kwa maafisa wa Huduma ya Uhamiaji ya Nigeria, Kamandi ya Mpaka wa Illela mwishoni mwa juma lililopita, na wamehifadhiwa katika makazi yao salama wakiendelea na uchunguzi wa familia ili kuwezesha wasichana hao kuunganishwa na familia zao.

    Maelezo ya waathiriwa yalionesha kuwa wanatoka zaidi kusini mwa Nigeria. Inasemekana waliibiwa simu na bidhaa zao katika vichaka vya Jamhuri ya Niger ambapo wafanyabiashara wao waliwatelekeza; kabla ya kuokolewa na Polisi wa Niger na kuwakabidhi maafisa wa uhamiaji wa Nigeria mpakani.

  18. Kimbunga Freddy: Malawi yatangaza maafa huku zaidi ya 200 wakipoteza maisha

    Uharibifu wa barabara na madaraja umetatiza juhudi za kutoa misaada

    Chanzo cha picha, EPA

    Zaidi ya watu 200 sasa wamethibitishwa kufariki nchini Malawi baada ya kimbunga Freddy kukumba eneo la kusini mwa Afrika kwa mara ya pili ndani ya mwezi mmoja. Kiasi kikubwa cha maji yametiririka katika vitongoji, na kusomba nyumba.

    Kituo cha kibiashara cha Malawi, Blantyre, kimerekodi vifo vingi, ikiwa ni pamoja na makumi ya watoto. Mashirika ya misaada yanaonya kwamba uharibifu huo utaongeza mlipuko wa kipindupindu nchini Malawi.

    Serikali imetangaza hali ya maafa katika wilaya 10 za kusini ambazo zimeathiriwa zaidi na kimbunga. Wafanyakazi wa uokoaji wamezidiwa, na wanatumia majembe kujaribu kuwatafuta manusura waliofukiwa na udongo.

    "Tuna mito inayofurika, tuna watu wanaobebwa na maji ya bomba, tuna majengo yanayoporomoka," msemaji wa polisi Peter Kalaya aliiambia BBC. Akikumbuka jinsi alivyosaidia kumwokoa mtoto, mkazi wa Blantyre, Aaron Ntambo alisema:

    "Mtoto huyo alikuwa amekwama hadi kichwani kwenye tope, alikuwa akilia kuomba msaada, japokuwa maji yalikuwa makali sana, tulifanikiwa kuvuka na kumuokoa. ilikuwa ngumu sana lakini tuliweza kumtoa nje."

    Maafisa katika hospitali kuu ya rufaa mjini humo walisema hawawezi kukabiliana na idadi kubwa ya miili ambayo walikuwa wakipokea.

    Shirika la misaada la kimatibabu la Madaktari Wasio na Mipaka lilisema kuwa zaidi ya watoto 40 walitangazwa kufariki walipofika hospitalini.

    Viongozi walitoa wito kwa familia zilizoachwa kuchukua maiti kwa ajili ya mazishi kwani chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo kilikuwa kinakosa nafasi.

    Shirika la serikali la kusaidia maafa limesema zaidi ya watu 20,000 wamekimbia makazi yao.

  19. Tunachofahamu kuhusu ndege isiyokuwa na rubani ya Marekani iliyogongana na ya Urusi Bahari Nyeusi

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Gazeti la Marekani la The Washington Post linaripoti kuwa droni ya Marekani MQ-9 Reaper drone iligongana na ndege ya mapigano ya Urusi Su-27 na kuanguka ndani ya Bahari Nyeusi karibu na jimbo lililotwaliwa na Urusi la Crimea.

    Hhuu ndiio ukweli kuihusu droni ya Marekani iliyodunguliwa:

    • Ndege hizi aina ya droni hutumiwa na jeshi la Marekanikwa ajili ya kukusanya taarifa za kijasusi, kufanya upelelezi, katika shughuli za uokoaji, na katika mashambulio dhidi ya maeneo ya thamani ya juu yanayolengwa. Awali, MQ-9 Reaper, miongoni mwa mambo mengine ilihusika katika vita vya Iraq, Afghanstan na Syria.
    • Droni hizi huongozwa kutoka mbali na timu ya watu wawili (rubani akishirikiana na mlenga shabaha) ambao kwa kawaida huwa katika mojawapo ya ngome 20 za Marekani zilizopo katika majimbo 17 ya Marekani
    • Droni za MQ-9 Reaper zinaweza kubeba makombora mepesi yanayoongozwa na makombota aina ya masafa ya aina ya 16 Hellfire.tangi yake ya mafuta ina uwezo wa kujaa lita 560 za mafuta.
    • Tangu mwaka 2007, wakati when General Atomics ilipoanza kutengeneza aina hii ya droni, kikosi cha Marekani US Air Force kimeagiza zaidi yaMQ-9 Reapers 360.
    • Kulingana na waraka rasmi wa Marekani, garama ya droni moja aina ya MQ-9 Reaper ni takriban dola milioni30. Urefu wake ni mita 11, urefu wa mbawa ni mita 20, ikiwa na uwezo wa kubeba tani 1.7 .
    • Droni hiyo ina ving’amuzi, kamera na mfumo wa kulenga shabaha

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi

    • Ndege ya Urusi yagongana na ndege isiyo na rubani ya Marekani juu ya bahari nyeusi
    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  20. Hujambo na karibu tena kwa matangazo yetu mubashara ya leo tarehe 15.03.2023